HASADI

Ikutoshe kuona na kutambua ubaya wa hasadi kwamba Allah alimuarisha Mtume wake Rehema na Amani zimshukie kujilinda na kujikinga na shari ya mtu hasidi sambamba na shari ya shetani.

“NA SHARI YA HASIDI ANAPOHUSUDU” (113:5).

Maana ya hasadi ni mtu kuwa na dhiki, uzito na chuki moyoni mwake kwa sababu ya neema yua Allah aliyomneemesha mja wake katika dini au ulimwengu wake.

Muislamu hamuhusudi mtu na hasadi si sifa wala tabia yake.

Hili linatokana na tabia yake ya kuwapendea kheri watu wote na kuwatanguliza kuliko nafsiyake, yeye mwenyewe.

Kwa mantiki hii basi, muislamu anaichukia hasadi, kwa sababu hasadi ni kupinga na kuingilia kati mgawanyo wa neema na fadhila za Allah baina ya waja wake.

Hasidi huungua moyoni mwake kwa kujiuliza, kwanini apate yeye, kwa nini nisipate mimi yeye akakosa.

Eeh mtu mbaya hasidi, huko ni kujipa kazi isiyo yake ugawaji wa neema katika milki yake Allah. Tusome na tuwaidhike “ (basi Allah anasema).

JE, WAO NDIO WANAIGAWA REHEMA YA MOLA WAKO (wakampa wampendaye wao na wakamnyima wamtakaye?) SISI TUMEWAGAWANYIA MAISHA YAO KATIKA UHAI WA DUNIA NA TUMEWAINUA BAADHI YAO DARAJA KUBWA JUU YA WENGINE, KWA HIVYO BAADHI YAO WANAWAFANYA WENGINE KUWA WATUMISHI WAO……………….”. (43: 32).

Hasidi hana fungu/sehemu katika miliki na ufalme wa Allah, sasa hadhi ya kugawa nema za Allah anaipata wapi? Allah anawauliza mahasidi:

“AU WANAYO SEHEMU YA UFALME (wa Allah, basi wanahamaki kwa nini kupewa mtu kitu pasina amri yao? ). BASI HAPO WASINGALIWAPA WATU HATA TUNDU YA KOKWA YA TENDE. AU WANAWAFANYA WATU HUSUDA KWA YALE ALIYOWAPA ALLAH KWA UKARIMU WAKE?……………” (4: 53-54)

Hasadi kama tabia mbaya inayochukiwa na kupigwa vita na Uislamu inagawanyika katika matapo (makundi) mawili yafuatayo:-

i.       Mtu kutamani neema aliyokuwa nayo mwenziwe kama mali, elimu, cheo au madaraka imuondokee na aipate yeye.

ii.     Kutamani kuondoka kwa neema aliyoneemeshwa mja na Mola wake hata kama hakuipata yeye.

Hasidi yuko tayari kutoa mali, muda na kila kilicho chake ili kuhakikisha kuwa lengo lake hilo linafanikiwa hata ikibidi kwa kutoa uhai wa mtu Rejea kisa cha watoto wa Nabii Adamu, Haabil na Qaabil ni ushahidi mzuri wa hili (5: 27-30) hapo tena ndipo hupumzika, akafurahi na kuona raha.

Hasadi ni maasi kama maasi mengine, ni dhambi kama dhambi nyingine, na ni haramu. Si halali kwa yeyote kumuhusudu yeyote kwa lolote.

Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie anatuasa akisema:

“Msibughudhiane, wala msihusudiane, wala msifanyiane uadui na wala msikatane  na kuweni ndugu enyi waja wa Allah. Si halali kwa Muislamu kumuhajiri nduguye zaidi ya siku tatu Bukhaariy na Muslim.

Mtume wa Allah anazidi kutuasa na kutuonya juu ya tabia hii mbaya ya hasadi, tumsikilize

“Jiepusheni/tahadharini na hasadi, kwani hasadi hula mema (ya mja) kama moto ulavyo kuni au majani:” Abuu Daawoud.

Muislamu akipitiwa/akijiwa na mawazo ya hasadi kutokana na ubinadamu wake na kutokuwa kwake na kinga dhidi ya madhambi hupambana nayo.

Akijikuta anamfanyia hasadi mtu yeyote, basi ni juuyake aichukie na aifiche moyoni mwake, asiidhihirishe kupitia kauli au matendo yake.

Atenda matendo yatakayokwenda kinyume na hasadi iliyomo moyoni mwake, amsifie na kumtaja kwa wema mtu anaymuhusudi, ajishughulishe na kumtukuza na kumsaidia.

Na akiona lolote au chochote kinachompelekea kufanya hasadi aseme:

MA SHAA-ALLAH, LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAH

Hii ndiyo dawa pekee inayofaa kuitibu na kuiondosha  hasadi au kuidhoofisha, kwani kwa kufanya hivyo hasadi haitamuathiri na atasalimika nayo. imepokewa:

“Utendaji wema huepusha mianguko miovu/mibaya” Al-baihaqiy. 

Si hasadi kufanya  “ghibtwah”’ ambalo ni kutamani kupata neema mithili ya neema aliyoneemeshwa nayo mtu mwingine bila ya kutamani imuondokee na uipate wewe.

Tena ikiwa ni  neema inayofungamana na dini kama vile elimu na ibada, basi kutamani huko kuwa katika daraja yenye kusifiwa.

Ama ikiwa ni neema ianyofungamana na dunia kama mali na cheo, kutamani huku huwa katika daraja ya jaizi na mubaaha. “Ghibtwah” inahalalishwa kupitia kauli yua Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie :

”Hapana (si halili kufanya) hasadi ila katika mambo mawili. Mtu aliyepewa mali na Allah na akampa mamlaka/nguvu ya kuitumia (mali hiyo) katika haki. Na mtu aliyepewa hekima na Allah naye akawa anatoa hukumu kwa kuitumia (hekima hiyo) na akaifundisha (kwa wenzake):” Bukhaariy.

\Hekima iliyokusudiwa hapa katika hadithi ni Qur-ani tukufu na suna ya Mtume (hadithi) tunasihike na tuwaidhike na ushauri nasaha huu alioutoa Imamu mmoja kwa kiongozi wa wakati wake, alimwambia.

·        “ Jiepushe na kibri kwani hiyo ndiyo dhambi awali aliyoasiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kisha akasoma: “NA (wakumbushe watu khabari hii) TULIPOWAAMBIA MALAIKA MSUJUDIENI ADAM (yaani mwadhimisheni kwa ile ilimu yake aliyopewa) WAKAMSUJUDIA WOTE ISIPOKUWA IBLISI, AKAKATAA NA AKAJIVUNA…………….” (2: 34)

·        Jiepushe na pupa kwani hiyo ndiyo iliyomtoa Adamu katika pepo aliyomuweka Mwenyezi Mungu, na akamwambia kula humo ila mti mmoja akamkataza. Kutokana na pupa yake akaula (mti ule) ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamtoa peponi.

Kisha akasoma (Allah) AKASEMA ONDOKENI HUMU NYOTE HALI YA KUWA NI MAADUI NYINYI KWA NYINYI (vizazi vyenu vitakuwa maadui wenyewe kwa wenyewe) NA UKIKUFIKIENI KUTOKA KWANGU UWONGOFU, BASI ATAKAYEUFUATA UWONGOFU WANGU HUO HATAPOTEA WALA HATATAABIKA” (20: 123)

·        Na jiepushe na hasadi kwani hiyo ndiyo iliyompelekea mwana wa Adamu kumua nduguye alipomuhusudi, kisha akasoma,

NA WASOMEE KHABARI ZA WATOTO WAWILI WA ADAMU KWA KWELI. WALIPOTOA SADAKA, IKAKUBALIWA YA MMOJA WAO NA YA MWINGINE HAIKUKUBALIWA. AKASEMA, (yule isiyokubaliwa sadaka yake) NITAKUUA, AKASEMA (yule aliyehadidiwa kuuawa) ALLAH HUWAPOKELEA WAMCHAO TU……………BASI NAFSI YAKE IKAMUWEZESHA KUMUUA NDUGUYE AKAMUUA NA AKAWA MIONGONI MWA WENYE KUKHASIRIKA” (5: 27-30)

Inasemekana sababu ya kumuua nduguye ni kwamba mke wa haabil aliyeuwawa alikuwa mzuri kuliko mke wa Qaabil muuaji. Akamfanyia hasadi nduguye na kamuua ili pate kumchukua mkewe aliye mzuri.

 

HASADI

Ikutoshe kuona na kutambua ubaya wa hasadi kwamba Allah alimuarisha Mtume wake Rehema na Amani zimshukie kujilinda na kujikinga na shari ya mtu hasidi sambamba na shari ya shetani.

“NA SHARI YA HASIDI ANAPOHUSUDU” (113:5).

Maana ya hasadi ni mtu kuwa na dhiki, uzito na chuki moyoni mwake kwa sababu ya neema yua Allah aliyomneemesha mja wake katika dini au ulimwengu wake.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *