Inajuzu/inafaa kustanji (kuchamba) kwa kutumia maji mutlaq (maji halisi) ambayo ndiyo asili katika kujitwahirisha na najisi. Pia inajuzu kustanji kwa kila kitu chenye sifa zifuatazo :
i.Kigumu (kigogofu)
ii.Chenye Kuparuza (kisichoteleza)
iii.Kinachoweza kuondosha najisi.
Vitu vyenye sifa hizi ni kama mawe, karatasi, kitambaa na kadhalika.
Ni vema kustanji, mtu akaanza kwa kutumia mawe/karatasi kisha ndio akamalizia na maji.
Kufanya hivyo ni kwa sababu mawe/karatasi huondosha juta (dhati) ya najisi na maji huondosha athari ya najisi bila ya kuchangayika na juta lake.
Ikiwa atatumia kimojawapo baina ya mawe/karatasi na maji, basi ni bora akatumia maji kwani ndiyo pekee yenye uwezo wa kuondosha juta (dhati) na athari ya najisi, kinyume na mawe na nduguze {karatasi, kitambaa na kadhalika}.
Imepokelewa kutoka kwa Anas Ibn Maalik – Allah amuwie Radhi – amesema :
Mtume wa Allah alikuwa akiingia mahala pa kukidhi haja, mimi na kijana wa rika langu tukimbebea chombo cha maji na fimbo/mkuki mfupi, basi akistanji kwa kutumia maji. Bukhariy na Muslim.
Maelezo : Fimbo/Mkuki ulikuwa ukitumika kama sitara na alama wakati wa kuswali ili mtu asiweze kupita mbele.
Imepokewa na Ibn Masoud – Allah amuwie Radhi – amesema :
Mtume – Rehma na Amani zimshukie – alienda kukidhi haja na akaniamrisha nimletee mawe matatu. Al-Bukhariy.
USISTANJI kwa kutumia najisi nyingine iliyo kavu au kitu kilichonajisika tayari kwani huenda kikaizidisha athari ya najisi badala ya kuipunguza.
Kadhalika ni haramu kustanji kwa kilicho chakula cha binadamu kama vile mkate au chakula cha majini kama vile mifupa. Amesema Bwana Mtume – Allah amshushie Rehma na Amani –
“Msistanji kwa (kutumia) kinyesi cha wanyama wala mifupa kwani hiyo (mifupa) ni chakula cha ndugu zenu majini” Tirmidhiy.