HIJRA YA PILI YA UHABESHI

Baada ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kuingia kambini katika boma la Mzee Abu Twaalib, yeye na jamaa zake kufuatia vikwazo vya Makurayshi dhidi yao, Bwana Mtume aliwaamrisha baadhi ya maswahaba wake kuhamia Uhabeshi kwa mara nyingine tena.

Wakahamia huko kufuatia agizo la Mtume wanamume themanini na tatu, wanawake wanane pamoja na watoto kadhaa.

Miongoni mwa waliokuwemo katika hijra hii ya pili ya Uhabeshi ni Uthmani Ibn Affaan akiambatana na mkewe Bi. Rukia binti ya Mtume, mtoto wa ami yake Mtume Jaafar Ibn Aby Twaalib akiwa na mkewe Bi. Asmaa bint Umays, Miqdaad Ibn Aswad, Abdullah Ibn Masoud, Zubeyr Ibn al-awaam, Ummu Habiybah Bint Abiy sufyaan na wengineo wengi.

Walipofika Uhabeshi baada ya safari ndefu na yenye kuchosha, walipokelewa vizuri na Najaash Mfalme wa nchi hii ya Uhabeshi.

Wakapata amani, utulivu, salama na uhuru wa kuabudu bila ya kubughudhiwa na yeyote.

Mwanachuoni wa sera Ibn Al-athiyr- Allah amrehemu – anaelezea katika kitabu chake “AL-KAAMIL” hali ilivyokuwa na hatua zilizochukuliwa na Makurayshi katika kuidhibiti hali hiyo, anasema:

“ Makurayshi walipoona kuwa wahamiaji/wakimbizi wa Uhabeshi wamepata utulivu na amani katika nchi hiyo na kwamba Mfalme Najaash amewapokea vizuri walipanga njama, wakamtuma Amri Ibn Al-aaswi na Abdullah Ibn Abiy Rabiah wampelekee Najaash na mawaziri wake zawadi zenye thamani kubwa (hongo).

Wakaenda mpaka wakafika Uhabeshi, wakampelekea mfalme na mawaziri wake zawadi zao na wakamwambia mawaziri :

Hakika watu wapumbavu miongoni mwetu wameiacha dini ya jamaa zao na wala hawakuingia katika dini ya Mfalme (wa nchi hii) na wamezua dini mpya tusiyoijua sisi wala nyinyi. Mabwana viongozi wa jamaa zao wametutuma kwa mfalme warudishe kwao.

 Basi Mfalme atakapowataka ushauri kuhusiana na watu hawa, mwambieni awarudishe kwetu na asizungumze nao chochote .

Makurayshi wawili wale walichelea Najaash akisikiliza maneno ya Waislamu hatowatoa. Mawaziri wa Najaash baada ya kupokea hongo ile wakawaahidi kuwasaidia katika suala lao hilo.

 Kisha wakapelekwa mbele ya mfalme wakamuelezea haja yao, mawaziri wake wakamshauri awatoe waislamu. Mfalme akaghadhibika na kusema;

“Hapana, Wallah, sitowasalimisha watu waliokimbilia kwangu, wakashukia katika nchi yangu na wakanichagua mimi na si mwingine mpaka niwaite na kuwauliza juu ya wasemayo wajumbe hawa (kwa mkurayshi). Wakiwa ni wakweli (katika wayasemayo wawili hawa) nitawasalimisha wakimbizi hawa. Kama hawako kama wasemavyo(wajumbe hawa) sitawasalimisha (sitawatoa) na nitawafanyia ukimbizi mwema.

Najaash akawatumia mjumbe maswahaba wa mtume, awaite waje mbele yake. Wakahudhuria barazani kwa mfalme wakiwa na azma ya kumwambia ukweli mtupu.

Msemaji wao alikuwa ni Bwana Jaafar Ibn Abiy Twaalib. Mfalme Najaash akawauliza;

 “Ni dini gani hii ambayo imekutenganisheni na jamaa zenu na wala hamkuingia katika dini yangu wala dini ya mila yeyote ?” Jaafar akajibu kwa niaba ya wenzake:

“Ewe mfalme, sisi tulikuwa ni watu majahili, tukiabudu masanamu na kula mizoga, tukifanya mambo machafu na kukata udugu, tukivunja haki ya ujirani, mwenye nguvu miongoni mwetu akimuonea mnyonge mpaka pale Mwenyezi Mungu alipotuletea Mtume miongoni mwetu.

Tunaijua vema nasabu yake, ukweli wake, uaminifu wake na kujizuia kwake na machafu. (Mtume huyu) akatulingania kumpwkesha Mwenyezi Mungu na tusimshirikishe na kitu/mtu yeyote.

 Tuache kuyaabudu masanamu na akatuamrisha kusema ukweli, kutekeleza amana, kuunga udugu, kutekeleza haki za ujirani kuacha mambo ya haramu na kumwaga damu.

Akatukataza mambo machafu kusema uongo kula mali ya yatima na akatuamrisha kuswali na kufunga na akaendelea kumtajia mambo kadhaa yaliyoletwa na Mtume na Uislamu mpaka akafikia kusema: Basi tukamuamini (Mtume huyu) na kumsadiki, tukayaharamisha aliyotuharamishia na tukayahalalisha aliyotuhalalishia.

Hapo ndipo jamaa na ndugu zetu walipoanza kutufanyia maadui, wakatuadhibu na kutufitinisha na dini yetu ili turejee katika ibada ya masanamu.

Basi walipotuzidi nguvu na kautufanyia dhulma na kutuzuilia na dini yetu, ndipo tulipokuchagua wewe na sio mtu mwingine na tukatoka kwetu kuja katika nchi yako na tunatarajia kutokudhulumiwa mbele yako ewe Mfalme”

Baada ya balozi wa kwanza wa Uislamu Jaafar Ibn Abiy Twaalib kwisha kusema maneno hayo, Najaash akamuuliza tena:

“Je, unacho chochote alichokuja nacho Mtume wenu kutoka kwa Mwenyezi Mungu?” Jaafar akajibu: “Naam”, na akamsomea aya za mwanzo za Suurat – Mariam. Mfalme Najaash na Maaskofu wake wakalizwa na aya hizo, Najaash akasema :

“Hakika maneno haya na yale aliyokuja nayo Issa yanatoka katika shubaka moja (asili/chanzo kimoja)! Nendeni zenu (akawambia wajumbe wa Makurayshi) Wallah! sitawasalimisha kwenu watu hawa katu!” Amri Ibn Al-aaswi akamwambia Najaash (Maneno ya uchochezi):

Hakika watu hawa wanamsema vibaya Nabii Issa (wewe huwajui tu)” Najaash akawauliza maswahaba wanasema nini kuhusiana na Nabii Issa Masibu Jaafar akajibu :

Tunasema juu yake yale aliyotuletea Mtume wetu kwamba :

“Yeye (Issa) ni mja na Mtume wa Mwenyezi Mungu na ni Roho itokanayo naye (Mwenyezi Mungu kama roho nyingine) na (ni kiumbe aliyeumbwa kwa) tamko lake (tu Mwenyezi Mungu ) alilolitia kwa bikira Mariam”. Najaash akasema baada ya kusikia maneno hayo:

“Nabii Masihi Issa yuko hivyo hivyo, kama ulivyosema”. Akawageukia waislamu na kuwaambia:

“ Enendeni katika amani, sipendi nipate jabali la dhahabu na nikawa nimemuudhi hata mtu mmoja tu katika nyinyi,” na akazirudisha zawadi zote alizoletewa na Makurayshi kama hongo ili awafukuze waislamu katika nchi yake na kuwarudisha kwao Makkhah.

Hivi ndivyo jaribio hili la Makurayshi kutaka kuwarejesha waislamu adhabuni na matesoni lilivyoshindwa vibaya kutokana na msimamo wa waislamu kusema kweli mbele ya Mfalme Muadilifu, Mpenda haki Mfuasi wa kweli wa dini yake.

Waislamu wakaishi raha Mustarehe kwa amani na salama katika nchi ya Mfalme huyu. Mfalme huyu kama vitabu vya sera na tarekh vinavyosema alisilimu yeye pamoja na makasisi na mapadri waliokuwa wakimzunguka mbele ya kiongozi wa wakimbizi wa haki Bwana Jaafar Ibna Abiy Twaalib.

Inasemekana hakuishi muda mrefu baada ya kusilimu kwake, akafa. Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie – akapelekewa khabari za kifo cha Mfalme huyu na Malaika Jibrilu – amani ya Allah imshukie – kwa amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Baada ya kupata khabari hizi, Bwana Mtume aliwakusanya maswahaba na kumswalia marehemu mfalme huyu swala ya maiti ghaibu na huo ulikuwa ni mwaka wa saba wa utume.

Ama tukirejea nyuma kuwaangalia maswahaba wa Mtume, wakimbizi waliopata amani, utulivu, ulinzi na usalama pia haki na uhuru wa kuabudu katika nchi hii ya ughaibuni, waliendela kuishi katika nchi hii baada ya kupata baraka zote za mfalme na hasa pale alipowarejesha maadui zake Makkah mikono mitupu.

Hakuna hata mtu mmoja kati yao aliyerejea Makkah ila Bwana Uthman Ibn Affaan, kwani yeye baada ya kuhakikisha kuwa waislamu wako katika hali ya amani na salama alirejea Makkah pamoja na mkewe Rukia binti aya Mtume ili kwenda kusaidiana na Mtume katika kuieneza da’awah ya Uislamu.

Ama wahamiaji wengine wote waliendela kuishi ugenini uhabeshi kwa kipindi cha muongo mmoja (takriban miaka kumi na moja).

Hii ni kwa mujibu wa watalamu wa sera na tarekh. Hawakurudi mpaka Bwna Mtume alipohamia Madinah na kurudi kwao ilikuwa ni baada ya mkataba wa suluhu ya Hudaibiyah baina ya Makurayshi na Bwana Mtume

 

HIJRA YA PILI YA UHABESHI

Baada ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – kuingia kambini katika boma la Mzee Abu Twaalib, yeye na jamaa zake kufuatia vikwazo vya Makurayshi dhidi yao, Bwana Mtume aliwaamrisha baadhi ya maswahaba wake kuhamia Uhabeshi kwa mara nyingine tena.

Wakahamia huko kufuatia agizo la Mtume wanamume themanini na tatu, wanawake wanane pamoja na watoto kadhaa.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published.