MTUME ATHIBITI MBELE YA ADUI AKIWA NA KUNDI LA MASWAHABA WALIOMUAHIDI KUFUNGAMANA NAE MPAKA KUFA

Ama Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisimama imara mbele ya adui akipambana nae mpambano wa kufa na kupona.

Akamnyeshea adui mvua ya mishale mpaka ikamuishia na upinde wake ukakatika kutokana na wingi wa kutumiwa.

Alipoishiwa mishale akaanza kuvurumisha mvua ya mawe mpaka akaanguka chini.

Katika kizaizai hiki na katikati ya kundi la maadui, Bwana Mtume alikuwa pamoja na maswahaba wake wachache.

Inaaminiwa kwamba mswahaba waliothibiti pamoja na Mtume wa Allah mbele ya adui hawakuzidi kumi.

Baada ya wengi wao kusambaratika huko na huko kutokana na shambulizi kali, kubwa, la nguvu na la kushtukiza likitokea kusikotazamiwa.

Hawa walikula kiapo cha utii kwa Mtume kwamba watakuwa pamoja nae mpaka kufa au ipatikane nusura ya Allah.

Baada ya Mtume wa Allah kuanguka chini, wakamzunguka na kuwa mithili ya ngome imara inayomuhami dhidi ya hujuma za adui mwenye uchu na roho yake.

Wakweli hawa waliyatoa maisha yao hidaya njema katika kumlinda Mtume wa Allah. Huyu hapa Sayyidina Twalhah Ibn Ubeidillah-Allah amuwiye radhi-anampigania Mtume wake kwa kuyatoa muhanga maisha yake asalimike Mtume wa Allah.

Akawa anamlinda mbele yake, nyuma, kuliani na kushotoni kwake kwa upanga wake uliokuwa ukizivuna shingo za maadui.

Kwa kuwa hivi ni vita, unapiga na kupigwa, Twalhah nae alifunikwa na wingu la panga za maadui huku mvua ya mishale ikimjia kutokea kila upande.

Pamoja na hali hii ngumu ya hatari, Twalhah aliendelea kuwa ni ngome imara ya Mtume wa Allah mpaka kikamuondokea kiwingu cha mushrikina hawa.

Siku hii Twalhah ndiye aliyekuwa nyota katika kumuhami Mtume wa Allah, mpaka Bwana Mtume akawa anasema: “Kwa yakini amejiwajibishia Twalhah!”

Yaani ameiwajibishia nafsi yake kuingia peponi kwa sababu ya kumlinda kwa dhati Bwana Mtume.

Huyu hapa Sayyidina Shamaas Ibn Uthman-Allah amuwiye radhi-hakuwa nyuma katika kumuhami Mtume wa Allah.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa hatupi jicho lake kuliani wala kushotoni ila alimuona bwana huyu upande huo akimlinda kwa upanga wake.

Pale Mtume alipozungukwa na kutiwa kati na adui, Shamaas akageuka ngao madhubuti iyazuiliayo mashambulizi makali ya adui  yaliyoelekezwa kwa Mtume wa Allah kwa lengo la kumtokomezelea mbali.

Mashambulizi yakamlemea na kumuacha chini maiti hali ya kuwa shahidi-Allah amrehemu yeye na maswahaba wote wa Mtume wa Allah.

Akasindikizwa Shamaas na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Simpatii Shamaas badali ila pepo”.

Abuu Twalhah-Allah amuwiye radhi-alikuwa mlenga shabaha hodari sana, akaumwaga mfuko wa mishale yake mbele ya Bwana Mtume.

Akaanza kutupa mishale kumlinda Mtume wa Allah, nae Bwana Mtume akawa anamwambia       ye yote anayepita miongoni mwa maswahaba wake: “Mmwagie mishale yako Abuu Twalhah”.

Kauli hii ya Bwana Mtume ilitokana na umahiri mkubwa aliouonyesha Sayyidina Abuu Twalhah katika kurusha mishale iliyowarudisha nyuma maadui.

Kila Abuu Twalhah alipokuwa akirusha mishale, Bwana Mtume alikuwa akiangalia kwa nyuma yake ili apate kuona matuko (mahala ulipoangukia) ya mshale.

Abuu Twalhah akawa anamwambia:

“Ewe Mtume wa Allah, nakufidia mama na baba yangu! Usiangalie, usije kupatwa na mishale ya watu hawa. Niuawe mimi kabla yako na uso wangu uwe ni fidia ya uso wako”.

Ngao nyingine ya Mtume wa Allah katika wakati huu mgumu, ilikuwa ni Sayyidina Abuu Dujaanah-Allah amuwiye radhi.

Huyu aliipa mgongo wake mishale ya adui itue juu yake isimpate kipenzi chake; Mtume wa Allah. Aliinamia mpaka akashindwa kuhimili uzito wa mashambulizi huku mgongo wake ukiwa hauna mahala pasipochomwa na mshale-Allah amuwiye radhi.

Sayyidina Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw-Allah amuwiye radhi-nae hakuwa nyuma katika kuonyesha ushujaa wake katika kumlinda Bwana Mtume.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akawa anamsaidia kwa kumpa mishale huku akimwambia: “Tupa nakufidia baba na mama yangu”.

Historia itakuwa haikutenda haki kama haitamtaja mwanamke aliyesimama kidete katika kumuhami Mtume wake.

Huyu si mwingine bali ni Ummu Umaarah; Nasiybah Bint Ka’ab-Allah amuwiye radhi. Mchango wake ulikuwa ni kuhakikisha kuwa jeshi la haki linapata maji ya kutosha ya kunywa katika kipindi chote cha vita hivi.

Mama huyu alipoona Bwana Mtume amezingirwa na maswahaba wanakimbizana hovyo wakimuacha mtume wao katikati ya kundi la maadui.

Chini akaitupa ndoo yake ya kuchotea maji, akautwaa upanga na kuingia mapambanoni akiwa amejifunga kibwebwe.

Akapambana katikati ya kundi la maadui wanamume kwa ajili tu ya kumuhami na kumnusuru Mtume wa Allah.

Akapigana mpaka akapatwa na majeraha yasiyopungua kumi na tatu, moja likiwa ni jeraha kubwa lililoacha shimo kubwa begani kwake.

Hapo ndipo mahala alipopigwa na Ibn Qamiah. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alisikika siku hiyo akisema: “Sikupata kugeuka kuliani wala kushotoni ila nilimuona akinilinda”.

Sayyidina Hubaab Ibn Mundhir-Allah amuwiye radhi-yeye alikuwa akiwakusanya mushrikina hawa kama mchungaji anavyowakusanya kondoo au mbuzi wake.

Wakamkusanyikia kwa wingi mpaka pakavumishwa kuwa kauawa, walipomtawanyikia hapo ndipo alipowainukia na upanga wake mkononi.

Akaanza kuliendesha mbio mojawapo la makundi yao, huku wengine wakitimua mbio.

Haya huyu hapa Ziyaad Ibn Sakan na kundi la maanswari-Allah awawiye radhi-walipigana kumuhami Mtume wa Allah.

Wakiua na kuuawa mmoja baada ya mwingine kwa ajili ya kumnusuru Bwana Mtume.

Wa mwisho kuuawa katika kundi hili alikuwa ni Sayyidina Ziyaad, alipigana  mpaka majeraha yakamuhemeza.

Mtume wa Allah akamtandikia miguu yake mitukufu iwe ni mto wake wa kupumzikia kutokana na kazi nzito aliyoifanya.

Mauti yakamjia-Allah amuwiye radhi na wote swahaba wa Mtume-akiwa miguuni mwa Bwana Mtume, eeh bakhti iliyoje! Musw’ab Ibn Umeir-Allah amuwiye radhi-anakufa katika kumnusuru Mtume wa Allah.

Huyu alikuwa akiyazuia kwa mwili wake mapigo ya panga za mushrikina yaliyoelekezwa kummaliza Bwana Mtume.

Aliuawa na Ibn Qamiah kwa kumdhania kuwa ni Bwana Mtume, kisha akakimbia  akitangaza baina ya mushrikina wenzake kuwa amemuua Mtume wa Allah.

Siku hii ndugu muislamu waliuawa maswahaba wengi katika kumnusuru Mtume wa Allah, kila mmoja akiitoa nafsi yake fidia kwa Bwana Mtume.

Akiwa ni ngome na ngao baina ya Mtume na adui aliye mithili ya mbwa mwitu katika kundi la wanakondoo.

 

MTUME ATHIBITI MBELE YA ADUI AKIWA NA KUNDI LA MASWAHABA WALIOMUAHIDI KUFUNGAMANA NAE MPAKA KUFA

Ama Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisimama imara mbele ya adui akipambana nae mpambano wa kufa na kupona.

Akamnyeshea adui mvua ya mishale mpaka ikamuishia na upinde wake ukakatika kutokana na wingi wa kutumiwa.

Alipoishiwa mishale akaanza kuvurumisha mvua ya mawe mpaka akaanguka chini.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *