Kumesuniwa katika adhana kufanya mambo yafuatayo:-
1. KUELEKEA QIBLAH: Ni suna muadhini kuelekea Qiblah wakati wa kuadhini, kwa sababu bora ya pande za kuelekewa kwa ajili ya ibada ni upande uliyoko Qiblah.
Na hakuna hata mmoja anayeweza kuthubutu kukanusha uibada wa adhana.
Na isitoshe imethibiti kwamba waadhini wa Bwana Mtume-Allah awawiye radhi-walikuwa wakielekea Qiblah wakati wa kuadhini.
2.TWAHARA YA HADATHI NDOGO NA KUBWA: Ni suna mtu kuadhini hali ya kuwa yu katika hali ya twahara, yaani hana hadathi ndogo inayompasishia udhu wala ile kubwa inayompasishia josho.
Kwa maana hii, ni karaha kuadhini mtu mwenye hadathi ndogo (asiye na udhu).
Na ukaraha unazidi zaidi kiasi cha kuelekea kwenye uharamu kwa mtu mwenye janaba (hadathi kubwa). Amesema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie:
“Nachukia (sipendi) kumdhukuru Allah Mtukufu ila niwe na twahara”.
Abuu Daawoud & wengineo
3. KUSIMAMA WIMA: Ni suna mtu kuadhini hali ya kuwa amesimama, hili linatokana na kauli ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie:
“Ewe Bilali simama unadi swala (uadhini)”.
Bukhaariy & Muslim
Ikiwa mtu ana udhuru kama ugonjwa akisimama ataanguka au maumivu yatazidi, basi ataadhini kwa kukaa kwa sababu:
“ALLAH HAIKALIFISHI NAFSI YO YOTE (kutenda) ILA YALIYO SAWA NA UWEZA WAKE…” [2:286]
4. KUGEUZA SHINGO KULIANI NA KUSHOTONI: Miongoni mwa suna za adhana kama zilivyothibiti kutoka kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.
Ni pamoja na muadhini kugeuza shingo yake kuliani wakati wa kusema: (Hayya alas-swalaah) na kushotoni anaposema: (Hayya Alal-falaah).
Imepokewa kwamba Abuu Juhayfah-Allah amuwiye radhi-amesema:
“Nilimuona Bilali akiadhini, nikawa ninaufuatilia mdomo (kinywa) wake huku na huko. (Akageuka) kuliani na kushotoni (wakati wa kusema): Hayya Alal-swalaah, Hayya Alal-falaah”. Bukhaariy
5. KUFANYA TARJI’I: Ni suna muadhini kuleta matamko ya shahada mbili.
Yaani (Ash-hadu An-laa Ilaaha Illal-laahu) na (Ash-hadu Anna Muhammadan Rasuulullaah) kwa siri (sauti ya chini), kabla ya kuyajihirisha (kuyatamka wazi/kwa sauti).
Suna hii imethibiti katika hadithi ya Abuu Mahdhuurah-Allah amuwiye radhi-kama ilivyopokelewa na Imamu Muslim-Allah amrehemu:
“…Kisha hurudia (hufanya Tarji’i) akasema: Ash-hadu An-laa Ilaaha Illal-laah…”
6. KURATILI MANENO YA ADHANA (KUYALETA KWA NJIA/MTINDO WA TARTIYLI): Ni katika jumla ya suna mtu kuadhini kwa “Tartiyli”.
Yaani ayatamke maneno ya adhana kwa mtungo wa utuvu mithili ya mtu aimbaye kidogo.
Na si kutetea kwa kuivuta mno sauti kiasi cha kutokueleweka maneno au kuharibika herufi.
Hili linatokana na kuizingatia adhana kuwa ni tangazo la kuwajulisha walio mbali kuingia kwa wakati wa swala. Ikawa mtindo huu wa “Tartiyli” ni fasaha zaidi katika kufikisha tangazo kwa walengwa.
7. KULETA “TATH-WIYBU” KATIKA ADHANA YA ALFAJIRI: “Tath-wiybu” ni muadhini kusema baada ya (Hayya alal-falaah x2); ASWALAATU KHAYRUN MINAN-NAUM, mara mbili.
Amesema Bilali-Allah amuwiye radhi: Aliniamrisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kuleta “Tath-wiybu” katika adhana ya Alfajiri”.
Ahmad, Abuu Daawoud & wengineo
8. SAUTI KALI (INAYOFIKA MBALI) NA NZURI: Ni suna muadhini kuwa na sauti kali na nzuri itakayomudu kuulainisha moyo wa msikilizaji na kumpelekea kuuitika wito huo.
Suna hii inatokana na kauli ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomwambia Abdullah Ibn Zayd-Allah amuwiye radhi-ambaye ndiye aliyeiona adhana usingizini: “Inuka/simama pamoja na Bilali, umtamkishe (maneno) uliyoyaona (usingizini) na aadhini kwayo. Kwani yeye ana sauti kali kuliko wewe”.
Abuu Daawoud & wengineo
9. TABIA NJEMA: Muadhini anapaswa kutangaa baina ya watu kwa tabia njema na uadilifu.
Hii ni kwa sababu tabia njema na uadilifu huwapelekea watu kumsadiki anapowapa khabari ya wakati (adhana).
10. KUTOKUTETEA: Ni suna kuacha kutoa adhana kwa kutetea, yaani kuvuta mno sauti kiasi cha kupelekea kuharibika kwa maana au kutokueleweka maneno. Adhana isigeuzwe nyimbo ambapo mtu hughani upeo wa sauti yake, hilo ni karaha.
11. WAADHINI WAWILI: Ni suna msikiti kuwa na waadhini wawili kwa ajili ya swala ya alfajiri. Mmoja ataadhini kabla ya kuingia kwa alfajiri na mwingine baada ya alfajiri.
Suna hii imethibiti kutokana na hadithi (riwaya) ya Abdullah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi: “Hakika Bilali huadhini usiku, basi kuleni na kunyweni mpaka muisikie adhana ya Ibn Ummu Maktuum”. Bukhaariy & Muslim
Falsafa ya adhana nje ya wakati ni kwa ajili ya kuwaamsha watu kujiandaa na kujitayarisha kwa ajili ya swala, hiyo ndio ilikuwa adhana ya Bilali.
Lakini kunatakikana kwa muadhini huyu anayeadhini nje ya wakati kuwa na wakati mmoja ili kuepuka kuwatatiza na kuwachanganya watu.
Kama ada yake ni kuadhini saa kumi kamili, basi siku zote aadhini ndani ya wakati huo. Sio leo kaadhini saa kumi, kesho saa tisa na keshokutwa saa kumi na nusu.
12. KUNYAMAZA (KUKAA KIMYA): Ni suna kwa mwenye kusikia adhana kukaa kimya na kuisikiliza adhana hiyo na kusema mithili ya anavyosema muadhini.
Dalili ya usuna huu ni kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Mtapousikia wito (wa swala), basi semeni mithili ya asemavyo muadhini”. Bukhaariy & Muslim
Lakini wakati muadhini ataposema: “HAYYA ALAS-SWALAAT X2, HAYYA ALAL-FALAAH X2”.
Yeye mwenye kumsikia atasema: “LAA HAWLA WALAA QUWWATA ILLA BILLAAH”. Haya ni sehemu ya mafundisho ya hadithi:
“Na (muadhini) ataposema: Hayya alas-swalaah, aseme (anayemsikia): Laa hawla walaa quwwata illa billaah. Na ataposema: Hayya alal-falaah, aseme: Laa hawla walaa quwwata illa billaah”. Bukhaariy & Muslim.
Ama katika “Tathwiybu”- yaani muadhini anaposema: “Asswalaatu khayrun mina-naumu” katika swala ya alfajiri, ni suna amjibu kwa kusema: “Swadaqta wabararta”.
13. KUOMBA DUA NA KUMSWALIA MTUME BAADA YA ADHANA: Kunasuniwa kwa wote wawili; muadhini na mwenye kumsikia muadhini kumswalia Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-mara tu baada ya kumalizika kwa adhana.
Kisha waombe dua iliyopokewa kutoka kwa Mtume na akatuhimiza sana kuisoma kila baada ya adhana. Haya yote ni kwa mujibu wa hadithi iliyopokewa na Abdullah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye alimsikia Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akisema:
“Mtakapomsikia muadhini, basi semeni mithili ya asemavyo kisha niswalieni. Kwani hakika mwenye kuniswalia mimi swala moja (tu), Allah atamswalia (mtu huyo kwa swala moja) hiyo swala kumi. Kisha niombeeni “wasiyla” kwa Allah, kwa sababu hiyo wasiyla ni daraja/cheo cha peponi. Haitakikani daraja/cheo hicho ila kwa mja miongoni mwa waja wa Allah na ninataraji kuwa mimi ndiye (mja huyo). Basi ye yote atakayeniombea wasiyla huo, umemuhalalikia (ameupata) uombezi wangu (siku ya kiyama)”. Muslim & wengineo
Na dua inayotakiwa kusomwa baada ya adhana ni kama ilivyopokelewa na swahaba Jaabir-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Atakayesema wakati (anapomaliza) kusikiliza adhana:
ALLAAHUMMA RABBA HAADHIHID-DA’AWATIT-TAAMMAH, WASSWALAATIL-QAAIMAH, AATI SAYYIDANAA MUHAMMADAN AL-WASIYLAH WAL-FADHWIYLAH, WAB-ATH-HU MAQAAMAN MAHMUUDANIL-LADHIY WA’ADTAHU, umemuhalalikia uombezi wangu siku ya kiyama”. Bukhaariy & wengineo.
MAANA YA MATAMKO YA DUA:
Allaahumma: Ewe Mola wa haki wee!
Rabba haadhihid-da’awatit-taammah: Bwana wa wito huu (wa Tauheed) uliotimia (usoingiliwa na mabadiliko).
Aati sayyidanaa Muhammadan: Ninakuomba umpe Bwana wetu Muhammad.
Al-wasiylah: Wasila (Ukaribu na Allah/daraja peponi).
Wal-fadhwiylah: cheo chenye kuzidi viumbe wote.
Wab-ath-hu: na umpe
Maqaaman mahmuudah: uombezi mkubwa siku ya kiyama.
Alladhiy wa’adtahu: ambao uliomuahidi.Ahadi hii ya Allah kwa mtume aliye kipenzi chake imo katika kauli yake: “…HUENDA MOLA WAKO AKAKUINUA CHEO KINACHOSIFIKA”. [17:79]
Muadhini anatakiwa kumswalia Bwana Mtume na kuomba dua kwa sauti ya chini na sio kwa sauti kama ile aliyoitumia katika kuadhini.
Isije kuchukuliwa na kudhaniwa kwamba hiyo swala ya mtume na dua ni sehemu ya adhana.
Ni vizuri kwa muadhini mwenye kutumia kipaaza sauti kumswalia Bwana Mtume na kuomba dua baada ya kuzima kipaaza sauti hicho.
14. UUNGWANA, UKUBWA, WEMA NA UJUZI WA WAKATI:
Kumesuniwa Muadhini kuwa:-
Muungwana (huru), yaani asiwe mtumwa anayeweza kuzuiwa na bwana wake kutoka kwenda kuadhini.
Mkubwa (mtu mzima) mwenye akili timamu anayejua anachokifanya, asiwe mtoto mdogo ambaye hajabaleghe bado.
Mtu mwema, mwenye tabia njema, anayekubalika na jamii, asiwe mtu fasiki mwenye mambo ya hovyo hovyo.
Mjuzi wa nyakati za swala.
Suna hii ni kama ilivyothibiti katika hadithi ya Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi:
“Akuadhinieni aliye mbora wenu na akuswalisheni msomi wenu zaidi wa Qur-ani”.
TANBIHI: Isieleweke kwamba haisihi adhana ya mtumwa wala mtoto mdogo, wakiadhini adhana yao itasihi lakini si suna kwao kuadhini kama wapo watu wenye sifa.
15. UONI WA MUADHINI: Ni suna muadhini kuwa mtu mwenye kuona, asiwe kipofu kwani kipofu hajui wakati ila kwa msaada.
Lakini kipofu akiadhini adhana yake itasihi kwa sababu Ibn Ummu Maktuum (swahaba wa Mtume aliyekuwa kipofu) alikuwa akimuadhinia mtume wa Allah.
Amesema Ibn Amrou katika riwaya iliyopokelewa na Imamu Bukhaariy:
“(Ibn Maktuum) alikuwa ni mtu kipofu, hanadi swala mpaka aambiwe: kumekucha kumekucha”.
16. KUWEKA VIDOLE MASIKIONI: Kumesuniwa kuweka vidole masikioni wakati wa kutoa adhana, kwa sababu kufanya hivyo kuna msaada mkubwa katika kunyanyua sauti.
Usuna huu wa kuweka vidole masikioni wakati wa kuadhini unatokana na riwaya iliyopokewa na Imamu Abuu Haniyfah-Allah amrehemu-
“Kwamba Bilali aliadhini na akaweka vidole vyake masikioni”. Bukhaariy & Muslim.
Kadhalika imepokelewa kutoka kwa Sa’ad; muadhini wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-
“Kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimuamrisha Bilali kuweka vidole vyake katika masikio yake na akasema: Hakika kufanya hivyo kunaiinua zaidi sauti yako”. Ibn Maajah, Al-Haakim, Twabaraaniy & Ibn Adiy.
17. KUJITOLEA (KUTOKUADHINI KWA UJIRA): Ni suna mtu kuadhini kwa kutaraji ujira kutoka kwa Allah, asichukue ujira kwa kazi hiyo.
Hili ndilo kongamano la wanazuoni wote, hii ni kwa sababu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Uthmaan Ibn Abul-Aaswi:
“Na umuweke muadhini asiyechukua ujira kwa adhana yake”. Abuu Daawoud, Ibn Maajah & Tirmidhiy.
TANBIHI: Ikiwa watu wataifanya adhana kuwa ni kazi maalumu kama zilivyo kazi nyingine, basi kutajuzu kuchukua ujira kwa kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ya uongozi wa msikiti husika na muadhini aliyeajiriwa.