KERO ZA MAKURAISHI DHIDI YA MTUME

Makurayshi walipoona juhudi zao za kumuendea kiongozi wao Mzee Abu Twalib ili amzuie mwana wa nduguye kuwatukania miungu wao zimegonga mwamba, hazikuzaa matunda yeyote.

Na moto wa Daawah ya dini mpya ndio unazidi kushika kasi na watu wanazidi kumfuata Nabii Muhammad.

Hapo ndipo wakaamua kujaribu kutumia mbinu ya kumfanyia kero na maudhi anuwai sambamba na kumfanyia maskhara. Khasa khasa alipokuwa akienda kuswali.

Katika jumla ya maudhi aliyofanyiwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – ni ile hekaya iliyopokelewa na Abdullah bin Masoud – Allah amuwie Radhi – amesema : Tulikuwa msikitini pamoja na Mtume wa Allah akiswali. Akasema Abu Jahli :

Hivi hapana mtu akayaendea matumbo ya kinyesi cha ngamia wa Baniy Fulani akaja akamtupia huyu Muhammad il-hali akiwa kasujudu?

Akainuka Uqbah bin Abiy Muaytwi akaenda kuyachukua matumbo ya kinyesi kile na kuja kumtupia Bwana Mtume il-hali akiwa kasujudu.

Hakuweza wala kuthubutu yeyote miongoni mwa waislamu waliokuwepo pale msikitini kumuondolea Bwana Mtume uchafu ule kwa sababu ya unyonge na udhaifu waliokuwa nao wakati ule.

Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akaendelea kusujudu na uchafu ule ukiwa juu yake mpaka alipokuja Bi Fatmah binti yake, yeye ndiye aliyemuondolea uchafu ule na kuutupilia mbali.

 Bwana Mtume alipoinuka alimuombea dua ya maangamivu mtu aliyefanya kitendo hiki kiovu akasema : Ewe Mola wa haki liangamize kundi la Makurayshi, na akawataja watu kadhaa. Ibn Masoud anasema : Nikawaona watu aliowataja Mtume wameuliwa katika vita vya Badri.

Abu Lahab ibn Abdul-Mutwalib, ami yake Mtume hakuwa nyuma katika kumfanyia maudhi Mtume bali yeye ndiye aliyekuwa mbaya zaidi kuliko watu baki wasiokuwa jamaa zake Mtume.

Huyu alikuwa ni jirani yake. Alikuwa na zoezi la kukusanya takataka za kila aina na kuja kuzitupia mlangoni kwa Bwana Mtume kila asubuhi.

Mtume akiamka na kufungua mlango wake, kitu cha mwanzo alichokutana nacho ni harufu mbaya iliyotokana na takataka zile.

Bwana Mtume akawa hana la kufanya bali kuuondosha uchafu ule na kwenda kuutupa panapostahiki huku akisema :

“Enyi wana wa Abdi Manaf ni ujirani gani huu ?! Ummu Jamiylah, mkewe Abuu Lahab alikuwa bega kwa bega na mumewe akishirikiana katika nae katika matendo haya maovu.

Bibi huyu alikuwa akimtukana Bwana Mtume mara kwa mara na akieneza maneno ya fitina na uchochezi dhidi ya Mtume, khasa khasa baada ya kushuka Suratil-Lahab, sura iliyotaja kuangamia kwa Abi Lahab na mkewe huyu.

Miongoni mwa matukio ya kero na maudhi dhidi ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – ni lile tukio lililoripotiwa katika sahihil-Bukhariy, Amesema Imaam Bukhariy – Allah amrehemu – Wakati ambapo Mtume alipokuwa akiswali katika kikuta cha Al-Kaaba, alijiwa na Uqbah na Abi Muaytwi akaiweka nguo yake shingoni mwa Mtume na kumtia kabari ya nguvu.

Akaja Abu Bakri akamshika Uqbah begani na kumsukumia mbali na Mtume, na akasema :

OH ! MTAMUUA MTU KWA SABABU ANASEMA MOLA WANGU NI ALLAH ? NA KWA YAKINI AMEKUJIENI KWA DALILI ZA WAZI ZITOKAZO KWA MOLA WENU ! (Muacheni msimuue)” [40:28]

. Hizi ni kero na maudhi machache tu aliyofanyiwa Bwana Mtume na Makurayshi ili yawe ni kichocheo cha kumfanya aache kulingania dini aliyokuja nayo.

Miongoni mwa watu waliokuwa mstari wa mbele kumfanyia maskhara na kumcheza shere Bwana Mtume ni Al-Aaswi bin Waail.

Huyu alikuwa ni adui mkubwa wa Bwana Mtume na alikuwa akisema : Muhammad amewadanganya wafuasi wake eti watafufuliwa na kuwa hai tena baada ya kufa, Wallah hakuna kinachotuangamiza ila ni upitaji wa masiku na miaka tu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu akamrudi kwa madai yake haya kwa kusema :

“NA WALISEMA HAUKUWA (uhai) ILA NI UHAI WETU HUU WA DUNIA, (hakuna mwingine); TUNAKUFA NA TUNAISHI, WALA HAKUNA KINACHOTUANGAMIZA ISIPOKUWA (huu huu) ULIMWENGU; (kwani ndiyo ada yake kufisha na kuhuisha) LAKINI WAO HAWANA ELIMU YA HAYO (wanayoyasema) WANADHANI TU” [45:24].

Katika kuzidi kumfanyia maskhara Bwana Mtume, Al-Aaswi huyu alikuwa anadaiwa na Khabbaab bin Al-Arratta mojawapo wa wafuasi wa Bwana Mtume, ulipofika wakati walioagana wa kulipa deni, muislamu huyu alimuendea Al-Aaswi ili amlipe deni lake.

 Al-Aaswi akamwambia : Si anadai huyo Muhammad ambaye wewe umeingia katika dini yake kwamba watu wa peponi watapata chochote wakitakacho ?

Khabbaab akamjibu : Ndiyo. Al-aaswi akasema : Basi nisubirie mpaka siku hiyo nitakapopewa mali na watoto ndipo nitakulipa deni lako. Hapo ndipo iliposhuka kauli yake Mola Mtukufu :

“JE UMEMUONA YULE ALIYEZIKANUSHA AYA ZETU NA AKASEMA KWA HAKIKA NITAPEWA (huko akhera) MALI NA WATOTO (kama nilivyopewa hapa) JE AMEPATA KHABARI ZA GHAIBU AU AMECHUKUA AHADI KWA (Allah) MWINGI WA REHEMA (juu ya haya) ? SIYO! HAKIKA TUNAANDIKA ANAYOSEMA NA TUTAMZIDISHIA MUDA (mkubwa) KATIKA ADHABU [19:77-79].

Hiki ni kisa kimojawapo miongoni mwa visa vya kumcheza shere alivyofanyiwa Bwana Mtume.

Lengo na madhumuni ikiwa ni kumkatisha tamaa ili aache kuendelea kuutangaza Uislamu, dini ambayo iko dhidi ya mfumo wa maisha waliojichagulia na ambao wameuzoea kwa miongo ya miaka.

Kuucheza kwao shere na kumfanyia maskhara hakukumfanya Mtume arudi nyuma, bali aliwapuuza na kuendelea na jukumu alilopewa na Mola wake na Mwenyezi Mungu Mtukufu akazidi kumtia nguvu kwa kuwaangamiza wote waliokuwa wakimcheza shere kama tunavyosoma :

“HAKIKA SISI TUNAKUTOSHA KUKUKINGIA (shari ya) WANAOFANYA DHIHAKA” [15:95].

Miongoni mwao wako waliouliwa vitani na wengine walipatwa na maradhi makubwa, wakafa kutokana na maradhi hayo. Hila na mbinu hizi za maudhi na dhihaka ziliposhindwa, wakabuni mbinu mpya.

Mbinu hii haikuwa nyingine bali ilikuwa ni ile mbinu ya kulichafua jina na sifa ya Mtume kwa kumpaka matope ya sifa mbaya ili kufuta kule kukubalika kwake na jamii.

Kwa hiyo wakaanza kumsingizia na kutangaza kuwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – ni mwendawazimu, asiyejua wala kulitambua alisemalo bali huropoka tu kutokana na wazimu wake.

Mara nyingine walidai eti ni mchawi na wakati mwingine walimuita kuwa ni kuhani na mtunga mashairi. Kwa sababu hizo wakawa wanawatahadharisha watu wasikutane nae, wasizungumze nae na wala kumsikiliza asije akawaroga na kuwafanya waache dini ya mababa zao na kumfuata yeye.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anamtakasa Mtume wake na tuhuma hizo za maadui wake, tusome :

 “BASI ENDELEA KUWAKUMBUSHA. NA WEWE KWA NEEMA ZA MOLA SI MCHAWI WALA SI MWENDAWAZIMU (kama wanavyosema). NDIYO WANASEMA KUWA HUYU (Muhammad) NI MTUNGA MASHAIRI, TUNAMTAZAMIA KUPATIKANA NA MAUTI (kama walivyokufa washairi wengine)” [52:29-30].

Hizi ni baadhi tu ya hila na mbinu walizotumia Makurayshi katika kujaribu kulizima wimbi la mageuzi ya kiitikadi yaliyokuwa yakiongozwa na Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

KERO ZA MAKURAISHI DHIDI YA MTUME

Makurayshi walipoona juhudi zao za kumuendea kiongozi wao Mzee Abu Twalib ili amzuie mwana wa nduguye kuwatukania miungu wao zimegonga mwamba, hazikuzaa matunda yeyote.

Na moto wa Daawah ya dini mpya ndio unazidi kushika kasi na watu wanazidi kumfuata Nabii Muhammad.

Hapo ndipo wakaamua kujaribu kutumia mbinu ya kumfanyia kero na maudhi anuwai sambamba na kumfanyia maskhara. Khasa khasa alipokuwa akienda kuswali.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *