NATIJA YA VITA VYA BADRI

UGOMBEZI WA NGAWIRA.

Ngawira walizozipata waislamu katika vita hivi zilikuwa ni nyingi ikiwa ni pamoja na ngamia, vyombo, mabusati ya ngozi, nguo na ngozi nyingi walizozichukua kwa ajili ya biashara.

Ngawira hii ikawa ni fitna inayokurubia kuwagawa maswahaba kutokana na mapenzi ya mali ambayo ni maumbile ya kila mwanadamu.

Wapiganaji waliokuwa katika medani ya vita wakipambana ana kwa ana na adui wakiua na kuteka wakadai kwamba wao ndio wana haki zaidi ya kupata ngawira hiyo.

Wakusanyaji wa ngawira hizo wakati wapiganaji wakisonga mbele nao wakadai kuwa na haki zaidi kuliko wengine.

Walinzi wa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-nao wakadai kuwa na haki zaidi ya kupata ngawira hizo.

Kutokana na kila kundi kudai haki zaidi ya kupata ngawira kuliko jingine, wakaamua kulipeleka suala hilo kwa Mtume wa Allah ahukumu baina yao.

Bwana Mtume akaamuru kurudishwa kwa ngawira zote zilizomo mikononi mwa watu ili kumpa fursa ya kuliamua suala hilo au Allah ashushe hukumu. Wakiwa katika hali hii ya mzozo wa ngawira ndipo ikaja hukumu kutoka mbinguni:

“WANAKUULIZA JUU YA MALI YALIYOTEKWA (ngawira yagawiwe vipi?) SEMA: MALI YALIYOTEKWA NI YA ALLAH NA MTUME WAKE (fuateni watakavyokugawieni). BASI MUOGOPENI ALLAH NA SULUHISHENI MAMBO BAINA YENU, NA MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE IKIWA NYINYI NI KATIKA WANAOAMINI (kweli)”. [8:1]

Haiwi kwa waislamu ila kumtii Allah na Mtume wake, wakampa nafasi Mtume ya kuwa mgawaji wa ngawira hizo.

Bwana Mtume akawagawia mali hiyo ya ngawira na kila mmoja akaridhia kwa kila alichopewa na Allah na Mtume wake.

Wanazuoni wa fani ya tafsiri wanazielezea sababu za kukhitalifiana kwa maswahaba katika suala zima la ugawaji wa ngawira.

Wanasema kulikuwa na sababu kuu mbili zilizokuwa na athari kubwa katika mtafaruku huu ambao kamwe haukutarajiwa kutokea.

Haukutarajiwa kutokea si kwa Muhaajirina ambao Allah alishuhudia kuwa wao ni waumini wa kweli kweli:

“…AMBAO WALIFUKUZWA KATIKA NYUMBA ZAO NA MALI ZAO (wakakhiari kuwacha hayo) KWA AJILI YA (kutafuta) FADHILA ZA ALLAH NA RADHI (yake) NA KUINUSURU (dini ya) ALLAH NA MTUME WAKE. BASI HAO NDIO WAUMINI WA KWELI”. [59:8]

Wala kwa Answaar ambao nao Allah aliwashuhudilia kwamba wao ndio waumini wa kweli:

“…WAKAWAPENDA HAO WALIOHAMIA KWAO, WALA HAWAPATI (hawaoni) DHIKI NYOYONI MWAO KWA HAYO WALIYOPEWA (hao Muhajirina) NA WANAWAPENDELEA ZAIDI KULIKO NAFSI ZAO INGAWA WENYEWE WANA HALI NDOGO…” [59:9]

Mojawapo ya sababu mbili hizo ni ya kiakili (kuwazika), kila mmoja aliipupia kuipata katika ushindi huu wa kwanza dhidi ya batili.

Walifikiri ushujaa wa mtu katika uwanja wa mapambano utapimwa kwa kipimo cha ngawira aliyopata.

Kila mwenye ngawira nyingi huyo ndiye atakayeonekana kuwa ni shujaa.

Sababu ya pili ni ya kimaumbile kwamba ni maumbile ya kila binadamu kupenda mali na kupenda kupata zaidi kuliko wenzake.

Na pengine tunaweza kusema kuwa hali ya dhiki na ufakiri waliokuwa nao waislamu wakati ule baada ya kuporwa mali zao Makkah, inaweza kuwa ni sababu ya tatu iliyochangia mzozo huu wa kugombea ngawira.

Linalotupelekea kusema hivi ni ile riwaya iliyopokelewa kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwatazama maswahaba wake wakati wakitoka kwenda katika vita vya Badri, hali yao ikamuathiri.

Akawaombea Mungu, akasema:

“Ewe Mola wa haki wee! Hakika waja wako hawa ni pekupeku (hawana mnyama wa kupanda waendapo vitani) basi (ninakuomba) uwabebe wewe (uwape mnyama wa kupanda). Hawana nguo, basi (ninakuomba) uwavishe na wana njaa (ninakuomba) uwashibishe na ni mafakiri basi (ninakuomba) uwakwasie (uwatajirishe) kutokana na fadhila zako”.

Sababu yo yote itakayokuwa bado ukweli utabakia kuwa pale pale kwamba tukio hili la mzozo wa ngawira liliwatia dosari waislamu.

Kiasi cha Allah kuwalaumu na kuwakaripia kutokana na tendo lao hilo lililotishia kuuvunja umoja wa waislamu.

 Tukio hili kwa upande mwingine likawa ni darsa iliyowafundisha maswahaba khasa na waislamu wote kwa ujumla namna gani wanatakiwa kuwa waumini wakweli.

Waumini wakweli wanatakiwa kuipenda zaidi akhera yenye maisha ya milele na starehe za kweli kuliko dunia yenye kuondoka na yenye starehe za muda mfupi zenye ghururi na khadaa:

“HAKIKA WAUMINI WA KWELI NI WALE AMBAO ANAPOTAJWA ALLAH NYOYO ZAO HUJAA KHOFU, NA WANAPOSOMEWA ALLAH ZAKE HUWAZIDISHIA IMANI, NA WAKAMTEGEMEA MOLA WAO TU BASI. AMBAO WANASIMAMISHA SWALA NA WANATOA KATIKA YALE TULIYOWAPA. HAO NDIO WAUMINI WA KWELI WAO WANA VYEO (vikubwa) KWA MOLA WAO NA MSAMAHA NA RIZIKI BORA (kabisa huko akhera)”. [8:2-4]

 

UGAVI (MGAWANYO) WA NGAWIRA.

Usiku ule wa mzozo wa ngawira, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alilala katika bonde la Badri.

Kulipopambazuka akafunga safari kuelekea Madinah pamoja na maswahaba wake wakiambatana na mateka wao na ngawira waliyoipata kutoka kwa mushrikina.

Akaenda mpaka katikati ya safari akapiga kambi na akaanza kazi ya ugavi wa ngawira, akawagawia wote kwa usawa.

Akampa farasi aliyeenda vitani fungu moja na mpanda farasi fungu jingine, kwa hiyo mwenye farasi akapata mafungu mawili; fungu lake binafsi na fungu litokanalo na farasi wake. Fungu la mashahidi akawapa warithi wao.

Kuna kundi jingine la waumini hawakuweza kushiriki katika vita hivi kutokana na majukumu mengine waliyopewa na Bwana Mtume. Mbali na kundi hili lililopewa majukumu, lilikuwepo pia na kundi la watu wenye udhuru mkubwa usiozuilika na Mtume alikuwa akilijua hilo.

 Makundi mawili haya pia Mtume aliyagawia mafungu sawa na yale waliyopata wapiganaji.

Wapokezi wa sira-Allah awarehemu-wanasema: Baadhi ya maswahaba walishangazwa na kustaajabishwa na ugavi huu wa ngawira uliomlinganisha sawa mwenye nguvu na mnyonge. Wakashindwa kuvumilia, wakamuuliza Bwana Mtume ili kupata ufafanuzi wa ugavi wake ule usio wa kawaida. Alisema Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw-Allah amuwiye radhi:

“Nikauliza: Ewe Mtume wa Allah, hivi unampa mpanda farasi ambaye anawaendesha mbio makafiri sawa na kile unachompa mtu mnyonge (anayepigana kwa miguu)?”

 Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:

“Afiliwe nawe mama yako, nyinyi hamnusuriwi (hampati ushindi) ila kwa sababu ya wanyonge wenu”.

Kama kwamba kwa kauli hii ya Bwana Mtume alitaka kuzielekeza fikra za waislamu kwamba hili (ushindi) si suala la nguvu tu.

Kwani ingelikuwa hivyo basi waliokuwa na haki na nafasi ya ushindi walikuwa ni makafiri kutokana na nguvu ya zana bora na idadi kubwa ya watu, lakini mbona hawakushinda?!

Ugavi wa Mtume wa Allah haukuzingatia nguvu, bali ulilenga kujenga umoja na mshikamano baina ya waislamu kiasi cha kupewa hata wasioshiriki vitani.

Baada ya kumaliza kazi ile ya ugavi na kuwakinaisha maswahaba juu ya ugavi wake huo, Bwana Mtume akavunja kambi na kuendelea na safari ya Madinah.

Wakaenda mpaka wakafika mahala panapoitwa ‘Rauhaa’, Mtume akalakiwa na waislamu waliokuja kumpongeza kwa ushindi alioupata. Na wengine wakawa wanamueleza sababu za kutokushiriki kwao vitani.

 

NATIJA YA VITA VYA BADRI

UGOMBEZI WA NGAWIRA.

Ngawira walizozipata waislamu katika vita hivi zilikuwa ni nyingi ikiwa ni pamoja na ngamia, vyombo, mabusati ya ngozi, nguo na ngozi nyingi walizozichukua kwa ajili ya biashara.

Ngawira hii ikawa ni fitna inayokurubia kuwagawa maswahaba kutokana na mapenzi ya mali ambayo ni maumbile ya kila mwanadamu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *