Waislamu wakaifanya kazi ya uchimbaji wa handaki mpaka waka ikamilisha kwa ufanisi mkubwa.
Wakalipanua, wakaliendesha kina mpaka likafikia mahala pa kumshinda farasi aliye hodari kulivuka.
Wakaweka kizuizi imara na mawe katika njia ielekeayo Madinah ili viwe ni kingamizi baina yao na adui yao na viwasaidie katika kupambana na adui pindi itakapojitokeza haja ya kufanya hivyo.
Wakaupachanisha mji wa Madinah kwa majengo, wanawake na watoto wakawekwa katika ngome.
Baada ya kuyafanya yote hayo ndipo Mtume na maswahaba wake wakapiga kambi kwenye sehemu ya chini ya mlima, migongo yao ikilielekea jabali.
Huku wakimuelekea adui kwa nyuso zao kutokea upande wa handaki na katikati yao kukiwa na ardhi yenye majimaji ya chumvi.
Waislamu walikuwa ni alfu tatu; wapiganaji wapanda farasi miongoni mwao wakiwa ni thelathini na sita tu, hii ikimaanisha kuwa wengine wote waliosalia ni askari wa miguu.
Wakati bado Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akiwa amefa dhaishwa na suala la handaki, kikajitokeza kikosi cha mwanzo cha jeshi shirika kikija Madinah kutokea upande wa Uhud.
Walipokaribia milango ya kuingilia Madinah, tahamaki hilo ni handaki kubwa mbele yao limeizuilia njia yao wasiweze kusonga mbele.
Hili likawa ni jambo la ghafla mno kwao, ambalo hawakulitarajia kabisa mpaka wakaambizana: Hiki ni kitimbi ambacho Waarabu hawakuwahi kukitumia. Handaki hili likayalazimisha majeshi shirika kusimama mbele ya kizuizi hiki cha ajabu.
Wakasita kidogo hapo ili kulitafakari hilo na kupanga upya mikakati yao. Makureishi, Wahabeshi na washirika wao wa Kinaanah na Tihaamah wakapiga kambi katika makutano ya mumbwi (torrential stream) mkabala na handaki.
Ghatwfaani na washirika wao katika makabila ya Najid wakapiga kambi katika eneo lililojulikana kama “Dhanabu Naqamaa”, kwa upande wa Uhud.
Wakawaachilia ngamia na farasi wao kula katika mashamba ya Madinah kwa lengo la kuwadhoofisha waislamu kiuchumi.
Lakini wapi, watu tayari walikuwa wameshavuna mazao yao mwezi mmoja kabla ya kuja kwa Ahzaabu.
Vikosi vya majeshi shirika vyasimama muda mrefu mbele ya handaki vikiizengea fursa ya kulivaa na kuvukia ng’ambo ya pili:
Vikosi vya majeshi shirika vikasimama mbele ya handaki vikiwa vimehemewa visijue nini cha kufanya.
Vilikuja na dhana kuwa vita hiyo itachukua siku moja tu au chini ya hapo, haitakuwa ila makundi haya ya muungano yatamzunguka Muhammad na maswahaba wake na kuwateketeza mara moja tu.
Kisha warejee makwao wakiwa na ngawira maridhawa huku wakiwa wameufyekelea mbali mzizi wa fitina ya dini hii mpya.
Dini iliyoteteresha hali yao ya amani, ikawagawa na kuyachafua mapokeo ya wahenga wao. Lakini ikaja kuwabainikia kuwa vita hii haitakuwa nyepesi kama walivyofikiria mwanzo na kwamba itawalazimu kusimama mbele ya handaki hili kwa muda mrefu kabla ya kupata njia na mbinu ya kulivuka.
Kama hivi makundi mawili haya; waislamu kwa upande mmoja na majeshi shirika kwa upande wa pili yakawa ana kwa ana mbele ya handaki.
Waislamu wakiwa wachache wenye silaha duni na mushrikina wakiwa katika muungano wao na maandalizi kabambe ya kutisha.
Lakini eeh tofauti iliyoje baina ya nguvu shikamana yenye imani na lengo moja na baina ya watu tapanyi wasio na lengo moja linaloziunganisha pamoja nyoyo zao!
Ama kwa upande wa kimaada majeshi shirika yalikuwa na wingi wa watu na zana, lakini havikuwepo viunganishi vinavyowapelekea kuwa na ikhlaswi na kusaidiana katika mapambano.
Mwanzoni ilionekana kuwa Abu Sufyaani ndiye kamanda na amiri jeshi mkuu wa majeshi shirika kwa jina si hakika.
Hii ni kwa sababu kila kundi lililotoka lilikuwa chini ya uongozi ambao linaona kuwa unafaa kuwaongoza na kwamba ndio unaostahiki kuyaongoza makundi mengine yote.
Majeshi mawili haya yakakaa siku kadhaa huku kila moja likizichunguza kwa makini nyendo za mwenzake na majeshi shirika yakilizunguka handaki mchana kutwa na usiku kucha.
Yalifanya hivyo yakitarajia kuwa huenda yakapata upenyo utakaowavusha ng’ambo ya pili au wakaitumia fursa ya kughafilika kwa waislamu kuvuka. Lakini wapi waislamu nao walikuwa hadhiri wakihakikisha kuwa hawatoi hata chembe ya mwanya itakayompatia ushindi adui yao.
Kila kilipojaribu kikundi cha adui kulijongelea handaki walikinyeshea mvua ya mishale na mawe na kukilazimisha kurejea kinyumenyume kule kilipotokea.
Muhammad Ibn Maslamah anasimulia:
“Usiku wetu katika handaki ulikuwa ni mchana na mushrikina wao walikuwa wakishikiana zamu. Siku moja akidamka Abu Sufyaan na kundi lake kujaribu kuvuka handaki. Siku nyingine akidamka Khaleed Ibn Al-Waleed, siku nyingine Amrou Ibn Al-Aaswi, siku nyingine Hubayrah Ibn Ubayyi, siku nyingine Ikrimah Ibn Abu Jahli na siku nyingine Dhwiraari Ibn Al-Katwaab. Majaribio haya yakaendelea mpaka balaa likawa kubwa na khofu kuu ikazitambaa nyoyo za waislamu. Walipokuwa wakidamka waliwatanguliza mbele yao warusha mishale, wakavurumisha mvua ya mishale kuelekea kwa Mtume kwa kitambo. Wakati wote huo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa juu ya farasi wake akiwaelekeza maswahaba wake namna ya kujibu mashambulizi hayo ya nguvu”