Ni maumbile ya wanadamu kukhitilafiana kifikra, kimawazo, kiufahamu na kiakili. Na mara nyingi watu huongozwa na matamanio na matashi ya nafsi zao bila ya kujali sheria au haki za wenzao.
Maumbile haya ya wanadamu ndio yanayowajibisha kuwepo kwa sheria zitakazowatawala na kuwahukumu.
Na ili sheria hizi zifanye kazi na kuheshimiwa ni lazima yawepo mamlaka/nguvu itakayosimamia utekelezaji wa sheria hizi.
Hapa ndipo inapojitokeza haja ya jamii yo yote ya wanadamu kuwa na kiongozi atakayekuwa na jukumu/dhima ya kuchunga maslahi ya uma kwa mujibu wa sheria iliyokubaliwa na kuridhiwa na jamii husika.
Kama ambavyo ni wajibu wa raia (waongozwa) kuheshimu sheria, kadhalika ni wajibu wa kiongozi kuhakikisha kuwa sheria zinaheshimiwa kupitia mamlaka aliyopewa.
Ni wajibu wa kisheria bali ni sehemu ya dini, waislamu kumsimika (kumtawalisha) kiongozi wanayemkubali atakayewatawalia na kuwaratibia mambo yao kwa mujibu wa sheria ya Allah (Qur-ani) na Suna (hadithi za Mtume).
Kunawawajibikia waislamu kumchagua miongoni mwao mtu anayefaa kubeba dhima ya uongozi wa uma.
Kiongozi atakayechaguliwa na uma ni lazima awe ni muislamu kweli anayeujua Uislamu wake, mcha-Mungu, muadilifu, mwenye elimu ya sheria, uongozi na mahusiano ya kijamii.
Suala la kumsimika kiongozi si suala geni katika historia ya jamii za wanadamu, na hii ni kutokana na umuhimu wa suala lenyewe kwa kila jamii.
Katika Uislamu, uongozi/kuwa na kiongozi ni suala lililothibiti katika Qur-ani (sheria mama) na suna (sheria shereheshi).
Tukiyapekua mabuku ya tarekh (historia) na sira, tutayakuta yametusajilia upelekaji wa vikosi vya vita alivyovituma Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-sehemu mbali mbali.
Mabuku haya yanaonyesha kwamba Bwana Mtume hakukituma kikosi cho chote, kikubwa au kidogo ila alikisimikia kiongozi atakayekiongoza na akakiusia kumtii kiongozi wao. Kadhalika Bwana Mtume hakuuacha mji wo wote wa Kiislamu bila ya kuutawalishia Amiri kama tarekh inavyolithibitisha hilo.
Kadhalika Mtume alipokuwa anaondoka nje ya Madinah kwa ajili ya kuongoza vita au kwa sababu nyingine, alimteua mmoja wa maswahaba wake kukaimu nafasi yake mpaka atakaporudi.
Matendo yote haya ya Bwana Mtume ni ushahidi wa wazi unaoonyesha nafasi ya uongozi katika Uislamu na kwamba ni lazima jamii ya Kiislamu bali jamii ya wanadamu bila ya kujali itikadi/imani kuwa na kiongozi.
Uislamu kama dini na mfumo sahihi wa maisha ili kuhakikisha kuwa haki na uhuru wa kila mtu unalindwa kupitia sheria zinazosimamiwa utekelezaji wake na kiongozi aliyekubaliwa na kuchaguliwa na uma.
Ili hili lifikiwe, Uislamu umeweka haki na wajibu baina ya kiongozi na raia (waongozwa). Kwa maneno mengine tunaruhusika kusema kuwa majukumu/wajibu wa kiongozi ndio haki za raia na wajibu wa raia ndio haki za kiongozi.
WAJIBU WA KIONGOZI/HAKI ZA RAIA:
Kiongozi akishachaguliwa ni wajibu apewe madaraka/mamlaka kamili kwa mujibu wa sheria bila ya kupingwa au kuingiliwa katika maamuzi/hukumu azitoazo maadam hazipingani na sheria.
Raia nao wana wajibu wa kumuunga mkono na kumsaidia kiongozi wao katika kuitekeleza dhima/majukumu waliyompa. Miongoni mwa majukumu/wajibu muhimu wa kiongozi ni kama yafuatavyo:-
i. WAJIBU WAKE KWA UPANDE WA DINI WENYE MASLAHI KWA RAIA WAKE:
Miongoni wa wajibu mkubwa aliobebeshwa kiongozi mabegani mwake ni kusimamia, kuhifadhi na kuiendeleza dini.
Ahakikishe kuwa anapanda mbegu ya mapenzi ya dini mioyoni mwa raia (uma) wake ili waweze kuzifuata kwa ukamilifu hukumu za dini.
Ni wajibu wa kiongozi kuona kuwa mwenendo, silka, tabia na utamaduni wa dini ndio unaoitawala jamii (uma) yake.
Kiongozi afunge mianya na milango yote inayoweza kuleta/kusababisha mmomonyoko wa maadili miongoni mwa raia wake.
Akate mizizi ya tamaduni zote zinazopingana na sheria ya Allah na badala yake awajengee raia wake mazingira ya kuupenda, kuuthamini, kuujali na kuufuata utamaduni wa dini yao. Sambamba na kushikamana na mwendo (suna) wa Mtume wao.
Kiongozi na jamii kwa ujumla itambue kuwa maovu na maasi yanayotapakaa katika jamii kwa kasi ya moto nyikani chini wa mwavuli wa kile kinachoitwa ‘kwenda na wakati’ na watu wakayazoea na kuyaona kuwa ni mema.
Watambue kuwa hilo ni gonjwa hatari litakaloisambaratisha na kuiangamiza jamii. Njia na dawa pekee ya kulitibu na kuliangamiza gonjwa hili na kuiokoa jamii na athari yake ni kwa kiongozi kuhakikisha kuwa hukumu ya sheria inamuangukia kila mtenda maovu aendaye kinyume na sheria.
Aadhibiwe na kutiwa adabu kwa mujibu wa sheria kulingana na kosa/dhambi aliyoitenda. Mbali na usimamiaji huu wa sheria, kiongozi anapaswa kuhakikisha kuwa raia wake wanaijua sheria sambamba na haki zao za kisheria bila ya kusahau wajibu wao.
Raia waelimishwe mpaka watambue kuwa sheria na adhabu zitolewazo kufuatia makosa mbalimbali zimewekwa kwa maslahi yao kama uma.
Sheria na adhabu hizi zina dhima kuu ya kuhifadhi na kulinda uhai, mali, dini, heshima na akili ya mtu.
Jamii ikipata hifadhi na ulinzi wa vitu hivi ndipo watu wanaweza kuishi kwa amani. Na ni chini ya mwavuli huu wa amani na utulivu raia wataweza kuendesha shughuli zao za kila siku kwa ufanisi mkubwa ili kujiletea maendeleo yao binafsi na ulimwengu kwa ujumla.
Ni katika mazingira haya ndipo watapata utulivu mkubwa utakaowawezesha kumuabuadu Allah Mola Muumba wao kwa unyenyekevu na utii.
Watu waelewe kuwa kama kungelikuwa hakuna sheria na wasimamiaji wa sheria (viongozi), basi ulimwengu huu ungelikuwa ni ulimwengu wa samaki. Ambamo samaki mkubwa hummeza aliye mdogo na hakuna wa kumuuliza.
ii. KUSIMAMISHA UADILIFU:
Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa na Uislamu kutambua kwamba kuwafanyia uadilifu raia wake ni wajibu wake yeye.
Na wao raia huo uadilifu wake ni haki yao ya kisheria waliyopewa na Allah, kwa hivyo hakuna wa kuwapokonya.
Ahakikishe kuwa anatoa hukumu ya haki, isiyo na upendeleo kwa kigezo cho chote kiwacho baina ya mahasimu wawili waliofika mbele ya sheria.
Achukue haki ya mdhulumiwa kutoka kwa dhalimu na kumpa huyo mdhulumiwa kwa namna anayostahiki.
Watu wote wawe sawa mbele ya sheria, usiwepo kabisa mwanya wa upendeleo. Mfalme asipewe haki kwa sababu tu ya ufalme wake, sheria isipindwe kwa tajiri kwa kigezo cha utajiri wake na mnyonge asionewe kwa ajili tu ya unyonge wake.
Ni wajibu wa kiongozi kuyasimamia yote haya kwa kuhakikisha kuwa uadilifu unakuwa juu ya utajiri, cheo na umaarufu wa mtu.
Kiongozi akumbuke kuwa uadilifu ndio msingi mkuu wa haki na utawala bora unaoenziwa na wapenda haki wote bali na Allah.
Kiongozi wa Kiislamu anatakiwa kujipangia utaratibu wa kusikiliza malalamiko na matatizo ya raia wake.
Awe karibu sana na watu wake, ashirikiane nao na kuwaenzi katika dhiki na faraja kiasi cha kuwafanya wamuhisi na kumkubali kuwa ni mwenzao.
Kiongozi muumini hatakiwi kujenga uzio baina yake na raia wake, akawa hana nafasi ya kukutana nao na kujua matatizo yao yanayowakabili, kwani kufanya hivyo ni kuwaghushi raia. Bwana Mtume, kiongozi muadilifu kuliko wote waliopata kuwepo na watakaokuwepo-Rehema na Amani zimshukie-anasema:
“Hapana mja ye yote atakayepewa uongozi na Allah Mtukufu, akafa siku ya kiyama na il-hali amewaghushi raia wake ila Allah atamuharamishia pepo (kiongozi huyo ghashashi)”. Bukhaariy & Muslim.
Na akasema tena:
“Ye yote atakayetawalishwa cho chote katika mambo ya waislamu, kisha asiwatumikie upeo wa juhudi yake na asiwape nasaha zake ila hataingia pamoja nao peponi”. Muslim
Na Allah Mola Mwenyezi anatuambia:
“HAKIKA ALLAH ANAKUAMRISHENI KUZIRUDISHA AMANA KWA WENYEWE (wanaozistahiki) NA MNAPOHUKUMU BAINA YA WATU MUHUKUMU KWA HAKI…” [4:58]
ii. KUKUBALI NASAHA NA USHAURI MWEMA WA RAIA WAKE:
Kiongozi wa Kiislamu hawi dikteta kama ambavyo hawi bendera akafuata upepo unakomuelekezea.
Ni haki yao raia kama uma kumnasihi na kumpa kiongozi wao ushauri mzuri unaolenga kujenga na sio kubomoa.
Na ni wajibu wa kiongozi kuukubali na kuupokea ushauri na nasaha hizo bila ya kinyongo.
Pamoja na kukubali nasaha na kupokea ushauri, kiongozi anapaswa kuwa na chujio/chekecheo la kuchekechea nasaha na kuuchujia ushauri huo aliopewa na raia wake.
Autupilie mbali ulio mbaya unaolenga kubomoa na aukumbatie na kuufanyia kazi ule ulio mzuri unaolenga kujenga na kudhamini maslahi ya uma.
Kukubali nasaha na kutaka ushauri ni miongoni mwa nguzo za sheria ya Uislamu. Hebu tumuangalie Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-namna alivyokuwa akiusikiliza ushauri na kuukubali.
Katika vita vya Badri, Mtume wa Allah alipiga kambi mahala fulani ili kukabiliana na mushrikina. Swahaba wake Al-Habaab Ibn Al-Mundhir-Allah amuwiye radhi-akamuendea Bwana Mtume na kumwambia kwa adabu:
“Ewe Mtume wa Allah, unaionaje kambi hii, je ndio kambi aliyokushusha hapo Allah (kama ni hivyo) hakutufalii sisi kuhoji wala kupinga. Au hizi ni fikra (zako tu) na mbinu za vita? (Mtume) akamjibu: Bali hii ni fikra yangu (sio amri ya Allah) na mbinu za vita. Akasema (Al-Habaab): Ewe Mtume wa Allah, hakika hapa si mahala panapofaa kupiga kambi. Ondoka na watu twende mpaka tufike eneo lenye maji lililo karibu na watu (mahasimu wetu), tupige kambi hapo. Kisha tuzibe visima vyoye vilivyo nyuma yetu, kisha tujenge mahodhi ya maji na kuyajaza maji. Halafu ndio tuanze kupambana nao wakati ambapo sisi tutakuwa tuna maji ya kunywa na wao hawana. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Hakika umetoa rai nzuri” na akaifuata na kuikubali rai hiyo ya Al-Hubaab. Angalia Siyratu Ibn Hishaam.
V. KUGAWA MADARAKA KWA KUWATEUA VIONGOZI WA CHINI YAKE.
Kiongozi mkuu ndiye mwenye dhima na jukumu la kuongoza serikali sambamba na kupanga mipango endelevu ya jamii (raia).
Ana wajibu mkuu wa kuhakikisha kuwa mipango na taratibu hizo zinahamishwa kutoka maandishini na kutiwa katika ulimwengu wa matendo kwa maslahi na manufaa ya jamii yake. Ni jukumu lake kuutumikia uma wake kwa uadilifu.
Kutokana na ukubwa, uzito na ugumu wa majukumu haya ya kiongozi kama mtumishi mkuu wa uma, ni dhahiri kuwa hataweza kulibeba furushi hili la majukumu peke.
Kutokana na ukweli huo usiokanushika ni haki ya msingi ya raia wake na ni wajibu wake wa lazima kuwateulia watu miongoni mwao watakaomsaidia katika majukumu ya utawala.
Hii ndio njia aliyoitumia Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-wakati wa ustawi (kupanuka) wa dola ya Kiislamu zama za uhai wake.
Ukizifungua kurasa za tarekh (history) hutoshindwa kuona kuwa Bwana Mtume aliwateua kwa vipindi maalumu mabwana Aliy Ibn Abuu Twaalib na Muaadh Ibn Jabal-Allah awawiye radhi-kuwa makhalifa wake katika nchi ya Yemen.
Kama alivyomteua Abuu Musa na maswahaba wengine-Allah awawiye radhi-kuwa makadhi baadhi yao na wengine kuwa magavana na walinganiaji dini sehemu mbalimbali za ulimwengu ule wa Kiislamu.
Bwana Mtume alipomteua mmojawapo wa maswahaba wake kuwa kiongozi wa uma katika ngazi fulani, hakumuachia kuongoza kwa maoni na matashi yake binafsi.
Bali alimpa muongozo kamili wa kufuata katika kazi yake hiyo, sambamba na miiko na mipaka ya kazi.
Na zaidi ya yote hayo alimuusia kumcha Allah na kuwa muadilifu katika kazi yake hiyo. Katika uteuzi huu wa viongozi (makhalifa) wa chini yake, Bwana Mtume alitumia vigezo maalumu. Aliangalia uaminifu, uwezo wa kazi (utawala), ucha-Mungu na baki ya sifa nyingine njema.
Hakumteua katu mtu ajizi, dhaifu wala mwenye pupa ya kupata uongozi ili awe bwana mkubwa (muheshimiwa).
Swahaba Abuu Dhari alimuomba Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kumpa nafasi ya uongozi. Mtume akamwambia:
“Wewe ni dhaifu (huuwezi uongozi) nao (huo uongozi) ni amana na siku ya kiyama ni fedheha na majuto. Ila kwa atakayeutwaa kwa haki yake na akayatekeleza yanayompasa katika huo uongozi”. Muslim
Utaratibu huu wa uteuzi ulirithiwa pia na makhalifa wa Mtume baada ya kufa kwake, na inatakikana urithiwe pia na viongozi wetu wakuu wa leo kwa maslahi ya uma.
V. JIHADI KATIKA DINI YA ALLAH NA ULINZI (HIMAYA) WA DOLA.
Allah Mola Mwenyezi amemleta Mtume wake Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-kwa watu wote:
“NA HATUKUKUTUMA (hatukukuleta) ILA KWA WATU WOTE, UWE MTOAJI WA KHABARI NZURI NA MUONYAJI…” [34:28]
Kwa kauli na tangazo hili la Allah, Bwana Mtume akabeba amana hii ya kuwa mjumbe wa Allah kwa ulimwengu mzima.
Akaitekeleza haki ya amana hii kwa kuufikisha ujumbe wa Allah kwa walimwengu wote kwa kipindi kisichotindika miaka kumi na tatu.
Hapo ndipo akatunukiwa shahada ya ustahiki iliyopigwa muhuri wa kukamilisha na kukhitimisha kazi kwa kauli yake Allah:
“…LEO NIMEKUKAMILISHIENI DINI YENU NA KUKUTIMIZIENI NEEMA YANGU NA NIMEKUPENDELEENI UISLAMU UWE DINI YENU…” [5:3]
Kutokana na vikwazo alivyokumbana navyo katika kuitekeleza kazi hii ya Mola wake, wakati mwingine kulimlazimu Mtume kujitoa muhanga kwa mali na nafsi yake ili kuipigania dini ya Allah.
Akapanga katika uhai wake mikakati ya kuwaandaa maswahaba wake kuchukua na kuiendeleza kazi aliyoianza. Baada ya kufa Mtume, maswahaba-Allah awaridhie-wakaibeba mabegani mwao bendera ya da’awah na kuufikisha Uislamu kule usikofika bado.
Wakashika hatamu za kuwaongoza watu katika mfumo sahihi wa maisha uliofumwa na Mola wao (Uislamu), mpaka sheria ya Allah ikatawala zaidi ya robo tatu ya dunia.
Elewa na ufahamu ewe ndugu muislamu khususan kiongozi, kuwa jihadi hii ya kuipigania dini ya Allah iliyoasisiwa na mtume wako na kuendelezwa na maswahaba wake watukufu.
Jihadi hii inaendelea muda wa kuwepo/kupatikana sababu zinazoiwajibisha mpaka kutoweka kwa mbingu, ardhi na vyote vilivyomo (kiyama).
Jihadi hii ni kwa ajili ya kulinda, kutetea na kuchunga heshima, uhai, mali na haki ya waislamu kama jamii.
Sambamba na haki yao ya kuabudu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu na kuutangaza Uislamu ulimwenguni kote bila ya kizuizi cha aina yo yote ile.
Nafasi ya Mtume katika kuuongoza uma katika jihadi unayo wewe ambaye ndio kiongozi wa waislamu leo.
Hii ni dhima isiyoepukika iliyo shingoni mwako, ni wajibu wako bali ni sehemu ya dini khasa kuwaongoza raia wako katika jihadi iwapo hali na mazingira yanalazimisha hivyo. Na kunawawajibikia raia wako wote wenye kumuamini Allah na siku ya mwisho kukutii katika hilo.
VI. USIMAMIZI, UENDELEZAJI NA ULINZI WA RASILIMALI YA DOLA NA KUHAKIKISHA MGAWANYO ADILIFU WA MALI HIZO MIONGONI MWA RAIA.
Mali ndio kano (mshipa) na zana ya maisha haya na pengine ndio sababu ya mafanikio ya maisha ya ulimwengu huu na ule ujao (akhera). Mali pia ni mojawapo ya nguzo za nguvu inayoamrishwa katika kauli tukufu ya Allah:
“BASI WAANDALIENI (wawakeeni tayari) NGUVU MZIWEZAZO (silaha) NA MAFARASI (vifaru, madege, manowari) TAYARI TAYARI (mipakani). ILI KWAZO (nguvu hizi) MUWAOGOPESHE MAADUI WA ALLAH NA MAADUI WENU…” [8:60]
Kadhalika mali ni uti wa mgongo wa maisha ya uma, kwa ukweli huu ni haki ya msingi ya raia na ni wajibu wa kiongozi kuwaratibia raia wake mipango mizuri ya kiuchumi.
Mipango itakayowashirikisha katika kuendeleza rasilimali za dola na kunufaika nazo katika nyanja za maisha yote ya kijamii.
Mipango itakayowahakikishia kupata mahitaji yao ya msingi kwa njia halali na rahisi.
Ni wajibu wa kiongozi kuanzisha ‘Baytul-Maali’-(Public Treasury) itakayokuwa na vyanzo vya mapato ili iweze kujitegema katika kutoa huduma kwa uma.
Kiongozi atakuwa na wajibu wa kusimamia mapato na matumizi ya Baytul-Maali moja kwa moja au kupitia kwa atakayemteua kwa kazi hiyo.
Miongoni mwa haki za raia kwa kiongozi wao ni kupata mgawanyo sawa wa rasilimali za dola na huduma sawa za kijamii bila ya upendeleo wa mahala fulani kwa sababu tu ndiko anakotoka kiongozi huyo.
Ahakikishe kuwa mali ya uma haihujumiwi na na kuibiwa na watu wa nje. Wanawazuoni wa kale na hawa wa sasa-Allah awarehemu-wameandika mengi katika ukumbi huu wa kisiasa khususan katika jukwaa hili la uongozi.
Sheikh Al-Maawardiy-Allah amrehemu-ni mmoja wa wanazuoni walioshika kalamu katika fani hii na kueleza kwa ufafanuzi wa kina. Yeye ameukusanya wajibu wa kiongozi katika vifungu kumi, kama ifuatavyo:-
KULINDA MISINGI YA DINI:
Ni wajibu wa kiongozi kulinda misingi ya dini na Ijmaa ya salafu. Akitokeza mzuzi (mzushi) au mpinzani wa misingi hiyo, ni wajibu wake yeye mwenyewe au kupitia mteule wake kumuwekea wazi mzuzi huyo hoja na kumbainishia ilivyo ndivyo. Ayafanye yote haya ili kuilinda dini dhidi ya kombokombo na kuulinda uma na mgawanyiko usio wa lazima.
KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA SHERIA:
Kunamlazimu kiongozi kama mtumishi wa uma kuhakikisha kuwa sheria ya Allah ndio inayotumika katika kuwahukumu mahasimu wawili na kukata magomvi baina ya wagombanao.
Ni wajibu wake kuhakikisha kuwa sheria inampa haki kila aistahikie mpaka mwenye nguvu asiweze kumuonea mnyonge kwa sababu tu ya nguvu zake.
KUIMARISHA NGUVU ZA DOLA:
Ni wajibu wakiongozi kuunda serikali imara na yenye nguvu itakayowahakikishia raia wake amani, salama na utulivu. Vitu ambavyo vitawawezesha kuendesha shughuli zao za kimaisha kwa uhuru na bila ya khofu wala bughudha. Watu waweze kusafiri wakiwa hawana khofu juu ya nafsi au mali zao.
KUWEKA MIPAKA:
Aweke mipaka itakayochunga maharamisho ya Allah yasitendwe na kulinda haki za waja wake zisivunjwe.
KUWEKA ULINZI IMARA KATIKA MIPAKA YA NCHI:
Kunampasa kuhakikisha kuwa kuna ulinzi wa kutosha na imara kuzunguka mipaka yote ya nchi. Ili kuilinda nchi dhidi ya uvamizi wa ghafla kutoka kwa maadui wa nje.
JIHADI DHIDI YA MPINZANI WA UISLAMU:
Kiongozi ana wajibu wa kumpiga vita mtu uliomfikia ujumbe wa Uislamu na akaupinga bila ya kuwa na hoja yenye kuzingatiwa. Ampige vita mpaka ima aukubali Uislamu (asilimu) au awe chini ya dhima ya Uislamu (awe Dhimiyu).
KUSIMAMIA MATUMIZI YA FEI NA SADAKA/ZAKAH KWA MUJIBU WA SHERIA:
Fei ni ile mali inayopatikana bila ya vita baada ya maadui kukimbia, mali hii na ile itokanayo na sadaka/zakah ni dhima na amana iliyo mikononi mwa kiongozi.
Kwa hivyo basi ni jukumu lake kuhakikisha kuwa mali hiyo inatumika kwa namna ilivyoagizwa na sheria.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI:
Kiongozi anapaswa kukadiria mapato na matumizi ya Baytul-Maali na kutoa kasimu (fungu) panapostahiki kwa wakati muafaka bila ya ubadhirifu au kuchelewa.
KUTEUA WATU STAHIKI WAAMINIFU NA WENYE SIFA STAHIKI KUENDESHA MAMBO:
Kunamuwajikia kiongozi kuwateua watu watakaomsaidia katika kuendesha shughuli mbalimbali za kiutawala.
Vigezo vya uteuzi huo viwe ni uaminifu na sifa stahiki kwa kazi husika ili huduma za kijamii ziendeshwe vema na mali ya uma iwe katika udhibiti wa watu waaminifu.
KUONGOZA NA KUSIMAMIA IDARA ZOTE ZA UTAWALA:
Kiongozi anawajibika kutoa muongozo wa uendeshaji wa shughuli za utawala katika idara/wizara mbalimbali za serikali yake.
Na kusimamia na kufuatilia kwa karibu utendaji wa watendaji aliowateua kushika nyadhifa hizo.
Ili kuyaona haya na mengi mengineyo yahusuyo mambo ya utawala na sheria, rejea kitabu “AL-AHKAAMUS-SULTWAANIYYAH” cha Al-Maawardiy.
2 – WAJIBU WA RAIA/HAKI ZA VIONGOZI.
Utakapofungamana uongozi kwa mtu ambaye waislamu wamemridhia kwa nafsi zao, dini na dunia yao.
Atakuwa tayari ana dhima na wajibu ambao ni haki ya Allah na haki ya uma (raia) wake. Sasa basi ili aweze kuutekeleza wajibu wake huu ipasavyo na kwa ukamilifu, Uislamu umempa haki kadhaa juu ya raia wake. H
aki hizi zimsaidie katika kumtumikia Allah na uma wake. Miongoni mwa haki hizi za kiongozi katika Uislamu ni kama zifuatavyo:-
KUSIKILIZWA NA KUTIIWA:
Miongoni mwa haki za kiongozi ambazo ni wajibu wa uma (raia) kumtekelezea kama mtumishi wao ni kumsikiliza na kumtii katika hali zote maadam hakuamrisha maasi. Haki hii anapewa na mwenyewe Allah, hebu na tuitegee siko Qur-ani Tukufu:
“ENYI MLIOAMINI! MTIINI ALLAH NA MTIINI MTUME NA WENYE MAMLAKA JUU YENU (viongozi) WALIO KATIKA NYIE (waislamu wenzenu)…” [4:59]
Hii ni nukuu ya Qur-ani inayowafaradhishia waumini kwanza kumtii Allah Mola Muumba wao na kadhalika kumtii Mtume wake. Na muislamu anapaswa kutambua kwamba kumtii Mtume ni kumtii Allah aliyemtuma kutuletea sheria hii:
“MWENYE KUMTII MTUME AMEMTII ALLAH (kwani anayoyaamrisha Mtume yametoka kwa Allah)…” [4:80]
Na suna ya Mtume ni sehemu ya sheria ya Allah (sheria mama), kazi yake ni kubainisha mujmali (ujumla) wa sheria mama.
Kwa mantiki hii suna ya Mtume inakuwa ni sheria shereheshi. Baada ya aya kuwaamrisha waumini kumtii Allah daraja la kwanza, kumtii Mtume wa Allah daraja la pili, ndipo ikawaamrisha kumtii kiongozi daraja la tatu.
Utaratibu huu wa twaa unaonyesha kuwa twaa ya kiongozi inaiandamia twaa ya Mtume ambayo nayo inaiandamia twaa ya Allah Mola Mwenyezi. Kwa utaratibu huu ni muhali kumtii Mtume bila ya kumtii kiongozi na hivyo hivyo ni muhali kumtii Allah bila ya kumtii Mtume wake.
Kadhalika utaratibu huu unafahamisha kuwa raia hawawajibiki kumtii kiongozi wao mpaka kwanza naye awe anamtii Allah na Mtume wake sambamba na kusimamisha sheria ya Allah. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema kuhusiana na haki hii ya kiongozi:
“Sikilizeni na kumtii hata kama atakutawalieni (mambo yenu) mtumwa wa kihabeshi mwenye kichwa mithili ya zabibu”. Bukhaariy. Akasema tena:
“Ni juu ya mtu muislamu kusikiza na kumtii (kiongozi) katika alipendalo na alichukialo maadam hakuamrishwa maasi. Ikiwa ataamrishwa maasi, basi (hapo) hakuna kusikiliza wala kutii”. Bukhaariy & Muslim.
Uislamu siku zote unapupia mshikamno na umoja wa uma na kuepusha njia za migongano na fitna.
Kwa kulizingatia na kulichunga hili, Uislamu umewatahadharisha na kuwaonya waislamu dhidi ya kujitoa katika twaa ya kiongozi na kumuasi.
Eti kwa sababu tu ya maasi na ufasiki unaotendwa na kiongozi huyo kama binadamu mwingine ye yote.
Si haki kumuasi muda wa kuwa hajatenda ukafiri wa waziwazi kabisa. Isieleweke kuwa Uislamu unamlea na kumlinda kiongozi fasiki, la hasha.
Uislamu unaangalia uzito na athari ya mambo mawili haya kwa jamii; uasi/ufasiki wa kiongozi na fitna/shari ya kumuasi kiongozi fasiki.
Uislamu ukaona kuwa fitna/athari ya ufasiki wa kiongozi kwa jamii si kubwa zaidi kuliko athari ya kumuasi kiongozi huyo.
Fitna hii ya kujitoa katika twaa ya kiongozi ni shari yenye kuendelea, kwani itaugawa uma katika matapo (makundi) mawili.
Tapo la kiongozi fasiki mwenye dola (nguvu) na tapo la hawa raia waliojitoa wasio na nguvu za kuwahami dhidi ya nguvu za dola watakazoshushiwa na kiongozi fasiki ili kuwarejesha katika twaa yake na kukomesha uasi wao kwake.
Katika hali hii ya mgawanyiko ni lazima patazuka vita ya wenyewe kwa wenyewe vitakavyozichukua muhanga roho za watu wengi wasio na hatia.
Kwa kulichelea hili ndio Uislamu ukautaka uma kusubiri na kustahamili juu ya ufasiki huu wa kiongozi wao huku ukiitumia haki yao ya kumuelekeza na kumnasihi kwa utaratibu wa kiislamu.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia:
“Atakayeung’oa mkono katika twaa (ya kiongozi), atakutana na Allah na ilhali hana hoja. Na atakayekufa na ilhali hana shingoni mwake kiapo cha utii (kwa kiongozi) atakufa mauti ya kijahilia”. Muslim. Akazidi kutuambia:
“Atakayelichukia kwa kiongozi wake jambo/tabia fulani, basi na asubiri. Kwani atakayejitoa katika twaa ya kiongozi kwa (kiasi cha) shubiri moja (tu), atakufa mauti ya kijahilia”. Bukhaariy & Muslim.
Mukhtasari wa kauli, hakumuhalalikii muislamu ye yote kumuasi kiongozi aliye muislamu mwenziwe kwa kisingizio cha uasi/ufasiki wa kiongozi huyo. Ni wajibu wake kuendelea kumtii pamoja na uasi wake huo maadam uasi huo haujafikia kiwango cha kufuru ya wazi isiyo na tafsiri nyingine ila kufru tu.
KUMSAIDIA NA KUSIMAMA NAE KATIKA JIHADI:
Ni wajibu wa raia (uma) kumuunga mkono na kumsaidia kiongozi wao katika kuwatumikia.
Na hii ni haki inayokwenda sambamba na haki ile ya twaa. Kila atakalolifaradhisha au kuliamrisha kiongozi ndani ya mipaka ya sheria kwa maslahi ya uma, dini ya Allah na kulinda heshima ya waislamu na dini yao.
Ni wajibu wa kila muislamu (raia) kuitekeleza amri hiyo ya kiongozi wake hata kama itagharimu uhai wake.
Hili linatokana na ukweli kwamba kiongozi kama binadamu hawezi kubeba dhima hii kuu ya kuutumikia uma mpaka raia wasimame upande wake na kumsaidia kwa mali na nafsi zao.
Kiongozi akitangaza jihadi dhidi ya maadui wa Uislamu, jihadi hii haitasimama ila kwa msaada na uungaji mkono wa raia.
Kama tulivyotangulia kueleza kuwa haki ya msaada na kusimama na kiongozi katika jihadi inaandamana na haki ya twaa. Kadhi Abuu Ya’alaa-Allah amrehemu-anasema:
“Imamu (kiongozi) atapotekeleza haki za uma (raia), zitamuwajibikia yeye juu yao (raia) haki mbili: (Haki ya) twaa na (haki ya) msaada (kuungwa mkono), muda wa kuwa halipatikani upande wake jambo litakalomtoa katika amana/uaminifu”.
TOSHA YA MAISHA YAKE:
Kiongozi wa kiislamu huutumia muda wake mwingi pengine hata ule wa mapumziko binafsi katika kuhakikisha kuwa anayatekeleza vema na ipasavyo majukumu yake kama mtumishi wa uma.
Huutumia muda wake huu kwa ajili ya maslahi na manufaa ya uma wake. Kwa kuuzingatia ukweli huu na kuuthamini mchango huu wa kiongozi, Uislamu unampa haki ya kuchukua tosha ya maisha yake katika mali ya waislamu.
Kiasi anachoruhusiwa kuchukua ni kile kinachoweza kukidhi mahitaji yake na familia yake kwa wema bila ya ubadhirifu.
Zama alipotawazwa Sayyidna Abuu bakri-Allah amuwiye radhi-kuwa Amirul-Muuminina kushika nafasi iliyoachwa wazi kwa kufariki kwa Bwana Mtume, maswahaba wa Mtume wakaambizana:
Mkadirieni khalifa wa Mtume kitakachomkwasia (kitakachomtoshelaza) Wakasema: Naam, nguo mbili atakapozichakaza atazivua na kuchukua nyingine mithili ya hizo.
Kipando (usafiri) anapotaka kusafiri na matumizi ya nyumbani kwake (outlay) kama alivyokuwa akitumia kabla ya kutawazwa khalifa. Abuu bakri akasema: Nimeridhia.
Yatizame haya katika “TWABAQAAT” ya Ibn Sa’ad juzuu ya tatu, sahifa 184 na 185.
Kadhalika amepokea Ibn Sa’ad kutoka kwa Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi-amesema: Alipotawazwa Abuu Bakri alisema: Kaumu yangu inatambua fika kwamba kazi yangu haikushindwa kuilisha familia yangu.
Na hivi sasa nimeshughulika na mambo ya waislamu na nitachuma katika mali yao na familia ya Abuu Bakri itakula kutokana na mali hiyo. (Twabaqaat).
Na wakati alipotawalia ukhalifa Sayyidna Umar Ibn Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-waliulizana baadhi ya maswahaba waliokuwa katika baraza ya Umar kuhusiana na kinachomuhalalikia katika mali ya Allah. Umar akawaambia:
Mimi nitakuelezeni kinachonihalalikia katika mali hiyo. Zinanihalalikia nguo mbili; nguo ya kiangazi (joto) na nguo ya kipindi cha baridi. Mnyama wa kuendea Hijjah na Umrah, chakula changu na familia yangu kama chakula cha mtu wa kawaida katika Makurayshi ambaye si tajiri wala fakiri wao. Kisha mimi nichukuliwe kama ye yote miongoni mwa waislamu, yananifika yanayowafika.
Riwaya hizi za tarekh na mithili ya hizi zinafahamisha kuwa kiongozi (Amirul-Muuminina) ana haki katika Baytul-Maali (khazina) ya waislamu.
Achukue/apewe katika mali hiyo kadri ya haja yake na familia yake ili asishughulike na kazi nyingine itakayomfanya ashindwe kutimiza majukumu kama kiongozi na mtumishi wa uma.