HAKI YA ALLAH NA MTUME WAKE

Muislamu kujua haki na wajibu wake kwa Mola Muumba wake na viumbe wenzake ni tabia isiyopambanuka naye.

Ni fardhi isiyo na shaka muislamu kuzijua haki zake na kuzidai pake anapozikosa. Na kuujua wajibu wake ili autekeleze kwa kadri ya uweza wake kama inavyompasa.

Neno “haki” ni dhana pana kabisa yenye maana adida (nyingi) kulingana na itakavyotumika, mahaka itumikapo na mtumiaji wa dhana hii.

Katika somo letu hili tutaliarifisha neno haki kuwa: Ni ile hali/jambo lililolazimu katika dhima. Ama kwa neno “wajibu” tunakusudia jambo/tendo linalomlazimu mtu kulitekeleza ili kujitoa katika dhima ya utekelezaji wake.

Maisha ya muislamu yamesheheni na kutawaliwa na hisia za majukumu ambazo humpelekea na kumsukuma kutekeleza wajibu ulio katika dhima yake.

Ni kwa kuutekeleza wajibu wake kwanza ndio muislamu hustahiki kupata/kudai haki yake. Kwani ni vema tukakumbuka na kutia akilini kwamba hakuna haki bila ya wajibu.

Haki ya mwanzo kabisa ambayo muislamu anapaswa kuijua na kuitekeleza ni haki ya Allah Muumba kwa waja wake; watumwa wake.

Hii ni haki ya Mola Mwenyezi ambaye amekutoa kutoka ambako hukuwa kitu kinachotajwa.

Haki ya Allah Mola Mlezi ambaye amekulea kwa neema zake ulipokuwa tumboni mwa mama yako.

Ambamo hakuna ye yote anayeweza kukufikishia chakula chako na kila ukihitajiacho kwa ajili ya maisha yako hayo, yanayopitia katika viza vitatu.

Ni haki yake YEYE aliyekufanyia haya na mengi yasiyodhibitika na akili yako.

Akayafanya yote hayo kwa fadhila na ihsani yake, kwa hivyo ni wajibu wako kuikabili ihsani yake hii

Umpwekeshe katika uungu, ibada na sifa zake (Tauhiyd).

Umtakasiye dini YEYE peke yake (Ikhlaaswi).

Umuabudu YEYE pekee bila ya kumshirikisha na cho chote.

Tusome na tuzingatie: “

NA MUNGU WENU NI MUNGU MMOJA TU, HAKUNA ANAYESTAHIKI KUABUDIWA ILA YEYE AMBAYE NI MWENYE KUNEEMESHA NEEMA KUBWA KUBWA NA MWENYE KUNEEMESHA NEEMA NDOGO NDOGO”. [2:163]

Ufuate na kuzitii sheria zake zote.

“KISHA TUMEKUWEKA JUU YA SHERIA YA AMRI YETU, BASI IFUATE, WALA USIFUATE MATAMANIO YA WALE WASIOJUA (kitu)”. [45:18]

“ENYI MLIOAMINI! INGIENI KATIKA HUKUMU ZA UISLAMU ZOTE, WALA MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI, KWA HAKIKA YEYE KWENU NI ADUI DHAHIRI”. [2:208]

Utekeleze maamrisho yake na ujiepushe na makatazo yake.

Umfuate na kumtii Mtume wake.

“SEMA: IKIWA NYINYI MNAMPENDA ALLAH, BASI NIFUATENI…” [3:31]

Na kwa ujumla utekeleze yale yote ambayo yatathibitisha maana ya uja na utumwa wako kwa Allah Mola Muumba wako.

Naye Allah kwa upande wake amejipangia mwenyewe kwa fadhila na ukarimu wake kuwalipa waja wake watakaoyatekeleza hayo malipo/jazaa adhimu na kuwaepusha na adhabu yake.

“…NA ANAYEMTII ALLAH NA MTUME WAKE, (Allah) ATAMUINGIZA KATIKA BUSTANI ZIPITAZO MITO MBELE YAKE, WAKAE HUMO MILELE. NA HUKO NDIKO KUFAULU KUKUBWA.” [4:13]

 

2- HAKI YA MTUME WA ALLAH.

Haki ya pili ambayo muislamu anatakiwa aijue na kuitekelezea wajibu wake ni haki ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Hii ndio haki kubwa na tukufu katika haki za viumbe. Kwani ni ukweli usiopingika kwamba hakuna haki kubwa baada ya haki ya Allah, kuliko haki ya Mtume wake. Allah anatuambia:

“HAKIKA TUMEKULETA UWE SHAHIDI NA MTOAJI WA KHABARI NJEMA NA MUONYAJI. ILI MUMUAMINI ALLAH NA MTUME WAKE, NA MUMTUKUZE NA MUMUHISHIMU…” [48:8-9]

Ni kwa ajili hii ndio ikawa ni wajibu kwa muumini kuyatanguliza mbele mapenzi ya Mtume juu ya mapenzi ya watu wote.

Ampende mtume zaidi kuliko mke, mali, mtoto, mzazi na hata nafsi yake. Katika hili Mtume wa Allah-Rehma na Amani zimshukie-anatuambia:

“Haikamiliki imani ya mmoja wenu mpaka niwe mimi (Mtume) ni kipenzi mno kwake yeye kuliko mwanawe, mzazi wake na watu wote”. Bukhaariy & Muslim.

Miongoni mwa haki za mtume wa Allah kwako wewe muislamu ni kumkubali, kumuadhimisha na kumuhishimu hishima inayolingana na daraja yake tukufu.

Bila ya kuvuka mipaka na kumtoa katika uanadamu na kumpa sifa ya uungu kama walivyofanya manaswara kwa Nabii Isa.

Kumkubali mtume katika uhai wake ni kuukubali na kuufuata mwendo wake (sunah) na khulka zake (tabia).

Na kumuhishimu na kumtukuza baada ya kufa kwake ni kushikamana na mwenendo na sheria yake aliyotuletea kutoka kwa Mola wake.

Mtu atakayebahatika kusoma jinsi maswahaba-Allah awawiye radhi-walivyomuhishimu na kumtukuza Mtume wa Allah.

Atatambua ni namna gani mabwana hawa watukufu walivyoutekeleza wajibu wao kwa Mtume wao. Baada ya kutambua haki zake zinazowapasa wao kumtekelezea.

Alisema Urwah Ibn Masoud kuwaambia Makurayshi wenzake wakati walipomtuma kuzungumza na Mtume katika suala la suluhu katika kisa cha Hudaybiyah, akasema:

“Nimeingia kwa wafalme (akina) Kisra, Qayswar na Najaash, sikupata kumuona ye yote akiadhimishwa mithili ya maswahaba wa Muhammad wanavyomuadhimisha Muhammad. Alikuwa akiwaamrisha jambo hukimbizana kuitekeleza amri yake hiyo. Na akitawadha hukurubia kuuana kwa kugombea maji yatokanayo na udhu wake. Na anapozungumza, hushusha sauti zao mbele yake na hawakupata kumkazia macho kwa kumuangalia kwa ukubwa wa kumuadhimisha kwao”.

Namna hivi ndivyo walivyokuwa maswahaba-Allah awawiye radhi-wakimuadhimisha na kumtukuza Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Walifanya hivyo pamoja na kuwa tayari Allah alishamuumba na kumfinyanga Mtume wake kwa tabia njema, ulaini na wepesi wa nafsi.

Tabia hizi za Mtume zilitoa msaada mkubwa uliowawezesha maswahaba kumuadhimisha na kumuhishimu, kwani Mola wake anamwambia:

“…NA KAMA UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA YA SHAKA WANGALIKUKIMBIA…” [3:159]

Na katika jumla ya haki za mtume kwa muumini ni kumsadikisha katika mambo yote aliyoyatolea khabari; yaliyopita na yale yajayo.

Na kuyatekeleza aliyoyaamrisha kutendwa na kukatazika na kuyaacha yote aliyoyakataza na kuyakemea. Na kuamini kwamba uongozi wake ndio mkamilifu wa miongozo yote na sheria yake ndio timilifu ya sheria zote. Na isitangulizwe sheria yo yote juu ya sheria yake:

“NAAPA KWA (haki ya) MOLA WAKO, WAO HAWAWI WENYE KUAMINI (kweli kweli) MPAKA WAKUFANYE (wewe ndiye) HAKIMU (muamuzi) KATIKA YALE WANAYOKHITALIFIANA. KISHA WASIONE UZITO NYOYONI MWAO JUU YA HUKUMU ULIYOTOA NA WANYENYEKEE KABISA”. [4:65]

Na miongoni mwa kumuhishimu na kumtukuza Bwana mtume ni kuitetea na kuilinda sheria na muongozo wake. Kwa upeo wa uweza wa mtu kwa mujibu wa hali na mazingira yalivyo.

Ikiwa adui anaishambulia sheria ya mtume kwa hoja, basi jawabu tosha la mashambulizi ya aina hii ni elimu na hoja zitakazoziponda hoja za adui.

Na kumbainishia ulemavu wa hoja zake, na wala sio matumizi ya nguvu. Na kama anahujumu kwa silaha, basi nasi tupambane naye kwa silaha:

“BASI WAANDALIENI (wawekeeni tayari) NGUVU MZIWEZAZO (silaha)…” [8:60]

Haimfalii muumini wa kweli kusikia sheria ya Mtume au hishima yake ikivunjwa, naye akae kimya tu bila ya kuchukua hatua yo yote na ilhali ana uwezo wa kurudi:

“NAYE AMEKWISHA KUTEREMSHIENI KATIKA KITABU (hiki) YA KWAMBA MNAPOSIKIA AYA ZA ALLAH ZINAKATALIWA NA KUFANYIWA STIHZAI, BASI MSIKAE PAMOJA NAO…” [4:140]

 

HAKI YA ALLAH NA MTUME WAKE

Muislamu kujua haki na wajibu wake kwa Mola Muumba wake na viumbe wenzake ni tabia isiyopambanuka naye.

Ni fardhi isiyo na shaka muislamu kuzijua haki zake na kuzidai pake anapozikosa. Na kuujua wajibu wake ili autekeleze kwa kadri ya uweza wake kama inavyompasa.

Neno “haki” ni dhana pana kabisa yenye maana adida (nyingi) kulingana na itakavyotumika, mahaka itumikapo na mtumiaji wa dhana hii.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *