Chimbuko la somo letu la leo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ndani ya Qur-ani Tukufu
“……….WALA USITAWANYE (mali yako ) KWA UBADHIRIFU HAKIKA WATUMIAO KWA UBADHIRIFU NI NDUGU WA MASHETANI (wanamfuata shetani) NA SHETANI NI MWENYE KUMKUFURU MOLA WAKE” (17: 26-27).
Huu ndio ukatikati wa matumizi, kutumia mali kwa kiasi cha haja kama ilivyo ndani ya Qur-ani na hii ndio desturi ya Uislamu. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akimuomba Mola wake akisema:
“Ewe Mola wa haki! Ninakuomba (uniwezeshe) kukuogopa katika siri na dhahiri, na ninakuomba neno la ikhlasi katika ghadhabu na ridhaa na ninakuomba ukatikati wa matumizi katika ufakiri na ukwasi” Nasaai na Al-Haakim kutoka kwa Ammaar Ibn Yaasir
Ukatikati wa matumizi ni kutokufanya ubadhirifu na ufujaji katika matumizi ya mali sambamba na kutokujidhili na kujidhiki katika matumizi.
Ukatikati wa matumizi ni pamoja na kuwa na mipango mizuri (bajeti) ya matumizi ya kila siku (ya muda mfupi) na yale ya muda mrefu (ya mwaka au miaka) .
Hii ni sifa/tabia ya msingi na muhimu anayotakiwa kila muislamu bali kila mtu kujipamba nayo. Inatakikana mtu awe anajiwekea akiba japo kidogo kutokana na pato lake ili iweze kumsaidia wakati wa dharura /haja na wakati wa utu uzima ambapo hataweza kuchuma tena.
Ni dhahiri kuwa hili la kujiwekea akiba halitawezekana ila kwa kuwa na mipango thabiti na matumizi mazuri ya mali.
Ukatikati wa matumizi ni kutokutumia zaidi ya haja kwani huo utakuwa ni ubadhirifu na ufujaji ambao tumekatazwa na kukemewa na Mola wetu na pia ni kutokutumia chini ya haya na il-hali unacho cha kukutosha, huko kutakuwa ni kujidhiki kusiko na nafasi katika Uislamu.
Utakuta mtu amehodhi na kumiliki mali kiasi alichojaaliwa na Mola wake lakini anajidhiki yeye mwenyewe, mkewe, wanawe, ndugu na jamaa zake .
Mola wake amemkunjulia yeye anajidhiki ni akili gani hii, ni ya nini basi neema hii? Wakati wa Bwana Mtume mtu mmoja alikuja kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – hali (namna alivyo) yake haikumpendeza Mtume, akamuuliza
“Unayo mali?” Akamjibu : Naam, (Mtume) akamuuliza tena, “Ni aina gani ya mali uliyonayo? “ Akajibu: Nina kila aina ya mali aliyonipa Mwenyezi Mungu (Yaani anao ngamia, ng’ombe, mbuzi, Kondoo, mazao na matunda) Mtume akamwambia , “Basi hakika Mwenyezi Mungu anapenda kuiona athari ya neema zake alizokuneemesha” Tirmidhiy na Al-Haakim.
Mwenyezi Mungu Mtukufu pia anatuambia juu ya hili:
“NA NEEMA YA MOLA WAKO ISIMULIE”. (93:11) yaani izungumze kwa njia ya kushukuru si kwa ajili ya kujisifia na kujigamba .
Ni vema ikakumbukwa kuwa kuizungumza neema ya Mwenyezi Mungu aliyokueneemesha hakukomelei tu kuitaja kwa ulimi bali kwa hali pia.
Huna sababu hata kidogo ya kujidhili kwa njaa, kuacha kujenga nyumba nzuri, kula chakula kizuri, kuvaa vizuri na kuwadhiki mkeo , wanao na wazazi wako na Il-hali neema ya Mola wako i mikononi mwako.
Hujakatazwa kutumia kwa nafasi na kiasi ulichokatazwa ni ubadhilifu na ufujaji, tusome na tutafakari
”……….. NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri) LAKINI MSIPITE KIASI HAKIKA YEYE (Mwenyezi Mungu) HAWAPENDI WAPITAO KIASI (wapindukiao mipaka)” (7:31).
Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuasa
“Bora ya dinari (pesa) anayoitumia mtu ni ile dInari anayoitumia kwa ajili ya familia yake, na dinari anayoitumia kwa ajili ya (chakula cha) farasi wake katika njia ya Mwenyezi Mungu na dinari anayoitumia kwa ajili ya wenziwe katika jihadi” Muslim na Turmidhiy.
Na akasema tena Mtume kumwambia Sa’ad Ibn Abiy waqasi
“Hakika hukutoa cho chote (chakula /matumizi) ukitafuta kwa utoaji huo radhi za Mwenyezi Mungu ila utapewa ujira kwa, hata kile unachokitia ktika kinywa cha mkeo” Bukhaariy na Muslim.
Ukatikati wa matumizi, kutumia kwa kiasi ni sifa/tabia muhimu sana na yenye faida kubwa sana. Tabia hii humuingiza Muislamu katika fungu la waja wa Mwenyezi Mungu awapendao. Mwenyezi Mungu anatuambia
“NA WAJA WA RAHMANI (Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema)…”(25:63) akaisifia hali yao wenyewe namna walivyo, hali yao pamoja na wanadamu wenzao yaani namna wanayoishi nao, hali yao naye yaani mahusiano na mafungamano yao na Mola wao, kisha ndipo akaitaja hali yao na mali zao. Akasema,
“NA WALE AMBAO WANAPOTUMIA HAWATUMII KWA FUJO WALA HAWAFANYI UBAHILI BALI WANAKUWA KATIKATI BAINA YA HAYO” (25: 67).
Hawa ndio waja wa Rahmani hawaitumii neema ya Mola wao kwa fujo na wala hawafanyi ubahili kwao wenyewe, familia zao, jamaa na ndugu zao pamoja na jirani zao.
Wala hawafanyi ubahili kutoa kuwasaidia waislamu wenzao katika majanga mbalimbali yanayowasibu kama vile kufuta ujinga, maradhi, umasikini uliokithiri, mafuriko, ukame na kadhalika. Na zaidi ya yote hayo hawafanyi ubahili kutoa haki ya Mwenyezi Mungu liyowapasa yaani Zakah.
Hawa hawafanyi kabisa ubadhilifu na ufujaji katika matumizi yao ubadhirifu/ufujaji ni pale mtu anapotumia neema ya mali aliyopewa katika njia za maasi kama vile ulezi, madawa ya kulevya, zinaa, kuchezea kamari, kuingilia disko na mambo mengine ya haramu au kutumia katika mambo ya Mubah kwa kupita kiasi, akawa anakula anasa na kutupa, anabadili nguo kutwa, mara nne, ana magari ya kutembelea yeye na familia yake zaidi ya matatu, hii pia ni aina ya ubadhirifu.
Muislamu hatakiwi kujitanua sana katika matumizi zaidi ya haja au uwezo wake, mtu ajikune pale unapofikia mkono wake.
Muislamu anatakiwa apime na kuwa na uwiano baina ya mapato na matumizi yake, matumizi yasizidi mapato yake, bali matumizi yawe chini kuliko mapato na ikiwezekana awe na akiba anayoiweka kutokana na mapato yake, hayo huu ndio ukatikati wa matumizi unaozungumzwa na Uislamu.
Muislamu hatakiwi kujitnua mno kusikokuwa na sababu ila ufakhari na sifa tu, kiasi cha kumweka katika mzigo wa madeni yasiyolipika.
Muislamu lazima atambue kuwa kuchukua deni bila ya kuwa na uhakika wa kulipa ni kosa/dhambi , ajue kuwa deni ni udhalili, ni utumwa, ni hangaiko la moyo na ni mzigo akhera. Kwanini basi ajitie kaitka janga hili bila ya sababu ya msingi?! Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuonya
“Atakayechukua mali za watu kwa lengo la kulipa, Allah atamlipia (yaani atampa uwezo wa kulipa ) na atakayechukua mali za watu (deni) kwa lengo la kuzitilifu, Allah atamtilifu (yaani atamuagamiza yeye na mali yake hiyo ya dhulma)”Bukhaariy na Ibn Maajah.
Hivi ndiyo anavyokuwa au anavyotakiwa kuwa Muislamu, anapotumia hatumii kwa fujo wala hafuji mali ovyo ovyo kwani anaitakidi kuwa Mtume -Rehema na Amani zimshukie- amekataza na kukemea ufujaji wa mali, ufujaji wa neema,
“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amekuharanishieni kuwaasi mama (zenu) kuwazika watoto wa kike wakiwa hai, kufanya ubahili na kuomba, na anachukia kwenu, usengenyi, kuuliza sana, na ufujaji wa mali” Suyuty al-Jaamii As-Swaghyr.
Itakidi kuwa mali yoyote uliyonayo mkononi unayomiliki si yako hiyo ni ya jamii nzima utakapoitumia usivyostahili utakuwa umejidhulumu wewe mwenyewe bali na jamii nzima.
Kwa mantiki hii, tunasema yeyote anayeitumia pesa yake katika kubugia tumbaku au kuvuta sigara kwa mfano, huyu anajifujia mali yeye na anaifujia jamii pia .
Anajidhuru yeye mwenywe kwa pesa yake mwenyewe kwa sumu ya tumbaku isio na chembe ya faida mwilini mwake.
Kumbuka mali ni neema inakupasa kuihifadhi na kuwa na matumizi sahihi/halali.
Kuna miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiislamu inayohitaji msaada wa mitaji, waislamu wanahitaji mashule, wanahitaji mahospitali, wanahitaji misikiti, mayatima wanahitaji kulelewa, wasiojiweza wanahitaji matunzo, waislamu wamegubikwa na umasikini na njaa wanahitaji kukwamuliwa.
Kwa nini basi, pesa hii tunayoifuja katika uvutaji wa sigara, ulevi, kamari, disko, na zina isielekezwe kule katika maeneo hayo?!
Ubadhirifu na ufujaji umekuwa ndio nembo yetu, tunafanya ubahili kutoa katika mambo ya kheri na tunaona fakhari na sifa kutoa katika mambo ya shari na haramu.
Tunatumia mamilioni ya pesa katika kudhamini mashindano ya urembo, matamasha ya muziki na kadhalika huku mayatima wanakosa haki yao ya kupatiwa elimu.
Waislamu tubadilike sasa, tuzidhibiti nafsi zetu, tuwe na kipimo na kiasi katika matumizi/utoaji wetu.
Tuwe wakatikati na matumizi yetu ya kila kitu, hii ndio sifa na tabia ya Muislamu.