Tumetangulia kueleza katika masomo yaliyotangulia kwamba vikwazo vya makurayshi dhidi ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshuke – jamaa zake Baniy Haashim na Bariy Mutwalib waumini na wasio waumini viliendelea bila kusita kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu.
Katika kipindi hiki kigumu, Bwana Mtume na jamaa zake walipata dhiki na taabu kubwa zisizo kifani ambazo zilipelekea kuathirika vibaya kiafya, kijamii na kiuchumi.
Mwanachuoni Ibn Saad – Allah amrehemu katika kitabu chake. “Twabaqaati” anasema
“Kisha Mwenyezi Mungu akamfunulia Mtume wake suala la karatasi ya mkataba (wa vikwazo) kwamba mchwa amezila sehemu zote (zilizoandikwa) dhulma (dhidi ya Mtume na jamaa zake) na kilichobakia (katika karatasi ile) ni utajo wa mwenyezi Mungu Mtukufu peke yake.
Mtume akamwambia khabari hizo ami yake Mzee Abu Twaalibu, naye Abu Twalibu akawaambia nduguze (wakubwa wenzie).
Wakatoka wakaenda zao mpaka msikitini, Abu Twaalibu akawaambia makafiri wa Kikurayshi: Hakika mwana wa ndugu yangu ameniambia, na kamwe hajapata kuniongopea kwamba Mwenyezi Mwenyezi Mungu ameisalitisha karatasi yenu ya Mkataba (wa vikwazo) mdudu mchwa, amekula sehemu yote iliyoandikwa dhulma au kukata undugu na sehemu iliyobakia ni pale alipotajwa Mwenyezi Mwenyezi Mungu tu.
Basi ikiwa mwana wa ndugu yangu ni mkweli (katika haya aliyoyaeleza) basi acheni azimio lenu hili na ikiwa ni muongo basi nitakupeni mumuueni. (Makurayshi) wakasema : Hakika sasa umetufanyia uadilifu.
Wakamtuma mtu kwenda kuileta ile karatasi ya mkataba, wakaifungua. Tahamaki ikawa iko kama alivyoeleza Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie-.
Wakapigwa na butwaa na kuinamisha chini vichwa vyao wakijutia maafikiano yao na mzee Abu Twaalib.
Abu Twaalib akawaambia: Suala limekwishakuwa wazi, tunaendelea kuwekewa vikwazo kwa lipi? Kwisha kusema hivyo, akaingia yeye na wenzie baina ya mapazia (maguo) ya Al-kaaba na Al-kaaba yenyewe na kuomba dua, akisema:
“Ewe Mola wa haki tunusuru dhidi ya waliotufanyia dhulma na kuukata udugu wetu na wakayahalalisha yale ambayo ni haramu kwao kutufanyia!” Kisha wakarudi zao kambini.
Mandhari na hali hii yenye kutia uchungu iliziathiri nyonyo za baadhi ya makurayshi wenye murua na kuwapata dhiki kubwa ya moyo kuona ndugu na jamaa zao wanarejea tena kambini na vikwazo dhidi yao vinaendelezwa mpaka waangamie kutokana na njaa.
Ikawajia fikrani sura ya ndugu zao hawa wakiteseka na adhabu ya kunyimwa chakula na adhabu ya kutengwa na watoto wao wakilizana kwa njaa bila ya kupata msaada wowote kutoka kwa baba na mama zao.
Hapa sasa, wakaanza kutupiana lawama juu ya ukatili waliowafanyia ndugu zao wenyewe. Wakapanga njama za kulitengua azimio hili la mkataba wa vikwazo na kukomesha mara moja utengaji huu usiowafikiana na utu.
Mwanachuoni, muandishi wa kitabu kiitwacho
……. SERA YA MTUME NA ATHARI ZA KIMUHAMMAD -Allah amrehemu – anasema:
“Hapo ndipo lilipoenda kundi moja la makurayshi kuutengua mkataba ule, nao ni Hisham Ibn Amri, Zuhary Ibiy Umayyah, Mut-im Ibn Adiy, Abul-bakhtary Ibn Uishaam, na Zum-ah In Al-as-wad. Hishaam Ibn Amri alimuendea Zuhary Ibn Umayyah, akamwambia; Hivi unaridhia kula chakula ukashiba, ukavaa nguo na kuoa wanawake, na wajomba zako wakiwa katika hali unayoijua ? Akajibu: Ole wako ewe Hishaam’
Nitafanya nini, mimi ni mtu mmoja tu, Wallah lau ningelikuwa na mtu mwingine (wa kuniunga mkono) ningeenda kuutengua (mkataba huo)! (Hishaam) akamwambia; Basi mimi ni pamoja nawe, akaendelea kusema; tumtafute mtu wa tatu. Wakaenda pamoja mpaka kwa Mutw-im Ibn Adiy, wakamwambia;
Hivi umeridhia kabisa ziangamie koo mbili za watoto wa Abdi Manaaf (babu wa Makurayshi) na wewe ukishuhudia! Akajibu: Hakika mimi ni mtu mmoja peke yangu.
Wakamwambia: Sisi tuko pamoja nawe. Akamwambia: tumtafute mtu wa nne. Wakamuendea Abul-bakhatary, naye akasema: tumtafute mtu wa tano.
Wakamfuata Zum-ah Ibn Al-as-wad, naye akawafikia na nao katika shauri hilo. Wakafanya kikao usiku nje kidogo ya mji wa Makkah, wakakubaliana kwa kauli moja kulitengua azimio lile la vikwazo na kuwatoa Bany Haashim na Bany Mutwalib kambini walikotengwa (Baada ya maafikiano hayo) Zuhary akawaambia:
Mimi ndiye nitakayeanza na kuwa wa mwanzo wenu kuzungumza. Kulipopambazuka asubuhi, wakadamkia kwenye vilabu (baraza) vyao na Zuhary akafika akiwa amevaa mavazi rasmi, akatufu Al-kaaba, kisha akawageukia watu (wana baraza) na kuwaambia.
Enyi watu wa Makkah! Hivi sisi tunakula chakula na kuvaa nguo na il-hali Baniy Haashim na Baniy Mutwalib wakiangamia (kwa njaa), hawauzi wala kuuziwa? Wallah!
Sitakaa chini mpaka uchanwechanwe mkataba huu wenye dhulma utenganishao!! Abu Jahli akamwambia: Mwongo wee!! Wallah hautachanwa!
Hapo ndipo aliposema Zum-ah Ibn Al-as-wad: Wallah wewe ndio mwongo mkubwa, hatukuridhia kuandikwa kwa mkataba huu! Abul-bakhtary akasema: Amesema kweli Zum-ah, naye Mut-im Ibn Adiy (akawaunga mkono) akasema:
Nyie ndio mmesema kweli na ni muongo yule aliyesema kinyume cha hivyo, tunajitakasa mbele ya Mwenyezi Mungu kutokana na mkataba huu na yote yaliyoandikwa ndani yake ! Naye Hishaam Ibn Amri akaunga mkono na kusema kama walivyosema wenzake. Hapo ndipo aliposema Abu Jahli: Suala hili (walisemalo hawa) limepitishwa usiku (hawa wamekubaliana haya usiku).
Makurayshi wakatofautiana katika suala hili, hawa wakiunga mkono na wengine wakipinga. Hapo ndipo aloposimama Mutw-im Ibn Adiy, (kwa ujasiri mkubwa) akaiendea ile karatasi ya mkataba na kuchanachana vipande vipande.”
Huo ukawa ndio mwisho wa vikwazo hivi vilivyodumu kwa kipindi cha miaka mitatu na kuondolewa huku kwa vikwazo ilikuwa ni katika mwaka wa kumi wa utume kwa mujibu wa wanahistoria wa kiislamu.
FAIDA / NYONGEZA
Turejee nyuma kidogo, tuangaliea Hijrah ya ushabeshi ilileta athari gani kwa makurayshi. Hijrah hii ya uhabeshi kwa upande wa makurayshi haikuleta athari njema bali ilidhihirisha kushindwa kwao vibaya katika jaribio lao la kutaka kuudhibiti na hatimaye kuufuatilia mbali uislamu katika uso wa dunia.
Ama kwa upande wa waislamu hijra hii yote ilikuwa ni kheri na baraka. Tunasema hivi kwa sababu Hijrah hii ililieta kizaizai kikubwa katika katika mji wa Makkah na kuzitikisa fikra na nyoyo za Makurayshi na kuwaacha wamehemewa wakiwa hawajui la kufanya.
Makurayshi walihisi na kuamini kuwa wakimbizi hawa (waislamu) wataleta madhara makubwa kwao hapo baadaye.
Hii ni kwa sababu huko walikokimbilia na kupokelewa vizuri wataishi kwa amani na hivyo kuwa ni wajumbe wazuri wa kuigwa wa Uislamu.
Si ajabu wahabeshi wataathirika na mawaidha na mwenendo mzuri wa waislamu, na wakaamua kusilimu.
Hawa wakishasilimu, tayari waislamu watakuwa wamejijengea himaya na dola ugenini, jambo ambalo litawafanya waislamu kuwa na nguvu na hivyo kuwaza kujibu mashambulizi yamkurayshi dhidi yao.
Katika kukabiliana na kupambana, waislamu wanaweza kushinda na ushindi hautamaanisha kingine zaidi ya kuanguka utawala wa makurayshi katika nchi ya Hijaazi na kufa kwa dini yao ya ushirikina.
Wakimbizi/wahamiaji hawa wa uhabeshi pia walikuwa ni mabalozi wazuri wa uislamu katika nchi hii ya ughaibuni.
Kushikamana kwao na mafundisho ya uislamu ililileta taathira kubwa katika nafsi ya mflame Naajash.
Na matokeo ya taathira hii ni kusilimu kwa mfalme huyu na baadhi ya wafuasi wake ushahidi wa kusilimu mfalme huyu ni ile swala ya maiti ghaibu aliyomswalia Bwana Mtume baada ya kuletewa habari za kifo cha mfalme Najaash na malaika Jibril, ni wazi kuwa mtume hawezi kumswalia kafiri.
Kwa hivyo Hijrah hili ilikuwa ni sababu ya kuuingiza uislamu katika bara la Afrika baada ya Makkah kwa mantiki hii uislamu umeingia Afrika kabla ya kuingia madinah.