Wakimbizi wa haki “Muhajirina” walipofika Madinah kwa mara ya kwanza, walisumbuliwa na hali ya hewa ya uhamishoni.
Hali hii ya hewa iliyotofautiana kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa ya kwao ilipelekea wengi wao kupatwa na homa za mara kwa mara.
Homa hizi zilisbabisha kuathirika na kutetereka kwa afya zao ambako kuliwaathiri kisaikolojia pia.
Wakaanza kuukumbuka mji wao waliozaliwa na kuishi hapo na kuizoea hali yake ya hewa na maisha yake.
Fikra na kumbukizi hizi ziikawatumbukiza katika dimbwi la utungaji na uimbaji wa mashairi ya kuusifia mji wao waliolazimika kuuhama kwa ajili tu ya Imani yao.
Walifanya hivi kwa lengo la kujiliwaza kutokana na maisha haya ya ugenini waliyomo na hali hii ya hewa inayowasumbua.
Hali ilipozidi na kuwafanya Muhajirina hawa kusindwa kustahamili, walimwendea Bwana Mtume kumshitakia hali yao hiyo.
Nae Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie akawa hana la kufanya ila kumuelekea Mola wake, akaomba:
“Ewe Mola wa haki wee! Tupendezeshee sisi Madinah kama ulivyotupendezeshea Makkah na zaidi. Na utubarikie katika vibaba na pishi zake, na uyahamishie maradhi yake juhfah.”
Mwenyezi Mungu Mtukufu akajibu dua ya Mtume wake, hali ya hewa ya Madinah ikawa nzuri na waislamu wakaupenda mno mji wa Madinah na wakaishi humo kwa amani na furaha.
iii/. UJENZI WA MSIKITI WA MTUME.
Mahala alipokita magoti ngamia wa Mtume wakati anaingia mjini Madinah palikuwa ni uwanja unaomilikiwa na vijana wawili yatima.
Uwanja huu ndio aliouchagua Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie kuwa ndio mahala pa kuujenga misikiti wake.
Mahala hapa lilikuwa ndio chaguyo la Mtume kutokana na ilhamu ya Mola wake. Mahala hapa palikuwa ni uwanja mpana uliokuwa ukitumika kama maanikio/makaushio ya tende baada ya kuvunwa.
Katika uwanja huu kulikuwepo na baadhi yta miti ya mitende na miti mingine. Pia yalikuwepo baadhi ya makaburi ya zamani ya mushrikina yaliyokuwa hayatumiki tena na mashimo machache yaliyokuwa madimbwi ya maji.
Mtume aliumiliki uwanja huu kwa kuununua kwa wamiliki wake wa mwanzo ambao walikuwa ni vijana wale yatima, japokuwa wao walikuwa radhi kumpa bura, lakini yeye hakuridhia ila kuununua.
Baada ya kuumiliki uwanja ule kihalali, ndipo shughuli nzima ya Ujenzi wa msikiti ilipoanza. Mtume akaamrisha miti yote iliyokuwepo ikatwe, makaburi yote yafukulwe na mifupa itakayotolewa ikazikwe sehemu nyingine na mashimo yote ya maji yafukiwe na ardhi isawazishwe.
Baada ya kutekelezwa yote haya ndipo Mtume akaianza kazi ya Ujenzi wa msikiti wake. Huu ulikuwa ni msikiti wa kawaida kabisa, haukuwa na sura ya misikiti yetu ya leo. Kimo chake kilikuwa ni dhiraa 35 na upana dhiraa 30.
Ukuta uliolizunguka jingo urefu wake haukuzidi kimo cha mtu mzima wastani wa kimo kusimama na kunyoosha mkono.
Msingi wake ulikuwa ni wa mawe, kuta zake ziliundwa na matofali ya udongo. Msikiti ulikuwa na milango mitatu, mmoja upande wa mashariki na mwingine upande wa magharibi na ule uliokuwa nyuma upande wa kusini.
Katika upande huu wa nyuma kulishushwa kipaa cha makuti ya mitende kikiegemea magogo ya mitende.
Sehemu hii ya msikiti ilijulikana kama “Swufah” ndipo palipokuwa makazi ya maswahaba mafakiri, wakitunzwa na kuhudumiwa na mwenyewe Bwana Mtume.
Wale wote waliokuwa wakiishi mahala hapa walijulikana kama “Ahlus swufah” na miongoni mwao akiwa ni mpokezi mkubwa wa hadithi Bwana Abuu Hurayrah Allah awawiye radhi wote.
Ama sehemu nuyinine ya msikiti ukiiondoa hii iliwachwa wazi bila ya kuezekwa. Sakafu ya msikiti ikabakia kuwa ni ardhi kama ilivyo bila ya kuitandikwa cho chote.
Sakafu ailibakia hivyo hivyo mpaka iliponyeesha mvua usiku mmoja, ardhi ikawa imelowa na kuwa tope.
Hapo ndipo ikawa kila ajae anafuangasha vijikokoto kadhaa katika nguo yake, akavitandika na kuswali juu yake. Mtume rehema na Amani zimshukie alipomaliza kuswali akasema “Eeh, uzuri ulioje wa busati/tandiko hilo!”
Mtume Rehema na amani zimshukie alishirikiana bega kwa bega na maswahaba wake katika shughuli nzima ya ujenzi wa msikiti huu. Alikuwa akibeba mawe na matofali mpaka kifua chake kikatapakaa vumbi. Jambo hili likazidi kuwashajiisha maswahaba kufanya kazi kwa nguvu zao zote, huku wakijikuta wakiimba ubeti huu wa shairi:
Na iwapo tutakaa na il-hali Mtume afanya kazi,
Hicho kwetu ni kitendo cha upotevu.
Pamoja na kuwa maswahaba walimsihi sana Bwana Mtume awaachie wao wamtoshee katika kazi hiyo, lakini yeye hakuona raha ila awe mmoja wao.
Akifanya kazi sawa na wao na akiimba kama waimbavyo. Mmoja wa maswahaba wake akakutana nae akiwa amebeba jiwe thaqili (zito), akamwambia: Nipe mimi ewe Mtume wa Allah. Akikusudia kumsaidia, Mtume akamwambaia:
“Nenda kachuke jingine, wewe sio fakiri zaidi kwa Allaha kuliko mimi.” Watu wote, waliifanya kazi hii kwa ukunjufu wa nyoyo na vifua, huku wakiimba beti mbalimbali za mashairi kuashiria furaha yao kwa kazi hii tukufu ambayo waliijua vema thamani na kima chake. Miongoni mwa beti zilizoimbwa ni huu.
Ewe Mola hapana kheri kama kheri ya akhera,
Basi warehemu Answaari na Muhajirina.
Ujenzi ulipokamilika, Mtume akaufanya msikiti kuwa ni:-
· Kituo cha mikutano, akikutana humo na maswahaba kujadili na hatimaye kutoa maamuzi ya pamoja juu ya masuala mbalimbali.
· Jengo la ibada, akiwaongoza kaswahaba katika ibada mama; swala na kutoa humo khutuba za Ijumaa na za kadhia mbalimbali zilizokuwa zikijitokeza.
· Chuo/shule ya kutoa taaluma ya dini. Akiwafundisha humo maswahaba masuala yote yahusianayo na dini yao kama mfumo mzima wa maisha.
· Mahakama, Akitoa humo hukumu mbalimbali kwa kesi zilizoletwa mbele yake.
· Kituo cha misaada, akiwalea na kuwahudumia humo maswahaba masikini.
· Idhaa, habari yo yote iliyowahusu waislamu ahitangaza humo kwa sababu msikiti ndio uliokuwa mahala pekee panapoweza kuwakusanya watu wote kwa wakati mmoja kwa hivyo kuwezesha ujumbe kufika kwa walengwa kwa haraka na wepesi.
· Kambi ya jeshi, maandalizi yote ya jeshi la kiislamu, jeshi la haki lililoligania dhidi ya batili aliyafanya humo.
· Huo ndio ulikuwa msikiti wa Mtume na hizo ni baadhi tu ya kazi ngingi zilizofanywa na msikiti huo kama kituo cha kijamii
Mtume Rehema na Amani zimshukie alipokuwa akiwahutubia maswahaba ndani ya msikiti wake huu alikhutubu akiwa ameswimama akijiegemeza kwenye kigogogo cha mtende Mtume aliendelea kukhutubu katika hali hiyo mpaka alipokuwa na umri mkubwa na hivyo kushindwa kusimama muda mrefu.
Hapo ndipo maswahaba wakamtengeneea mimbari nyepesi ya mbao na ya kawaida kabisa isiyo na mapambo ya aina yo yot ile.
Mimbari hii ilikuwa na vidato viwili na sehemu ya kuakalia ambapo Mtume alikaa mpaka anapotaka kuanza kukhutubu ndipo husimama chini ya vile vidato viwili na akaanza kukhutubu.
Msikiti huu haukuwa na taa zinazonurisha wakati wa usiku, giza linaposhitadi walikuwa wakileta kuni na kuwasha moto ambao uliwaangazia mpaka wakamaliza swala yao.
Waliendelea na hali hii ya kuswali kisa bila ya taa mpaka pale alipowajia Bwana Tamiym Addaariy akitokea shamu.
Huyu ndiye mtu wa kwanza aliyewasha taa na kuzitundika katika nguzo za vigogo vya mitende zilizokuwemo msikitini humo.
Kitendo hiki kilimfurahisha sana Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie, na akamwambia “Umeutia nuru msikiti wetu, Allah akunawirishia nawe.”
Msikiti huu uliendela kubakia na hali yake hii bila ya mabadiliko yoyote zaidi ya kupanuliwa kidogo tu. Mtume aliufanya upanuzi huu kutokana na ongezeka kwa idadi ya waislamu Madinah na msikiti kushindwa kukidhi haja. Upanuzi huu ulifanyika katika mwaka wa saba wa Hijrah.
Makazi ya Mtume.
Baada ya Ujenzi wa msikiti kukamilika ndipo Bwana Mtume akaanza ujenzi wa makazi yake akaanza kwa kujenga vyumba viwili pembezoni mwa msikiti, kimoja kikiwa ni cha mkewe Bi Saudah Bint Zam-ah na kingine kilikuwa ni cha Bi Aysha Bint Abuu Bakri. Mtume akaendelea kuyaongeza makazi yake kidogo kidogo kila alipooa mke mwingine mpaka idadi ya vyumba vyake ikafikia tisa sawa na idadi ya wake hao, Allah awawiye radhi wote.
Baadhi ya vyumba hivi vilikuwa upande wa kusini mwa msikiti na vingine upande ule wa mashariki. Makazi haya ya Bwana Mtume yalikuwa katika hali ya kawaida kabisa inayolingana na maisha ya watu wa tabaka la chini.