Vita hivi vya Banin-Nadhwiyr ni miongoni mwa athari zilizotokana na vita vya Uhud.
Vita hivi vilitokea katika kile kipindi kigumu ambacho waislamu bado walikuwa wakipatwa na machungu yaliyotokana na kushindwa katika vita hivyo.
Bado walikuwa katika hali ya kutapanyika kifikra wakiwa wamezungukwa na visasi.
Mayahudi na wanafiki ambao wanaishi pamoja nao Madinah, mabedui waishio katika vitongoji jirani yao na mushrikina wa Makkah.
Wote hawa walikuwa wakishirikiana katika hisia; hisia ya bughudha na uadui dhidi ya waislamu. Na wakisaidiana katika fikra moja, nayo ni kumfagilia mbalini Bwana Mtume na maswahaba wake wote.
Na wakilenga lengo moja, nalo si lingine bali ni kuua Uislamu na da’awa (mahubiri) yake. Katika mazingira kama haya, adui aliye karibu anakuwa ni khatari zaidi kuliko yule aliye mbali. Na khatari ya ndani inakuwa na athari mbaya na ya kina zaidi kuliko ile itokayo nje.
Na hali ya hewa inakuwa imesheheni vitimbi, hila, kuaibishana na kuviziana baina ya mahasimu. Bila ya shaka mayahudi na wanafiki ndio waliokuwa adui wa karibu kwa waislamu.
Alama za uadui zilikuwa zikichemka nafsini mwao na kutamkwa na ndimi zao na haikuwa muhali kwao kusubiri fursa ya kuwachoma waislamu kwa nyuma yao.
Kwa hakika katika kipindi hiki waislamu walikuwa wakitazamia khiyana na usaliti kutoka kwa maadui zao.
Kwa mazingira haya na hali hii ya hewa iliyochafuka, utaona kuwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa na muamana na usaliti na khiana ya mayahudi na wanafiki wa Madinah.
Na hakuwa na imani tena na ukweli na utekelezaji wao wa makubaliano baina yao na waislamu.
Ama wanafiki, hawa walijificha nyuma ya pazia la Uislamu na haikuwaelea maswahaba wala Bwana Mtume kuwafunulia pazia hili la Uislamu walilolifanya kama kichaka chao cha kujifichia.
Na kwa upande wa mayahudi, hawa walikuwa wamefunga ahadi na Mtume wa Allah kwamba yeye Mtume asiwaingilie katika dini yao na hali kadhalika wao wasimbughudhi na dini yake. Na kwamba wasiwaunge mkono na kuwasaidia maadui wa kila upande.
Lakini pamoja na ahadi yao hii, bado mayahudi hawakuwa ni watu wa kuaminiwa katika utekelezaji wa ahadi. Hii ni kwa sababu tayari ulikuwa umekwishadhihiri usaliti na khiana yao katika matukio mengi huko nyuma.
Na kundi moja miongoni mwa makundi yanayounda jamii ya mayahudi Madinah lilidhihirisha uadui wao waziwazi kiasi cha kumlazimisha Bwana Mtume kulifukuza na kulitoa Madinah.
Haya yalitokea wakati waislamu wakiwa katika kile kipindi cha nguvu nyingi na ustawi uliotokana na ushindi wa kishindo walioupata katika vita vya Badri.
Haya hali sasa itakuwaje katika kipindi hiki cha kizaizai cha kushindwa katika vita vya Uhud? Je, usaliti na khiana katika hali kama hii si unatarajiwa zaidi, jambo hili kwa mayahudi haliko mbali.
Kwani kama walithubutu bila ya uoga katika kile kipindi cha nguvu ni lipi litakalowazuia katika kipindi hiki cha kitatange cha kushindwa?! Katika kipindi hiki ambacho ndugu zao Baniy Qayunqaa wametolewa na kufukuzwa Madinah na waislamu na isitoshe wamemuua kiongozi na mshairi wao Ka’ab Ibn Al-Ashraf.
QUR-ANI TUKUFU YAWATAHADHARISHA WAISLAMU NA KHIANA YA MAYAHUDI.
Allah akawakashifia waislamu siri za mayahudi katika kipindi hiki na akawatahadharisha kutowaamini, akasema-utakatifu ni wake:
“ENYI MLIOAMINI! MSIWAFANYE WASIRI WENU WATU WASIOKUWA KATIKA NYINYI, HAO HAWATAACHA KUKUFANYIENI UBAYA. WANAYAPENDA YALE YANAYOKUDHURUNI. BUGHUDHA (yao juu yenu) INADHIHIRIKA KATIKA MIDOMO YAO NA YANAYOFICHWA NA VIFUA VYAO NI MAKUBWA ZAIDI. TUMEKUBAINISHIENI DALILI (zote) IKIWA NYINYI NI WATU WA KUFAHAMU. OH! NYINYI MNAWAPENDA (maadui zenu hao), HALI WAO HAWAKUPENDENI! NANYI MNAAMINI VITABU VYOTE (chenu na vyao) NA WANAPOKUTANA NANYI HUSEMA, TUMEAMINI. LAKINI WANAPOKUWA PEKE YAO WANAKUUMIENI VYANDA KWA UCHUNGU (wa kukuchukieni). SEMA: KUFENI KWA UCHUNGU WENU (huo); HAKIKA ALLAH ANAYAJUA (hata) YALIYOMO VIFUANI. IKIKUPATENI KHERI HUWASIKITISHA NA IKIKUPATENI SHARI WANAIFURAHIA. NA KAMA NYINYI MKISUBIRI NA MKAMCHA ALLAH HILA ZAO HAZITAKUDHURUNI KITU. HAKIKA ALLAH ANAYAJUA VIZURI YOTE WANAYOYATENDA”. [3:118-120]
Katika kipindi hiki waumini wakawa na hadhari kuu juu ya mayahudi na ilikuwa hapana budi Bwana Mtume apate fursa ya kuwatahini ukweli wao.
Ili apate kuzifichua dhamira zao katika hali na mazingira haya magumu. Bwana Mtume akaamua kuitumia fursa ya wale watu wawili wa ukoo wa Baniy Aamir waliouawa na swahaba wake Amrou Ibn Umayah.
Akawaendea mayahudi wa Banin-Nadhwiyr kuwaomba msaada katika kulipa fidia ya wauliwa wawili hawa. Na ni vema ikaeleweka kwamba Baniy Aamir ambao waliuliwa watu wao walikuwa ni washirika na ndugu wa yamini wa Banni-Nadhwiyr.
II/. BANINI-NADHWIYR WAFANYA JARIBIO LA KUMUUA MTUME WA ALLAH.
Ibn Is-haq-Allah amrehemu-amesema katika kulielezea jaribio hilo: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka kuwaendea Banin-Nadhwiyr kuwaomba wamsaidie kulipa fidia ya wauliwa wawili hawa wa Baniy Aamir.
Mtume wa Allah aliwaendea kwa mujibu wa mafungamano aliyofunga nao na baina ya Banin-Nadhwiyr na Baniy Aamir kulikuwa na mafungamano na udugu wa yamini. Mtume wa Allah alipowaendea kuwataka msaada, walimwambia:
“Naam, ewe Abul-Qaasim, tutakusaidia ukitakacho katika ombi lako hili kwetu”.
Kisha wakakaa faraghani wao kwa wao wakaambizana:
“Kwa yakini nyinyi hamtaweza tena kumpata mtu huyu katika hali kama hii”.
Na wakati huo Mtume alikuwa amekaa pembezoni mwa kiambaza cha nyumba zao. Wakaendelea kuambizana:
“Basi ni nani atakayepanda juu ya nyumba hii akamuangushia mwamba (jiwe kubwa), akatupumzisha nae?” Amrou Ibn Hijaash akajipasishia jukumu hilo, akasema:
“Mimi ni tayari kwa hilo”.
Akapanda juu ili amuangushie Bwana Mtume mwamba kama alivyoahidi na wakati huo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa amekuja pamoja na kundi la maswahaba wake.
Miongoni mwao alikuwemo Sayyidina Abuu Bakri, Umar na Aliy-Allah awawiye radhi.
Khabari za dhamira mbaya ya watu hawa zikamjia Mtume kutoka mbinguni, akainuka na kuondoka kurudi Madinah.
Maswahaba wake walipomsubiri kwa muda bila ya kurudi, wakaanza kumtafuta. Katika kumtafuta kwao huku wakakutana na mtu ajaye kutoka Madinah wakamuuliza juu ya Bwana Mtume, akawajibu:
“Nimemuona akiingia Madinah. Maswahaba wa Mtume wa Allah wakaenda mpaka alipokuwepo, naye akawapasha khabari za dhamira ya mayahudi kutaka kumuua. Kisha akaamrisha yafanyike maandalizi ya kwenda kupigana nao”.
Hivi ndivyo anavyosema Ibn Is-haq na waandishi wengine wa Sira ya Bwana Mtume hawakutofautiana nae sana.
Kwani wote wamekongamana kwamba Banin-Nadhwiyr walidhamiria kumuua Bwana Mtume katika fursa hii.
Bwana Mtume akazitambua njama zao hizo dhidi yake, akawaonya na kuwaamuru waondoke Madinah wenyewe kwa khiari yao, wakakataa.
Baada ya kugoma kutoka Madinah, ndipo akatangaza vita dhidi yao, akawazingira katika makazi yao kwa siku kadhaa, mpaka akafanikiwa kuwatoa Madinah.
Na hivi ndivyo Ibn Sa’ad anavyolisimulia tukio hilo kwa ukamilifu wake:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawapelekea mjumbe; Muhammad Ibn Maslamah kuwaambia: (Tokeni katika mji wangu, hamtaishi nami humo na ilhali mlikusudia kufanya usaliti. Ninakupeni muda wa siku kumi mtoke kwa khiari zenu wenyewe, atakayeonekana baada ya kumalizika muda huo, itapigwa shingo yake {atauawa}).
Mayahudi wakaendelea kukaa kwa siku kadhaa wakijiandaa, Ibn Ubayyi akawatumia ujumbe akiwaambia:
“Msitoke katika majumba yenu na bakieni katika ngome zenu, kwani mimi ninao jamaa zangu alfu mbili na makabila mengine ya Kiarabu. Wote hawa wataingia pamoja nanyi katika ngome zenu na watapigana pamoja nanyi na kufa mpaka wa mwisho wao. Na Baniy Quraydhwah na washirika wao wa Ghatwfaan watakusaidieni”.
Hubayyu Ibn Akhtwab akayatumai maneno yaliyomo ndani ya ujumbe wa Ibn Ubayyi, akampelekea ujumbe Bwana Mtume akimwambia:
“Kwa hakika sisi hatutakoka majumbani mwetu na wewe fanya utakavyo”. Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akapiga takbira na waislamu wakaipokea takbira yake hiyo na akasema: “Mayahudi wametangaza vita”.
Akawaendea na maswahaba wake, akaswalia Alasiri katika uwanda (mbuga) ya Banin-Nadhwiyr. Na Sayyidina Aliy-Allah amuwiye radhi-akibeba bendera yake na akamtawaza Ibn Ummu Maktuum kukaimu Madinah.
Walipomuona Mtume wa Allah, wakajitoma ngomeni mwao wakiwa na mishale na mawe. Baniy Quraydhwah wakawatupa mkono wasiwasaidie (kama walivyoahidi), na Ibn Ubayyi na washirika wao wa Ghatwfaan wakaacha kuwanusuru.
Hapo wakakata tamaa ya kunusurika, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawazingira na kukata mitende yao.
Wakasema (baada ya kuona kuwa hawana hila): Sisi sasa tunatoka katika mji wako.
(Bwana Mtume) akawaambia:
“Leo siikubali kauli yenu hiyo, lakini tokeni mkiwa na damu zenu na mali inayoweza kubebwa na ngamia ila silaha”.
Mayahudi wakatoka kwa sharti hilo, wakawabeba wanawake, watoto na kujipakia katika ngamia mia sita]. Mwisho wa kunukuu.
Ibn Is-haq-Allah amrehemu-anasema:
“Akawa mtu miongoni mwao akiibomoa nyumba yake na kung’oa kizingiti cha mlango wake na kukipakia juu ya ngamia wake na kuondoka nacho. Wakatoka kuelekea “Khaybar” na wengine wakaelekea Shamu, wakamuachia mali Mtume wa Allah. Mali yote iliyoachwa ikawa ni ya Mtume wa Allah, akawagawia Muhajirina bila ya kuwapa Answari”.
Allah Taala amelisajili tukio hili ndani ya Qur-ani Tukufu, tusome na tuzingatie:
“YEYE NDIYE ALIYEWATOA WALIOKUFURU MIONGONI MWA WATU WA KITABU (Mayahudi wa Kibanin-Nadhwiyr) KATIKA NYUMBA ZAO (huko Madinah) WAKATI WA UHAMISHO (wao) WA KWANZA. HAMKUDHANI YA KUWA WATATOKA (kwa nguvu zao walizokuwa nazo Madinah), NAO WALIDHANI YA KUWA NGOME ZAO ZITAWALINDA NA (kufikwa na amri ya) ALLAH. LAKINI ALLAH ALIWAJIA KWA MAHALI WASIPOPATAZAMIA NA AKATIA WOGA KATIKA NYOYO ZAO (wasiweze kupigana na waislamu walipokuja kupigana nao). WAKAWA WANAZIVUNJA NYUMBA ZAO KWA MIKONO YAO NA KWA MIKONO YA WAISLAMU, BASI ENYI WENYE MACHO (maoni) ZINGATIENI. NA LAU KAMA ALLAH ASINGALI WAANDIKIA UHAMISHO ANGALIWAADHIBU HAPA DUNIANI (adhabu kubwa zaidi kuliko hii), NA KATIKA AKHERA WATAPATA ADHABU YA MOTO. HAYO NI KWA SABABU WALIMKHALIFU ALLAH NA MTUME WAKE. NA ANAYEMKHALIFU ALLAH (Allah humtesa tu), KWANI ALLAH NI MKALI WA KUADHIBU. MTENDE WO WOTE MLIOUKATA (katika hicho kiambo cha Mayahudi) AU MLIOUACHA UMESIMAMA VILE VILE KATIKA MASHINA YAKE. YOTE HAYA NI KWA IDHINI YA ALLAH (hapana lawama juu yenu) NA KWA KUWADHALILISHA WAVUNJAO SHARIA”. [59:1-5]