WAISLAMU WALISAMBARATIKA NA KILA MMOJA ALISHUGHULIKA NA YA KWAKE

Na tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu katika safu za waislamu, yaliyofichuliwa na kushindwa katika vita hivi. Ni kwamba adui alipowazingira na kuwaweka kati, hawakuungana na kushikamana pamoja.

Bali walitapanyika kila upande kutokana na kizaizai kilichowakumba pasipo kutarajia. Hata yasemekana kwamba baadhi yao walitimua mbio mpaka Madinah, lakini wakashindwa kuingia kutokana na kuona haya.

Suala la kila mtu kutaka kuiokoa nafsi yake likawashughulisha mpaka wakamsahau Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Wakamuacha pekee katika uwanja wa vita akipatwa na jeuri  na kushukiwa na nguvu ya adui aliye na uchu wa kumfyekelea mbali.

Wakamuacha Bwana Mtume na pote la watu wachache mno ambao wasingemtosheleza kwa cho chote lau si kupata ulinzi wa Allah.

Katika kimtim hiki ambacho jeshi liliwajibika kumzunguka kamanda na jemadari wao ndipo jeshi likamkimbia na kumuacha, kila mmoja akitafuta kuiponya nafsi yake.

Ni jambo la kushangaza mno waislamu kumsahau Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika mshindo huu mkuu uliokurubia kuyagharimu maisha yake matukufu.

Wanamuacha pamoja na kupaaza kwake sauti kuwaita, lakini wapi hao wanaendelea kukimbia mithili ya watu walio katika mashindano ya mbio.

Hivi ndivyo Allah anavyoielezea hali ilivyokuwa:

“(Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIKIMBIA MBIO, WALA NYINYI HAMUMSIKILIZI YO YOTE, HALI MTUME ALIKUWA ANAKUITENI, YUKO NYUMA YENU…” [3:153

] Katika ibara hii fupi, Qur-ani Tukufu inawachorea waumini mandhari kamili ya kukimbia inayosawirisha “harakati hisia sambamba na harakati nafsi”.

Kosa na kunguwao hili lililofanywa na waislamu ni katika jumla ya makosa ya udhaifu yaliyowapitikia waislamu katika kipindi hiki kigumu na kizito.

 Allah Mola Mwenyezi akataka kuwafichulia waislamu kosa hili ili walione na waihisi na kuionja athari yake ili waweze kulisahihisha na wasilirudie hapo baadaye:

 “WALE WALIORUDI NYUMA (waliokimbia) MIONGONI MWENU SIKU AMBAYO MAJESHI MAWILI YALIPOKUTANA (katika vita vya Uhud; jeshi la makafiri na la waislamu). SHETANI NDIYE ALIYEWATELEZESHA KWA (sababu ya) BAADHI YA (makosa) WALIYOYAFANYA, NA ALLAH (sasa) AMEWASAMEHE. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MPOLE SANA”. [3:155]

 

BAADHI YA WAISLAMU WALIACHA KUENDELEA KUPIGANA WALIPOSIKIA KHABARI YA UZUSHI KUWA BWANA MTUME AMEUAWA.

Na tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu, lililofichuliwa na tukio hili la vita. Ni pale zilipotangaa khabari za kifo cha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, hapo baadhi ya waislamu waliacha kuendelea kupigana na kukubali kushindwa.

Wakasema baadhi ya walioacha kupigana:

“Laiti tungelimpeleka mjumbe kwa Abdillah Ibn Ubayyi, akatuchukulia amani kwa Abu Sufyaan! Enyi kaumu zetu, bila ya shaka Muhammad amekwishauawa, basi rejeeni mkajiunge na jamaa zenu kabla hawajakujieni na kukueni”.

Kana kwamba kwa kauli yao hii walidhania kuwa wamefanya kosa kubwa kuja kushiriki vitani na kwamba ushauri wa kutinda ni ule wa kurejea nyuma aliouchukua Ibn Ubayyi. Na kana kwamba hawakuja vitani kwa ajili ya kuilinda itikadi na kufa kwa ajili ya itikadi hiyo.

Bali walikuja vitani kwa kufitinishwa na ama kwa kuitii amri ya Bwana Mtume ya kwenda vitani na kuepuka kumkhalifu.

Au kwa kutekeleza ile ahadi ya kumlinda waliyompa wakati anahamia kwao. Basi  maadam Bwana Mtume amekwishakufa, imekufa pamoja nae sababu ya vita. Kwa mantiki hii, vita havina nafasi tena na wao hawana sababu ya kujiangamiza kwa kuendelea kupigana.

Hili lilikuwa ni kosa baya mno ambalo waislamu walikuwa hawana budi kuling’amua, kwani lengo walililokuwa wakilipigania halikuwa ni Muhammad; Mtume wa Allah.

Hakika si vinginevyo walipaswa kuelewa kuwa lengo la mwanzo na la mwisho lilikuwa ni kuinusuru dini ya Allah na kuliinua neno lake.

Na hiyo ndiyo akida (itikadi) waliyoiamini na wakatoka kwenda kupigana kwa ajili ya kuilinda kwa kuutoa muhanga uhai wao. Kwa hivyo basi, haikustahiki kabisa kwa waumini kusalimu amri na kukubali kushindwa kwa vyo vyote vile itakavyokuwa.

Bali walilotakiwa kulifanya ni kuipigania akida yao mpaka wajipatie udhuru mbele ya Allah. Kwani kwa yakini walitakiwa kuelewa kuwa wanaitetea na kulinda akida ya dini ya Allah na wala hawapigani kwa ajili ya dhati ya Bwana Mtume.

Basi iwapo Mtume amekufa, hakika Allah yu hai milele hafi:

“NA HAKUWA MUHAMMAD ILA NI MTUME TU. WAMEPITA KABLA YAKE MITUME (wengi kabisa). AKIFA AU AKIUAWA NDIO MTARUDI NYUMA (kwa visigino vyenu), MUWE MAKAFIRI KAMA ZAMANI? NA ATAKAYERUDI NYUMA KWA VISIGINO VYAKE HATAMDHURU ALLAH CHO CHOTE. NA ALLAH ATAWALIPA WANAOMSHUKURU”. [3:144]

 

NA KUNDI JINGINE LILISHUGHULISHWA NA SUALA LA KUZINUSURU NAFSI ZAO.

Na tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu, tukio lililosajiliwa na vita vya Uhud. Ni kwamba lilikuwepo kundi la waislamu ambalo halijaamini  misingi ya kujitoa muhanga kwa ajili ya kuilinda itikadi (akida).

Na bado walikuwa hawajazijua kanuni za Allah  ziendeshazo ulimwengu, kana kwamba wao walikuwa wakipima uzuri (kufaa) na ubaya (kutofaa) wa itikadi kwa ushindi au ushindwa unaowafika wafuasi wa itikadi husika.

Au walikuwa wakidhania kwamba kufaa kwa itikadi pekee  kunatosha kuinusuru na kuipa ushindi itikadi husika, hata kama waumini wake hawakufuata sababu zipelekeazo katika ushindi na nusra. Sasa basi waliposhindwa katika vita hivi wakawa wanajiuliza:

“…AH! TUNA AMRI SISI KATIKA JAMBO HILI?…”

Kana kwamba wanaeleza kwa ibara hii wasiwasi na mashaka yanayojiri ndani ya nafsi zao kuhusiana na suala la akida (itikadi) hii; je akida hii yafaa na dini hii ni ya haki kweli?! Iwapo hii ni akida ifaayo na dini ya haki, kwa nini basi kumepatikana kuuliwa na kushindwa huku?! Allah Mtukufu ameisawirisha hali ya pote (kundi) hili na kulisahihishia kosa lao hili kwa kauli yake tukufu:

“…NA KULIKUWA NA KUNDI JINGINE NAFSI ZAO ZIMEWASHUGHULISHA (hawajijui hawajitambui); WAKIMDHANIA ALLAH DHANA ZISIZOKUWA NDIZO, DHANA ZA UJINGA; WAKISEMA: AH! TUNA AMRI SISI KATIKA JAMBO HILI? SEMA: MAMBO YOTE NI YA ALLAH. WANAFICHA KATIKA ROHO ZAO (hao wanafiki) WASIYOKUBAINISHIA. WANASEMA: TUNGEKUWA NA CHO CHOTE KATIKA JAMBO HILI TUSINGEUAWA HAPA. SEMA: HATA MNGALIKUWA MAJUMBANI MWENU, BASI WANGALITOKA WALE WALIOANDIKIWA KUFA, WAKENDA MAHALI PAO PA KUANGUKIA WAFE. (Amefanya haya Allah ili) AYADHIHIRISHE YALIYO NYOYONI MWENU. NA ALLAH ANAYAJUA (hata) YALIYOMO VIFUANI”. [3:154]

Kwa kauli hii, Allah Mtukufu akafichua waliyoyaficha nyoyoni mwao na akawafundisha kwamba kushinda ama kushindwa hakuna uhusiano wala mafungamano yo yote na kufaa au kutokufaa kwa akida.

Na kwamba mauti na uhai havina uhusiano na vita au amani, bali huo uhai na hayo mauti ni kanuni maalum iliyowekwa na vina muda maalumu vilivyokadiriwa.

Kwa hivyo basi, atakayeandaa na kufuata sababu za ushindi ndiye atakayestahiki kupata ushindi.

Na utakayemfikia muda wake wa kuondoka ulimwenguni, atakwenda mwenyewe katika mahala pake pa kuangukia, ili afie pale alipoandikiwa na Allah kufia.

 

WAISLAMU WALISAMBARATIKA NA KILA MMOJA ALISHUGHULIKA NA YA KWAKE

Na tukio jingine miongoni mwa matukio yaliyoonyesha udhaifu katika safu za waislamu, yaliyofichuliwa na kushindwa katika vita hivi. Ni kwamba adui alipowazingira na kuwaweka kati, hawakuungana na kushikamana pamoja.

Bali walitapanyika kila upande kutokana na kizaizai kilichowakumba pasipo kutarajia. Hata yasemekana kwamba baadhi yao walitimua mbio mpaka Madinah, lakini wakashindwa kuingia kutokana na kuona haya.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *