BANY QURAYDHWAH WAVUNJA AHADI (AHZAAB)

I.   Baniy Quraydhwah wavunja ahadi yao:

Kukarepa kungojea na kusubiri kwa majeshi shirika (Ahzaabu) na kukawa hakuna kinachoendelea baina yao na waislamu ila kurushiana mishale na kutupiana mawe kwa mbali.

Huyay Ibn Akhtwab akachelea kuipoteza fursa hii adhimu aliyoipata na washirika wake; Makurayshi na Ghatwfaan wasije kuchoshwa na huku kukaa kwa muda mrefu wakaamua kuchukua uamuzi wa kurejea makwao bila ya kutimia lengo la kuja kwao.

Khususan ikizingatiwa kwamba hicho ni kipindi cha pepo za Kusi na ukame na akiba ya chakula cha wanyama waliokuwa nayo inakaribia kuisha na ngamia na farasi wanakurubia kufa kwa ukondefu wa njaa.

Huyay Ibn Akhtwab akaona hakuna njia yo yote ya kuingia Madinah ila kwa kupitia upande wa Baniy Quraydhwah.

Lakini kikwazo kikawa kwamba Baniy Quraydhwah walikuwa wamefunga mkataba wa amani na ujirani mwema na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Akaamua kujaribu bahati yake, mguu mosi mguu pili akamuendea kiongozi wa Baniy Quraydhwah; Ka’ab Ibn Asad, akaingia nae chembani. Hapo akaanza kumwambia madhumuni ya majaji yake, akasema:

“Ewe Ka’ab! Hakika si vinginevyo mimi nimekuleta utukufu wa milele, nimekuletea Makurayshi na watukufu wao na Ghatwfaani na makamanda wao. Wote hawa wamefunga ahadi ya kummaliza Muhammad na walio pamoja nae”. Ka’ab akamjibu:

 “Wallah, umeniletea udhalili wa milele na wingu danganyifu; lisilo na mvua, ole wako ewe Huyay! Hebu achana na mimi kwani sitofanya uniitialo kwa sababu bado sijaona kwa Muhammad ila utekelezaji wa ahadi na ukweli”. Huyay akaendelea kumshikilia Ka’ab huku akimpa  ahadi kibao na kumlaghai mpaka akafanikiwa. Huyay akamwambia Ka’ab:

 “Makurayshi na Ghatwfaan wakiondoka kurudi makwao, mimi na watu wangu wote tutakuwa pamoja nanyi hadi tuijue hatima yenu”.

 

Mtume ataka kuthibitisha usahihi wa khabari zilizomfikia:

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoutambua usaliti wa Baniy Quraydhwah, aliwatuma wajumbe wake kwao; Sa’ad Ibn Muaadh kiongozi wa kabila la Ausi na Sa’ad Ibn Ubaadah kiongozi wa kabila la Khazraj pamoja na kundi la maswahaba wake.

Akawaambia wajumbe wake hawa:

Waendeeni Baniy Quraydhwah, ikiwa haya tuliyo ambiwa ni kweli basi tufahamisheni na wala msionyeshe udhaifu kwao na ikiwa ni uongo basi watangazieni/waambieni khabari hizi”.

 Haoo wakashika njia mpaka kwa Baniy Quraydhwah, wakawakuta katika hali mbaya zaidi kuliko walivyoambiwa, wakamtukana Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie, wakasema:

“Hana mkataba nasi”.

 Sa’ad Ibn Ubaadah akaanza kuwakumbusha juu ya utekelezaji wa ahadi ya mkataba waliouridhia wao wenyewe na kuwatahadharisha juu ya matokeo ya khiana na usaliti wao huo wanaotaka kuwafanyia waislamu. 

Akawaambia katika jumla ya aliyowaambia:

“Nakucheleeni kufikwa na kama yaliyowafika Banin-Nadhwiyr na machungu zaidi kuliko hayo!” Wakamjibu maneno machafu kiasi cha kufikia kumtukana nae akala zimika kuyajibu matusi yao hayo, Sa’ad Ibn Ubaadah akamkataza:

 “Acha kuwatukana, kwani lililo baina yetu na wao ni kubwa mno kuliko hayo matusi”.

Halafu haoo akina Sa’ad wakarejea kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakamkuta akiwa na kundi la waislamu, wakamwambia:

 “Ni za kweli kabisa khabari ulizozisikia, wamevunja mkataba na kujiunga na adui yetu”. Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Furahini enyi kusanyiko la waislamu!”.

 

II.  Waislamu wasongwa na taabu, Mtume wa Allah azijaza nyoyo zao matumaini:

Khabari hizi za usaliti wa Baniy Quraydhwah zikawafikia waislamu na kuwaogofya na wakadhania ya kwamba tayari wamekwishazungukwa. Wakawa kama alivyosema Allah Taala”

“WALI POKUJILIENI (kukushambulieni) KUTOKA JUU YENU NA KUTOKA CHINI YENU; NANYI MKAANZA KUMDHANIA ALLAH DHANA MBALI MBALI. HAPO WAISLAMU WALITIWA MTIHANI (kweli kweli) NA WAKA TETEMESHWA KWA MATETEMESHO MAKALI”. [33:10-11]

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipoiona hali hii ngumu iliyo wagubika maswahaba wake, akaidiriki kwa kuwapa bishara njema akiwaambia:

 “Namuapia yule ambaye nafsi yangu i mkononi mwake, Wallah Allah atakupeni tu faraja ya shida mliyonayo na mimi ninataraji kutufu katika nyumba kongwe (Al-Ka’abah) nikiwa mwenye amani. Na kwamba Allah atazitia mikononi mwangu funguo za         Al-Ka’abah na bila shaka Allah atawaangamiza Kisraa na Qaisari nanyi mtazitoa khazina zao katika njia ya Allah!”

Ni katika kipindi hiki kigumu ndimo wanafiki walimojidhihirisha wao wenyewe na kuianika juani kweupe siri yao. Wako miongoni mwao waliosema:

 “Hakika nyumba zetu ni tupu, hapana watu haya na tuziendee kwani tunazichelea kufikwa na madhara”. Pia wako wale waliosema:

“Eti huyu Muhammad anatuahidi kuzifungua khazina za Kisraa na Qaisari na ilhali leo tu mmoja wetu hana amani hata ya kwenda kukidhi haja!” Wakaanza kupenya vikundi vikundi huku wakihimizana kukimbia na kumuacha Mtume na waumini peke yao.

Hali hii ndio inayoelezwa na kauli ya Allah:

 “NA WALIPOSEMA WANAFIKI NA WALE WENYE MARADHI NYOYONI MWAO, ALLAH NA MTUME WAKE HAWATUAHIDI ILA UDANGANYIFU TU. NA TAIFA MOJA MIONGONI MWAO LILIPOSEMA: ENYI WENYEJI WA YATHRIBU (Madinah)! HAMNA MAHALI PA KUKAA NYINYI, BASI RUDINI (makwenu, msiingie katika jeshi pamoja na Muhammad). NA KUNDI JINGINE MIONGONI MWAO LIKAOMBA RUHUSA KWA MTUME KWA KUSEMA: HAKIKA NYUMBA ZETU NI TUPU (hapana watu, tunakwenda zetu), LAKINI HAZIKUWA TUPU, HAWAKUTAKA ILA KUKIMBIA TU…..BILA SHAKA ALLAH ANAWAJUA WALE WANAO JIZUIA MIONGONI MWENU (wasende vitani pamoja na Mtume) NA WAWAAMBIAO NDUGU ZAO: NJOONI KWETU (wala msende kwa Muhammad), WALA HAWENDI KATIKA MAPIGANO ILA KIDOGO TU (ili kuwadanganya waislamu)”. [33:12-18]

 

 III.   Vikosi shirika vyazidisha mbinyo kwa waislamu kiasi cha kufikia baadhi yao kulitambuka handaki:

Huyay Ibn Akhtwab akarejea kwa washirika wake na kuwapasha khabari njema za Baniy Quraydhwah kuvunja mkataba na waislamu na badala yake kuamua kushirikiana na wao.

Khabari hizi zikayatia nguvu mpya majeshi shirika haya na kuamsha mori wao wa mapambano.

Wakawasha moto mkubwa mno kupata kuwashwa tangu kupiga kwao kambi hapo ili kuwakhofisha na kuwa dhoofisha waislamu kabla ya kuanza kwa mapambano rasmi.

Baniy Quraydhwah walikuwa wamemuomba Huyay Ibn Akhtwab awape muda wa siku kumi za kujiandaa na kujiweka sawa.

Na kwa sharti vikosi shirika vizidishe mbinyo wa mashambulizi dhidi ya waislamu katika kipindi chote hicho ili kuwashughulisha waislamu na suala lao hili la usaliti.

Mashambulizi ya majeshi shirika yakaongezeka kufuatia matakwa haya ya Baniy Quraydhwah yakiwa kama ni masharti ya kujiunga nao.

Yakatoa upinzani mkubwa kwa waislamu kiasi cha kuwapeleka puta na kuwataabisha upeo.

Baada ya mashambulizi haya ya utangulizi, ndipo viongozi wa makundi haya ya mushrikina walipokongamana kusonga mbele wote kwa pamoja na kuishambulia kambi ya waislamu kwa hujuma moja kuu.

Wapanda farasi wao wakaanza kulizunguka handaki wakitafuta upenyo wa kuwapenyezea farasi wao upande wa pili wa handaki.

Wakaendelea kuzungukazunguka mpaka wakaupata upenyo uliosahauliwa kulindwa na waislamu. Baadhi ya viongozi wa majeshi shirika wakiwemo Amrou Ibn Abu Jahli, Naufal Ibn Abdillah, Dhwiraar Ibn Akhtwab, Hubeirah Ibn Abiy Wahab na Amrou Ibn Wuddi wakafanikiwa kupenya upande wa waislamu kwa kupitia mahala hapo.

Tukumbuke kwamba Amrou Ibn Wuddi alikuwa ni shujaa na jasiri ambaye hakuthubutu ye yote katika Waarabu kupambana nae.

Alikuwa na majivuno mno kiasi cha kujiitakidi kwamba yeye ni tosha ya watu alfu, pamoja na kuwa na umri mkubwa wa miaka tisini bado alikuwa na nguvu za kijana mbichi. Alipolivuka handaki pamoja na wenzake akaanza kutamba na kutoa wito:

“Je, yuko mbarizi (mtaka mapambano ya wawili)?”.

Waislamu wakalitambua kosa lao na haraka wakaja kuuziba upenyo ule ili wasiweze kupenya wengine na kuwapa fursa nzuri ya kuwafyeka hawa waliokwisha fanikiwa kupenya.

Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib akamtokea Amrou kupambana nae, Amrou alipomtambua kuwa ni yeye akambeza na kumwambia:

“Kwa nini ewe mwana wa ndugu yangu? Wallah mimi sipendi kukuua”. Aliy akamwambia:

“Lakini mimi wallah, napenda kukuua”. Kauli hii ya Imamu Aliy ikaziamsha hasira za Amrou, akashuka jua ya farasi wake na kumchinja kwa upanga kuonyesha kuwa hapo hakimbii mtu ni mapambano tu hadi mwisho.

 Kisha akamuendea Aliy na kumuelekezea pigo la nguvu kwa upanga wake, Imamu Aliy akaliepa kwa kutumia ngao ya ngozi aliyo kuwa nayo ambayo iliruhusu kupasuliwa kichwa chake kutokana na uzito wa pigo la shujaa Amrou.

Sayyidina Aliy akatumia mbinu ya kurejea kinyumenyume huku Amrou akimsukumizia mapigo ya haraka haraka akidhihirisha uhodari wake katika vita.

Akazidi kumvuta mpaka zikamjia fikra Amrou kwamba kuna mtu anataka kumshambulia kwa nyuma yake, akageuka nyuma kuangalia. Bila kuchelewa Imamu Aliy akaitumia vema fursa hiyo na kosa hilo la Amrou kwa kumshushia pigo kali lililouacha mguu wake ukitengana na mwili wake.

 Amrou kama mbogo aliyejeruhiwa akauokota mguu wake na kumvurumishia Imamu Aliy usoni.

Lakini baada ya hapo akaanza kupepesuka mpaka akaishiwa nguvu na kuanguka chini huku akiugulia kwa maumivu makali.

Hapo hapo Sayyidina Aliy akamuendea na kumshindilia panga na kummaliza. Kuona yaliyo mpata shujaa, fakhri na tegemeo lao, wenzake haoo wakatimua mbio wakawaendesha shoti farasi wao ili kulivaa handaki kurudi waliko tokea.

Pwaa! Akabwagwa Naufal Ibn Abdillah handakini na farasi wake, humo akapopolewa na mvua ya mawe ya waislamu mpaka akafa na wenzake kufanikiwa kukimbia.  

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *