BANI QURAYDHWAH WAZINGIRWA

Kwa sababu zote hizi na kwa kuyazingatia yote yaliyojiri, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-aliharakisha kuwazingira Baniy Quraydhwah siku ile ile yaliyoondoka Madinah majeshi shirika (Ahzaab).

Aliona ni wajibu wa mwanzo kuwaendea ghafla kabla hawajakamilisha maandalizi yao ya vita na kuziimarisha ngome zao. Kabla kidogo ya kuingia wakati wa swala ya Adhuhuri, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Bilali-Allah amuwiye radhi-kuwanadia watu:

“Ye yote aliye msikivu na mtii kwa (Allah na Mtume wake), basi asiiswali swala ya Laasiri ila kwa Baniy Quraydhwah”.

Waislamu waliousikia wito huu wa Mtume wa Allah, pale pale wakaanza kuchukua silaha zao na kumiminikia kwenye ngome za Baniy Quraydhwah.

Wako miongoni mwao walioidiriki swala ya Laasiri katika kitongoji cha Baniy Quraydhwah kutokana na wepesi wao na wengine iliwadiriki njiani, wakaiswali hapo hapo ilipowadiriki.

Pia wako walioichukulia amri ya Mtume kwa njia ya dhahiri, hawa hawakuswali njiani, bali waliendelea  kwenda  huku wakati wa Laasiri ukitoka na kuipisha Maghribi iingie.

Wakaiswali Laasiri nje ya wakati wake (Qadhaa) walipofika kitongojini kwa Baniy Quraydhwah.

Vyo vyote ilivyokuwa kila kundi lilikuwa na lengo la kuharakia kuitekeleza amri ya Mtume wa Allah kwa namna ya uweza na uelewa wake.

Basi haukuingia wakati wa swala ya Ishaa ila waislamu wote tayari walikuwa wamekusanyika nje ya ngome za Baniy Quraydhwah wakiwa katika maandalizi kamili ya vita. Idadi yao ikiwa ni askari alfu tatu wa miguu na wapanda farasi thelathini.

Mtume wa Allah-Rahema na Amani zimshukie-alikuwa amempa bendera ya vita Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi.

Akampa bendera hiyo aliongoze kundi la Muhajirina na Answari kwenda kwa Baniy Quraydhwah. Mayahudi walipowaona Waislamu wakawapokea kwa matusi, wakimtukana Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na wake zake, waislamu hawakuyajibu matusi haya zaidi ya kuwaambia:

Leo ni upanga tu ndio utakaozungumza baina yenu nasi na wala sio matusi”.

Halafu Mtume-Rehema na Amani zimshukie-nae akampanda mnyama wake kwenda kuungana na maswahaba wake waliotangulia kwa Baniy Quraydhwah. Baniy Quraydhwah walipomuona Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amefika kujiunga na maswahaba wake, wakaingia ngomeni mwao kwa kutambua kuwa sasa ni vita tu na wala si maskhara.

Mtume wa Allah na maswahaba wake wakawazingira kwa kipindi kisichopungua majuma mawili, katika kipindi chote hiki ikawa hakuna atokaye wala aingiaye.

Kwa maana hii wakawa wanaitumia akiba ya maji na chakula walicho nacho bila ya kupata ziada kutoka nje.

Wakachoshwa na kukimwa na mzingiro huu mrefu na Allah akatia khofu ndani ya nyoyo zao.

Hili likawapelekea kufikia uamuzi wa kutuma ujumbe maalumu kwa Mtume wa Allah.

Ya kwamba awaruhusu kuhama wao, wake na watoto wao pamoja na mali inayoweza kubebwa na ngamia kama ilivyokuwa kwa watangulizi wao; Banin-Nadhwiyr.

Mtume akawakatalia ombi lao hilo, nao hawakuchoka wakatuma ujumbe mwingine wakiomba waruhusiwe kutoka wao wenyewe tu bila ya kuchukua mali wala silaha.

Ombi lao hili pia likakataliwa na Mtume na wakataka airidhie hukumu atakayoitoa yeye tu na si vinginevyo kama watakavyo wao.

Baada ya maombi yao yote mawili kukataliwa, kiongozi wao; Ka’ab Ibn Asad akawashauri waingie katika Uislamu huku akiwa kumbushia ufahamu (elimu) walionao juu ya utume wa Muhammad kutoka katika vitabu vyao, hawakuukubali ushauri wake huu.

Akawaambia ikiwa hamlitaki shauri hili la kusilimu, basi waueni wake na watoto wenu, kisha nyinyi tokeni mkapigane na waislamu mpaka mshinde au muuawe nyote.

Ushauri huu pia wakaukataa, ndipo akawashauri wawatokee ghafla waislamu usiku wa kuamkia siku ya Sabato (Jumamosi) na kuwafyekelea mbali. Wakamwambia kiongozi wao:

“Hatuwezi kuvunja utukufu/heshima ya Sabato”, wakakhitilafiana na kujuta kwa yote waliyowatendea jirani zao wema (waislamu).

 

IV.            Ishara ya Abu Lubaabah:

Mzingiro ulipowazidia na kuwachosha, wakapeleka ujumbe kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ya kwamba tunaomba umruhusu Abu Lubaabah aje tushauriane nae katika suala letu hili.

Ombi lao hili likakubaliwa, Mtume akawapelekea Abu Lubaabah Ibn Al-Mundhir Al-Answaariy Al-Ausiy ambaye alikuwa mshauri mkuu wa Baniy Quraydhwah na mali na familia yake ilikuwa kwao.

Walipomuona, wanamume wakamuinukia na wanawake na watoto wakaangusha kilio, kwa hali aliyoiona huruma ikamuingia Abu Lubaabah. Baniy Quraydhwah wakamzunguka wakimuuliza:

“Unaonaje shauri hili ewe Abu Lubaabah, hakika Muhammad hasikii wala kukubali lo lote ila tuiridhie hukumu yake”.

Abu Lubaabah akawajibu kwa kuashiria kooni kwake na akasema: “Shukeni katika hukumu hiyo”, akimaanisha kuwa hukumu inayowasubiri ni kuchinjwa tu ikiwa mtajisalimisha.

Abu Lubaabah akadiriki kuwa kwa ishara yake hii aliyoitoa amekwishaifichua siri ambayo adui hakupaswa kuijua na kwamba kwa kitendo chake hicho tayari amekwishamkhini Allah na Mtume wake.

Akashindwa kuonana uso kwa uso na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaamua kwenda msikitini, humo akajifunga kamba barabara kwenye mojawapo ya nguzo. Akaapa ya kwamba hataonja chakula wala maji mpaka afe au Allah amkubalie toba yake kutokana na aliyoyatenda.

Na akachukua ahadi kwa Allah ya kwamba kamwe hatoikanyaga ardhi ya Baniy Quraydhwah; ardhi ambamo amemkhini ndani yake Allah na Mtume wake. Khabari ya Abu Lubaabah ilipozigonga ngoma za masikio ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:

 “Ama lau yeye angenijia ningelimuombea maghufira, lakini maadam amefikia uamuzi alioufikia basi mimi siye nitakayemuacha huru mpaka Allah amkubalie toba yake”.

Abu Lubaabah akakaa hapo nguzoni siku sita bila ya kula chakula wala kunywa japo funda ya maji.

Mkewe akawa anamjia katika kila wakati wa swala akimfungua ili apate kuswali, akimaliza kuswali humfunga tena na kuendelea na kifungo chake hicho alichojihukumu yeye mwenyewe.

 Hali yake ikawa taabani mpaka akazimia, hapo ndipo Allah Taala alipomkubalia toba yake na akaishusha kwa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-kauli yake tukufu:

“NA (wako) WENGINE WAMEKIRI DHAMBI ZAO (wametubia kwa Allah, wakapokelewa). WAMECHANGANYA VITENDO VIZURI NA VINGINE VIBAYA. ASAA ALLAH AKAPOKEA TOBA ZAO, HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MWINGI WA KUREHEMU”. [9:102]

Allah alipompokelea toba yake, Abu Lubaabah akakataa kufunguliwa ila na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomfungua akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, hakika katika jumla ya toba yangu ni mimi kukihama kitongoji cha kaumu yangu ambamo humo ndimo nilimotenda dhambi na niitasadaki mali yangu yote”. Mtume akamwambia: “Inakutosha kutoa sadaka theluthi ya mali yako na sio mali yote”.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *