HUKUMU YA SHERIA KATIKA FIQHI

Baada ya kuona faida na umuhimu wa fiq-hi hatuna budi kujua hukumu ya sheria katika elimu hii.

Kila elimu katika Uislamu ina hukumu yake, elimu ya uchawi kwa mfano ni haramu kujifunza, elimu ya udaktari ni fardhi ya kutoshelezeana ndani ya mji, kama hakuna mwenye elimu hiyo ndani ya mji mzima basi wakazi wote wa mji ule huwa na madhambi.

Elimu ya fiq-hi ni fardhi kwa muislamu kujifunza kwani kwa kupitia elimu ndiyo huweza kutekeleza maamrisho ya Mwenyezi Mungu.

Lakini ufaradhi huu unatofautiana baina ya mtu na mtu. Kwa mwengine huwa ni fardhi ya lazima kujua vipengele fulani na kwa mwengine huwa ni fardhi kifaaya.

 

FARADHI YA LAZIMA:

Kujifunza, kuijua na kutumia elimu hii ya fiq-hi inakuwa ni faradhi ya lazima kwa kila Muislamu mwanamume na mwanamke katika mambo ya ibada ya kila siku, kwa mfano sala na funga.

Kujua kutoa zaka, au kujua jinsi ya kuhiji wakati hana uwezo si fardhi ya lazima bali ni faradhi kifaaya, ama kwa mwenye uwezo ni fardhi ya lazima kujua elimu hizo.

Kwa mantiki hiyo hiyo, mwenye kufanya biashara ni fardhi ya lazima kujua vipengele vya kufanya biashara ndani ya fiq-hi ili biashara yake iwe kwa mujibu wa sheria ya kiislamu, na kama hajafanya hivyo atakuwa na makosa mawili, kosa la kwanza ni kutojifunza hukmu ya uislamu ndani ya kazi yake na kosa la pili ni kutokufanya biashara yake kwa mujibu wa sheria kwa hivyo fahamu.

 

FARADHI YA KUTOSHELEZEANA

Elimu hii inakuwa ni faradhi ya kutoshelezeana katika masuala ya mirathi, elimu ya ukadhi, elimu ya kutoa fat-wa na elimu nyingine zinazofanana na hizo.

Sasa ikiwa ndani ya mji hakuna anayejua masuala ya mirathi, wakazi wote huwa na madhambi kwa kutojifunza elimu hiyo.

Huu ndio mgawanyo wa hukumu ya sheria kuhusiana na fani hii ya elimu ya fiq-hi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *