UNYENYEKEVU

Unyenyekevu ni katika jumla ya sifa njema ambazo zimekusudiwa ziwe ni pambo la muislamu.

Tunaweza tukaueleza unyenyekevu kuwa ni hali ya kuizuia na kuiepusha nafsi kuwadharau na kuwaona duni watu wengine, kutokuwa na kibri, maringo, kutokuwa na jeuri na kuilazimisha nafsi kuwaheshimu watu na kuwaona kuwa wao ni bora zaidi kuliko wewe.

Unyenyekevu ni sifa nzuri, kwa sababu humpelekea mtu kupendana na kusaidiana na pia ni alama ya usafi na twahara ya moyo.

Unyenyekevu haumaanishi kujidhalilisha wala kujidunisha, kwa mantiki hii Muislamu hunyenyekea, hajidhalilishi wala kujidunisha kama ambavyo hafanyi kibri.

Muislamu hunyenyekea ili ainuliwe na kupandishwa daraja na wala hafanyi kibri ili asije akawekewa chini ya vilivyo chini.

Hii ndiyo kawaida/kanuni za Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwainua wanyenyekevu na kuwatweza wenye kibri. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –

“Sadaka haiipunguzi mali, na Mwenyezi Mungu hakumzidishia mja kwa sababu ya kusamehe (kwake) ila utukufu na hapana yeyote atakayenyenyekea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ila humnyanyua/humuinua (daraja)” Muslim.

Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kumuamrisha Mtume wake ajipambe na sifa njema ya unyenyekevu :

“NA UINAMISHE BAWA LAKO KWA YULE ANAYEKUFUATA KATIKA WALE WALIOAMINI” [26:215].

Na akasema tena :

“WALA USITEMBEE (usiende) KATIKA ARDHI KWA MARINGO HAKIKA WEWE HUWEZI KUIPASUA ARDHI WALA HUWEZI KUFIKIA UREFU WA MLIMA (Basi unajivunia nini ?)” [17:37].

Na akasema tena Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kuwasifia mawalii (wapenzi wake) kwa sifa nzuri ya unyenyekevu :

“ENYI MLIOAMINI ! ATAKAYEIACHA MIONGONI MWENU DINI YAKE, BASI HIVI KARIBUNI ALLAH ATAWALETA WATU AMBAO (Yeye) ANAWAPENDA NAO WANAMPENDA, WANYENYEKEVU KWA WAISLAMU (wenzao) WENYE NGUVU JUU YA MAKAFIRI …..” [5:54]

Na akatuambia tena kuhusiana na malipo na jazaa ya watu wenyenyekevu :

“HIYO NYUMBA YA AKHERA TUTAWAFANYIA WALE WASIOTAKA KUJITUKUZA KATIKA ARDHI WALA (kufanya) UFISADI, NA MWISHO (mwema) UTAWATHUBUTUKIA WACHA-MUNGU” [28:83].

Naye Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – mfasiri mkuu wa Qur-ani tukufu antufasiria na kutubainishia aya ya hizo za Qur-ani, hebu na tumtegee sikio la usikivu :

“Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu amenifunulia ya kwamba kuweni wanyenyekevu mpaka mtu asijifakharishe juu ya mwingine na wala mtu asimuonee mwenzake” Muslim.

Na akasema tena – Rehema na Amani zimshukie – katika kuraghibisha na kupondokesha unyenyekevu :

“Lau ningealikwa kwenye karamu ya maguu/makongoro ya mbuzi au dhiraa basi ningeliitika na lau ningelipewa hidaya ya dhiraa au maguu ya mbuzi ningelipokea” Bukhariy.

Hapo ndipo unyenyekevu ulipomfikisha Bwana Mtume. Kadhalika Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuasa juu ya sifa mbaya ya kibri :

“Watu wa aina tatu, Mwenyezi Mungu hatozungumza nao siku ya kiyama na wala hatawatakasa na kuwatazama (kwa jicho la rehma) na watapata adhabu kali iumizayo. (Watu hao ni) : Mtu mzima (mzee mwenye umri mkubwa) mzinifu, mfalme muongo na masikini jeuri” Muslim.

Na anazidi kutuasa katika hadithi qudusi :

“Amesema Mwenyezi Mungu mtukufu : Utukufu ni shuka yangu, na kibri ni kishali changu, basi yeyote atayenivua mojawapo ya (nguo) mbili, bila shaka nitamuadhibu” Muslim.

Mambo yafuatayo yanatoa picha na sura ya unyenyekevu :

  1. Mtu akiwatangulia wenziwe, huyo ana kibri, akijiweka nyuma ya wenzie, huyo ni mnyenyekevu.
  2. Akimuinukia mwenye elimu na utukufu na kumpisha mahala alipokaa akae yeye, akiondoka akamuwekea sawa viatu vyake na akamsindikiza, basi matendo haya yanatoa picha ya unyenyekevu alionao mtu huyu.
  3. Akimuinukia mtu wa kawaida na kumpokea kwa bashasha na uso mkunjufu, akamuuliza kwa upole, akaitika wito wake atakapomuita/kumualika, akaijali na kuishughulikia haja yake na wala asijione kuwa yeye ni bora zaidi kuliko mtu huyo. Mwenye matendo haya ni mtu mnyenyekevu.
  4. Akimtembelea mwenzie aliye na hali duni kuliko yeye au kama yeye na akambebea mzigo wake na kumsaidia katika haja yake, huyu ni mnyenyekevu.
  5. Akikaa pamoja na mafakiri, masikini, wagonjwa na walemavu, akaitikia mialiko yao, akala pamoja nao na akatembea nao, matendo haya yenye utu ya mtu huyu yanaonyesha unyenyekevu alionao.
  6. Akila au kunywa bila ya israafu na akavaa bila ya kujifakharisha wala kuonyesha maringo, hii ni alama au dalili ya unyenyekevu.

Haya ni baadhi tu ya mambo mengi ambayo yanaonyesha na kutoa sura/picha ya unyenyekevu alionao mtu.

Kwa maneno mengine tunaruhusika kusema kuwa utakapomuona mtu amepambika na sifa/mambo haya tuliyoyataja, basi mshuhudie kwamba mtu huyo ni mnyenyekevu, ni mtu asiye na kibri, ni mtu asiyejiona kuwa ni bora kuliko wenzake, ni mtu asiye na maringo wala fakhari.

 Hebu sasa tuiangalie kwa jicho la kutafakari, kujifunza na hatimaye kuiga mifano hai hii ionyeshao unyenyekevu wa wenzetu waliotutangulia katika maisha haya :

1.      Imepokelewa kwamba Khalifa Umar bin Abdul Aziz alijiwa na mgeni usiku, naye akiwa anaandika. Taa aliyokuwa akiitumia ikakurubia kuzimika.

Yule mgeni akamwambia : Unaonaje nikiinuka na kwenda kuishughulikia taa ile ? Umar akamjibu mgeni wake :

” Si katika ukarimu mtu kumtumikisha na kumtuma mgeni wake“. Mgeni akasema : “basi nimuamshe mtumishi?” Umar akamwambia : “Mtumishi ndio kwanza analala, kwa hiyo usimuamshe”.

Akainuka mwenyewe akaenda kuitia taa mafuta, na mgeni wake alipomwambia : Umeinuka wewe mwenyewe ewe Amirul- Muuminina?. Akamjibu kwa kusema :

“Nimeenda/nimeinuka na il-hali nikiwa Umar na nimerudi na il-hali nikiwa Umar yule yule bila ya kupungua chochote, na bora ya watu ni yule aliye mnyenyekevu mbele ya Mwenyezi Mungu”.

Ni vema ikafahamika ikakumbukwa kwamba huyu Umar bin Abdul Aziz alikuwa ni kiongozi (khalifa)wa waislamu.

2.      Imepokelewa kwamba siku moja Amirul-Muuminina Sayyidna Ali – Allah amuwie radhi – alinunua nyama na kujitayarisha kuichukua, akaambiwa : Ubebewe ewe Amirul-Muuminina ? Akajibu : Hapana, mwenye mzigo ndiye anayestahiki zaidi kuubeba mzigo wake. Na mfano wa haya pia yamepokewa kwa Mtume.

 

3.      Alisema Abu Salamah : Nilimwambia Abu Said Al-Khudriy : Unayaonaje haya waliyoyazua watu katika mavazi, vinywaji, vipando na malaji ?.

 

Akamjibu : Ewe mwana wa ndugu yangu, kula kwa ajili ya Allah, kunywa kwa ajili ya Allah, na vaa kwa ajili ya Allah, na chochote katika hivyo (kula, kunywa na kuvaa) kitachoingiwa na kujiona, kujifakharisha au kujulikana, hilo ndilo maasi na israfu.

Na fanya utumishi nyumbani kwako kama alivyokuwa akifanya Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie – nyumbani kwake.

Alikuwa akimlisha na kumfunga ngamia mchota maji, akifagia nyumba na kukama mbuzi, akisafisha viatu na kushona/kutia kiraka nguo.

Akila pamoja na mtumishi wake, na akimtwangia anapochoka, akienda sokoni kununua mahitaji na haya haikumzuia kubeba mkononi mzigo wake au kuufunga katika ncha ya nguo yake na kurudi kwa wakeze.

Na alipokuwa akipeana mkono na tajiri na masikini mkubwa na mtoto. Na akianza kumtolea salamu kila aliyekutana nae, mkubwa au mdogo, mweusi au mweupe, mtumwa au mwungwana.”

Hebu na tujiulize kuna kiumbe bora na mtukufu kuliko Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – ?

Bila shaka jawabu ni hapana, kama tunakongomana katika hilo, basi hebu muangalie namna alivyokuwa akishiriki katika kazi za nyumbani pamoja na kuwa alikuwa na wake wengi na watumishi chungu nzima.

Yeye alikuwa ni mtu wa kukaa mguu juu na kuamrisha tu, lakini hakufanya hivyo. Je, sisi leo majumbani mwetu tunakula pamoja na watumishi wetu ?!

Chakula tulacho ndicho walacho wao ?! Je, leo majumbani mwetu tunawasaidia kazi wake zetu ?! Kama hatuyafanyi haya, hicho si kibri na kujiona ?!

Je, tunamfuata na kumuiga nani ili hali Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuambia :

“BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA (ruwaza nzuri) KWA MTUME WA ALLAH, KWA MWENYE KUMUOGOPA ALLAH NA SIKU YA MWISHO NA KUMTAJA ALLAH SANA” [33:21].

Je, sisi waislamu wa leo, hatumuogopi Allah na siku ya mwisho ? Kama tunamuogopa, kwa nini basi hatumfanyi Bwana Mtume kuwa ndio kigezo chetu ?!

 Tuufuate mwenendo wa Mtume wetu na tuwe wanyenyekevu ili tupate kunadi sada na kufaulu duniani na akhera. 

FALSAFA YA SWALA: 3.UNYENYEKEVU

Unyenyekevu unapatikanaje ndani ya swala?

Huoni kuwa ni upeo wa unyenyekevu usio ni mithali pale muislamu anapokiweka mavumbini kiungo chake kitukufu “Uso” kumsujudia Mola wake.

Tena wakalingana sawa katika unyenyekevu huu watu wote, wakubwa kwa wadogo, wanaume na wanawake, mabwana na watwana.

Hapana kichwa cho chote kinachoweza kuwa juu ya kichwa kingine katika rukuu na sujudi.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *