KUPAKAZA MAJI JUU YA VICHACHA (P.O.Ps) NA UTEPE (BANDAGE)

Ni vema kabla hatujaanza kuelezea hukumu na namna ya upakazaji juu ya vichacha na utepe, tukabainisha kichacha na utepe ni nini?

Tuanze na kichacha, hiki ni kiungio kinachofungwa juu ya kiungo kilichovunjika ili kipate kuungana. Kiungio hiki kinaweza kuwa ni aina Fulani ya mbao au chenye kufanana na mbao kama vile P.O.P maarufu “muhogo” zinazotumika mahospitalini leo.

Tukija katika utepe, tunaweza kusema utepe ni aina Fulani/maalumu ya kitambaa kinachowekwa juu ya jeraha ili kulihifadhi kutokana na vumbi,wadudu kama inzi na vitu vingine vyenye madhara mpaka jeraha lipone.

Kwa kuuzingatia ule ukweli kwamba uislamu ni dini ya maumbile, dini iliyojengwa katika misingi ya wepesi, tusome sote kwa pamoja: “… ALLAH ANAKUTAKIENI YALIYO MEPESI WALA HAKUTAKIENI YALIYO MAZITO…” (2:185)

Ndipo tunaona uislamu ukiyazingatia maumbile na hali zinazomsibu na kumtokea binadamu katika maisha yake ya kila siku, ikiwa ni pamoja na matukio ya kuvunjika baadhi ya viungo au kupatwa na majeraha.

Majanga yote haya yanapompata binadamu, hana budi kuirekebisha hali hiyo kwa kujitibu na kufanya dawa, jambo ambalo limeruhusiwa na sheria.

Katika hali hii binadammu huyu anakabiliwa na mambo mawili kwa pamoja ambayo yote yamempasa kuyatekeleza; moja lilnahuhusu mwenyewe pekee (kujitibu) na jingine linamuhusu yeye na Mola wake (ibada).

Ni kwa kulizingatia hili ndipo sheria/uislamu ukamuwekea binadamu huyu mazingira mazuri ya utekelezaji wa ibada sambamba na kujitibia kwa kumuwekea sheria hii ya upakazaji maji juu ya vichacha na utepe, sheria na kanuni ambazo zitadhamini mambo yote mawili; utekelezaji wa ibada na kuhifadhi afya na usalama wa mwili wa binadamu.

Baada ya kuwazihisha (kuweka wazi )maana ya vichacha na utepe, hebu sasa kwa msaada wa Allah, tuziangalie:-

HUKUMU ZA VICHACHA NA UTEPE

Mgonjwa aliyepatwa na jeraha au mvunjiko, huweza kuhitajia kufunga kichacha/utepe na kuweka dawa juu ya jeraha hilo au mvunjiko na wakati mwingine asihitajie kabisa. Iwapo atahitajia kuweka kichacha au kufunga utepe, basi imemlazimu katika hali hii mambo matatu yafuatayo;

1. Wakati wa kutawadha/kuoga ni lazima aoshe ile sehemu nzima ya kiungo kisichopatwa na masaibu (jeraha/mvunjiko)

2. Apakaze maji juu ya kichacha chenyewe au utepe wote.

3. Atayamamu badala ya kuosha kiungo kigonjwa atakapokifikia wakati wa kutawadha.

Kutokana na mambo matatu hayo tuliyoyataja hapo juu tutafahamikiwa kwamba mtu atakapoweka kichacha au kufunga utepe itamlazimu: (i) Kuosha (ii) Kupakaza na (iii) Kutayamamu.

Sasa, ni wapi ataosha, atapakaza na kutayamamu yarejee vema maelezo hayo hapo juu. Ikiwa mtu hahitaji kufunga kichacha juu ya kiungo kilichovunjika au utepe juu ya jeraha, itamuwajibikia kuosha kiungo kilicho kizima na kutayamamu kwa sababu ya jeraha iwapo hawezi kuosha mahala palipo pagonjwa.

Kadhalika itamuwajibikia kurudia kutayamamu kila anapotaka kuswali swala ya faradhi hata kama hakuhuduthi na wala si wajibu kuosha viungo vyake vingine vilivyosalia ila atakapohuduthi.

DALILI NA USHAHIDI WA KUWEKWA SHERIA HII YA UPAKAZAJI JUU YA VICHACHA.

Ushahidi wa kuwekwa sheria hii ni riwaya iliyopokelewa na Jaabir-Allah amuwiye radhi – amesema: Tulikwenda safarini, mwenzetu mmoja akapatwa na jiwe likampasua kichwani, kasha (usiku alipolala) akajiotelea, akawauliza wenzake: Je, mnanipatia rukhsa ya kutayamamu? Wakamjibu; Hatukupatii rukhsa na il-hali unaweza (kutumia) maji. Basi akakoga, akafa ( kutokana na maji kuingia katika jeraha). Tuliporudi kwa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alieleza khabari hizo, akasema: “Wamemuua, Mwenyezi Mungu awauwe na wao, kwanini wasiulize waliokuwa hawajui? Bila shaka dawa ya ujinga ni kuuliza, hakika si vinginevyo ilikuwa inamtoshea kutayamamu na kufunga juu ya jeraha lake kitambaa (utepe) kisha akapakaza maji juu yake na kuosha viungo vingine.” Abuu Daawoud.

Kadhalika ushahidi mwingine ni ile riwaya ya Imamu Aliy Ibn Abiy Twaalib – Allah amridhie – amesema: Kilivunjika kiwiko cha mkono wangu (nikafunga kichacha) nikamuuliza mtume – Rehema na Amani zimshukie – akaniamrisha nipakaze maji juu ya vichacha..”

MUDA WA UPAKAJI JUU YA KICHACHA NA UTEPE

Upakaji maji juu ya kichacha na utepe haukuwekewa muda maalumu na sheria. Mtu ataendelea upakaza mpaka pale udhuru utakapoondoka, kiungo kilichovunjika kiunge au jeraha lipone hapo ndipo ruhusa ya upakaji itakuwa imemalizika na kumuwajibikia sasa kuosha.

Hukumu ya vichacha ni moja tu, ni mamoja ikiwa twahara hiyo (pamoja na vichacha) ni kwa sababu ya hadathi ndogo au kubwa. Isipokuwa katika hadathi kubwa, upakaji utakapobatilika itamuwajibikia kuosha mahala palipokuwa na kichacha au tepe tu na wala si wajibu kuosha sehemu nyingine ya mwili zaidi ya hiyo.

MAS-ALA:

Itamuwajibikia mfungaji wa kichacha kukidhi swala katika maeneo au mazingira yafuatayo:

  • Atakapokiweka bila ya kuwa na twahara na ikashindikana kukivua.
  • Au kichacha kilikuwa katika viungo vya tayamamu ambavyo ni uso na mikono.
  • Au kichacha kitakapochukua sehemu kubwa ya mahala palipo pazima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *