Kabla hatujaingia moja kwa moja kuilezea swala na uchambuzi, ni vema kwanza tukajiuliza swala ni nini, ili tutakapokuwa tunalitaja neno swala, tujue na kuelewa tunazungumzia kitu/jambo gani.
Haya sasa, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu Mtukufu Mjuzi wa yote tuanza kuingalia maana ya swala, tunasema:- swala ni neno la Kiarabu lililobeba maana mbili, maana ya kilugha na maana ya istilahi ya fiq-hi (sheria).
Tukiipekuwa na kuiangalia Qur – ani Tukufu tutalikuta neno swala limetumika kwa maana ya dua njema na hii ndiyo maana ya swala kilugha, tusome:-
“CHUKUA SADAKA KATIKA MALI ZAO UWASAFISHE NA KUWATAKASA KWA AJILI YA HIZO (sadaka zao) NA KUWATAJA KWA VIZURI (mbele yangu) NA UWAOMBEE DUA. HAKIKA KUWAOMBEA KWAKO KUTAWAPA UTULIVU (watengenekewe) NA ALLAH NDIYE ASIKIAYE NA AJUAYE” (9:103).
Ama katika Istilahi ya kifiq-hi (sheria) neno “swala” linajulikana kama ibada maalum inayokusanya kauli (maneno) na matendo maalum yanayoanzwa kwa Takbira na kukhitimishwa kwa kutoa salaamu.
Hiyo ndio swala kwa mtazamo wa sheria, kwa nini basi ibada hii ikaitwa “swala” na sio jina jingine lisilo hili ?
Katika kulijibu swali hili tunaweza kabisa kusema kuwa ibada hii imeitwa swala kutokana na kukusanya kwake dua/maombi maalum ya mja kwa Mola wake kitu ambacho ndio sehemu kubwa ya Ibada nzima ya Swala.