Swala za fardhi ambazo Muislamu amefaradhiwa na Mola wake kuziswali kila siku, mchana na usiku ni swala tano.
Kila moja miongoni mwa swala tano hizi ina wakati wake maalum ambao muislamu anawajibikiwa kuiswali ndani ya wakati huo.
Hii ndiyo amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama tunavyosoma ndani ya Qur-ani Tukufu.
“……..KWA HAKIKA SWALA KWA WAUMINI NI FARDHI ILIYOWEKEWA NYAKATI MAKHSUSI (maalumu) “. (4:103).
Tumejua kutokana na aya hii kwamba kumbe kuswali kwa wakati ni nembo na alama ya Imani ya mja.
Haisihi na wala haijuzu kwa muislamu kuiswali swala kabla ya kuingia wakati kama isivyofaa kuiswali bada ya kutoka wakati wake ila kwa dharura ya kisheria.
Suala la wakati wa kila swala halikuwa mikononi mwa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – bali lilitawaliwa na wahyi (ufunuo) kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Imethibiti katika hadithi nyingi sahihi kwamba Jibril – Amani imshukie – alimjia Bwana Mtume – baada ya kufaradhishwa swala tano kumfahamisha nyakati za swala, swala ipi inaingia wakati gani na kumalizika wakati gani.
Kisha naye Bwana Mtume akaubainishia umma wake nyakati hizo kwa maneno na matendo.
Hadithi iliyokusanya kwa pamoja nyakati za swala zote tano ni ile iliyopokelewa na Imam Muslim ikiwa ni riwaya ya Abuu Muusa Al-Ash-ariy-Allah amuwiye radhi -kutoka kwa Mtume Rehema na Amani zimshukie kwamba yeye Mtume alijiwa na mtu akimuuliza juu ya nyakati za swala (Mtume) hakumjibu chochote .
Na katika riwaya nyingine Mtume alisema:
“Njoo uswali pamoja nasi. Akasema (Abuu Muusa): (Mtume) akaisimamisha Alfajiri (Swala ya Alfajiri) wakati ilipochimbuka Alfajiri na ilhali watu wanakurubia kutofahamiana (kutokana na muangaza hafifu).
Kisha akamuamrisha kuisimamisha Adhuhuri wakati jua lilipopinduka na il-hali akisema msemaji: Mchana umegawika nusu, naye alikuwa ni mjuzi mno wa hilo (la nyakati) kuliko wao.
Halafu akawaamrisha, akaisimamisha Al-asri na ilhali jua likiwa limepanda. Kisha akamuamrisha akaisimamisha Maghribi wakati jua lilipotua/lilipozama.
Kisha akamuamrisha akaisimamisha Isha wakati yalipozama mawingu (mekundu) kisha kesho yake akaichelewesha Alfajiri, mpaka akamaliza kuiswali na msemaji akisema: Jua limechomoza au limekurubia (kuchomoza).
Kisha akaiakhrisha Adhuhuri mpaka ikawa karibu na wakati wa Al-asiri ya jana.
Kisha akaichelewesha Al-asiri mpaka akamaliza kuiswali na ilhali akisema msemaji: Jua limekuwa jekundu.
Halafu akaiakhirisha Maghribi mpaka ikawa wakati wa kuzama mawingu mekundu. Kisha akaiakhirisha Ishaa mpaka ikafika theluthi ya kwanza ya usiku. Kisha kulipopambazuka akamuita yule muulizaji na kumwambia:
“Huo wakati (uliokuwa ukiuulizia) uko baina (ya nyakati) mbili hizi (ule wa juzi na wa jana)”.
Zipo hadithi nyingine ambazo zimekuja kutoa tafsiri na ufafanuzi juu ya kauli jumla zilizomo ndani ya hadithi hii. Zikiitaja kila swala na wakati wake. Tufuatane pamoja na tujifunze.
WAKATI WA ALFAJIRI.
Wakati wa swala ya Alfajiri huingia kwa kuchomoza Alfajiri ya kweli (Alfajiri halisi) na huendelea mpaka kuchomoza kwa jua.
Amesema Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie: “Wakati wa swala ya Sub-hi ni tangu kuchomoza Afajiri maadamu jua halijachomoza.” Muslim
WAKATI WA ADHUHURI.
Huanza wakati wa swala ya Adhuhuri kwa kukengeuka jua nusu ya mbingu kuelekea upande wa Magharibi, huku ndiko kunakoitwa kutenguka/kupondoka jua.
Wakati huu kivuli cha kitu huonekana kidogo tu, kinachoanza kuelekea upande wa Mashariki, na hiki ndicho kinachoitwa kivuli cha kitu mfano (Mithili) wa kitu chenyewe.
Amepokea Imam Muslim kwamba Mtume wa Allah Rehema na Amani zimshukie amesema
“Wakati wa Adhuhuri ni zama litakapotenguka jua na kikawa kivuli cha mtu kama mfano wa urefu wake (Mtu huyo) muda wa kuwa haijaingia Al-asiri.”
WAKATI WA AL-ASIRI.
Huanza wakati wa swala ya Al-asiri kwa kumalizika wakati wa Adhuhuri na huendelea mpaka kuzama kwa jua.
Haya tunayafahamu kutokana na kauli ya Bwana Mtume Rehema na Amani zimshukie. “Na atakayeidiriki (atakayeiwahi) rakaa moja ya Al-asiri kabla ya kuzama jua, hakika ameidiriki Al-asiri” Bukhaariy na Muslim.
Lakini ni bora mtu asiicheleweshe swala ya Al-asiri mpaka wakati huu, bali apupie kuiswali mwanzo wa wakati.
WAKATI WA MAGHRIBI:
Wakati wa swala ya maghribi huanza kwa kuzama jua na huendelea mpaka kuzama kwa mawingu mekundu bila ya kubakia athari yake upande wa Magharibi.
Mawingu (makungu) mekundu ni matokeo ya kubakia athari ya mwangaza wa jua ambayo hudhihiri upande wa Mashariki wa pambizo za mbingu wakati jua linapozama.
Hatimaye giza huyafukuzia upande wa Magharibi kidogo kidogo mpaka hupotea/hutoweka kabisa.
Kiza kikifunga na kuenea pambizo la Magharibi na kutoweka kabisa kwa athari ya mawingu mekundu, hali hii humaanisha kumalizika kwa wakati wa swala ya Magharibi na kuingia kwa wakati wa swala ya Ishaa.
Hivyo ndivyo tulivyofahamu kutokana na hadithi jumla ya nyakati za swala tuliyoitaja huko nyuma pamoja na kauli ya Mutume isemayo:
“Wakati wa Maghribi ni muda wa kuwa hayajazama mawingu mekundu”.
WAKATI WA ISHAA.
Huingia wakati wa swala ya Ishaa kwa kuisha/kumalizika wakati wa swala ya Magharibi na huendelea mpaka kudhihiri kwa Alfajiri ya kweli.
Lakini ni bora isicheleweshwe mpaka kupita theluthi ya kwanza ya usiku.
Hizi ndizo nyakati za swala tano. Inapendeza au imependekezwa kwa Muislamu kuiswali swala mwanzoni mwa wakati wake kwa sababu jambo hili huonyesha ukomavu wa Imani ya mja na kuijali kwake ibada ya swala.
Pia si vema kuichelewesha kwa makusudi ukaiswali ukingoni mwa wakati kwa hoja ya ukunjufu wa wakati, kwa sababu uchelewashaji huu unaweza kusababisha kuiswali nje ya wakati wake.
Na pengine huweza kusababisha kuzembea na kuacha kuiswali kabisa. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliulizwa ni amali ipi iliyo bora kuliko zote ? Akajibu ! “ Ni kuswali kwa wakati wake”. Bukhaary na Muslim.
Yaani kuswali mwanzo na wakati.
FAIDA!
Jua na ufahamu kwamba mtu iliyotuka baadhi/sehemu ya swala yake ndani ya wakati na baadhi nyingine nje ya wakati wake.
Angalia akiipata mtu rakaa moja ndani ya wakati, swala hiyo, itakuwa ni ADAA – yaani itahesabika kuwa imeswaliwa ndani ya wakati.
Na iwapo hakuwahi kuipata rakaa moja ndani ya wakati, yaani kaipata sehemu tu ya rakaa, basi swala hiyo itakuwa ni KADHAA, yaani imeswaliwa nje ya wakati.
Ushahidi wa haya ni ile hadithi iliyopokelewa na Abu Hurayrah – Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – amesama;
“Atakayediriki katika (swala ya ) Sub-hi rakaa moja kabla ya kuchomoza jua, hakika ameidiriki sub – hi. Na atakayeidiriki rakaa moja katika swala ya Alasiri kabla ya kuzama jua, hakika atakuwa amediriki Alasiri”.
Na kauli ya Mtume isemayo:
“Atakayeidiriki rakaa moja katika swala, hakika ameidiriki swala hiyo”. Bukhaariy na Muslim.