VITA VYA AHZAAB

Mtume wa Allah autia ngomeni mji wa Madinah kwa kuchimba handaki kubwa kuzunguka  sehemu zote zilizo na upenyo.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipozijua khabari za jeshi hili shirika, akaitisha kikao cha dharura na maswahaba wake.

Ili kujadili hatua muafaka na ya haraka inayopaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na hatari inayowajongelea. Ndipo Salmaan AL-Faarisiy aliposema:

“Ewe Mtume wa Allah! Sisi kwetu katika nchi ya Uajemi (Fursi/Irani ya leo), tulikuwa tunapomchelea adui hujichimbia handaki (trench/ditch)”.

 Waislamu wakapendezwa na fikra hii ya kuchimba handaki na wakaiunga mkono na kuipitisha bila ya kupingwa.

Huyoo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akampanda mnyama wake akiwa na kundi la maswahaba wake katika Muhajirina na Answari.

Akawa akienda na kurudi katika eneo moja lililoko kaskazini mwa mji wa Madinah nyuma ya jabali “Sahli”, hapo akaweka alama za handaki, lichimbwe kuanzia sehemu kadha na kuishia mahala kadha.

Eneo hili la kaskazini mwa Madinah ndilo lililokuwa eneo wazi pekee ambalo adui anaweza kupenya na kuingia Madinah kwa urahisi.

Ama maeneo mengine yote yaliyosalia yalikuwa na ngome imara, kwa kuwa nyumba (maboma) zake kwa upande wa kusini zilikuwa ndefu zilizoungana na kufanya mithili ya ukuta madhubuti usioweza kupenywa kirahisi.

Na eneo la ardhi yenye mawe meusi kwa upande wa mashariki na lile la “Wabrah” kwa upande wa magharibi, kwa pamoja yaliunda ngome asili kwa pande mbili hizo.

Hali kadhalika vilima vya Bani Quraydhwah katika ule upande wa kusini-mashariki vilikuwa vinatosha kabisa kutoa ulinzi/himaya kwa kikosi cha nyuma cha jeshi.

Kwa hivyo kukawa hakuna uwezekano wa kushambuliwa waislamu kutokea upande huo ila kama Baniy Quraydhwah watawasaliti. Na kulikuwa baina yao na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-mkataba wa amani unao zitaka pande mbili hizi kutomsaidia adui wa mwenzake.

 

Mtume wa Allah ashirikiana na maswahaba wake katika kazi ya uchimbaji wa handaki.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawahamasisha maswahaba wake katika kazi ya uchimbaji wa handaki uliotokana na rai ya Salmaan Al-Faarisiy.

Akawapasha khabari ya kwamba adui yao yu karibu kuingia Madinah, kwa hiyo akatoa amri ifanyike jitihada maradufu katika kazi hiyo ili imalizike haraka kabla ya kuwasili adui.

Wakaomba msaada wa ziada ya vitendea kazi mithili ya sululu, majembe na machepe (makoleo) kutoka kwa Baniy Quraydhwah.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawapanga maswahaba wake katika makundi na kila kundi akalipangia sehemu yake ya kuchimba.

Kazi ikaanza kwa haraka na nguvu kubwa kiasi cha kumfanya Sayyidina Abu Bakri na Umar-Allah awawiye radhi-kubeba mchanga ndani ya kanzu zao kutokana na haraka waliyokuwa nayo.

Nae Bwana Mtume akawa anashirikiana na maswahaba wake katika kazi hiyo ili kuwahamasisha na alifanya kazi kwa jitihada kubwa kuliko ye yote miongoni mwa maswahaba.

Mara utamuona akichimba ardhi ngumu kwa sululu, wakati mwingne akiutoa mchanga handakini kwa kutumia chepeo/sepetu na wakati mwingine akiubeba mchanga kuuweka mbali na handaki.

Kutokana na kazi ngumu hii, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa taabani mno siku hiyo, akaegemea jiwe na kuchukuliwa na usingizi.

Sayyidina Abu Bakri na Umar-Allah awawiye radhi wakasimama mahala alipolala ili kuwazuia watu wasimuamshe.

Mara akazinduka kutoka usingizini, akavumburuka na kusema: “Kwa nini msiniamshe?”, akainuka na kuchukua vitendea kazi vyake na kusema:

Ewe Mola wa haki wee! Hakika maisha ni maisha ya akhera, basi ninakuomba uwaghufirie Muhajirina na Answar! Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba uwalaani watu wa Adhwala na Qaarah kwani wao ndio wamenikalifisha kuhamisha (kubeba) mawe!”.

Waislamu nao walikuwa wakiifanya kazi ya kuchimba handaki huku wakipandishana mori kwa kuimba mashairi, jambo lililowafanya waihisi nyepesi kazi hiyo nzito.

 Nae Mtume wa Allah hakuwa nyuma katika hili, akawa anaitikia nyimbo na mashairi yao. Imepokewa kutoka kwa Al-Baraai Ibn Aazib-Allah amuwiye radhi-amesema:

“Ilipokuwa siku ya vita vya Ahzaab na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akachimba handaki. Nilimuona akiutoa mchanga handakini mpaka sikuweza kuiona ngozi ya tumbo lake kutokana na kufunikwa na mchanga. Na alikuwa mwingi wa mashairi, nikamsikia akiyaimba maneno yaliyomo katika shairi la Abdullah Ibn Rawaahah wakati akihamisha mchanga:

{Ewe Mola wa haki wee! Lau si wewe sisi tusingeliongoka,

Wala tusingelitoa zakkah na wala tusingeliswali.

Basi tunakuomba utushushie utulivu juu yetu,

Hakika watawala wamefanya jeuri juu yetu,

Na wajapotaka kutufitini na dini yetu tumekataa}.

Halafu akiinua sauti yake anapousoma ubeti wa mwisho”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Kazi ikapamba moto, waislamu wakaifanya kwa upeo wa uweza wao mpaka ikafikia mmoja wao anapopatwa na dharura imuhitajishayo kutoka.

Humuendea Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kumtaka idhini, hata alipokwishakidhi haja yake hurejea tena kazini.

Wanafiki wao wakawa wanajiweka nyuma nyuma na wakifanya kazi nyepesi nyepesi na wakipenya na kwenda majumbani mwao bila ya idhini ya Mtume. Hapo ndipo Allah Taala alipoishusha kauli yake kwa waumini hawa:

“WAUMINI WA KWELI NI WALE WALIOMUAMINI ALLAH NA MTUME WAKE; NA WANAPOKUWA PAMOJA NAE KWA JAMBO LINALOHUSIANA NA WOTE, HAWAONDOKI MPAKA WAMUOMBE RUHUSA (Mtume). KWA HAKIKA WALE WANAOKUOMBA RUHUSA, HAO NDIO WANAOMUAMINI ALLAH NA MTUME WAKE. NA WATAKAPOKUOMBA RUHUSA KWA AJILI YA BAADHI YA KAZI ZAO, MRUHUSU UMTAKAYE MIONGONI MWAO (ukiona kuwa kweli ana udhuru), NA UWAOMBEE MAGHUFIRA KWA ALLAH. HAKIKA ALLAH NI MWINGI WA MSAMAHA (na) MWINGI WA REHEMA”. [24:62] Kisha akasema juu ya wanafiki: “MSIFANYE WITO WA MTUME BAINA YENU KAMA WITO WA NYINYI KWA NYINYI. HAKIKA ALLAH ANAWAJUA MIONGONI MWENU WALE WAONDOKAO KWA UTORO WAKIJIFICHA. BASI WAJIHADHARI WALE WANAOKAIDI AMRI YAKE, USIJE UKAWAPATA MSIBA AU ADHABU IUMIZAYO”. [24:63]

 

Mtume na maswahaba wapata taabu kubwa katika kazi ya uchimbaji wa handaki:

 Kazi hii ngumu iliwachukua waislamu takriban mwezi mzima tena katika kipindi cha baridi kali na upungufu mkubwa wa chakula. Hali ilikuwa ngumu mno kiasi cha kuwafikisha kufunga mawe matumboni mwao ili kujipa nguvu kutokana na njaa kali waliyokuwa nayo.

Lakini hili halikuinyongesha azma yao wala halikuidhoofisha ari na hamasa yao, kwani Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiwashajiisha na kuwatia nguvu.

Akitia nyoyoni mwao matumaini ya Uislamu kupata ushindi na kudhihiri sambamba na kuenea katika nchi jirani za Uajemi, Urumi na Yemen.

Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-amesema: Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake walichimba handaki wakiwa wame yafunga matumbo yao mawe kutokana na njaa. Mtume wa Allah alipoiona hali hiyo akasema:

Je, mmefahamishwa mtu atakayetulisha chakula?”, mtu mmoja akajibu: Naam. (Mtume) akasema: “Twende basi ukatuonyeshe”.

Wakaondoka kuelekea nyumbani kwa mtu huyo nae akiwa handakini akitekeleza wajibu wake, mkewe akamtumia mtu kumwambia: Njoo, hakika Mtume wa Allah-Rehema na Mani zimshukie-ametujia. Mtu yule akaja mbio mbio akasema: Kwa fidia ya baba na mama yangu!

Nae alikuwa na mbuzi jike mwenye mtoto, akamrukia kutaka kumchinja, Mtume akasema:

“Mchinje mtoto”. Basi akamchinja yule mtoto na mkewe akakanda unga na kuoka mikate, ilipoiva akaitia sahanini na kumuandikia Mtume wa Allah na maswahaba wake.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatia kidole chake sahanini na akasema:

“Bismillaah…Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba utubarikie katika chakula hiki! Haya kuleni”.

Wakala wote mpaka wakashiba na hawakuweza kula ila theluthi moja tu ya chakula chote na kubakia theluthi mbili. Mtume akawaambia wale watu kumi aliokuwa nao:

Nendeni mkawaite wenzenu. Wakaenda wakawaita nao wakaja wakala  mpaka wakashiba na kusaza. Halafu Mtume akainuka na kumuombea Mungu mama mwenye nyumba yeye na watu wa nyumba yake.

Halafu haoo wakaondoka kwenda kuendelea na kazi ya uchimbaji wa handaki. Mtume akasema: “Twendeni kwa Salmaan”, tahamaki ni huyoo mbele yake kuna mwamba mkubwa uliomuhemea, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema:

“Niacheni mimi ndio niwe wa mwanzo kulipiga (kulipasua) jiwe hili”. Akasema:

“Bismillaah!”, akalipiga kikaanguka kipande; theluthi yake, akasema:

Allaahu Akbar! Majumba ya Shamu na Mola wa Ka’abah!”. Kisha akapiga kwa mara nyingine, kikameguka kipande kingine, akasema:

“Allaahu Akbar! Majumba ya Uajemi na ninamuapia Mola wa Al-Ka’abah!”.

Hapo wanafiki wakasema:

“Sisi tunachimba handaki kwa ajili ya kujihami nafsi zetu nae anatuahidi majumba ya Uajemi na Urumi (wapi na wapi)!”

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *