VITA VYA SWIFFIIN…Inaendelea

Kipindi cha kutoingia vitani kilipo malizika, Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-akamuamuru mpiga mbiu kupiga mbiu (aseme): Enyi watu wa Shamu nyie! Amirul-Muuminina anakuambieni ya kwamba yeye alikupeni muda ili mpate kuichunga haki. Lakini nyinyi bado hamjauacha upotofu/uasi wenu na wala hamjaiitika haki. Na hakika mimi nimesha kutupieni ahadi yenu, hakika Allah hawapendi watu makhaini.

 

Kisha akawausia watu wake, akawaambia: “Msiwapige mpaka wao waanze kukupigeni, kwa kufanya hivyo nyinyi mtakuwa na hoja (ya kuingia vitani) nanyi kuacha kuwapiga hiyo ni hoja nyingine. Na mtakapo washinda, basi msimuue mtimua mbio, msimmalizie majeruhi, msimkashifu mtu (kwa kumvua nguo) na wala msiikate kate maiti. Na mtakapo fika kwenye maskani ya hasimu wenu, basi msivunje heshima na wala msiingie ndani ya nyumba na wala msitwae chochote katika mali zao. Na wala msiamshe hasira za wanawake kwa kuwafanyia kero/maudhi, hata kama watakutusini na kuwasubu viongozi na watu wema wenu, kwani wao ni madhaifu wa nguvu na nafsi”.

Halafu akalipanga na kuliweka tayari jeshi lake na akawasimika maamiri jeshi. Na Muawiyah naye akafanya kama hivyo kwa jeshi lake. Mapigano yakaanza siku ya Jumanne, mwezi mosi Swafar (Mfunguo tano). Kikatoka kikosi vita cha watu wa Iraq, kadhaalika kikatoka kikosi cha watu wa Shaam, vikapambana mchana kutwa. Na hali ikawa kama hiyo katika siku zilizo fuatia, hata ilipo ingia jioni ya siku ya Jumanne, mwezi 8 Swafar, Imamu Aliy-Allah amuwiye radhi-akawakhutubia wafuasi wake. Akaanza kwa kumuhimidi Allah na kumsifia, akasema: “Sifa zote njema ni milki na stahiki yake Allah, ambaye halifungwi alilo litengua Yeye na alilo lifunga hawawezi kulitengua watenguaji. Na lau angeli taka Allah, basi wasingeli khitalifiana wawili katika viumbe wake na wala umma usingeli tofautiana katika jambo lolote. Na wala aliye zidiwa kwa ubora asingeli upinga/ukanusha ubora wa aliye bora (kuliko yeye). Nasi sote na watu hawa tumeswagwa na kadari (kuingia vitani). Basi sisi tuko kwenye uoni na usikivu wa Mola wetu Mlezi na lau atataka ataiharakisha fitina. Na kutokana na kuharakishwa huko yakapatikana mabadiliko yatakayo uonyesha uwongo wa aliye dhaalimu na ikajulikana haki inako elekea. Lakini (Yeye Mola wetu Mlezi) ameifanya Dunia kuwa ni nyumba (uwanja) ya amali (matendo) na Akhera kuwa ndio nyumba ya makaazi ya milele. Amefanya hivyo ili apate kuwalipa waovu kwa yale waliyo yatenda na apate kuwalipa mema mazuri wale walio tenda mema. Ehee fahamuni! Hakika nyinyi mtakutana na watu hao kesho, basi usiku wa leo refusheni kisimamo cha usiku (swalini sana swala za usiku) na kithirisheni kusoma Qur-ani. Na muombeni Allah (akupeni) nusra na subira na kutaneni nao kwa azma na kupania na kuweni wakweli”.

Na Sayyidna Aliy-Allah amuwiye radhi-akakata shauri kukutana na jeshi la Muawiyah wakati wa jioni. Siku ya Al-Khamis, mwezi 10 Swafar (Mfunguo tano), hakika kisago cha vita kilizunguka kwa nguvu baina ya makundi mawili. Na katika kitimtim hicho ukadhihiri ufasaha wa watu walio fasaha na umahiri wa kusema wa watu mahiri wa kusema. Na kila mmoja akijiona kuwa yeye yuko katika twaa ya Allah, basi akawa mmoja wao anapo kiona kipote kilicho choshwa na vita, hukirushia makombora ya ulimi wake kikarejea tena katika mori na hamasa yake. Bwana Al-Ashtar bin Al-Haarith alikuwa na ushawishi mkubwa, yeye aliendelea kusonga mbele na watu wake mpaka akamkaribia Muawiyah. Na baada ya fitina ile Muawiyah alikuwa akisema nilikuwa nakaribia kushindwa, basi nikayakumbuka mashairi ya hamasa ya Ibn Al-Itwnaabah. Mashairi hayo yakanihamasisha na hivyo kunizuia kukimbia. Akazungukwa na majeshi ya Shaamu, nyoyo zao zikaingiwa na mori na wala kuingia kwa usiku hakukuwazuia kupigana. Wakaendelea na hali hiyo ya mapambano katika usiku zinazo hesabika na kuchukuliwa katika Tarekh (Historia) ya Uislamu, kuwa ni usiku wa kiza, ulio utia kiza Uislamu. Wakapambazukiwa na ilhali ukimwa na uchovu ukiwa dhaahiri katika jeshi la Shaamu.

[TAARIKHUT-TWABARIY 02/82]

Leave a Reply

Your email address will not be published.