HAKI ZA MAKHADIMU(WATUMISHI WA NYUMBANI), VIBARUA NA WAAJIRIWA

Huduma/utumishi ni suala lisilopuuzwa wala kudharauliwa katika mfumo sahihi wa maisha (Uislamu).

Umuhimu wa suala hili unatokana na ukweli kwamba maisha ya watu katika jamii yo yote ile ni maisha ya kutegemeana na kushirikiana.

Ni ukweli usiohitaji ubishi kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kujitegemea mwenyewe kwa kila hali.

Kwa mantiki hii maisha ya mwanadamu ni maisha ya nihudumie nikuhudumie ili tusonge mbele kimaisha.

Huduma na utumishi unaotolewa katika jamii unatofautiana baina ya mtu na mtu. Tofauti hii inatokana na uwezo, ujuzi na vipawa vya watu kwani kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Kila mmoja amewepesishiwa aliloumbiwa kwa ajili yake”. Ahmad, Bukhaariy, Muslim & Abuu Daawoud.

Katika anga la udugu wa kiislamu, ndugu hawa wa imani wote husaidiana katika misingi ya wema na taqwa (ucha-Mungu).

Hii ni katika jumla ya kuitekeleza amri ya Mola wao:

“…NA SAIDIANENI KATIKA WEMA NA TAQWA…” [5:2] Na kigezo na kipimo cha ubora wa mtu katika Uislamu hakitokani na elimu, cheo, mali au kazi aifanyao.

Bali msingi wa ubora umo katika tamko tukufu la Allah:

“ENYI WATU! KWA HAKIKA TUMEKUUMBENI (nyote) KWA (yule) MWANAMUME (mmoja; Adamu) NA (yule yule) MWANAMKE (mmoja; Hawwa). NA TUMEKUFANYENI MATAIFA NA MAKABILA (mbalimbali) ILI MJUANE (tu basi, siyo mkejeliane). HAKIKA AHISHIMIWAYE SANA MIONGONI MWENU (mbora) MBELE YA ALLAH NI YULE AMCHAYE ALLAH ZAIDI KATIKA NYINYI. KWA YAKINI ALLAH NI MJUZI, MWENYE KHABARI (za mambo yote)”. [49:113]

Taqwa (ucha-Mungu) kama ijielezavyo aya ndio kigezo pekee cha ubora wa mtu katika Uislamu.

 Kwa yakini Uislamu umelihimiza sana suala la mtu kufanya kazi na kula kutokana na jasho lake.

Uislamu unawataka waumini wake kujifunza kazi/ufundi mbalimbali utakaowawezesha kujitafutia riziki zao kwa njia za halali.

Kwani kufanya kazi ndio njia pekee ya kuistawisha na kuijenga dunia yetu hii. Uislamu umetangaza kwamba chakula chema na kizuri anachokila mtu kwa raha na furaha ni kile anachokipata baada ya taabu na uchovu mkubwa unaotokana na harakati za kukitafuta.

Mwanadamu huonja katika chakula hicho shida/taabu ya kazi yake na starehe ya matunda yake. Kuhusiana na hili Mtukufu Mtume wetu-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia:

“Kamwe hajapatapo ye yote kula chakula kilicho bora kuliko kula kutokana na kazi ya mikono yake. Na kwa yakini nabii wa Allah; Daawoud alikuwa akila kutokana na kazi ya mikono yake”. Bukhaariy

Mja anapojitahidi kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta maisha na riziki/chakula chake binafsi na cha familia yake.

Na kwa ajili ya kujizuia na vilivyomo mikononi mwa watu, mtu huyu afahamu kwamba ana ujira adhimu mbele ya Allah kutokana na amali yake hiyo. Imepokelewa kwamba:

“Mtu mmoja alimpitia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-maswahaba wa Mtume wakaiona juhudi na bidii yake ya utendaji kazi. Wakasema: Ewe Mtume wa Allah, (waonaje) lau (juhudi na bidii) hii ingelikuwa (ingelitumika) katika njia (ya kuipigania dini) ya Allah? Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:-

Ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya riziki ya) wanawe wadogo (ambao hawajaweza kujitegemea), basi yeye yuko katika njia ya Allah.

Na ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya chakula cha) wazazi wake wawili walio watu wazima wakongwe, basi huyo yuko katika njia ya Allah.

Na akiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili (ya riziki ya) nafsi yake ili aizuie na kuomba, basi huyo yuko katika njia ya Allah.

Na ikiwa ametoka akifanya juhudi kwa ajili ya kujionyesha na kujifakharisha (mbele za watu kuwa yeye ni mfanyakazi bora), basi huyo yuko katika njia ya shetani”. Twabaraaniy

Kadhalika imepokewa kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwamba yeye amesema: “Hakika Allah anampenda muumini mwenye ustadi/ujuzi wa kazi”. Al-Baihaqiy

Pamoja na Uislamu kuwahimiza waumini wake kufanya kazi, kadhalika haukulisahau suala la haki za msingi za watumishi, vibarua sambamba na waajiriwa.

Uislamu umeweka katika misingi ya sheria yake haki zinazolinda maslahi, hadhi na heshima ya watumishi, vibarua na waajiriwa. Katika jumla ya haki ambazo Uislamu umeziweka ni kama zifuatavyo:-

HAKI YA UDUGU WA KIISLAMU NA KUSHIRIKIANA KATIKA CHAKULA NA MAVAZI:

Uislamu unasema muislamu ni ndugu ya muislamu na mafungamano ya udugu huu wa kiislamu ni mafungamano ya imani/itikadi.

Imani ambayo inawajumuisha na kuwakusanya pamoja watumishi na watumikiwa, waajiri na waajiriwa na wafanyakazi na wafanyiwa kazi (mabwana).

Uhusiano na mafungamano ya wawili hawa ni huu udugu wa kiimani.

Kwa mantiki hii, ni wajibu chakula na mavazi ya ndugu hawa yawe mamoja kwa njia ya kusaidiana na si kwa njia ya usawa wa moja kwa moja (wa kila kitu).

Wale chakula cha aina moja hata kama hawakukaa pamoja wakati wa kula, haya ndiyo mafundisho sahihi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Watumishi wenu ni ndugu zenu (katika imani), Allah amewaweka chini ya mamlaka yenu. Basi ye yote ambaye nduguye (huyo) atakuwa chini ya mamlaka yake na amlishe anachokula yeye na amvishe anachokivaa yeye”. Bukhaariy & Muslim.

HAKI YA UJIRA (MSHAHARA):

Ujira/malipo ya kazi au utumishi, hii ni haki iliyowajibishwa na Uislamu.

Hili linatokana na ukweli kwamba kila amali (kazi) ina ujira wake bila ya kuzingatia uzuri au ubaya wa amali hiyo.

Kigezo na kipimo cha ujira wa amali katika Uislamu ni msingi usemao: (Jazaa/malipo ni kwa kadri ya amali iliyotendwa).

Yaani ujira uzingatie ukubwa, uzito, hatari, mazingira na muda uliotumika katika kuitenda kazi husika.

Mtumishi/muajiriwa/kibarua atapoitekeleza kazi yake kama walivyokubaliana na kuelekezwa na muajiri wake.

Tayari amestahiki kulipwa ujira wa kazi hiyo kwa ukamilifu, uadilifu na kwa mujibu wa makubaliano na maagano yao kabla ya kuanza kwa kazi.

Kuhusiana na haki hii ya ujira Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anatuambia:

 “Mpeni muajiriwa ujira wake kabla jasho halijakauka”. Ibn Maajah

Yaani apewe ujira wake bila ya kucheleweshewa au kusumbuliwa kwa kuambiwa njoo kesho, kesho akija anaambiwa tena njoo kesho, basi ilimradi kesho hiyo haitofika kamwe.

Huu si Uislamu na muislamu wa kweli anayemtii Allah, Mtume wake na siku ya mwisho hathubutu katu kuyafanya hayo. Vipi atathubutu kuyafanya na ilhali anaikiri, anaiamini na kuikubali kauli ya Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie:

“Mbea tatu za watu, mimi ni khasimu wao siku ya kiyama”….akataja miongoni mwao….

“Mtu aliyemuajiri muajiriwa akamtekelezea kazi yake (kwa ukamilifu), naye asimpe ujira wake”. Ahmad & Ibn Maajah

Na hoja si tu kulipa ujira, bali je huo ndio ujira mliokubaliana au baada ya kufanyiwa kazi unaamua kumlipa kinyume na makubaliano yenu.

Na je, ujira huo unalingana na kazi aliyoifanya?

Kama wewe ndio ungekuwa katika nafasi yake-yaani muajiriwa na yeye ndio muajiri wako, ungeridhika na ujira huo unaompa yeye?!

Ni vema ndugu muislamu ukajiuliza kwanza maswali haya kabla hujaamua kutoa ujira unaotaka kuutoa.

 

3. HAKI YA KUFANYA KAZI KULINGANA NA UWEZO:

Katika jumla ya haki za mtumishi/mfanyakazi ni kuwa kazi anayopewa ilingane na uwezo wake. Kwa maneno mengine mtumishi asikalifishwe kufanya kazi asiyo na uwezo nayo. Hii ni kwa sababu:

“ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE…”. [2:286]

Ikiwa Allah Mola Muumba na Bwana Mlezi mwenye kustahiki kutumikiwa na kuabudiwa na kila kiumbe ukiwemo wewe muajiri, haikalifishi nafsi ila yaliyo katika uweza wake.

Ni dhahiri basi, kwamba hakuna mwenye haki ya kumkalifisha mtumishi/muajiriwa kufanya kazi nzito na ngumu asiyoimudu.

Au kumkalifisha mtu mmoja kufanya kazi inayohitaji nguvukazi ya zaidi ya mtu mmoja hata kama anamlipa.

Huu si Uislamu na wala si ubinadamu kamwe, ni lazima kazi husika iende sambamba na nguvukazi inayohitajika katika kuitekeleza kazi hiyo.

Hivi ndivyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anavyoielezea haki hii:

“…Na wala msiwakalifishe (kufanya kazi) wasiyoiweza na iwapo mtawakalifisha basi wasaidieni”.Bukhaariy & Muslim 

Katika kusaidia utekelezaji wa haki hii ni lazima uwepo muda maalumu wa kuanza na kumaliza kazi. Muda huu ni wajibu uheshimiwe na pande zote mbili; mtumishi na mtumikiwa (muajiri) ili kuwepo na ufanisi katika utendaji mzima wa kazi.

 

4. DHAMANA YA MAHITAJI MUHIMU NA HIMAYA DHIDI YA MAJANGA YA KIMAUMBILE:

Uislamu unampa mfanyakazi/mtumishi haki ya dhamana ya mahitaji yake muhimu kiasi ya tosha ya maisha yake.

Hivi ndivyo inavyofahamisha kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

 “Atakayetawalishwa (atakayetawazwa) kwetu sisi (kufanya) kazi fulani (kwa maslahi ya uma wa kiislamu) na (akawa) hana nyumba, basi na ajifanyie nyumba (kutokana na mali ya waislamu). Au (akawa) hana mnyama (kipando/gari), basi na ajitwalie mnyama (kwa mali hiyo)”. Bukhaariy & wengineo

Kauli hii ya Bwana Mtume kwa lugha ya leo inamaanisha dhamana (guarantee) ya maisha bora kulingana na zama anazoishi mtumishi huyo wa uma. Dhamana hii inahusisha:-

v     maskani (nyumba) bora na salama ya kuishi,

v     mke wa kumliwaza baada ya machovu yatokanayo na utumishi wa uma,

v     usafiri utakaomuwezesha kwenda katika utumishi wa uma na kurudi nyumbani.

 

Ijapokuwa hadithi hii imepokelewa katika kutaja na kubainisha haki za watumishi wa dola/serikali ya kiislamu.

Kwa yakini sababu iliyompelekea mtumishi huyu wa dola kuyapata haya, ambayo ni kumuhakikishia na kumdhaminia tosha ya maisha yake ili aweze kuifanya kazi aliyopewa kwa amani, utulivu na ufanisi.

Hapana shaka kwamba sababu hii inapelekea kuenea kwa hukumu kwa wafanyakazi na watumishi wengine.

Sherehe (ufafanuzi) hii ya kauli ya Mtume haikusudii kusema kwamba kila muajiri analazimika kumpa muajiriwa wake mahitaji yake yote ya lazima zaidi kuliko ujira anaoustahiki.

Bali maana yake ni kwamba dola ina wajibu wa kumtimizia mwananchi/raia wake huyu kile asichoweza kukipata kutokana na kazi aifanyayo.

Baadhi ya nchi za Kiarabu na baadhi ya madola ya kimagharibi yamejaribu kwa kiwango kikubwa kulitekeleza zoezi hili ambalo ni sehemu ya mfumo sahihi wa maisha (Uislamu).

Katika kulitekeleza zoezi hili nchi hizi zimefikia hatua ya kumlipa mtoto mchanga aliyezaliwa, bila ya kumsahau mzee kikongwe asiyejiweza.

Huu ndio Uislamu, mfumo wa maisha waliochaguliwa wanadamu na Mola Muumba wao:

“…NA NIMEKUPENDELEENI (nimekuridhieni) UISLAMU UWE NI DINI YENU…” [5:3]

Dola ya kiislamu imdhaminie mwanadola haki ya tosha ya maisha yake na himaya ya familia yake kutokana na maradhi, uzee au kifo. Hivi ndivyo ilivyokuja katika hadithi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

“Atakayeacha mali (baada ya kufa), basi mali hiyo ni (haki) ya warithi wake. Na atakayeacha watoto walio dhaifu (hawana mali), basi na wanijie kwani mimi ndio mlinzi/msimamizi wao”. Bukhaariy

Katika hadithi hii, Bwana Mtume anawapa yatima walioachwa bila ya mali haki ya kupata mali ya dola, kwa kiasi kitakachowahakikishia kupata mahitaji yao ya msingi.

 

5. HAKI YA KUTENDEWA VEMA (KIBINADAMU):

Tabia na umbile la Uislamu ni umbile la sawa linalowaweka watu wote katika daraja moja la usawa.

Mkubwa na mdogo, tajiri na masikini, mtumishi na mtumikiwa wote hawa ni sawa mbele ya macho ya Uislamu.

Dhana hii ya usawa katika Uislamu haikinzani na ukweli wa utukufu na ubora waliopewa baadhi ya watu na Allah kwa hekima na busara azijuazo yeye mwenyewe.

Haikanushi kuwaweka watu kulingana na daraja zao mbele ya Allah na mbele ya jamii.

Kwa tabia na umbile hili la Uislamu ndio Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alivyoishi na watumishi wake.

Tukimchulia Sayyidina Anas-Allah amuwiye radhi-kama kigezo chetu, Bwana Mtume hakupata kumkaripia, wala kumtolea maneno yenye kuumiza hisia zake au kumvunjia heshima.

Huyu hapa Anas mwenyewe anaelezea namna ulivyokuwa utumishi wake kwa Mtume wa Allah:

 “Nilimtumikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa kipindi cha miaka kumi. Basi (katika kipindi chote hicho) hakupata kuniambia japo ‘ah!’ au ‘kwa nini umefanya?’ au ‘kwa nini hukufanya’. Muslim

Chini ya kivuli cha hali hii ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuelekea watumishi wake. Tunagundua kosa baya kabisa linalotendwa na wengi wetu leo.

Ni ukweli uonekanao kwamba matajiri au waajiri walio wengi leo hawawatendei vema watumishi/waajiriwa wao, hili li bayana mbele ya macho ya kila mmoja wetu.

Watumishi leo wanadharauliwa, wananyanyaswa, wanapuuzwa, wanapunjwa na kudhulumiwa haki zao na pengine hupigwa. Haya yanapingana na misingi ya sheria ya Uislamu.

Katika hadithi iliyopokelewa na swahaba Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:

“Inatosha (kabisa) shari mtu kumdharau nduguye muislamu”. Muslim

Imepokelewa kutoka kwa Ibn Masoud-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Nilikuwa nikimpiga bakora mtumwa wangu, nikasikia sauti nyuma yangu (ikisema): Tambua ewe Ibn Masoud. Sikuweza kuitambua sauti ile kutokana na ghadhabu (niliyokuwa nayo). Alipokurubia (mwenye sauti) tahamaki ni Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-naye akiniambia: “Tambua kwamba ewe Ibn Masoud Allah ana uwezo zaidi juu yako kuliko uwezo ulio nao wewe juu ya mtumwa huyu”. Nikasema sitampiga tena mtumwa ye yote baada ya leo.

Katika riwaya nyingine:

“Bakora ile ilinianguka mkononi kutoka na khofu ya (maneno yale ya) Mtume”. Na katika riwaya nyingine: “Nikasema: Ewe Mtume wa Allah, nimemuacha huru kwa ajili ya Allah. Mtume akasema: “Ama lau usingelifanya hivyo, ungeliunguzwa na moto (wa Allah)”. Muslim

 

HAKI ZA MAKHADIMU(WATUMISHI WA NYUMBANI), VIBARUA NA WAAJIRIWA

Huduma/utumishi ni suala lisilopuuzwa wala kudharauliwa katika mfumo sahihi wa maisha (Uislamu).

Umuhimu wa suala hili unatokana na ukweli kwamba maisha ya watu katika jamii yo yote ile ni maisha ya kutegemeana na kushirikiana.

Ni ukweli usiohitaji ubishi kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kujitegemea mwenyewe kwa kila hali.

Kwa mantiki hii maisha ya mwanadamu ni maisha ya nihudumie nikuhudumie ili tusonge mbele kimaisha.

Huduma na utumishi unaotolewa katika jamii unatofautiana baina ya mtu na mtu. Tofauti hii inatokana na uwezo, ujuzi na vipawa vya watu kwani kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *