BWANA MTUME AAMURU KUUAWA KWA MATEKA WAWILI

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie akaondoka pale Rauhaa alipolakiwa na maswahaba wake kuendelea na safari yake ya Madinah.

Alipofika mahala panapoitwa “Al–Uthayl” akawakagua mateka na akaamuru kuuliwa wawili miongoni mwao ambao ni An–nadhwru Ibn Al–Haarith na Uqbah Ibn Abiy Muaitw.

Hawa walikuwa ni miongoni mwa mashetani wa Makuraishi waliokuwa na maudhi makubwa kwa Mtume na maswahaba kuliko wengine.

Hawa walikuwa wakikizulia kitabu cha Allah na Mtume wake. Mtume wa Allah wakati akiwakagua mateka wale alimtupia An–nadhwru Ibn Al–Haarith jicho lililoupapatisha moyo wake mateka yule An-nadhwru akamwambia mateka aliye pembeni mwake:

“Wallah, Muhammad ataniua kwani amenitazama kwa macho yanayoashiria mauti”. Mwenziwe akamwambia

“Wallah, hiyo ni khofu yako tu, hatafanya hivyo. An–nadhwru akaanza kutafuta mtu atakayemuombea kwa Mtume asiuawe, akamuendea swahaba Musw’ab Ibn Umeir–Allah amuwiye radhi. Musw’ab ndiye muislamu aliyekuwa ndugu yake wa nasabu mwenye nasabu ya karibu nae kuliko waislamu wengine Akamwambia:

 “Hebu zungumza na mtu wako huyu (Mtume) anijaalie kama ye yote miongoni mwa Makuraishi. Kwani yeye, Wallah ataniua tu kama hukuzungumza nae. Musw’ab akamwambia:

“Hakika wewe ulikuwa ukisema katika kitabu cha Allah na Mtume wake kadha wa kadha na ulikuwa ukiwaadhibu maswahaba wake”. An-nadhwru–akasema:

“Lau Makuraishi wangelikuteka wewe, kamwe wasingelikuua maadam mimi ni hai”.

Musw’ab akamjibu: “Wallah, hakika mimi sikuoni wewe kuwa ni mkweli, isitoshe mimi si kama wewe (si kafiri) na Uislamu umekwishakata ahadi na makafiri”.

 Huyu An–nadhwru alikuwa ni mateka wa Al–Miqdaad Ibn Amrou–Allah amuwiye radhi, swahaba huyu aliposikia mazungumzo yanayojiri juu ya kuuliwa mateka wake akapiga ukelele akisema : An–nadhwru ni mateka wangu”.

Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akamwambia:

“Ipige upanga shingo yake. Ewe Mola wa haki wee! Mtajirishe Al– Miqdaad kwa fadhila zako”. Akauawa An–nadhwru kwa pigo la upanga wa Al–Miqdaad.

Ama Uqbah Ibn Abiy Muaitw, Mtume aliamuru auliwe walipofika mahala paitwapo ‘Arqid–dhwabyah, Uqbah akapiga mayowe kwa kupapatika:

“Nani atawaangalia wanangu ewe Muhammad (nikiuwawa)?

“Mtume akamjibu: “Moto”.

Imepokelewa kutoka kwa Sha’abiy kwamba Mtume alipoamuru kuuliwa kwa Uqbah, alisema Uqbah:

“Hivi unaniua mimi miongoni mwa makurayshi hawa (yaani katika wote hawa hukumuona wa kumuua ila mimi tu)?” Mtume akamjibu:

“Naam, je, mnajua huyu alinifanyia nini mimi? Huyu siku moja alinikuta nimesujudu, akanikanyaga shingoni na kusigina (kukandamiza) hakuuondoa mguu wake mpaka nikadhani kwamba macho yangu yatatoka kutokana na mkandamizo ule wa nguvu Mara nyingine tena akaja na matumbo ya mbuzi akanitupia kichwani nami nikiwa nimesujudu.

Akaja Fatmah binti yangu akayaondosha. Kisha kusema hivyo akaamuru auliwe, akauawa. Baada ya kuuawa, huyoo Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akashika njia kuendelea na safari yake ya Madinah .

Akaingia mjini Madinah kabla ya mateka wale kwa siku moja akitokea upande wa njia ya Thaniyah. Hiyo ilikuwa ni siku ya Jumatano mwezi ishirini na mbili–Ramadhani, watu wakamlaki na kumpongeza kwa ushindi aliopewa na Allah.

 

BWANA MTUME AWATAKA USHAURI MASWAHABA WAKE KUHUSIANA NA KADHIA YA MATEKA.

Mateka walipowasili Madinah, Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie-akawagawa baina ya maswahaba wake na kuwaambia:

“Usianeni kuwatendea wema mateka hawa”. Maswahaba wakaipokea kwa mikono miwili amri hii ya Mtume wa Allah, wakawakirimu mateka wao kiasi cha kuwapendelea wao chakula kizuri kuliko wanachokula wao. Abuu Aziyz Ibn Umay, mmoja wa mateka anasema katika riwaya iliyopokelewa na Ibn Is–haaq:

“Nilikuwa katika kundi la Answaar wakati waliponileta mateka kutoka Badri, wakawa wanapoleta chakula chao cha mchana na usiku, hunikhusisha mimi kwa kunipa mkate na wao wakala tende kwa ajili ya kuutekeleza wasia wa Mtume wa Allah aliowapa kwetu.

 Hakikuangukia kipande cha mkate mkononi mwa ye yote miongoni mwao ila alinipa. (Akaendelea kusema): Basi mimi huona haya na kumrudishia naye hunirudishia bila ya kukila”.

Kisha Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–akawataka ushauri maswahaba wake wakubwa kuhusiana na suala la mateka, wawafanyeje.

 Ushauri uliotolewa na baadhi yao ulikuwa ni kuwauwa kwa kukatwa shingo zao na panga au kwa kuchomwa moto. Sababu ya hukumu yao hii kali ni kwamba walimwambia Mtume hawa ni mashina ya ukafiri na viongozi wa upotevu na waliwanyanyasa sana waislamu na kuwatesa walipokuwa Makah.

Baadhi ya maswahaba wakawapinga wenzao katika shauri hili la kuwauwa mateka, wao wakasema tukiwauwa hatutafaidika na cho chote, bora ni kuwapa fursa ya kujikomboa kwa kutoa fidia.

Ili watakachokitoa kisaidie katika kuimarisha nguvu ya Waislamu. Na huenda Allah akazielekeza nyoyo zao katika Uislamu, wakasilimu na kutubia.

Mtume wa Allah akausikiliza kwa makini ushauri uliotolewa na makundi mawili haya ya maswahaba wake na ukamuathiri zaidi ushauri wa fidia kuliko ule wa kuua.

Hii ilitokana na hali ya dhiki na ufakiri waliokuwa nayo maswahaba wakati huo.

Amepokea Imamu Ahmad–Allah amrehemu–kutoka kwa Abdallah Ibn Masoud–Allah amuwiye radhi-amesema: Alisema Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–siku ya vita vya Badri:

 “Mnasemaje katika suala la mateka hawa?” Abuu Bakri-Allah amuwiye radhi-hawa ni kaumu yako na ni ndugu zako (Makurayshi wenzako)! usiwauwe, wape nafasi (muda) huenda Allah akawakubalia toba yao”.

Na Umar–Allah amuwiye radhi- akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, hawa walikutoa (walikufukuza) Makah na wakakukadhibisha! Wasogeze karibu uzipige shingo zao kwa panga”.

Abdullah Ibn Rawaahah–Allah amuwiye radhi–nae akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, angalila jangwa (bonde) lenye kuni nyingi uwaingize humo kisha uwawashie moto (wafilie mbali)” (Akaendelea kusema Ibn Masoud): Mtume wa Allah akaingia ndani bila ya kusema lolote. Watu wakasema: Atafuta kauli ya Abuu Bakri na wengine wakasema atafuata kauli ya Umar. Kundi jingine likasema atafuata kauli ya Abdallah Ibn Rawaahad. Mara Mtume akawatokea na kuwaambia: Bila shaka Allah atazilainisha atazilainisha nyoyo za watu kwake mpaka zitakuwa laini zaidi kuliko maziwa (yanapokuwa tumboni). Na bila shaka Allah atazifanya nguvu nyoyo za watu kwake mpaka ziwe ngumu zaidi kuliko mawe. Na nyinyi ni mafakiri (hamna kitu) basi asibakie asibakie ye yote ila kwa kutoa fidia (na kama hana) na ipigwe upanga shingo yake.”

 

III/. UTOZAJI WA FIDIA KWA MATEKA

Allah Mola mjuzi wa siri na dhahiri akamlaumu Mtume wake –Rehema na Amani zimshukie kwa kitendo chake cha kukubali kupokea fidia kuliko kuwauwa mateka, akasema:

“HAIMPASII NABII (ye yote) KUWA NA MATEKA MPAKA APIGANE (sana) NA KUSHINDA (barabara) KATIKA NCHI (ndipo achukue mateka). MNATAKA VITU VYA DUNIA HALI ALLAH ANATAKA (mpate thawabu za) AKHERA! NA ALLAH NI MWENYE NGUVU (na) MWENYE HEKIMA. ISINGALIKUWA HUKUMU ILIYOTANGULIA KUTOKA KWA ALLAH (kuwa mwenye kujitahidi mwisho wa jitihada yake hateswi) BILA SHAKA INGELIKUPATENI ADHABU KUBWA KWA YALE MLIYOYACHUKUA.” (8:67–68)

Wapokezi wanasema kwamba Mtume wa Allah–Rehema na Amani zimshukie–alilia sana na Abuu Bakri iliposhuka aya hii na akatamani lau angelifuata rai ya kuwauwa mateka.

Kutokana na kwamba Allah alimsamehe Mtume wake kwa kosa hili kama inavyosema aya, akamuhalalishia yeye na waislamu ile ngawira waliyoitwaa, akasema:

“BASI KULENI KATIKA VILE MLIVYOTEKA (vitani) NI HALALI (yenu sasa) NA VIZURI, NA MCHENI ALLAH. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU.” (8:69)

Bwana Mtume–Rehema na Amani zimshukie akawafanyia ihsani kubwa mateka walio mafakiri kwa kuwaacha huru bila ya kuwatoza fidia.

Akafanya fidia ya wanaojua kusoma na kuandika ni kila mmoja wao kuwafundisha kusoma na kuandika watoto kumi wa Kiislamu.

Ama mateka waliokuwa matajiri, aliendelea kuwashikilia mpaka waje kukombolewa na ndugu zao kwa kutoa fidia. Fidia ya kila mmoja wao ilikuwa ni kati ya Dirham alfu moja mpaka Dirhamu alfu nne. Fidia hii ilizingatia hali na uwezo wa mateka binafsi au ndugu zake mateka huyo.

Miongoni mwa watu waliofanyiwa ihsani ya kuachwa huru bila ya fidia na Bwana Mtume, alikuwa ni Abuu Azzah;Umar Ibn Abdillah Al- Jumahiy.

Huyu alikuwa fakiri mwenye watoto wa kike, akamzungumza Mtume wa Allah akamwambia:

“Ewe Mtume wa Allah, bila shaka wewe wajua vema kwamba mimi sina mali na unajua mimi ni fakiri na nina familia inayonitegemea, basi nakuomba unifanyie ihsani.”

 Mtume wa Allah akamkubalia ombi lake hilo na kumuacha huru bila ya fidia nae akaipokea ihsani na ukarimu huu wa Mtume kwa kumuahidi kwamba hatamuunga mkono wala kumsaidia kwa namna yo yote ile mpinzani wake.

 

BWANA MTUME AAMURU KUUAWA KWA MATEKA WAWILI

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie akaondoka pale Rauhaa alipolakiwa na maswahaba wake kuendelea na safari yake ya Madinah.

Alipofika mahala panapoitwa “Al–Uthayl” akawakagua mateka na akaamuru kuuliwa wawili miongoni mwao ambao ni An–nadhwru Ibn Al–Haarith na Uqbah Ibn Abiy Muaitw.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *