NGUZO ZA SWALA YA IJUMAA

Swala ya Ijumaa inasimama juu ya nguzo mbili ambazo ndio msingi wa swala hii tukufu. Nguzo hizo ni:-

KHUTBA MBILI:

Hii ndio nguzo ya kwanza ya msingi miongoni mwa nguzo mbili zinazoijenga swala ya Ijumaa.

Nguzo hii inaambatana na sharti kadhaa ambazo hujulikana kama “sharti za khutba mbili” na sharti hizo ni kama zifuatavyo:-

a.  Kusimama na kutenganisha baina ya khutba ya kwanza na ile ya pili kwa kitako kifupi.

Kumeshurutizwa khatibu akhutubu ilhali akiwa kasimama ikiwa anaweza huko kusimama na akishindwa kusimama basi atakhutubu akiwa amekaa kitako.

Kadhalika anapaswa kukaa kitako kifupi ili kutenganisha baina ya khutba ya kwanza na ile ya pili. Hivi ndivyo alivyofanya mwenyewe Bwana Mtume.

Imepokelewa kutoka kwa Jaabir Ibn Samurah-Allah amuwoye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikhutubu khutba mbili akikaa baina ya (khutba) mbili hizo. Na alikuwa akikhutubu ilhali akiwa amesimama.

Muslim-Allah amrehemu.

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema:

“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akikhutubu ilhali kasimama kisha hukaa (baada ya khutba ya kwanza) kisha huinuka (husimama tena kwa ajili ya khutba ya pili) kama mfanyavyo nyinyi hivi sasa”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

 

b.  Khutba ziitangulie swala.

Ni sharti swala ya Ijumaa itanguliwe na khutba mbili, zikimalizika ndio swala ikimiwe.

Haiwi kama inavyokuwa katika swala za Eid ambapo hutangulia swala kisha ndio zikafuatia khutba mbili.

Sharti hii inatokana na eleweko jumuisho la hadithi zilizopokelewa katika kutaja swala ya Ijumaa na kwa Ijmaa  ya waislamu katika hili.

Twahara ya hadathi ndogo na kubwa na ya najisi isiyosameheka katika nguo, mwili na mahala pa kukhutubia na kusitiri tupu.

Kumeshurutizwa kwa khatibu kuwa twahara; asiwe na hadathi ndogo itakayompasishia udhu wala ile kubwa itakayomuwajibishia josho. Pia inatakikana mwili wake, nguo na mahala pa kukhutubia pawe twahara; isiwepo najisi isiyosameheka kisheria. Kadhalika kumeshurutizwa khatibu awe amejisitiri kwa mujibu wa sheria.

Sharti hii inatokana na kuichukulia khutba kuwa ni kama swala ya Ijumaa.

Ni kwa ajili ya msimamo huu ndio khutba mbili zinakuwa ni badali ya zile rakaa mbili za fardhi ya Adhuhuri.

Kwa mantiki hii khutba zikashurutiziwa sharti zote zilizoshurutiziwa swala, kuanzia twahara na baki ya sharti nyinginezo.

 

Khutba (nguzo) itolewe kwa lugha ya Kiarabu.

Kunampasa khatibu kukhutubu kwa lugha ya Kiarabu hata kama wanaokhutubiwa hawaijui lugha hiyo. Sharti hii inazikhusu zile nguzo tano za khutba kama tutakavyozitaja.

Ama waadhi unaweza kutolewa kwa lugha inayofahamika na watu wa mahala husika kama yamivyoelezwa hayo katika vitabu vya Fiq-hi pamoja na makindano ya wanazuoni juu yake, zinduka!

Kufululiza baina ya nguzo za khutba, kufululiza baina ya khutba ya kwanza na ile ya pili na baina ya khutba ya pili na swala.

Kumeshurutizwa kutokuwepo mwanya mkubwa baina ya nguzo na nguzo fuatizi, baina ya khutba na khutba ambatizi na hali kadhalika baina ya khutba na swala.

Angalia lau utakuwepo mwanya mkubwa baina ya khutba ya kwanza na ile ya pili au mwanya huo ukawa ni baina ya khutba mbili na swala, khutba hiyo haitasihi.

Ikimkinika kuidiriki kutawajibika kuirudia na kama haikumkinika, basi swala hiyo itageuka na kuwa Adhuhuri na sio Ijumaa tena.

Kuwasikilizisha nguzo za khutba watu arobaini wanaofungamanikiwa na Ijumaa.

 Kunampasa khatibu kunyanyua sauti yake wakati wa kukhutubu kiasi cha kuweza kusikiwa na wale anaowakhutubia ambao hawana matatizo katika usikivu wao.

Hizi ndizo shatri za khutba mbili kama zilivyotajwa katika vitabu vya Fiq-hi kwa rejea za hadithi, virejee utaziona.

 

NGUZO ZA KHUTBA MBILI:

Baada ya kuangalia sharti za khutba, inatupasa tuelewe kuwa khutba ya Ijumaa inazo nguzo ambazo hutambulika kama “nguzo za khutba” hizi ni kama zifuatavyo:-

1)      Kumuhimidi Allah kwa tamko lo lote lenye luleta maana ya himda.

Kama khatibu kusema: “Al-hamdulillah” au “Ahmadullah” na mithili ya matamko haya.

2)      Kumswalia Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwa tamko lo lote la swala ya mtume.

Imeshurutizwa khatibu alitaje jina la Bwana Mtume kwa ufumbulizo. Mithili ya kusema: “Nabiyyi”, ama “Rasuuli”, au “Muhammad”, kwani hakutoshi kutaja dhamiri (kiwakilishi-pronoun) kama vile kusema: (Allaahumma swalli alayhi) bila ya kutaja jina.

3)      Kuwausia watu kumcha Allah kwa tamko lo lote lenye kubeba maana hiyo.

Mtihili ya kusema: “Uuswiykumu bitaquwallaah”, au “Ittaquwalaah” na kadhalika.

Nguzo tatu hizi; himda, swala ya Mtume na wasia wa kumcha Allah, ni nguzo shiriki kwa kila mojawapo ya khutba mbili. Yaani zinaletwa katika khutba zote mbili.

4)      Kusoma aya ya Qur-ani katika mojawapo ya khutba mbili.

Imeshurutizwa kuwa aya hiyo iwe ni yenye kufahamika na yenye maana ya wazi na ni bora isomwe mwishoni mwa khutba ya pili.

5)      Kuwaombea dua waislamu katika khutba ya pili kwa tamko linaloweza kuitwa dua.

 

2.      KUSWALI RAKAA MBILI KATIKA JAMAA:

Hii ndio nguzo ya pili ya  msingi ya swala ya Ijumaa kwa ushahidi wa hadithi zifuatazo:-

ü     Imepokelewa kutoka kwa Sayyidina Umar-Allah amuwiye radhi-amesema: “Swala ya ya Ijumaa ni rakaa mbili (haya ni) kwa ulimi wa Muhammad-Rehema na Amani zimshukie”. Nasaai-Allah amrehemu.

ü     Imepokelewa kutoka kwa Twariq Ibn Shihaab-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ijumaa ni haki ya wajibu kwa kila muislamu katika jamaa…” Abuu Daawoud-Allah amrehemu.

Fungamano na kongamano la wanazuoni katika hili la kuswaliwa rakka mbili za Ijumaa katika jamaa limejengeka juu ya hadithi hizi.

Kumeshurutizwa katika kuidiriki (kuipata) jamaa kudiriki rakaa moja ya Ijumaa.

Mtu akiidiriki rakaa moja hiyo, swala yake (Ijumaa) itasihi na kama hakudiriki rakaa kutamuwajibikia kuihawilisha (kuigeuza) Adhuhuri.

Na ni wajibu maamuma wanaounda jamaa ya Ijumaa ambao kwao Ijumaa inafungamana isipungue idadi yao watu arobaini.

Kwa msingi huu, lau mtanguliwa (mtu aliyechelewa) atakuja na akamfuata Imamu katika rakaa ya pili, Ijumaa yake itasihi kutokana na  kule kuidiriki kwake rakaa moja ya swala ya Ijumaa.

Baada ya Imamu kutoa salamu, yeye atapaswa kuinuka kuswali rakaa moja nyingine ili kutimiza idadi ya rakaa mbili za Ijumaa.

Ama ikiwa huyu mtanguliwa atamdiriki Imamu baada ya kuinuka kutoka katika rukuu ya rakaa ya pili, haikutuka kwake Ijumaa.

Kwa hivyo atawajibika kumfuata Imamu hapo alipomdiriki kwa nia ya Ijumaa na baada ya salamu ya Imamu atainuka na kuitimiza Adhuhuri rakaa nne.

Ni kwa kuuzingatia msingi huu huu pia, lau maamuma watamfuata Imamu katika swala ya Ijumaa na wakatimiza pamoja nae rakaa moja.

Kisha ikazuka sababu inayowapelekea wote kumkhalifu Imamu au baadhi yao. Wakamfariki na kila mmoja akatimiza rakaa ya pili ya Ijumaa hali ya kuwa mpweke (anaswali pekee), Ijumaa yao wote itakuwa ni sahihi.

Ama lau sababu hii ya mfaraka itazuka kabla ya kumalizika kwa rakaa ya kwanza. Wakamfariki, basi bila shaka yo yote Ijumaa yao haitasihi na itageuka kwa upande wao kuwa Adhuhuri.

Maelezo na uchambuzi huu ni natija ya riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema: Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Atakayeidiriki rakaa moja ya swala ya Ijumaa na swala nyinginezo, basi na aiongezee nyingine na hakika swala yake itakuwa imetimia”. Nasaai, Ibn Maajah & Daaruqutwniy-Allah awarehemu.

 

NGUZO ZA SWALA YA IJUMAA

Swala ya Ijumaa inasimama juu ya nguzo mbili ambazo ndio msingi wa swala hii tukufu. Nguzo hizo ni:-

KHUTBA MBILI:

Hii ndio nguzo ya kwanza ya msingi miongoni mwa nguzo mbili zinazoijenga swala ya Ijumaa.

Nguzo hii inaambatana na sharti kadhaa ambazo hujulikana kama “sharti za khutba mbili” na sharti hizo ni kama zifuatavyo:-

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *