MAMBO YANAYOBATILISHA SWALA

Swala ni miongoni mwa ibada tukufu kabisa, kwa hivyo inamuwajibikia kila muislamu wakati wa kuitekeleza ibada hii, kujipamba na ikhlaaswi, unyenyekevu na utulivu mkubwa kabisa.

Na kuyaelekeza mawazo, akili na fikira zake zote humo ndani ya swala. Mafaqihi wametaja mambo mengi ambayo yakitokea ndani ya swala huibatilisha na kuifisidi, miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo:-

 

1.      KUZUNGUMZA KWA MAKUSUDI:                                                 

Maneno yanayokusudiwa hapa ni yale yasiyo Qur-ani, dhikri na dua za swala.

Imepokelewa kutoka kwa Zayd Ibn Arqam-Allah amuwiye radhi-amesema: Tulikuwa tukizungumza ndani ya swala, mmoja wetu akizungumza na mwenziwe katika haja yake mpaka iliposhuka aya hii:

“ANGALIENI SANA SWALA(zote kuziswali, khasa jamaa) NA (khasa) ILE SWALA YA KATI NA KATI. NA SIMAMENI KWA UNYENYEKEVU KATIKA KUMUABADU ALLAH”. [2:238] Bukhaariy & Muslim.

Imepokewa kutoka kwa Muaawiyah Ibn Hakam Assulamiy-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia- alipomshemua mpiga chafya ndani ya swala yake:

“ Hakika ya hii swala hakifalii ndani yake cho chote miongoni mwa maneno ya watu. Hakika si vinginevyo hiyo ni tasbihi, takbira na kisomo cha Qur-ani”. Muslim.

Na maneno yanayobatilisha swala ni yale yaliyotungika kuanzia na herufi mbili na kuendelea, hata kama hayana maana.

Au yakawa yanawakilishwa na herufi moja tu yenye maana, mithili ya neno ‘QI’ linalomaanisha ‘kinga’ na neno ‘i’ lenye maana ya ‘hifadhi/tunza’ na neno ‘fi’ ambalo maana yake ni ‘tekeleza’.

Ama ikiwa atazungumza kwa kujisahau kuwa yumo ndani ya swala au akawa hajui kuwa ni haramu kuzungumza ndani ya swala, kwa kuwa ndio kwanza ameingia uislamuni .

katika hali na mazingira haya atasamehewa maneno machache, na haya ni yale yasiyozidi maneno sita.

 

2.      MATENDO MENGI:

Muradi na mapendeleo ya matendo mengi ni yale yote yanayopingana na matendo ya swala kwa sharti yawe mengi na yafuatane.

Haya yanabatilisha swala kwa sababu ya kule kupingana kwake na nidhamu (utaratibu) ya swala. Na kipimo cha wingi ni haraka tatu na kuendelea na kipimo cha mfuatano ni matendo kwa mujibu wa ada/desturi.

Ama matendo machache mithili ya mtu kuweka vizuri kilemba chake, kupiga hatua moja mbele kwa ajili ya kuziba pengo (nafasi) lililo katika safu ya mbele. Au kukinyooshea mkono kitu haraka moja, haya yote hayabatilishi swala.

Kwa sababu ya riwaya sahihi iliyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kwamba “yeye alimnyanyua Umaamah na kumuweka chini na ilhali akiwa ndani ya swala akiwaswalisha watu”. Bukhaariy.

Umaamah ni mtoto wa kike wa Bibi Zaynabu Binti ya Mtume wa Allah.

 

3.      NGUO AU MWILI KUGUSANA/ KUKUTANA NA NAJISI:

Makusudio ya kugusana/kukutana na najisi ni hiyo nguo au mwili kupatwa na sehemu ya najisi, kisha mswaliji hasifanye haraka kuikung’uta pale pale.

Kwa sababu hiyo ni hadathi inayopingana na mojawapo ya sharti za swala ambayo ni twahara ya mwili na nguo kutokana na najisi.

Najisi ikimpata kwa kupeperushwa na upepo au mfano wake na akaweza kuiondosha haraka na ikawa ni kavu, swala yake haibatiliki.

 

4.      KUFUNUKA UTUPU (UCHI):

Umekwishajua mpaka wa uchi kwa mwanamke na mwanamume ndani ya swala katika masomo yaliyotangulia.

Sehemu yo yote ya utupu wa mswaliji ikifunuka kwa makusudi, swala yake itabatilika kwa hali yo yote ile.

Ama ukifunuka bila ya kukusudia na akafanya haraka kujisitiri, swala haitabatilika.

Na akitojisitiri pale pale utupu ulipomfunuka, swala yake itabatilika kwa sababu ya kukosekana mojawapo ya sharti za swala katika mojawapo ya sehemu za hiyo swala.

 

5.      KULA AU KUNYWA:

Kula au kunywa makusudi ndani ya swala kunabatilisha swala kwa sababu kunapingana na mfumo na utaratibu wa ibada hii.

Na kipimo cha chenye kubatilisha ni kiasi cho chote cha chakula au kinywaji hata kama ni kichache.

 

6.      KUZUKIWA NA HADATHI KABLA YA KUTOA SALAMU YA KWANZA:

Mtu akihuduthi kwa kutokwa na ushuzi mathalan, swala itabatilika bila ya kuangalia ni makusudi au ni kwa kujisahau (kushindwa kujizuia).

Swala itabatilika kwa sababu ya kukosekana mojawapo ya sharti za kusihi swala kabla ya kutimia kwake, nayo ni twahara ya hadathi.

Ama ikiwa mtu atahuduthi baada ya kutoa salamu ya kwanza na kabla ya kutoa ile ya pili, swala yake itakuwa sahihi na imetimia na hili ni kongamano la wanazuoni.

Hii ni kwa kuzingatia kwamba  mwanzo wa swala ni takbira ya kuhirimia na mwisho wake ni salamu ya kwanza ambayo ndiyo nguzo.

 

7.      KUJIKOHOZA, KUCHEKA,KULIA NA KUUGULIA (KUDIHA):

Yote haya yatabatilisha swala iwapo tu zitadhihiri herufi mbili kutokana na kuyatenda, hata kama hazifahamishi maana.

Hivi ni iwapo alifanya kwa makusudi, ama ikiwa ni kwa kushindwa kama vile kujiwa na kikohozi cha nguvu au kulipukwa na kicheko, swala haitabatilika.

Kadhalika swala itabatilika kwa kuleta dhikri au dua kwa kukusudia kumsemeza mtu kwa dua au dhikri hiyo. Kama vile mtu kusema ndani ya swala:

YARHAMUKAL-LAAHU-(Allah akurehemu), hii ni dhikri ambayo wakati huo itazingatiwa kuwa ni kuzungumza na mtu.

Na umekwishajua kwamba haifai kuzungumza ndani ya swala. Ama kutabasamu hakubatilishi swala.

 

8.      KUBADILI NIA:

Iwapo mswaliji ataazimia kutoka ndani ya swala au akakutungikia huko kutoka na jambo fulani kama vile ujaji wa mtu.

Akasema moyoni mwake fulani akija nami sijamaliza kuswali nitaikata swala yangu. Au simu ikilia nitakata swala na kwenda kuipokea.

Kwa kufanya hivi swala yake itabatilika pale pale atakapotia nia ya kuikata.

Kwa sababu swala haisihi ila kwa nia ya kutinda (ya moja kwa moja). Na azma au kusudi hili la kuikata swala kwa jambo fulani, linakinzana na nia ya kutinda.

 

9.      KUKIPA MGONGO QIBLAH/KUKENGEUKA NA QIBLAH:

Swala itabatilika iwapo mswaliji atakengeuka na Qiblah kwa kukipa mgongo, kwa sababu kuelekea Qiblah ni sharti ya msingi ya swala.

Swala itabatilika bila ya kujali kuwa alifanya hivyo kwa makusudi au alikengeushwa na mtu kwa nguvu. Angalia ikiwa atarudia kuelekea Qiblah haraka, swala yake haitakuwa ni batili.

 

10.  KULETA ZIADA YA MFANO WA SWALA KWA KUSAHAU:

Mswaliji akijisahau akaswali adhuhuri rakaa nane badala ya nne au akaswali magharibi rakaa sita badala ya tatu.

Swala yake itakuwa batili kwa sababu kusahau kwake kumevuka mpaka kiasi cha kuleta ziada ya mfano wa swala.

Na hii ni dalili ya wazi ya kutokuwemo kwake ndani ya swala kwa moyo, fikra, akili na mawazo yake yote (unyenyekevu).

 

11.  KUKUMBUKA KUTOKUSWALI SWALA YA KABLA YA SWALA HII YA SASA:

Ikiwa mswaliji ataingia kuswali Alasiri na akakumbuka ndani ya swala hiyo ya Alasiri kwamba hajaswali swala ya Adhuhuri.

Swala ya Alasiri itabatilika pale pale mpaka kwanza aswali adhuhuri, kwa sababu utaratibu baina ya swala tano ni FARDHI.

Kwa kule kupokewa kwake  kutoka kwa Bwana Mtume kwa mtungo na utaratibu maalum wa fardhi baada ya fardhi. Kwa mantiki hii, swala haisihi kabla ya kuswali ile ya kabla yake.

 

12.  KUACHA MOJAWAPO YA NGUZO ZA SWALA:

Mswaliji akiacha nguzo mojawapo miongoni mwa nguzo za swala kama vile kuacha rukuu. Kisha hasiidiriki kwa kuileta ndani ya swala, swala yake itakuwa ni batili.

Ubatili huu unatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alipomwambia yule mkosaji wa swala yake.

Wakati alipoacha kutulizana na itidali ambazo hizo ni nguzo mbili: “Rejea ukaswali tena kwani hakika wewe bado hujaswali”. Muslim.

 

13.  KUMTANGULIA IMAMU:

Iwapo maamuma atamtangulia imamu wake kwa makusudi, kama vile akarukuu kabla ya imamu hajarukuu. Au akasujudu kabla ya kusujudu imamu wake, katika hali hii swala yake itabatilika. Ubatili huu unatokana na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika si vinginevyo, imamu amewekwa ili afuatwe”. Bukhaariy & Muslim.

MAMBO YANAYOBATILISHA SWALA

Swala ni miongoni mwa ibada tukufu kabisa, kwa hivyo inamuwajibikia kila muislamu wakati wa kuitekeleza ibada hii, kujipamba na ikhlaaswi, unyenyekevu na utulivu mkubwa kabisa.

Na kuyaelekeza mawazo, akili na fikira zake zote humo ndani ya swala. Mafaqihi wametaja mambo mengi ambayo yakitokea ndani ya swala huibatilisha na kuifisidi, miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo:-

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *