BWANA MTUME APELELEZA WANAKOELEKEA MAKURAYSHI

Baada ya kurushiana maneno na waislamu, Abuu Sufyaan akageuza hatamu za farasi wake na huyoo akashika njia kurejea kwa watu wake.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapendelea kujua Makurayshi wanaelekea wapi. Akamtuma Sayyidina Aliy, akamwambia:

“Wafuatilie watu hawa, chunguza wanafanya nini na wanaelekea wapi. Angalia wakiwaweka kando farasi na kupanda ngamia, basi bila ya shaka watakuwa wanaelekea Makah. Na iwapo watapanda farasi na kuwaswaga ngamia, basi bila ya shaka watakuwa wanaelekea Madinah”. Sayyidina Aliy-Allah amuwiye radhi-akaipokea amri hii ya Bwana Mtume kwa utii mkubwa, huyoo akatoka na kuanza kuwafuatilia. Katika fuatilia yake hiyo, akawaona Makurayshi wamewaweka kando farasi na kupanda ngamia wakielekea upande wa Makah. Akarudi kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-na kumpasha khabari, Mtume akasema: “Namuapia yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, ikiwa watakwenda Madinah, nitawaendea tu huko kisha nitapambana nao”.

Makurayshi walipoondoka zao, maswahaba wa Mtume wa Allah-Allah awawiye radhi-wakamzunguka Bwana Mtume na kuanza kumtibu majeraha yake.

Abuu Ubeidah akainuka na kuving’oa vile vijimsumari viwili vilivyokuwa vimekita usoni kwa Bwana Mtume kwa kutumia meno yake.

Kijimsumari cha kwanza kikang’oka na jino moja la pembeni la Abuu Ubeidah, wakati kile cha pili nacho kikiondoka pamoja na jino jingine.

Ikawa Bwana Mtume kang’olewa vijimsumari viwili  na kubakia na majeraha ya kuuguza, huku Abuu Ubeidah akipoteza meno yake mawili na kuwa mapengo kwa ajili ya Mtume wa Allah.

 Sayyidat Faatimah Bint ya Mtume wa Allah akaja na kundi la wanawake kutoka Madinah, alipomuona Mtume wa Allah (baba yake) akitokwa na damu usoni akambusu na kuangusha kilio.

Akamkosha damu na kuipangusa lakini haikukoma kutoka, akatwaa kipande cha jamvi/mkeka akakiunguza moto mpaka kikawa majivu. Akayachukua majivu yale na kumbandika nayo Bwana Mtume majerahani mwake, hapo ndipo damu ikakatika.

 

BWANA MTUME APATWA NA SIMANZI (HUZUNI) KUU JUU YA MASHAHIDI.

Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akashuka kwenye medani ya vita kuangalia waliouliwa miongoni mwa maswahaba wake.

Alipomuona ami yake; Hamzah-Allah amuwiye radhi-akiwa  amepigwa mueleka na mauti na kufanyiwa unyama aliofanyiwa wa kukatwakatwa na kupasuliwa tumbo. Alishikwa na huzuni kuu juu yake na akapandwa na chuki na hasira kuu kwa wale waliomfanyia ami yake unyama huo. Bwana Mtume akafikia kusema:

“Sijapatapo kushuhudia tukio litialo uchungu na simanzi kuliko tukio hili”.

Kisha akamtazama swahaba wake; Musw-ab Ibn Umeir-Allah amuwiye radhi-amelala chini akiwa amevaa guo lake, akasema kwa huzuni:

“Mtu niliyekuona Makah na ilhali kukiwa hakuna mwenye kuvaa nguo nzuri kukushinda, mwenye mkusanyiko mzuri wa nywele. Leo umelala chini na guo hili tena tim tim wa nywele!”.

 Kisha akawaangalia mashahidi wengine wote na kusema:

“Mimi ni shahidi juu ya hawa, hakika ya hali ilivyo hapana majeruhi yo yote aliyejeruhiwa kwa ajili ya Allah ila Allah atamfufua siku ya kiyama na ilhali jeraha lake hilo likitoka damu. Rangi yake rangi ya damu na harufu yake ni harufu ya miski”.

Handhwalah Ibn Abiy Aamir-Allah amuwiye radhi alikuwa ndio kwanza katoka kufunga ndoa na kuingia ndani.

Aliposikia la mgambo la vita likilia, akatoka haraka kuelekea vitani kabla hata ya kukoga janaba. Huyu hakurudi tena kwa Bi. harusi, akawa ni miongoni mwa mashahidi-Allah awawiye radhi. Bwana Mtume alipomuona, akasema:

 “Hakika mwenzenu huyu anakoshwa na malaika”. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaamrisha mashahidi wazikwe pale pale walipofia, akaagiza:

“Wazingirishieni pamoja na damu na majeraha yao, kisha muangalieni aliyekusanya (aliyehifadhi) Qur-ani zaidi kuliko wenzake na mumuweke mbele ya wenzake kaburini”.

 Wakawa wanazikwa na nguo zao zilizolowa damu bila ya kukoshwa. Na walikuwa wakizikwa wawili wawili au watatu watatu katika kaburi moja.

Hili lilitokana na udhaifu na uchovu mkubwa waliokuwa nao maswahaba na hivyo kushindwa kumchimbia kila shahidi kaburi la peke yake.

Idadi ya mashahidi haikupungua sabini, mashahidi wanne wakitoka kwa Muhajirina na waliosalia walikuwa ni katika Maanswari. Kwa upande wa mushrikina waliuliwa watu ishirini na nne.

 

MTUME WA ALLAH AWAFARIJI JAMAA ZA MASHAHIDI. 

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipomaliza shughuli nzima ya mazishi ya maswahaba wake.

Akapanda farasi wake na kuanza safari ya kurudi Madinah akiwa kazungukwa na maswahaba wake, wengi wao wakiwa ni majeruhi.

Maswahaba wanarudi Madinah huku kila alama ya machovu ikidhihiri kutokana na kuendeshwa mbio na makafiri kulikowapata.

Wakenda njiani wakitupiana lawama kutokana na kuikhalifu kwao amri ya Bwana Mtume. Wakawa hawana la kufanya kwa yote yaliyotokea ila kutaraji maghfira ya Allah na awasamehe kuteleza kwao huku.

Bwana Mtume alipowasili Madinah aliwakuta wanawake mlangoni kwake wakiwalilia jamaa, waume na ndugu zao waliokufa mashahidi.

Wanawake hawa walipomuona Mtume wa Allah akija wakasahau huzuni ya ndugu zao, wakaharakia kutaka kujua kama Mtume hakufikwa na dhara.

Walipomuona yu salama, msiba wao ukawepesika na Ummu Aamir Al-Ash-haliyah-Allah amuwiye radhi-akamwambia Mtume:

“Kila msiba baada yako ni mwepesi”.

Ummu Sa’ad Ibn Muaadh-Allah amuwiye radhi-akaja mbio kuelekea aliko Mtume kukagua hali yake.

Hata aliposhusha pumzi baada ya kumuona amesalimika, akasema: “Ama nilipokuona umesalimika, bila ya shaka kila msiba ni mwepesi”.

Bwana Mtume akayapokea maneno haya yaliyobeba imani ya kweli ya mama huyu kwa kumfariji kutokana na kufiliwa na mwanawe; Amrou Ibn Muaadh-Allah amuwiye radhi-katika vita hivi. Kisha akamwambia:

“Ewe Ummu Sa’ad, furahi! Na wape bishara njema jamaa zao (mashahidi) kwamba wauliwa wao wanafuatana peponi”. Ummu Sa’ad akasema:

“Tumemridhia Mtume wa Allah na ni nani atakayewalilia baada ya bishara hii?”

Kisha akamwambia Mtume:

“Ewe Mtume wa Allah! Waombee Mungu waliowaacha (wafiwa)”.

 Bwana Mtume akalipokea ombi lake hili kwa mikono miwili na akawaombea dua kwa kusema: “Ewe Mola wa Haki wee! Ninakuomba uondoshe huzuni ya nyoyo zao, uunge msiba wao na uwape badali njema”.

Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapitisha azimio kwamba maswahaba wake wote waliojeruhiwa wabakie majumbani mwao kwa siku kadhaa ili kuganga majeraha waliyoyapata.

Majeruhi wote wakalipokea azimio hili la Bwana Mtume, wakakesha kwenye mioto wakiyabandika dawa majeraha yao.

Bwana Mtume nae akashika njia kuelekea nyumbani kwake, alipofika hakuweza kushuka kutoka kwenye farasi wake mpaka aliposaidiwa.

Alisaidiwa kushuka na kuingia ndani na maswahaba wake wawili; Sa’ad Ibn Ubaadah na Sa’ad Ibn Muaadh-Allah awawiye radhi.

Sayyidina Bilali-Allah amuwiye radhi-alipotoa adhana ya Maghribi, Bwana Mtume alitoka kwenda kuswalisha kwa msaada wa watu wawili waliomshika upande huu na huu. Baada ya swala kumalizika akarudi nyumbani mwake.

Viongozi wa makabila ya Ausi na Khazraj wakakesha mlangoni kwa Mtume wakimlinda kwa kuchelea asije kushambuliwa ghafla na Makurayshi.

Bwana Mtume alitoa idhini ya kuwalilia mashahidi kwa sababu ya falsafa ya machozi.

Bwana Mtume alitambua kuwa mbubujiko wa machozi huiosha huzuni iliyomo moyoni na kuondosha machungu ya huzuni ya kuondokewa na kipenzi chake mtu.

Pamoja na rukhsa hii ya kulia aliyoitoa, Bwana Mtume alikataza kulia kwa kunyoa nywele, kupara nyuso makucha, kuchana nguo na kuomboleza.

 

BWANA MTUME APELELEZA WANAKOELEKEA MAKURAYSHI

Baada ya kurushiana maneno na waislamu, Abuu Sufyaan akageuza hatamu za farasi wake na huyoo akashika njia kurejea kwa watu wake.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akapendelea kujua Makurayshi wanaelekea wapi. Akamtuma Sayyidina Aliy, akamwambia:

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *