RUHUSA YA KUPIGANA VITA

UISLAMU HAURUHUSU VITA ILA KWA AJILI TU YA KULINDA NA KUTETEA IMANI.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliendelea kulingania dini kwa nguvu za hoja na kubashiri na kukhofisha katika mji wa Makkah, kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu.

Katika kazi yake hii, Makurayshi walimpinga vikali kabisa na kumfanyia kila aina ya maudhi na madhila.

Pamoja na maudhi yote hayo, bado Bwana Mtume na maswahaba wake waliendelea kustahamili na kusubiri bila ya kujibu.

Walifanya hivyo wakiamini kuwa wanaitii amri ya Mola wao:

“BASI SUBIRI KAMA WALIVYOSUBIRI WALE MITUME WENYE USTAHAMILIVU(kama Nabii Nuhu, Ibrahimu, Musa na Isa)WALA USIWAHIMIZIE (adhabu)…” [46:35]

Makurayshi hawakutosheka na maudhi tu bali wakifikia hatua ya kupanga njama za kumuua Mtume na kuwafyagilia mbali maswahaba wake.

Ni njama hizi ndizo zilizomlazimisha Bwana Mtume kuukimbia mji wa Makkah na ilhali anaupenda na kwenda kuishi uhamishoni Madinah.

Makurayshi bado hawakuridhika na kutoka kwa Mtume Makkah na kuhamia Madinah, wakazielekeza nguvu zao za uadui huko huko Madinah.

Kwa hatua hii sasa ikawa hapana budi tena Uislamu utetewe, ulindwe na kuhamiwa dhidi ya kila aliyejitokeza kama adui.

Ni lazima sasa ziwepo hatua na juhudi za makusudi za kulinda heshima, uhuru, amani na utulivu wa waislamu.

Waislamu wakiwa na haki na uhuru wa kuabudu kwa mujibu wa dini yao bila ya kuingiliwa au kubughudhiwa na mtu ye yote, hapo tena Mtume aseme:

“…HUU NI UKWELI ULIOTOKA KWA MOLA WENU, BASI NA ANAYETAKA NA AAMINI NA ANAYETAKA NA AKUFURU…” [18:29]

Kwani:

“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia)KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU…” [2:256]

Ni kwa ajili tu ya kulinda imani na uhuru wao wa kuabudu ndio Allah akawapa sasa idhini ya kupigana. Wapigane tu kwa ajili ya kujitetea wao wenyewe na itikadi yao.

Hapa sasa ndio zikaanza kushuka aya za jihadi zikiwa na mipaka maalumu.

Waumini wapigane na wale tu wanaowapiga:

“NA PIGANENI KATIKA NJIA YA ALLAH NA WALE WANAOKUPIGENI, WALA MSIPINDUKE MIPAKA (mkawapiga wasiokupigeni) KWANI ALLAH HAWAPENDI WARUKAO MIPAKA”. [2:190]

Waumini wapigane na wale tu waliowatoa (waliowafukuza) makwao:

“NA WAUWENI (hao wanaokupigeni bure) PO POTE MUWAKUTAPO, NA MUWATOE PO POTE WALIPOKUTOENI KWANI KUWAHARIBU WATU NA DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUUA. WALA MSIPIGANE NAO KARIBU NA MSIKITI MTAKATIFU (wa Makkah) MPAKA WAKUPIGENI HUKO. WAKIKUPEGENI (huko) BASI NANYI PIA WAPIGENI. NAMNA HIVI NDIVYO YALIVYO MALIPO YA MAKAFIRI”. [2:191]

Waumini wapigane tu na wale ambao wanakuwa ni pingamizi na kikwazo cha kuueneza Uislamu:

“NA PIGANENI NAO MPAKA KUSIWE NA MATESO (fitna, wao kuwatesa waislamu bure) NA DINI IWE KWA AJILI YA ALLAH TU. NA KAMA WAKIACHA BASI USIWEKO UADUI ILA KWA MADHALIMU”. [2:193]

Waumini wenye nguvu wapigane kwa ajili ya kuwatetea waumini wenzao wanyonge wanaoteswa na makafiri:

“NA MNA NINI HAMPIGANI KATIKA NJIA YA ALLAH NA (katika kuwaokoa) WALE WALIO DHAIFU (wanyonge) KATIKA WANAUME NA WANAWAKE NA WATOTO AMBAO HUSEMA: MOLA WETU! TUTOE KATIKA MJI HUU AMBAO WATU WAKE NI MADHALIMU, NA TUJAALIE TUWE NA MLINZI ANAYETOKA KWAKO, NA TUJAALIE TUWE NA WA KUTUNUSURU ANAYETOKA KWAKO”. [4:75]

Waumini wapigane katika njia ya Allah tu:

“WALE WALIOAMINI WANAPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH, LAKINI WALIOKUFURU WANAPIGANA KATIKA NJIA YA SHETANI. HAKIKA HILA ZA SHETANI NI DHAIFU”. [4:76]

Waumini wapigane na wale wavunjao ahadi ya mkataba wa amani baada ya kuwatahadharisha natija ya kuvunja ahadi:

“NA KAMA UKIOGOPA KHIYANA KWA WATU (mliofanya nao ahadi) BASI WATUPIE (ahadi yao) KWA USAWA, HAKIKA ALLAH HAWAPENDI MAKHAINI”. [8:58]

Haya ndiyo malengo na ndio maeneo ambayo yanampa idhini na uhalali muislamu wa kuingia vitani kwa mali na nafsi yake. Muislamu hapigani na ye yote ila tu pale itakapopatikana mojawapo ya sababu hizi.

 

VITA KATIKA UISLAMU SIO NJIA YA KUWALAZIMISHA WATU KUINGIA KATIKA DINI HII BILA YA RIDHAA YAO.

Msingi mkuu wa vita katika Uislamu ni:

“…NA WANAOKUSHAMBULIENI NANYI PIA WASHAMBULIENI KWA KADRI WALIVYOKUSHAMBULIENI. NA MUOGOPENI ALLAH (msiongeze kuliko walivyokufanyieni)…” [2:194]

Ye yote atakayewafanyia uadui waislamu, akawapiga vita, waislamu nao wana haki ya kujibu mashambulizi hayo.

Ye yote atakayewafukuza na kuwatoa waislamu katika makazi yao, waislamu nao wanapewa idhini ya kutetea na kulinda haki yao ya kuishi po pote katika ardhi ya Mola wao.

Ye yote atakayewafitini na kuwazuilia waislamu na dini yao, basi atambue kwamba waislamu wanaambiwa na Mola wao:

“…KUWAHARIBU WATU (kuwazuilia watu) NA DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUWAUA…”

Kwa msingi huu awe na yakini kuwa waislamu wa kweli hawataweza kukaa kimya na kuangalia macho tu mtu aichezee dini yao na kuwazuia kuufikisha ujumbe wa Mola wao, hili ni muhali halitokuwa kamwe. Kutokana na maelezo haya utaoana kuwa lengo la vita katika Uislamu ni kwa ajili ya:-

Kutokutoa nafasi ya kuzuiliwa waislamu na dini yao.

Kutokufukuzwa waislamu katika miji yao kwa sababu tu ya imani yao.

Kutokuvunjwa heshima na utukufu wa dini ya Allah.

Kuwepo uhuru na haki ya kuabudu bila ya kubughudhiwa na ye yote.

Kutokumzuia mtu kuingia katika Uislamu kwa radhi yake.

Ilimradi vita katika Uislamu viwe ni kwa ajili ya kuilinda na kuitetea dini ya Allah na neno lake liwe juu na kushinda:

“YEYE NDIYE ALIYEMTUMA MTUME WAKE KWA UONGOFU NA DINI ILIYO YA HAKI ILI AISHINDISHE JUU YA DINI ZOTE…” [48:28]

Na inatakiwa taq-wa (kumcha Allah) ndio iwe nembo na alama ya waumini katika hali zao zote: “…NA MUOGOPENI ALLAH (msiongeze kuliko walivyokufanyieni) NA JUENI KWAMBA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOMUOGOPA”. [2:194]

Na vita vinatakiwa vikome mara moja pale tu linapokomeleka lengo la vita hivyo:

“…NA KAMA WAKIACHA (kuwatesa bure) BASI USIWEKO UADUI ILA KWA MADHALIMU”. [2:193]

Tena waislamu wanatakiwa wapupie zaidi mazungumzo ya amani ikiwa adui yao ataonyesha nia ya kuwa na mazungumzo yenye kulenga kuleta amani baina ya pande mbili hizi hasimu:

 “NA KAMA (hao maadui) WAKIELEKEA KATIKA AMANI,NAWE PIA IELEKEE NA MTEGEMEE ALLAH. HAKIKA YEYE NDIYE ASIKIAYE (na) AJUAYE. NA KAMA WAKITAKA KUKUKHADAA BASI ALLAH ATAKUTOSHELEZA…” [8:61-62]

Kwa mantiki hii basi, utaona vita katika Uislamu haviko kwa ajili ya kuwalazimisha watu kuingia katika Uislamu bila ya ridhaa zao.

Wala si kwa ajili ya kupata ngawira na manufaa vitani, si kwa lengo la kukalia ardhi na mali ya watu kwa mabavu.

Si kwa madhumuni ya kuwafanya watu watumwa, wala si kwa makusudi ya utawala, wala….wala……

Bali vita katika Uislamu; mfumo sahihi wa maisha ni kwa ajili tu ya kulinda uhuru wa itikadi na kuhifadhi na kutetea heshima ya waumini.

Waumini wasiteswe na kudharauliwa kwa sababu tu ya imani yao.

Ama itikadi kwa maana ya imani, kimaumbile ni kitu kisichokubali kulazimishwa na kupandikizwa kwa nguvu.

Wala huwezi kuilazimisha itikadi katika nafsi ya mwanadamu hata kwa mtutu wa bunduki. Hiyo haitakuwa kamwe itikadi ya moyo bali itikadi ya mwili, yaani sura tu ya itikadi na si dhati ya itikadi.

Itikadi halisi na ya kweli ni ile fikra/jambo linalokubaliwa na kuridhiwa na moyo kwa njia ya khiyari bila ya kulazimishwa.

Na hakutoshi tu kukubaliwa na moyo bali ni lazima pia akili ishirikishwe na ilikubali jambo/fikra hiyo kwa nguvu za hoja.

 Kwa hivyo matumizi ya nguvu siku zote si njia sahihi ya kupandikiza itikadi katika nyoyo za watu. Hili Allah Mtukufu amelibainisha bayana katika kitabu chake kitukufu, haya na tuukiri na kuukubali ukweli huu:

“HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI…” [2:256]

Akasema tena:

“KWA HAKIKA HII (Qur-ani) NI MAWAIDHA, BASI ANAYETAKA ATAJIFANYIA NJIA (nzuri ya kwenda) KWA MOLA WAKE”. [73:19]

Akaendelea kusema:

“NA SEMA: HUU NI UKWELI ULIOTOKA KWA MOLA WENU, BASI ANYETAKA NA AAMINI NA NAYETAKA NA AKUFURU…” [18:29]

Tena Allah Taala akamuwekea Mtume wake mipaka katika kazi yake hiyo:

“…SI JUU YAKO ILA KUFIKISHA TU…” [42:48]

Akazidi kumwambia:

“HUKUWA WEWE ILA NI MUONYAJI TU”. [35:23]

Kadhalika akamtahadharisha kufanya matumizi ya nguvu kuwa ndio njia/chombo cha kuwafanya watu waamini, akamwambia:

“BASI KUMBUSHA, HAKIKA WEWE NI MKUMBUSHAJI (tu). WEWE SI MWENYE KUWATENZA NGUVU”. [88:21-22]

“NA KAMA ANGALITAKA MOLA WAKO (kuwalazimisha kwa nguvu kuamini) BILA SHAKA WANGALIAMINI WOTE WALIOMO AKTIKA ARDHI (hasibakie hata mmoja. Lakini Allah hataki kuwalazimisha watu kwa nguvu) BASI JE, WEWE UTAWASHURUTISHA WATU KWA NGUVU HATA WAWE WAUMINI? NA HAKUNA MTU ANAYEWEZA KUAMINI ISIPOKUWA KWA IDHINI YA ALLAH…” [10:99-100]

Zaidi ya yote haya Allah Taala alimlaumu Mtume wake kutokana na huzuni aliyokuwa nayo kutokana na kutoamini kwa watu wake:

“HUWENDA (wewe Nabii Muhammad) UTAANGAMIZA NAFSI YAKO KWA SABABU HAWAWI WAISLAMU”. [26:3]

Aya zote hizi ni ushahidi wa wazi kabisa kwamba matumizi ya nguvu hayakuwa na wala hayatakuwa ndio chombo/njia ya kuwafanya watu waukiri na kuukubali Uislamu.

Hakika matumizi ya nguvu hayakuwa ila ni kwa ajili ya kupambana na wale watumiao nguvu katika kuupinga na kuuzuia Uislamu.

Ndio ikawa jino kwa jino ili kuwatia adabu maadui hawa na kujilinda na shari lao.

Itikadi/imani ndio kitu kitukufu kabisa anachokimiliki mwanadamu, kwa sababu ndio kitu pekee kinachomtofautisha mwanadamu na hayawani wengine.

Kwa mantiki hii kuichezea imani/itikadi ya mtu ni kuuchezea utu wake.

Uislamu kwa kuutambua umuhimu na thamani ya imani, ukafanya kuizuia/kuishambulia imani ni kosa/hatia/jinai kubwa zaidi kuliko jinai ya kutoa uhai wa mtu. Kwa kulizingatia hili ndio ikawa:

“…KUWAZUILIA WATU NA DINI YAO NI KUBAYA ZAIDI KULIKO KUWAUA…” [2:191]

Na ikawa waumini kuilinda, kuitetea na kuihami itikadi/imani yao ni jambo lisiloepukika na ni dharura isiyokimbilika.

 

RUHUSA YA KUPIGANA VITA

UISLAMU HAURUHUSU VITA ILA KWA AJILI TU YA KULINDA NA KUTETEA IMANI.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliendelea kulingania dini kwa nguvu za hoja na kubashiri na kukhofisha katika mji wa Makkah, kwa kipindi kisichopungua miaka kumi na tatu.

Katika kazi yake hii, Makurayshi walimpinga vikali kabisa na kumfanyia kila aina ya maudhi na madhila.

Pamoja na maudhi yote hayo, bado Bwana Mtume na maswahaba wake waliendelea kustahamili na kusubiri bila ya kujibu.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *