UVIVU NA AJIZI

Muislamu si mtu wa ajizi wala hawi mvivu bali ni mtu thabiti, mtendaji kazi na huwa na pupa ya maendeleo.

Ajizi na uvivu, hizi ni tabia mbaya ambazo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akimuomba Allah amkinge na kumuepusha nazo. Ni mara nyingi sana Bwana Mtume alikuwa akiomba:

“Ewe Mola wa haki! Hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na ajizi, uvivu, uoga, udhaifu wa ukongwe na ubakhili”.Bukhaariy & Muslim.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakuwa mvivu, bali mwenyewe alikuwa mchapa kazi hodari na akauusia umati wake kufanya kazi,akasema:

“Yapupie yenye manufaa kwako, na jilinde kwa Allah na wala usifanye ajizi. Likikupata jambo usiseme lau ningefanya kadha ingekuwa kadha, lakini wewe sema amelikadiria Allah (linipate) na yeye hulitenda alitakalo. Kwa sababu (neno) lau hufungua amali ya shetani”. Muslim.

Kwa kuwa muislamu ameamrishwa kumfuata Mtume wake na kumfanya kuwa ndio kigezo chake ndio maana huwezi kumuona muislamu akiwa mvivu au mwenye ajizi.

Kama ambavyo huwezi kumshuhudia muislamu kwa maana ya neno lenyewe akiwa  muoga wala bakhili.

Itamkinika vipi muislamu kubweteka na kuacha kufanya kazi na kupupia manufaa na maendeleo yake.

Na ilhali yeye ni muumini wa “mfumo sababu” na kanuni ya ulimwengu ya “tafuta utapata”, “panda utavuna”.

Muislamu hupupia kufanya amali njema zitakazomnufaisha leo hapa katika uso wa ardhi na kesho kule akhera kwenye maisha ya milele.

Kwa sababu anauamini wito wa Allah unaomtaka kuwa mshindani katika mambo ya kheri:

 “YAENDEENI UPESI (mambo ya kukupatieni) SAMAHANI YA MOLA WENU NA PEPO AMBAYO UPANA WAKE NI KAMA UPANA WA MBINGU NA ARDHI…”. [57:21]

Tukiizingatia aya hii itatudhihirikia kwamba mambo yote mazuri kama pepo ya Allah, maisha mazuri duniani na akhera hayapatikani bure bure tu.

Mtu abweteke, afanye uvivu, aache kuhangaika na kujishughulisha, kisha atarajie kupata maisha bora na pepo ya Allah! La, hasha hili ni muhali ni lazima ayaendee mbio kama inavyosema aya. Aingie mashindanoni khasa katika kuhakikisha kuwa anayapata mambo mazuri mazuri:

“…NA KATIKA (kupata) HAYA WASHINDANE WENYE KUSHINDANA”. [83:26]

SURA ZA AJIZI NA UVIVU.

Ukitaka kujua kama tayari umeshatambaliwa na tabia mbaya za ajizi na uvivu, zifuatazo ni baadhi ya sura zake.

Hebu jikague mwenyewe kama umeshakumbwa na umuombe Mola wako akunasue.

  1. Mtu kusikia adhana na akaacha kuuitikia wito huo wa swala, akaendelea na utamu wa usingizi au akaendelea na baraza ya porojo.

Au kazi isiyo ya dharura mpaka wakati wa swala ukawa finyu (karibu kutoka). Kisha tena ndio anainuka wangu wangu kwenda kuswali peke yake mwishoni mwa wakati. Hii ni ajizi na uvivu , jiepushe.

  1. Mtu kutumia muda mwingi mno katika baraza za kahawa, karata, bao, kutumbulia macho runinga (televisheni) kutwa au kuzungukazunguka hovyo mitaani bila ya malengo wala muelekeo.

Anapoteza muda wote huo na ilhali anakabiliwa na mlolongo wa mambo mengi muhimu yanayomlazimu kuyatekeleza. Hii kama sio ajizi au uvivu ambo utakaokugharimu maishani ni nini basi?!

  1. Mtu kuacha kujishughulisha na mambo yenye manufaa kwake kama vile kusoma na kujiendeleza kielimu au kufanya kazi halali na kujipatia riziki yake ya halali.

Kazi ambazo zitamdhaminia mafanikio duniani na akhera, akaziacha na kuendekeza uvivu na huku akitoa hoja za uzee.

Au kazi hii mimi siiwezi ni ngumu au mimi si mtu wa kufanya kazi kama hizi au kazi hii inaninyima hata fursa ya kupumzika.

Siku, majuma, miezi na hatimaye miaka inapita na yeye kabweteka tu hataki kufanya kazi kwa manufaa yake mwenyewe ya ulimwengu huu na ule ujao. Huu nao ni uvivu na ajizi aliyokua akijilinda nayo Mtume wa Allah kwa Mola wake.

  1. Mtu kufungukiwa na milango ya kheri kama vile kupata fursa ya kwenda kuhiji. Allah amemneemesha kwa kumpa neema ya mali na afya njema na bado asiitumie fursa na neema hii kuitekeleza nguzo hii ya Uislamu.

 Au kupata fursa ya kukutana na mtu mwenye shida anayehitaji huruma na msaada, akaacha kumsaidia na ilhali Allah amempa uwezo wa kumsaidia.

Au mtu akapata bahati ya kuudiriki mwezi mtukufu wa Ramadhani, akiwa mzima mwenye afya njema na amani.

 Kisha akaacha kuzivuna fadhila adhimu za mwezi huo mtukufu kwa kushindwa kusimama usiku kufanya ibada.

Au mtu kapata bahati ya kuwadiriki wazazi wake wawili, au mmoja wao katika hali ya utu uzima.

Kisha akashindwa kuivuna pepo na samahani (maghfira) ya Mola wake eti kwa sababu tu ya kuacha  kuwatendea wema kama alivyoagizwa na Mola wake.

Hii pia haiachi kuwa ni aina ya uvivu na ajizi itakayokutia khasarani leo na kesho. Muombe na umbembeleze Mola wako akuepushe navyo.

  1. Mtu kuishi maisha duni na ya dhiki huku akimsingizia Mola wake kuwa ndiye aliyemkadiria maisha hayo.

Hachukui hatua zo zote za makusudi ili kujikwamua kutokana na hali hiyo kwa kuzidisha bidii katika kazi. Hii nayo ni sura nyingine ya uvivu na ajizi ambao si sifa ya muislamu.

Uvivu na ajizi hujishakilisha katika sura nyingi, hizi ni baadhi yake tu na ni kipimo cha hizo nyingine ambazo hatukuwafikiwa kuzitaja.

 

UVIVU NA AJIZI

Muislamu si mtu wa ajizi wala hawi mvivu bali ni mtu thabiti, mtendaji kazi na huwa na pupa ya maendeleo.

Ajizi na uvivu, hizi ni tabia mbaya ambazo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akimuomba Allah amkinge na kumuepusha nazo. Ni mara nyingi sana Bwana Mtume alikuwa akiomba:

“Ewe Mola wa haki! Hakika mimi ninajilinda kwako kutokana na ajizi, uvivu, uoga, udhaifu wa ukongwe na ubakhili”.Bukhaariy & Muslim.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *