Mji wa Makkah ndio kitovu na chimbuko la kuenea dini ya Kiislamu. Mji huu upo katika nchi ya Hijazi, nchi ambayo imechukua eneo kubwa la Bara Arabu. Nchi hii ya Hijazi ilikaliwa na makabila mengi ya Kiarabu, kabila mashuhuri zaidi lilikuwa ni Qurayshi.
Historia ya mji wa Makkah na kuanzishwa kwake inaanzia pale alipofika katika mji huo kwa mara ya kwanza Nabii Ibrahimu – Amani na Rehma za Allah zimshukie – akitokea nchi ya Palestina akiwa pamoja na mkewe Haajira na mwanawe Ismail.
Wakati huo mji wa Makkah ulikuwa ni jangwa tupu lililozungukwa na majabali.
Nabii Ibrahimu akamuacha mkewe na mwanawe katika jangwa hilo tupu lisilo na mimea na kurejea Palestina.
Kabla ya kufunga safari ya kurudi Palestina Nabii Ibrahimu alimuomba Mola wake Mtukufu rehema zake ziyatawale maisha mapya ya mkewe na mwanawe jangwani hapo na Mola Muumba aliipokea na kuikubali dua ya Mtume wake kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani. Mwenyezi Mungu akamchimbulia mama Haajira na mwanawe Ismail chemchem ya Zamzam katika ardhi kame ya jangwani.
Wasafiri wapitao njia ile walipokiona kisima cha Zamzam walikwenda mahala pale na kuamua kuishi kandokando ya chemchem ile, hii ni kutokana na shida sugu ya maji jangwani.
Tangu wakati huo kitongoji hicho kikaanza kustawi mpaka kikawa ndio kitongoji mama cha nchi ya Hijazi.
Mtoto Ismail alipofikia umri wa kuoa alioa katika makabila yale ya Waarabu waliokuja kukaa pale na kuuanzisha mji wa Makkah. Akajaaliwa kupata watoto.
Ibrahimu baba yake Ismail akawa anafanya ziara za mara kwa mara kujulia hali mkewe, mwanae na wajukuu zake.
Katika mojawapo ya ziara zake hizi ndipo Mwenyezi Mungu alipompelekea wahyi wa kuijenga A-kaaba.
Ibrahimu na mwanawe wakaitekeleza amri ya Mola wao wakaijenga Al-kaaba. Mwenyezi Mungu akamuamrisha Nabii Ibrahimu awaite watu kuja kuhiji na kufanya ibada katika nyumba yake hiyo tukufu.
Ujenzi huu wa nyumba tukufu ya Mwenyezi Mungu na ibada tukufu ya Hijjah ndivyo vilivyoufanya mji wa Makkah kuwa ni mji mtakatifu. Hii ndio historia fupi ya kuasisiwa mji wa Makkah.