MAKURAISHI WATOFAUTIANA

Makurayshi kwa upande wao walitoka wakubwa na watukufu wao takriban wote katika mandhari inayoonyesha ubabe na mbwembwe nyingi.

Mandhari inayoieleza wazi azma yao ya kumsagasaga Mtume na maswahaba wake. Watu ambao wamejaribu kuonyesha upinzani dhidi yao na kuthubutu kufanya jaribio la kuteka msafara wao wa biashara.

Makurayshi walitaka kuwaonyesha na kuwahakikishia waislamu kwamba wao ni watukufu wasiodhalilishwa. Wao ndio wazalendo na watumishi wa nyumba tukufu ya Allah (Al-Ka’abah). Qur-ani Tukufu inakielezea kiburi na jeuri hii ya Makurayshi:

“NA (kumbukeni) SHETANI ALIPOWAPAMBIA VITENDO VYAO (wale makafiri) NA KUSEMA: LEO HAKUNA WATU WA KUKUSHINDENI, NA MIMI NI MLINZI WENU…” [8:48]

Wakatoka Makurayshi wakijienzi kwa nguvu na wingi wao, huku wakijivunia utukufu waliokuwa nao baina ya makabila ya Kiarabu.

Wakiitakidi na kuamini kwamba wanakwenda kutoa pigo moja takatifu litakalouacha uislamu na waislamu wakisambaratika.

Kama kwamba hali yao hii ni ulimi unaosema kama alivyosema Firauni kuwaambia watu wa Nabii Musa:

“HAKIKA HAWA (Mayahudi) NI KIKOSI KIDOGO. NAO WANATUKASIRISHA (wanatuudhi) NA SISI NI WENGI NA (juu ya hivi) TUNAWAOGOPA”. [26:54-56]

Pamoja na khofu ya kukutana na waislamu mapambanoni iliyozitambaa nyoyo zao, bado walijipa ujasiri na ushujaa wakatoka.

Abuu Sufyaan alipofanikiwa kuunusuru msafara wao usiingie mikononi mwa waislamu, aliwapelekea khabari hizo za furaha.

Wengi miongoni mwao walipopata khabari hizi hawakupenda kuendelea mbele kwa lengo la vita.

Kwa kuwa sababu ya vita ilikuwa ni kuuhami msafara na sasa haipo tena. Kundi hili kubwa likaazimia kurudi Makkah, lakini Abuu Jahli aliyekuwa miongoni mwa watukufu na mabwana wakubwa hakukubali.

Yeye alionelea kwamba kitendo cha kurudi bila ya kupigana na ilhali walitoka kwa ajili hiyo, kitapunguza nguvu, haiba na utisho wao baina ya makabila mengine ya Kiarabu kwa kuwa wataonekana waoga.

Na isitoshe kitendo hiki mbali ya kuwa ni cha kioga, kwa mtazamo wake kitawatia waislamu tamaa kwamba wanaogopwa na kumbe wanaweza kupambana nao.

Akaanza kuwapigia kelele wenzake akisema: Wallah, haturudi Makkah mpaka tufike Badri na kukaa hapo siku tatu.

Tuchinje ngamia, tule na kunywa pombe huku vimwana walimbwende wakituburudisha kwa muziki laini na mororo.

Hapo ndipo waarabu watakapopata khabari yetu na kuwafanya waendelee kutuogopa milele”. Akaanza kuwahimiza na kuwahamasisha watu waendelee kwenda wasirudi nyuma.

Hapo ndipo Makurayshi walipotofautiana na kugawika makundi mawili. Kundi moja liliona kwamba sababu ya kutoka ilikuwa ni kuuhami na kuukoa msafara wao wa biashara.

Msafara umeshanusurika, sasa kuna mantiki gani kuendelea kwenda? Kundi jingine likawa na msimamo kama ule wa Abuu Jahli, likisisitiza kuwa kwenda ni muhimu ili waarabu wasipate fursa ya kuwakejeli kwa uoga.

Katika kundi lile la mwanzo; lenye msimamo baridi wa kurudi zilikuwemo koo za Baniy Adiy na Baniy Zuhrah, hawa wakaamua kurejea Makkah.

Kwa kurejea kwao, idadi ya makurayshi ikawa imepungua sana. Ukiwaondoa hawa, wengine wote waliobakia waliamua kundelea kwenda Badri chini ya ushawishi na msukumo wa Abuu Jahli na kundi lake.

Wakaenda wakipiga kambi njiani, wakichinja ngamia, wakila na kuwalisha chakula na kunywa na kuwanywesha pombe wenyeji wa mahala wanapopiga kambi.

Wakaimba na kucheza kwa furaha huku wakijitangaza na kujinadi kwa nguvu na ushujaa wao mpaka wakafika katika bonde la Badri. Wakapiga kambi katika eneo la bonde lilio mbali kwa kutokea Madinah na linaloelekea Makkah.

 

IMANI YA KWELI NDIO SABABU KUU YA USHINDI NA NUSRA.

 

Hivi ndivyo Allah Mola Mwenyezi alivyoyakutanisha makundi mawili haya katika bonde la Badri. Kundi la waislamu likiwa limepiga kambi kando ya bonde lililo karibu na Madinah na makafiri (Makurayshi) wakipiga kambi kando ya bonde lililo mbali linaloelekea Makkah.

Ama msafara ambao ndio sababu ya kutoka kwa makundi mawili haya, Abuu Sufyaan aliambaambaa nao ufukweni mwa bahari na akafanikiwa kuuokoa.

Kibinadamu kuokoka kwa msafara huu ilikuwa ni sababu tosha ya kuwafanya waislamu na makafiri kurudi nyuma kwa kuwa walilolitokea lilikuwa halipo tena.

Lakini mipango ya Allah iko juu ya mipango ya wanadamu na matashi yake yako juu ya matashi ya viumbe.

Allah aliye na hekima na busara ya juu kwa kila alipangalo na kulitaka, aliyakutanisha majeshi mawili haya bila ya miadi kama ilivyokuwa imezoeleka.

Akapanga baina yao sababu za kukutana pamoja na uchache na maandalizi dhaifu ya waislamu na wingi wa idadi na maandalizi makubwa na ya kutosha ya washirikina.

Allah Mola Mwenye hekima aliyafanya yote haya ili mkutano na mpambano huu wa ajabu ambao dalili na ishara za wazi za ushindi zilikuwa upande wa mushrikina.

Na kwa upande wa waumini kulikuwa na alama zote za kushindwa. Akayapambanisha majeshi mawili haya ili mpambano huu uwe ni darsa itakayofundisha kwamba wingi wa idadi, maandalizi makubwa na ya kutisha ya jeshi lenye kuambatana na propaganda.

Vyote hivi si ndio sababu ya kweli ya ushindi na nusra. Bali hivi vikitumika vema huweza kutoa msaada wa ushindi. Sababu za kweli za ushindi ni pamoja na:-

Itikadi safi isiyo na nafasi ya shirki.

Imani ya nguvu/imara kuielekea itikadi hiyo.

Subira njema isiyochoka juu ya itikadi hiyo.

Jihadi ya kweli katika kuipigania itikadi hiyo.

Yakikusanyika yote haya kwa watu hapana shaka watu hao (waumini) watashinda tu kwa idhini ya Allah (wanayemuamini) pamoja na uchache wao na zana zao duni na wingi wa makafiri na zana zao bora. Kuhusiana na ukweli huu Allah anatuambia:

“…MAKUNDI MANGAPI MADOGO YAMESHINDA MAKUNDI MAKUBWA KWA IDHINI YA ALLAH. NA ALLAH YU PAMOJA NA WAFANYAO SUBIRA”. [2:249]

“…NA MSAADA (ushindi) HAUTOKI (kwa mwingine yo yote) ISIPOKUWA KWA ALLAH, MWENYE NGUVU NA MWENYE HEKIMA”. [3:126]

Hekima ya Allah kuyakutanisha majeshi mawili haya; jeshi lenye nguvu ya zana na watu (makafiri) na jeshi lenye nguvu ya imani (waislamu).

Ilifanana sana na ile hekima ya kuwakutanisha watu wa Nabii Musa na jeshi kubwa la Firauni, tusome:

“NA TUKATAKA KUWAFANYIA IHSANI WALE WALIODHOOFISHWA KATIKA ARDHI HIYO NA KUWAFANYA VIONGOZI, NA KUWAFANYA WARITHI (wa neema hizo). NA KUWAPA NGUVU ARDHINI; NA KUMUONYESHA FIRAUNI NA HAMANA NA MAJESHI YAO, YALE WALIYOKUWA WAKIYAOGOPA”. [28:5-6]

Sayyid Qutbu-Allah amrehemu-katika tafsiri yake iitwayo “Fiy Dhwilaalil-Qur-aani” ana haya ya kusema kuhusiana na mpambano huu:

“Allah alitaka vita vipiganwe katika mazingira kama haya, navyo ni vita vya baina ya wingi umshirikishao Allah na uchache wenye imani (ya Mungu mmoja).

Ili viwe ni upambanuzi baina ya taswira na mitazamo miwili ya sababu za ushindi na ushindwa. Na ili nguvu ya itikadi (imani) iushinde wingi wa nguvu za ushirikina na utayarifu wake.

Hapo ndipo itawabainikia watu ya kwamba nusra (ushindi) ni wa itikadi njema, safi na imara na si wa silaha na utayarifu (maandalizi).

Na kwamba imewapasa watu wenye itikadi sahihi kupigana jihadi na kuingia katika uwanja wa vita bila ya kusubiri kulingana sawa kwa nguvu za kimaada za kidhahiria.

Kwani wao wanaimiliki nguvu nyingine yenye uzito wake katika mizani, hiyo ndio nguvu ya haki. Na kwamba haya si maneno tu ya mdomo bali yametokea na kuonekana na macho”.

Hii ndio sababu ya kauli ya Allah alipowaambia waumini kuhusiana na vita hivi:

“ENYI MLIOAMINI! MKUTANAPO VITANI NA WALE WALIOKUFURU BASI MSIWAGEUZIE MIGONGO (mkakimbia). NA ATAKAYEWAGEUZIA MGONGO WAKE SIKU HIYO ISIPOKUWA AMEGEUKA KWA KUSHAMBULIA AU AMEGEUKA AKAUNGANE NA SEHEMU NYINGINE ZA JESHI HILI LA WAISLAMU-(ikiwa si hivyo) ATASTAHIKI GHADHABU YA ALLAH, NA MAHALA PAKE NI JAHANAMU NAPO NI MAHALA PABAYA PA KURUDIA (mtu). HAMKUWAUWA NYINYI LAKINI ALLAH NDIYE ALIYEWAUWA; NA HUKUTUPA WEWE (Mtume ule mchanga wa katika gao la mkono wako) ULIOTUPA (ukawaingia wote machoni mwao, hukufanya wewe haya) WALAKINI ALLAH NDIYE ALIYEUTUPA (yaani ndiye aliyeufikisha katika macho yao wote yakawa yanawawasha kuliko pilipili, wakenda mbio). ALIFANYA HAYA ALLAH ILI AWAPE WALIOAMINI HIDAYA NZURI ITOKAYO KWAKE. HAKIKA ALLAH NDIYE ASIKIAYE NA AJUAYE. BASI HAYA (mumefanyiwa safari hii) NA HAKIKA ALLAH ATAZIDHOOOFISHA NGUVU ZA MAKAFIRI (atazivunja)”. [8:15-18]

Baada ya kwisha kuzungumza na waumini, Allah akawageukia washirikina na kuwaambia:

“KAMA (nyinyi Makurayshi) MNATAKA HUKUMU (ya kupambana baina ya haki na batili) BASI HUKUMU IMEKWISHA KUFIKIENI (mumeona kuwa nyinyi ndio mlio katika batili, mmeshindwa na chembe ya watu). NA KAMA MKIJIZUIA (na kupigana na Waislamu) BASI ITAKUWA BORA KWENU. NA KAMA MTARUDIA (kupigana nao) SISI PIA TUTARUDIA (kuwatia nguvu wakushindeni). NA WATU WENU HAWATAKUFAENI CHO CHOTE HATA WAKIWA WENGI NA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOAMINI”. [8:19]

Kisha akazungumza na Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie:

“ (Kumbuka) ALLAH ALIPOKUONYESHA KATIKA USINGIZI WAKO (kwamba wao makafiri) NI WACHACHE (mkapata nyoyo za kukabiliana nao). NA KAMA ANGALIKUONYESHA KUWA WAO NI WENGI MNGALIVUNJIKA NYOYO NA MNGALIZOZANA KATIKA JAMBO HILO (kuwa tupigane nao au tusipigane nao). LAKINI ALLAH AKAKULINDENI (na hayo) BILA SHAKA YEYE NI MJUZI WA YALIYOMO VIFUANI (seuze yaliyo dhahiri). NA (kumbukeni) ALIPOKUONYESHENI MACHONI MWENU MLIPOKUTANA KWAMBA WAO NI WACHACHE (ili mjasirishe kupigana nao); NA AKAKUFANYENI NYINYI KUWA WACHACHE (mno kabisa) MACHONI MWAO (waone upuuzi kupigana kwa hima na watu wachache kama nyinyi. Allah amefanya hivyo) ILI ALITIMIZE JAMBO ALILOAMRISHA LITENDEKE NA MAMBO YOTE HUREJESHWA KWA ALLAH”. [8:43-44]

Zimesheheni tele ndani ya Qur-ani Tukufu aya zinazoubainisha ukweli huu, ambazo mara nyingi watu hushindwa kuzifahamu vema.

Mara nyingi hudhahiria wa mambo na uhalisia wa hali huwafanya wazisahau aya kama hizi. Uhalisia wa mambo hauko kama ulivyo katika udhahiria wake.

Hali/mambo hayawi kama wanavyoyasawirisha watu wakati unapowakhadaa wingi wa jeshi la batili na maandalizi yake makubwa sambamba na zana bora walizonazo.

Basi wakaitakidi kwamba ushindi u pamoja na wingi na haki i pamoja na wengi.

Wakatatizika kiasi cha kusahau kwamba nguvu ni ya haki wajapochacheka watu wake (hata kama ni wachache). Hii ni kwa sababu daima Allah yu pamoja na haki:

“…NA ALLAH NDIYE MWENYE KUSHINDA JUU YA JAMBO LAKE (alitakalo, lazima liwe) LAKINI WATU WENGI HAWAJUI”. [12:21]

 

MAKURAISHI WATOFAUTIANA

Makurayshi kwa upande wao walitoka wakubwa na watukufu wao takriban wote katika mandhari inayoonyesha ubabe na mbwembwe nyingi.

Mandhari inayoieleza wazi azma yao ya kumsagasaga Mtume na maswahaba wake. Watu ambao wamejaribu kuonyesha upinzani dhidi yao na kuthubutu kufanya jaribio la kuteka msafara wao wa biashara.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *