AUSI AWAOMBEA SHAFAA BANI QURAYDHWAH

Naam, hivyo ndivyo ilivyomalizika kadhia ya Abuu Lubaabah. Ama Baniy Quraydhwah baada ya kukataliwa maombi yao yote, hawakuwa na uchaguzi tena ila kujisalimisha kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Mtume akaamuru wanaume wafungwe kamba na kuwekwa kando, wanawake na watoto nao wawekwe upande mwingine.

Hapo ndipo wakatoka wazee wa Kiausi wakamuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuwaombea msamaha ndugu zao hawa wa yamini.

Wakamuomba Bwana Mtume awatendee Baniy Quraydhwah; washirika wao kama alivyowatendea Baniy Qayunqaa; washirika wa Khazraji.

Wakataraji Mtume awaachie Baniy Quraydhwah kutoka kama alivyowaachia Baniy Qayunqaa na kwamba atawakubalia uombezi wao huo kwa washirika wao kama alivyowakubalia Khazraji kwa washirika wao.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaambia:

“Je, nyinyi kusanyiko la Ausi hamridhii mimi kuweka mtu miongoni mwenu (Muasi mwenzenu) baina yangu na washirika wenu?”, wakajibu: “Kwa nini tusiridhie!”. Mtume akawaambia: “Basi waambieni hao washirika wenu wamteue ye yote wamtakaye”. Mayahudi wakamchagua Sa’ad Ibn Muaadh; kiongozi wa Ausi kuwa ndio msuluhishi baina yao kwa upande mmoja na Mtume wa Allah kwa upande wa pili.

Sa’ad Ibn Muaadh alikuwa ni majeruhi kutokana na mshale aliopigwa katika vita vya Khandaq na alikuwa akipata matibabu katika hema la mwanamke mmoja aliyeitwa Rufaydah.

Huyu ni mwanamke aliyekuwa na hema msikitini akitoa humo huduma kwa majeruhi wa vita. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ndiye aliyewaomba jamaa za Sa’ad wampeleke katika hema hilo la matibabu la Bi. Rufaydah.

Aliwaomba hivyo ili apate kuwa karibu nae na hivyo kupata fursa ya kumjulia hali mara kwa mara. Mtume wa Allah alipompa Sa’ad dhima ya hukumu kama walivyoomba Mayahudi, jamaa zake walimuendea na kumbeba juu ya punda.

Wakawa wanakuja nae njiani na huku wanamwambia:

“Ewe Aba Amrou, watendee wema washirika wako, kwani hakika si vinginevyo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amekutawalisha suala lao ili upate kuwatendea wema. Nawe uliona namna Ibn Ubayyi alivyowatendea nduguze wa yamini (washirika wao)”.

Wakamshikilia na kumkariria maneno hayo, nae akiwasikiliza tu bila ya kuwajibu japo kwa kipande cha neno. Walipozidi nae akawa amekereka na maneno yao hayo, ndipo alipowaambia: “Bila shaka umemfikia Sa’ad wakati wa kutoogopa kulaumiwa kwa ajili ya Allah”.

 

    II.          Hukumu ya Sa’ad Ibn Muaadh:

 Sa’ad alipofika kwenye baraza ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie-Mtume aliwaambia maswahaba wake muinukieni Bwana wenu.

Wakasimama na kujipanga safu mbili, akipita kati yao na kila mtu akimuamkua mpaka akafika mahala alipokuwa amekaa Mtume. Mtume akamwambia:

Wahukumu ewe Sa’ad”, akamjibu: “Allah na Mtume wake ndio wenye haki zaidi ya kuhukumu”. Mtume akamwambia:

“Allah ndiye aliyekuamuru kuwahukumu”. Kwa kauli hii ya Mtume, ndipo Sa’ad alipougeukia upande wa waislamu na kuwaambia:

“Je, mnachukua ahadi kwa Allah kwamba hukumu yao itakuwa ni ile nitakayohukumu mimi”, wakajibu: “Naam”. Akasema:

Na hapa pia nimepata ahadi hiyo hiyo?” – huku akiashiria upande alioko Mtume wa Allah huku akiwa amefumba macho kwa ajili ya kumuheshimu Bwana Mtume. Mtume wa Allah akamjibu: “Naam”.

Halafu tena ndipo Sa’ad alipowaambia Baniy Quraydhwah: “Je, mtairidhia hukumu yangu?”, wakajibu: “Naam”. Akachukua kwao ahadi ya Allah ya kwamba hukumu itakuwa ni ile itakayotolewa nae, halafu ndipo aliposema:

“Basi hakika mimi ninahukumu wanaume wauawe, mali zao zigawanwe na wanawake na watoto wachukuliwe mateka”.

Alipomaliza kutoa hukumu yake hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:

“Kwa yakini kabisa umewahukumu kwa hukumu ya Allah kutoka juu ya mbingu ya saba”.

 III.          Machinjwaji ya Baniy Quraydhwah:

Baada ya kutolewa hukumu hiyo kwa wasaliti hawa wasiouheshimu hata mkataba waliouandika na kuuridhia wenyewe, hukumu iliyopata baraka zote za Allah na Mtume wake.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaamuru mateka wote wapelekwe Madinah; makao makuu ya dola ya Kiislamu.

Wakapelekwa na kuwekwa katika boma la Usamah Ibn Zayd, wanawake na watoto wakawekwa katika boma la Kaysah Bint  Al-Haarith.

Na akaamrisha silaha, samani na mali yote itwaliwe, ngamia, kondoo na mbuzi waachwe kwenye malisho yao huko huko.

Kisha akaamuru Baniy Quraydhwah wamwagiwe magunia ya tende, nao wakakesha wakizila kwa midomo yao kama walavyo ngamia.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akadamkia kwenye soko la Madinah na kuamuru lichimbwe hapo handaki kubwa.

Baada ya handaki kuchimbwa, akatoa amri waletwe wanaume wa Kibaniy Quraydhwah, wakawa wanaletwa makundi makundi zikipigwa panga shingo zao na kutupwa handakini.

Huyay Ibn Akhtwab alikuwa amejitia ngomeni pamoja na Baniy Quraydhwah mara tu baada ya kuondoka kwa majeshi shirika.

Alifanya hivyo kwa ajili ya kuitekeleza ahadi yake aliyoitoa kwa Ka’ab Ibn Asad. Alipoletwa ili auawe, Mtume wa Allah alimuangalia na kusema:

“Je, Allah hajakutia mikononi mwetu ewe adui ya Allah?”, akajibu:

“Khasaa, Allah amekataa ila kunitia mikononi mwako! Wallah, nafsi yangu bado haijaacha uadui nawe hata sasa, lakini ni kwamba mwenye kuacha kumnusuru Allah nae huachwa kunusuriwa”.

Alipokwisha kusema maneno yake haya, akawageukia Mayahudi na kuwaambia:

“Enyi watu! Hakika amri ya Allah haina ubaya, ni hukumu na qadari iliyopitishwa na ni malanyama waliyoandikiwa Baniy Israil na Allah”. Alipomaliza kusema akakaa, ikapigwa shingo yake na kutumbukizwa handakini.

 

  IV.          Kuokoka kwa waliosilimu:

Wakasilimu watatu miongoni mwa Baniy Quraydhwah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawapa amani ya nafsi, watu wao (wake na watoto) na mali zao.

Mwenzao Amrou Ibn Sa’ad hakuwa amewafikiana na fikra ya Baniy Quraydhwah ya kutengua mkataba wao na waislamu.

Huyu akaachiwa, akaenda kusikojulikana, Mtume wa Allah akasema:

“Huyo ni mtu aliyeokolewa na Allah kwa sababu ya kutekeleza kwake ahadi yake”.

Bwana mwingine Rifaa Ibn Samuel alikuwa ameomba hifadhi kwa Ummul-Mundhir Al-Answaariyyah, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akampa hiba mtu wake huyo, nae akasilimu kwa sababu hiyo. Thabit Ibn Qaysi Al-Answaariy nae akataka kumlipa Zubeir Ibn Baatwaa kwa wema aliopata kutendewa nae.

Akamuomba Mtume ampe hiba mtu huyu, nae akamkubalia, akampa yeye, familia na mali yake.

 Lakini Myahudi huyu; Zubeir akaikataa ihsani na jazaa aliyopewa na kutaka aambatishwe na wapendwa wake miongoni mwa mayahudi wenzake, ikapigwa shingo yake.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiwachukulia upole mateka wao na akiusia watendewe wema.

Mara moja alipata kumuona mmoja wa mateka akiwa kapigwa usoni na kuvuja damu za pua, Mtume akamwabia mlinzi wake:

“Kwa nini umemtendea hivi? Kwani panga halikutosha?”. Halafu akasema:

“Wafanyieni wema uteka wao, wapeni muda wa kulala na wapeni maji na wala msiwakusanyie joto la jua na joto la silaha”.

Na siku hiyo ilikuwa na joto kali mno, wakawapa mapumziko, wakawapa maji na chakula. Jua lilipopungia, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaenda na kuamuru kuuawa waliobakia.

Mauaji yakaendelea mpaka usiku hadi walipouliwa wote na walikuwa baina ya mia sita na mia saba. Kauli nyingine inasema walikuwa ni baina ya mia nane na mia tisa na nyingine walikuwa ni mia nne tu.

Hakuuliwa katika wanawake wao ila mwanamke mmoja tu, huyu aliwaangushia jiwe la kusagia nafaka waislamu waliokuwa wamepumzika chini ya ngome zao. Akamuua Khalaad Ibn Suweid-Allah amuwiye radhi.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *