ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI:
Allah Mtukufu anasema:
“ENYI MLIOAMIMNI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH. SIKU CHACHE TU (kufunga huko). NA ATAKAYEKUWA MGONJWA KATIKA NYINYI AU KATIKA SAFARI (akafungua baadhi ya siku), BASI (atimize) HISABU KATIKA SIKU NYINGINE. NA WALE WASIOWEZA, WATOE FIDIA KWA KUMLISHA MASIKINI. NA ATAKAYEFANYA WEMA KWA RADHI YA NAFSI YAKE, BASI NI BORA KWAKE. NA (huku) KUFUNGA NI BORA KWENU IKIWA MNAJUA. (mwezi huo mlioambiwa kufunga) NI MWEZI WA RAMADHANI AMBAO IMETEREMSHWA KATIKA (mwezi) HUO HII QUR-ANI ILI IWE UWONGOZI KWA WATU, NA HOJA ZILIZO WAZI ZA UWONGOFU NA UPAMBANUZI (wa baina ya haki na batili). ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE. NA MWENYE KUWA MGONJWA AU SAFARINI, BASI (atimize) HISABU (ya siku alizoacha kufunga) KATIKA SIKU NYINGINE. ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI NA WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO, NA PIA (anakutakieni) MTIMIZE HISABU HIYO. NA (anakutakieni) KUMTUKUZA ALLAH KWA KUWA AMEKUONGOZENI, ILI MPATE KUSHUKURU”. [2:183-185]
Aya hii tukufu imeanza kwa kuwaita waislamu kwa jina la imani ili kuiamsha kani ya imani ndani ya nyoyo zao.
Na kuwaandaa kiroho kuitika na kupokea amri/maagizo watakayopewa kwa mujibu wa imani yao.
Kwa sababu shani na tabia ya muumini wa kweli ni kumtii Mola wake Mtukufu katika kila analomuamrisha kutenda au kutotenda.
Aya hii imebainisha ubainifu kamili na timilifu wa fadhila (ubora) ya swaumu ya Ramadhani. Falsafa/hekima yake na rehema ya Allah Mtukufu kwa waja wake kupitia fardhi hii ya swaumu.
Katika jumla ya hukumu nyingi tunazozipata ndani ya aya hii. Ni kwamba aya imewazihisha kwamba muislamu ana hali tatu katika kuilekea fardhi hii ya swaumu ya Ramadhani:-
HALI YA KWANZA:
Muislamu atakapokuwa mgonjwa ndani ya mwezi wa Ramadhani, anaumwa maradhi ambayo ghalibu mtu hutarajiwa kupona.
Na kama atafunga maradhi yatazidi au atachelewa kupona. Au yumo safarini, katika hali mbili hizi; hali ya ugonjwa na ile ya safari.
Uislamu unampa rukhsa ya kula katika mwezi wa Ramadhani kwa sharti kwamba ukiondoka udhuru uliomuhalalishia kula.
Azikidhi (azilipe) siku zote alizokula ndani ya Ramadhani.
Na kuondoka kwa udhuru kunapatikana kwa mgonjwa kupona na kurejea katika siha yake ya kawaida.
Itakayomuwezesha kumudu makali ya njaa na joto la kiu. Na kwa msafiri ni kwa kurejea katika makazi yake au kuamua kuwa mkazi huko alikokwenda. Na dalili ya rukhsa hii ya kula aliyopewa mgonjwa na msafiri na kisha kukidhi ni kauli yake Allah:
“…NA ATAKAYEKUWA MGONJWA KATIKA NYINYI AU KATIKA SAFARI (akafungua baadhi ya siku), BASI (atimize) HISABU KATIKA SIKU NYINGINE…” [2:184]
HALI YA PILI:
Muislamu atakapokuwa mgonjwa katika mwezi wa Ramadhani, anaumwa maradhi ambayo kupona hakutarajiwi.
Au akawa ni mzee mkongwe hasiyeweza kufunga. Katika hali na mazingira haya, sheria imewahalalishia kula na kumpa masikini kibaba cha chakula kwa kila siku.
Hii ni kwa sababu hawa wana nyudhuru zisizotazamiwa kuondoka kama ilivyo kwa watu wa hali ile ya kwanza.
Ni kwa mantiki hii ndio Uislamu ukawawajibishia hawa kutoa fidia bila ya kulipa kwa dalili ya kauli yake Allah Mtukufu:
“…NA WALE WASIOWEZA, WATOE FIDIA KWA KUMLISHA MASIKINI…” [2:184]
HALI YA TATU:
Muislamu atakapokuwa ndani ya mwezi wa Ramadhani mzima (sio mgonjwa) na akawa ni mkazi (sio msafiri).
Na wala hana udhuru unaomzuia kufunga mithili ya mwanamke kuwemo hedhini. Katika hali na mazingira haya Allah amemuwajibishia na kumfaradhishia swaumu kwa dalili ya kauli tukufu ya Allah:
“…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…” [2:185]
Kwa hivyo ni haramu kwa muislamu ambaye ni mzima na si msafiri kuacha kufunga kwa makusudi swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Akiamua kutokufunga bila ya idhini ya sheria atakuwa miongoni mwa waliopata khasara duniani na akhera kwa sababu ya kuivunja amri ya Allah.
Imepokewa na Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Ye yote atakayefungua (atakayekula) siku moja katika Ramadhani bila ya rukhsa wala maradhi. Haitoikidhi (siku hiyo) swaumu ya umri mzima ajapofunga”.Tirmidhiy, Abuu Daawoud, Nasaai, Ibn Maajah, Ibn Khuzaymah & Al-Baihaqiy
MAANA YA SWAUMU:
Swaumu ni neno la Kiarabu lililobeba dhana ya ibada ya funga ambayo ni nguzo ya nne miongoni mwa nguzo tano za Uislamu. Neno hili linafasiriwa kwa maana mbili; maana ya kilugha (maana isiyo rasmi) na maana ya kisheria (maana rasmi).
SWAUMU KATIKA LUGHA:
Kilugha isimu (nomino)- “swaumu”-inabeba dhana ya kujizuia kutenda kitu cho chote kiwacho. Maana hii ya swaumu kilugha inachimbuka kupitia kauli tukufu ya Allah:
“…HAKIKA MIMI NIMEWEKA NADHIRI KWA (Allah) MWINGI WA REHEMA YA SWAUMU (kufunga), KWA HIVYO LEO SITASEMA NA MTU”. [19:26]
Yaani Bibi Maryamu mama yake Nabii Isa-Amani ya Allah iwashukie-aliwaambia waliomuuliza kuhusiana na suala la mwanawe huyo.
Naye akaambiwa na Allah awajibu, mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema kutokuzungumzia suala la mwanangu huyu; Isa. Katika kauli yake Bi.Maryamu ndani ya aya hii amelitumia neno SWAUMU kumaanisha KUJIZUIA kuongelea suala la mwanawe. Na hapa ndipo ilipotwaliwa maana ya swaumu kilugha.
SWAUMU KATIKA SHERIA:
Kwa mtazamo wa sheria swaumu ni kujizuia na vyote vyenye kubatilisha swaumu kwa lengo la kuabudu.
Katika kipindi kinachoanzia na kuchomoza kwa alfajiri na kumalizikia na kuzama/kutua kwa jua. Kujizuia huku kunaambatana na nia ya swaumu ambayo ni wajibu iletwe kabla ya kuanza kwa kipindi cha swaumu yenyewe.
SWAUMU YA RAMADHANI IMEFARADHISHWA LINI?
Kumbukumbu sahihi za tarekh (history) zinaonyesha kwamba Allah Mtukufu amewafaradhishia waislamu swaumu ya Ramadhani.
Katika mwezi wa Shaabani, mwaka wa pili wa Hijrah. Hii inamaanisha kwamba katika kipindi chote cha utume cha Makkah; kipindi cha miaka isiyopungua kumi na tatu, swaumu ilikuwa bado haijafaradhishwa.
Ikaja kufaradhishwa mwaka wa pili tangu tangu Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kuhamia Madinah.
NINI HUKUMU YA SWAUMU YA RAMADHANI NA DALILI YAKE NI IPI?
Swaumu ya Ramadhani ni mojawapo ya nguzo za Uislamu na wala haisihi kwa muislamu kulitilia shaka hilo. Kwani swaumu ya Ramadhani imethibiti kwa “nassi”-nukuu ya Qur-ani Tukufu ambayo muislamu hawi muislamu ila kwa kuiamini. Tena imethibiti kwa Sunnah Tukufu ya Mtume wa Allah na kwa Ijmaa ya wanazuoni wa Kiislamu.
Ama kuthibiti kwake katika Qur-ani kunapatikana kupitia katika kauli tukufu ya Allah:
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH”. [2:183]
Na katika kauli yake:
“…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…” [2:185]
Na katika Sunnah swaumu ya Ramadhani imethibiti kupitia hadithi nyingi sahihi za Bwana Mtume. Miongoni mwake ni kauli yake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano:
1. Kushuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allah, na
2. Kusimamisha swala, na
3. Kutoa zakkah, na
4. Kufunga Ramadhani, na
5. Kuhiji nyumba ya Allah kwa mwenye kumudu gharama za njia ya kuendea huko”.
Na uma umekongamana juu ya uwajibu na ufaradhi wa swaumu ya mwezi wa Ramadhani kwa kila muislamu.
Na atakayeupinga uwajibu huo, huwa amejitoa mwenyewe uislamuni. Anakuwa si muislamu tena kwa kuipinga kwake mojawapo ya nguzo za Uislamu.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Kishiko cha Uislamu na nguzo za dini ni tatu, juu yake (nguzo hizo) umejengwa Uislamu. Atakayeiacha moja miongoni mwake, basi yeye kwa (kuiacha nguzo) hiyo ni KAFIRI aliye halali (kumwagwa) damu (yake):
Kushuhudia kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila Allah,
Swala za fardhi, na
Swaumu ya Ramadhani”.
Abuu Ya’alaa & Dailamiy
NINI HEKIMA/FALSAFA YA KUFARADHISHWA SWAUMU?
Allah Mtukufu amewafaradhishia waja wake ibada ya swaumu ya Ramadhani kwa hekima tukufu. Na malengo mema ambayo manufaa yake huwarejea wenyewe, hekima hizo ni pamoja na:-
Kupandikiza Ikhlaaswi na ucha-Mungu nyoyoni. Kwa sababu mfungaji hakusudii kwa swaumu yake ila radhi ya Muumba wake.
Na kutumainia kupata thawabu zake na kuichelea adhabu yake. Hii ndio sababu aya inayoitaja swaumu imekhitimishwa na kauli yake Allah:
“…ILI MPATE KUMCHA ALLAH…” Yaani enyi waumini kwa kuitekeleza kwenu fardhi hii ya swaumu mtajihakikishia kupata daraja ya ucha-Mungu.
Na kinga ya nafsi zenu dhidi ya kila lisilolingana na kwenda sambamba na imani yenu.
Swaumu inauadilisha na kuuadabisha moyo sambamba na kuisadia nafsi kuwa katika mstari wa wima na usafi. Na inauvika moyo utoharifu na utakaso.
Swaumu inamjengea mwanadamu uwezo wa kujimiliki na kujiendesha. Na hivyo kumuwezesha kuushinda utumwa wa matamanio na matashi mabaya ya nafsi.
Na kumuundia mja silaha muhimu kabisa katika maisha yake. Silaha ya subira na ujasiri mbele ya machungu na magumu yote ya maisha ambayo huja bila ya hodi wala taarifa.
Swaumu ina mchango mkubwa sana katika kumfundisha mwanadamu kiamalia (kwa njia ya matendo). Kwani ni sehemu ya maumbile ya mwanadamu kutokuijua thamani ya neema aliyonayo ila baada ya kuikosa neema husika au wakati wa kuihitajia.
Mfungaji atakapoyahisi machungu ya njaa na joto la kiu. Hisia hizi zitamfanya kuitambua kiamalia hali ya mafakiri na wahitaji na hivyo kumpelekea kuwaonea huruma. Na hatimaye kuwakunjulia mkono wa msaada.
Hili ndilo lililowasukuma baadhi ya wanazuoni kusema: Swaumu ni unyimi uliowekwa na sheria, kuadabishwa kwa njia ya njaa na ni unyenyekevu na kujitupa kwa Allah.
Swaumu ni tiba ya mwili iupao uimara na siha njema na pozo la baadhi ya maradhi. Kwa sababu aktharia ya watu hupatwa na maradhi kwa ajili ya israfu yao katika kula na kunywa. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema:
“Mwanadamu hajapatapo kujaza chombo shari kuliko tumbo lake. Vinamtosha mwanadamu vijitonge vitakavyousimamisha uti wa mgongo wake. Ikiwa hapana budi, basi theluthi moja (ya tumbo) iwe ni ya chakula, theluthi nyingine ya maji na theluthi nyingine ya pumzi yake”. Tirmidhiy
Swaumu ya Ramadhani hulipa tumbo mapumziko ya mwezi mmoja kila mwaka. Mapumziko ambayo hupelekea kutumika kwa ziada ya chakula na mafuta iliyojikusanya mwilini kwa kipindi cha miezi kumi na moja.
Ziada ambayo lau itaendelea kusalia mwilini huwa ni sababu na chanzo cha maradhi mengi ambayo yanawataabisha wengi katika wanadamu wa zama hizi.
Hizi ni baadhi ya hekima na sehemu ndogo ya falsafa ambazo kwa ajili yake Allah Mtukufu ameufaradhishia umati huu swaumu kama alivyozifaradhishia nyumati za kabla yetu. Na amesema kweli Allah pale aliposema:
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYOLAZIMISHWA WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH”.
MWEZI MWANDAMO WA RAMADHANI HUTHIBITIJE?
Kuingia na kuanza kwa mwezi wa Ramadhani huthibiti kwa mojawapo ya mambo mawili yafuatayo:-
Kukamilika na kumalizika kwa mwezi wa Shaabani. Siku thelethini za mwezi wa Shaabani zikikamilika, basi siku ya thelathini na moja ndio itakayokuwa siku ya kwanza ya Ramadhani kwa kutinda (kukata).
Kuona mwezi mwandamo. Ukionekana mwezi mwandamo wa Ramadhani katika usiku wa mwezi thelathini Shaabani. Ramadhani itakuwa imekwishaingia na kuwajibisha swaumu kwa mujibu wa kauli ya Allah:
“…ATAKAYEKUWA KATIKA MJI KATIKA HUU MWEZI (wa Ramadhani) AFUNGE…”
Na kauli ya Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Fungeni mtakapouona mwezi na fungueni mtakapouona. Na mkifunikwa na wingu (mkashindwa kuuona), basi kamilisheni idadi ya siku thelathini (za Shaabani)”. Muslim
Na kunatosha katika kuthibiti kuonekana kwa mwezi kuona kwa mtu mmoja muadilifu au watu wawili waadilifu.
Kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alijuzisha uonaji wa mtu mmoja kwa mwezi mwandamo wa Ramadhani.
Kama ilivyokuja katika hadithi sahihi iliyopokelewa na Abuu Daawoud na wengineo. Ama kuonekana kwa mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi) kwa ajli ya kufungua, hakuthibiti ila kwa kuona mashahidi wawili waadilifu.
Kwa sababu Bwana Mtume hakujuzisha kuona kwa mtu mmoja muadilifu katika mwezi wa kufungua. Kama lilivyothibiti hilo mbele za Twabaraaniy na Daaruqutwniy
TANBIHI:
Atakayeuona mwezi mwandamo wa Ramadhani kutamuwajibikia yeye kufunga hata kama ushahidi wake wa kuuona mwezi hautathibiti mbele ya kadhi na ukakataliwa.
Na atakayeuona mwezi wa kufungua na ushahidi wake usikubaliwe, hatafungua kwa dalili ya kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Huko kufunga ni siku mnayofunga na kufungua ni siku mnayofungua. Na kuchinja ni siku mnayochinja”. Tirmidhiy
Ni fardhi kifaaya kwa waislamu kujishughulisha kuutafuta mwezi wa mwandamo magharibi ya siku ya ishirini na tisa ya miezi ya Shaabani (kwa kufunga).
Na Ramadhani (kwa kufungua), ili wawe katika ithibati ya kuanza na kumalizika kwa swaumu na kujitoa katika shaka.
Kwani imekuja katika hadithi tukufu iliyopokelewa na Bi.Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akijihifadhi (akijichunga) katika Shaabani zaidi kuliko anavyojihifadhi katika miezi mingine.
Kisha hufunga kwa kuuona mwezi (mwandamo wa) Ramadhani. Ukimgubikia (yaani huo mwezi mwandamo wa Ramadhani) huhisabu siku thelathini (za Shaabani), kisha ndipo hufunga”.
MIONGONI MWA FADHILA ZA RAMADHANI.
Zimepokelewa hadithi nyingi katika kutaja fadhila za mwezi wa Ramadhani, miongoni mwazo ni kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:-
“Umekujieni mwezi wenye baraka, Allah Mtukufu amekufaradhishieni swaumu yake. Hufunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto na mashetani hutiwa pingu. Ndani yake kuna usiku mmoja ambao ni bora kuliko miezi alfu moja”. Ahmad, Nasaai & Al-Baihaqiy
“Hakika Allah Mtukufu amekufaradhishieni swaumu ya Ramadhani, nami nimekusunishieni kisimamo chake. Basi atakayeufunga (mwezi huo) kwa imani na kwa kutaraji malipo kwa Allah. Hutoka madhambi yake kama siku aliyozaliwa na mama yake”.
“Namuapia yule ambaye nafsi ya Muhammad iko mikononi mwake, harufu ya kinywa cha mfungaji mbele ya Allah ni nzuri zaidi kuliko harufu ya miski. Yuna mfungaji furaha mbili anazozifurahikia; anapofuturu hufurahia futari yake na atakapokutana na Mola wake ataifurahia swaumu yake.
Mbeya (aina) tatu za watu dua yao hairejeshwi:-
1. Mfungaji mpaka afungue, na
2. Haji mpaka arejee, na
3. Dua ya mwenye kudhulumiwa”.
Hii ni sehemu ndogo tu ya hadithi za Mtume zilizopokelewa katika kutaja fadhila, utukufu na ubora wa mwezi wa Ramadhani.
Na ikiwa hizo ndizo thawabu za wafungaji wa mwezi huu kwa imani, kwa kutarajia malipo ya Allah, kwa kutumai kupata radhi yake na kwa kuichelea adhabu yake.
Basi bila ya shaka khasara ya wasiofunga katika mwezi huu bila ya udhuru unaozingatiwa kisheria. Hakuna aijuaye khasara yao hiyo ila Allah pekee ambaye ndiye atakayeilipa kila nafsi kwa yote iliyoyatenda.
NGUZO ZA SWAUMU, SHARTI ZA KUSIHI SWAUMU NA SWAUMU NI WAJIBU KWA NANI?
NGUZO ZA SWAUMU:
Swaumu ya Ramadhani ina nguzo kuu mbili za msingi, ambazo kusihi kwa swaumu kunazitegemea.
Kujizuia na yote yenye kufunguza tokea kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua, kwa ushahidi wa neno lake Allah Mtukufu: “…NA KULENI NA KUYWENI MPAKA UBAINIKE KWENU WEUPE WA ALFAJIRI KATIKA WEUSI WA USIKU. KISHA TIMIZENI SWAUMU MPAKA USIKU…” [2:187]
Nia, kwa maana ya muislamu kunuia kufunga mwezi wa Ramadhani. Na nia mahala pake ni moyoni na sio lazima kama ambavyo si vibaya kuitamka kwa ulimi.
Na jopo la mafaqihi linaona ni wajibu kuileta nia katika kila usiku wa Ramadhani kabla ya kuchomoza kwa alfajiri. Huku ni kuifanyia kazi kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Asiyeleta nia ya swaumu usiku, hana swaumu”. Tirmidhiy
Na uwajibu huu wa nia ni kwa upande wa swaumu ya fardhi tu. Ama swaumu za suna, nia inatosha hata baada ya kuingia kwa mchana maadamu mtu hajatenda lo lote miongoni mwa yabatilishayo swaumu.
Kwani imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliingia kwake siku moja na kuuliza: “Je, mna cho chote?” Nikamjibu: Hapana, akasema: “Basi hakika mimi nimefunga”. Muslim
SWAUMU NI WAJIBU KWA NANI?
Mafaqihi wamekongamana kwamba swaumu ya Ramadhani ni wajibu kwa kila:-
· Muislamu,
· Mwenye akili timamu,
· Baleghe (mtu mzima),
· Asiye na udhuru wenye kumuhalalishia kula.
Sharti hizi za kuwajibisha swaumu ya Ramadhani kwa mja, mafaqihi wamezichimbua katika kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Kalamu imeondoshwa kwa mbeya (aina) tatu za watu:
1. Kwa mwendawazimu mpaka arudiwe na akili, na
2. Kwa mtu aliyelala mpaka aamke, na
3. Kwa mtoto mdogo mpaka afikiliye baleghe”.
Ahmad & Abuu Daawoud
Na kauli yake Bwana Mtume katika kubainisha upungufu wa dini kwa mwanamke: “Je, hakuwa anapoingia hedhini haswali na hafungi?” Bukhaariy
UFAFANUZI:
Ama sharti ya Uislamu ni kwa sababu Uislamu ndio msingi mkuu wa taklifu (kulazimiwa na hukumu za sheria) kwa mja. Baleghe (ukubwa) kwa sababu ndio wakati/mahala ambapo taklifu huanza kwa mja.
Akili timamu ni kwa sababu ndio chombo kinachomuwezesha mja kumaizi na kutambua mambo. Na ama kutokuwa na udhuru ni kwamba katika jumla ya fadhila zake Allah kwa waja wake.
Ni kuyaondoshea ufaradhi wa swaumu baadhi ya makundi ya waja wake. Mara nyingine uondoshaji huo unakuwa ni kwa njia ya wajibu wa muda maalumu kama ilivyo kwa mwanamke mwenye hedhi au nifasi.
Hawa ni haramu kwao kufunga katika kpindi chote cha hedhi/nifasi mpaka watakapotwaharika. Na wakati mwingine huwa ni kwa ajili ya rukhsa maalumu (msamaha wa Allah) kama ilivyo kwa mgonjwa, msafiri, kikongwe na wengineo kama tutakavyowabainisha baadaye-Inshaallah Taala.
SHARTI ZA KUSIHI SWAUMU:
Na mambo manne haya tuliyoyataja yaani Uislamu, baleghe, akili timamu na kutokuwa na udhuru uhalalishao kula, ndio sharti za kuwajibisha swaumu.
Na wakati huo huo yanafaa kuwa sharti za kusihi kwa swaumu. Ila baadhi ya mafaqihi wameongezea sharti nyingine ya tano nayo ni kuwa wakati uwe unaruhusu kufunga.
Kwani hakusihi kufunga katika siku za Idi mbili; Idi ya mfunguo mosi na ile ya mfunguo tatu.
Wala katika zile siku tatu za kuanika nyama ambazo ni mwezi kumi na moja, kumi na mbili na kumi na tatu katika mfunguo tatu. Kwa sababu ni haramu kufunga katika siku hizi.
HUKUMU YA SWAUMU KWA WATOTO.
Watoto ambao hawajafikilia umri wa baleghe si WAJIBU kwao swaumu ya Ramadhani. Lakini ni jukumu la wazazi kuwazoesha kidogo kidogo kufunga tangu wadogo, ili wainukie na mazoea ya ibada ukubwani.
Kwani imepokewa kutoka kwa Rubayyi Bint Muaadh-Allah amuwiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipeleka salamu mchana wa siku ya Ashura katika vitongoji vya Answaari akisema:
“Aliyepambazukiwa hali ya kuwa kafunga, basi na aitimize swaumu yake. Na aliyepambazukiwa ilhali hakufunga, basi na afunge baki ya siku yake”. Tukawa tukiifunga siku hiyo (ya Ashura) baada ya hapo na tukiwafungisha watoto wetu wadogo.
“Na tukienda msikitini na kuwafanyia wanasesere wa sufi, mmoja wao akililia chakula tunampa (mwanasesere huyo kuchezea)”. Bukhaariy & Muslim
Hadithi hii sahihi inafahamisha kwamba hakuna kizuizi kuwazoesha watoto wadogo kufunga kabla ya kufikilia umri wa kubaleghe; umri wa taklifu. Lakini iwe ni kwa hatua baada ya hatua.
HUKUMU YA KUFUNGA SIKU YA SHAKA.
Makusudio ya “siku ya shaka” ni mwezi thelathini Shaabani iwapo mwezi haukuandama usiku wa kuamkia siku hiyo.
Ikaingia shaka je, siku hiyo ni mwezi thelathini Shaabani au ni mwezi mosi Ramadhani? Basi ni karaha/haramu kufunga siku hii ila itakapowafikiana na ada ya mtu ya kufunga, hapo si karaha wala haramu.
Hii ni kama vile mtu kuwa na mazoea ya kufunga suna za Jumatatu na Alkhamisi, na siku ya shaka ikaangukia katika mojawapo ya siku mbili hizi.
Na sababu ya ukaraha huu wa kufunga siku ya shaka ni kule kupingana kwake na kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Fungeni kwa kuuona (mwezi mwandamo wa Ramadhani) na fungueni kwa kuuona (mwezi mwandamo wa Shawwal). Na mkifunikwa na wingu (mkashindwa kuuona), basi kamilisheni idadi ya siku thelathini za Shaabani”.
Na kwa sababu ya kauli yake: “Msiitangulie swaumu ya Ramadhani kwa (kufunga) siku moja au siku mbili (kabla yake). Ila iwe ni swaumu anayoifunga mtu (kwa ada), basi na afunge siku hiyo”. Tirmidhiy, Ahmad, Bukhaariy, Muslim, Abuu Daawoud, Nasaai & Ibn Maajah.
NYUDHURU ZINAZOMUHALALISHIA MTU KUACHA KUFUNGA.
Allah Mtukufu ameiasisi na kuisimamisha sheria ya kiislamu juu ya misingi ya wepesi, huruma, kuondosha uzito na madhara na kuwakalifisha watu lililomo katika uweza wao. Hili linashuhudiwa na kauli tukufu za Allah:
“…ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO…” [2:185]
“…HAPENDI ALLAH KUKUTIENI KATIKA TAABU, BALI ANATAKA KUKUTAKASENI NA KUTIMIZA NEEMA YAKE JUU YENU ILI MPATE KUSHUKURU”. [5:6]
“ALLAH ANATAKA KUKUKHAFIFISHIENI MAANA MWANADAMU AMEUMBWA DHAIFU”. [4:28]
“ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE…” [2:286]
Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Hakika dini hii ni nyepesi na hakuna ye yote atakayeitilia mikazo ila itamshinda tu…”
Allah Mtukufu kwa fadhila na huruma yake kwa waja wake amewahalalishia baadhi ya watu kula katika mwezi wa Ramadhani, kwa sababu zinazowalazimisha kutokufunga.
Watu hawa wenye kibali cha Mola wao kinachowahalalishia kutokufunga wanagawika katika makundi kadhaa kama ifuatavyo:-
WALIOPEWA RUKHSA YA KULA NA KUWAJIBISHIWA KUKIDHI SIKU WALIZOKULA BAADA YA KUONDOKEWA NA UDHURU:
Kundi hili linawajumuisha:-
· Wagonjwa wanaougua maradhi ambayo hutarajiwa kutibika na kupona baada ya kupata tiba. Na wanachelea swaumu itawazidishia maradhi au kuchelewesha kupona au itawapa taabu kubwa.
· Wasafiri kwa sharti safari hiyo iwe ni ya
· Halali,
· Inaruhusiwa kupunguza swala ndani yake,
· Ianze mchana.
· Wanawake wajawazito na wale wanyonyeshao. Hawa wamehalalishiwa kula kwa ajili ya kuwaondoshea uzito.
WALIOPEWA RUKHSA YA KULA NA KUWAJIBISHIWA KUTOA FIDIA.
Walio chini ya kundi hili ni:-
Wagonjwa walio na maradhi ambayo hayatarajiwi kupona. Hawa ni kama vile wagonjwa wa saratani (cancer), kifua kikuu kilichopevuka (T.B.), kisukari (diabetes) na maradhi mengine kama haya.
Watu wazima vikongwe wenye umri mkubwa sana ambao wamekuwa kama watoto wadogo. Hawa wamehalalishiwa kula na kutoa fidia kwa kumlisha masikini chakula kwa kila siku au kumpa thamani ya chakula hicho. Na hiyo fidia ni kutoa kibaba kimoja cha chakula rasmi cha mahala pale, mithili ya mchele kwa ukanda huu wa pwani ya Afrika Mashariki. Na kibaba ni sawasawa na robo tatu ya kilo takriban.
C: WALIOWAJIBISHIWA KUKIDHI NA KUTOA KAFARA NA HEKIMA/FALSAFA YA KAFARA.
Kafara ni lile lifanywalo kwa ajili ya kufuta dhambi itokanayo na kukhalifu sheria. Ye yote atakayeikhalifu sheria kwa
· Kumuingilia mkewe katika mchana wa Ramadhani.
· Kula au kunywa kwa makusudi bila ya kuwa na udhuru unaozingatiwa kisheria.
Atalazimika kutoa kafara kwa mujibu wa sheria, mbali ya dhambi iandamiayo tendo hilo la mukhalafa wa sheria.
Na kafara ya huku kukhalifu sheria ni kutenda mojawapo ya mambo matatu haya:-
· Kumuacha huru mtumwa muislamu, au
· Kufunga miezi miwili mfululizo, au
· Kuwalisha masikini sitini, kila mmoja kibaba kimoja cha chakula.
FALSAFA YA KAFARA.
Falsafa ya kuwekwa kafara hii ni kuilinda na kuihifadhi sheria dhidi ya kuchezewa na kuvunjwa hovyo kwa matashi ya mtu. Pia inamtwaharisha muislamu kutokana na dhambi ya kukhalifu sheria aliyoitenda bila ya udhuru.
HUKUMU YA ALIYEKUFA KABLA YA KUKIDHI SWAUMU YA RAMADHANI.
Mtu atakayekufa kabla ya kumakinika kukidhi siku alizokula ndani ya mwezi wa Ramadhani, kwa sababu ya udhuru unaozingatiwa kisheria.
Walii wake miongoni mwa wenye haki ya kumrithi, au jamaa yake au ye yote anayehusiana na marehemu huyu, atamfungia.
Na akimfungia pamoja na kumlishia chakula ni bora zaidi ikiwa anaweza kufanya hivyo. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-
“Kwamba mtu mmoja alikuja kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika mama yangu amekufa na ilhali anawiwa na swaumu ya mwezi (Ramadhani), basi je, nimkidhie? (Mtume) akamwambia: Lau mama yako angekuwa na deni ungemlipia? Akajibu: Naam, Mtume akamwambia: Basi deni la Allah linastahiki zaidi kulipwa”. Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Ibn Maajah & wengineo.
SUNA ZA SWAUMU NA ADABU ZAKE.
Siku zote mtu mwenye akili huhangaika na kupupia kufikia ukamilifu katika utekelezaji wa ibada zake na baki ya mambo yake mengine.
Na kila muislamu anatambua kwamba swaumu ni miongoni mwa ibada tukufu zenye daraja kubwa mbele za Allah.
Kwa hiyo basi, inamuwajibikia kila muislamu kuitekeleza ibada hii kwa namna ambayo itakusanya kwa pamoja dhana ya uchaji-Mungu, unyenyekevu na kumuunganisha na Mola wake. Ili kuyafikia hayo, mfungaji anatakiwa kuyachunga na kuyatekeleza mambo haya yaliyosuniwa katika swaumu:-
KUHARAKIA KUFUTURU:
Ni suna kufanya haraka kufuturu baada ya kuwa na yakini kuwa jua limezama. Huku ni kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume-rehema na Amani zimshukie: “Watu wataendelea kuwa katika kheri muda wa kuharakia kufuturu”. Bukhaariy & Muslim
KUFUTURU KWA TENDE:
Mara nyingi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akifuturu kwa kula tende au funda ya maji kama hakupata tende. Haya ni kwa mujibu wa riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Bwana Mtume: “Atakapofuturu mmoja wenu, basi na afuturu kwa tende kwani hiyo ni baraka. Na asiyepata (tende), basi na afuturu kwa kunywa maji, kwani hayo ni twahara”. Abuu Daawoud & Tirmidhiy
Kufuturu huku kwa tende au maji au kitu cho chote chenye kufanana na hivyo kuwe ni kabla ya kuswali Magharibi. Kisha ndipo aswali na baada ya swala ndio aende kupata futari yake kamili, hivi ndivyo alivyofanya Bwana Mtume.
KUOMBA DUA:
Inatakikana kwa mfungaji kumuomba Allah mambo ya kheri wakati wa kufuturu bali katika kipindi chote cha swaumu. Imepokelewa kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye radhi-amesema:
“Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa anapofuturu husema: DHAHABAD-DHWAMAU, WABTALLATIL-URUUQ, WATHABATAL-AJRU INSHAALLAH (Kimeondoka kiu, mishipa imerowa na ujira umethibiti apendapo Allah)”. Abuu Daawoud
KULA DAKU:
Ni suna mfungaji kula daku kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Kuleni daku kwani mna baraka katika daku”. Bukhaariy & Muslim
Na imependelewa kuakhirisha kula daku kiasi ambacho mfungaji atakapomaliza kula daku iwe imebakia saa moja au chini yake kabla ya kuingia alfajiri. Imepokelewa kutoka kwa Zayd Ibn Thaabit-Allah amuwiye radhi-amesema:
“Tulikula daku pamoja na Mtume-Rehema na Amani zimshukie-kisha akainuka kwenda kuswali (yaani swala ya alfajiri). Akauliza muulizaji: Kulikuwa na muda gani baina ya adhana (ya alfajiri) na daku? Akajibu: Kiasi cha (mtu) kusoma aya khamsini”. Bukhaariy & Muslim
KUJIEPUSHA NA MANENO YA FEDHULI NA VTENDO VYA KIPUUZI:
Miongoni mwa adabu ambazo mfungaji anatakiwa kujipamba nazo ni kuuzuia ulimi wake kutamka maneno ya kifedhuli na kipuuzi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Asiyeacha maneno ya uwongo (uzushi) na kuyafanyia kazi, Allah hana haja na kuacha kwake chakula chake na kinywaji chake”. Bukhaariy
“Atakapopambazukiwa mmoja wenu siku moja ilhali amefunga, basi asitamke maneno machafu na wala asifanye upumbavu. Basi iwapo mtu atamtukana au kugombana naye na aseme: Hakika mimi nimefunga, hakika mimi nimefunga”. Bukhaariy & Muslim
KUJIPAMBA NA UKARIMU, KUKITHIRISHA KUSOMA QURAN, KUUPISHA TOBA, KUDUMISHA ISTIGHFAARI NA KUJITAHIDI KATIKA IBADA KHASA KHASA KATIKA KUMI LA MWISHO:
Haya ni katika jumla ya mambo mema mazuri ambayo mfungaji anapaswa kujipamba nayo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na kuendelea kuishi nayo nje ya Ramadhani.
Imepokelewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi-amesema: “Alikuwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mkarimu kushinda watu wote kwa kheri na alikuwa mkarimu mno katika Ramadhani kuliko katika miezi mingine…” Bukhaariy
Imepokelewa kutoka kwa Bibi Aysha-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Alikuwa linapoingia kumi la mwisho uhuhisha usiku (hukesha kwa ibada) na huwaamsha wakeze (kufanya ibada) na hufunga kibwebwe” Bukhaariy & Muslim
Kwa ujumla mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kheri, subira, ukarimu na baraka.
Kwa hivyo inatupasa tuitumie vema fursa ya mwezi huu ambayo hupatikana mara moja tu kila mwaka.
Tuitumie fursa hii katika kuziadabisha na kuziadilisha roho zetu na kuzitwaharisha nyoyo na nafsi zetu.
Na kuvizuilia viungo vyetu na kila ovu na kuiendea kwa upeo wa jitihada zetu zote kila ibada na mambo ya twaa. Ili tuwe kwa fadhila zake Allah miongoni mwa waja wake atakaowaridhia na wao kuyaridhia malipo na jazaa maridhawa atakazowapa.
MAMBO YENYE KABATISHA SWAUMU.
Mambo yenye kubatilisha swaumu ya mfungaji yanagawika katika makundi mawili haya:-
YENYE KUBATILISHA SWAUMU NA KUWAJIBISHA KADHAA (KULIPA).
Mambo yaliyo chini ya kundi hili ni pamoja na
Kula au kunywa kwa makusudi. Mfungaji akila au kunywa kwa kukusudia, pale pale swaumu yake itabatilika na atawajibika kuikidhi.
Lakini iwapo alikula au kunywa kwa kusahau, basi hana kadhaa wala kafara. Haya ni kwa mujibu wa kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Atakayesahau na ilhali ana swaumu, akala au kunywa, basi na aitimize swaumu yake. Hakika si vinginevyo, Allah ndiye aliyemlisha na kumnywesha”. Tirmidhiy, Bukhaariy, Muslim & wengineo.
Kujitapikisha kwa makusudi pia kunaiharibu swaumu ya mfungaji na kumuwajibishia kadhaa.
Lakini iwapo atatapika na si kujitapikisha, haitamuwajibikia kadhaa wala kafara. Imepokelewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema:
“Yatakayemshinda matapishi (yakamtoka bila khiari), hakuna kadhaa juu yake. Na atakayejitapikisha kwa makusudi basi na akidhi”. Ahmad, Abuu Daawoud, Tirmidhiy, Ibn Maajah, Ibn Hibban & Al-Haakim.
Hedhi na nifasi hata kama imetoka katika kipindi kifupi tu kabla ya kuchwa (kuzama) kwa jua. Hili ni kwa mujibu wa IJMAA ya wanazuoni.
Kujitoa manii kwa kupiga punyeto, kumbusu au kumkumbatia mke, hili pia linabatilisha swaumu.
TANBIHI:
Ikiwa manii yatatoka mchana kwa sababu ya kuangalia tu, swaumu haitabatilika na hakitomuwajibikia cho chote zaidi ya kukoga janaba.
Hali kadhalika kutoka kwa madhii pia hakuiathiri swaumu kwa cho chote bila ya kujali kuwa ni mengi au machache.
v. Mfungaji kuingiza kitu katika uwazi wa ndani kwa
khiyari yake mwenyewe kupitia tundu zilizo wazi.
Mithili ya masikio, pua, tundu ya nyuma na
kadhalika. Kitu hicho kikawa ni chakula, kinywaji, dawa na mfano wa hivyo.
Na ni wajibu kwa mtu aliyeifisidi swaumu yake na kuwajibikiwa na kadhaa, kwa sababu ya kutenda mojawapo ya mambo madhukuru (tajwa) haya. Kufanya haraka kuzikidhi siku zote alizofungua, hii ni kwa sababu umri wake u mikononi mwa Allah.
YENYE KUBATILISHA SWAUMU NA KUWAJIBISHA KADHAA SAMBAMBA NA KAFARA.
Kundi hili linahodhi jambo moja tu, nalo ni kumuingilia mke katika mchana wa Ramadhani katika mazingira ya khiari. Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema:
Alikuja mtu mmoja kwa Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Nimehiliki ewe mtume wa Allah. (Mtume) akamuuliza: Ni lipi lililokuhilikisha? Akajibu: Nimemuingilia mke wangu katika (mchana wa) Ramadhani. (Mtume) akamuuliza:
Je, una uwezo wa kumuacha huru mtumwa? Akajibu: Hapana sina. Akamuuliza (tena): Je, unaweza kufunga miezi miwili mfululizo? Akajibu: Hapana. Akasema (mpokezi): Kisha akakaa, Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaja na kapu la tende, akasema: Kalitoe hili sadaka. Akasema: Je, yuko fakiri zaidi kuliko sisi?
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akacheka mpaka magego yake yakaonekana na akamwambia: Nenda ukawalishe watoto wako” Bukhariy, Muslim, Tirmidhiy & wengineo.
Thanks for an important lesson, Allah bless you
Allah bless you