KUWAHURUMIA WANYAMA

 KUWAHURUMIA WANYAMA

Wanyama ni miongoni mwa viumbe hai ambao Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa fadhila zake ametuambia tuwahurumie ili watusaidie na kututumikia katika maisha yetu hapa duniani.

Kwa hivyo ni wajibu wetu kuwanea huruma. Mwenyezi Mungu atuambia:

“NA (pia) AMEWAUMBA WANYAMA KATIKA HAO MNAPATA (vifaa vitiavyo) JOTO NA MANUFAA (mengine); NA WENGINE MNAWALA: NA MNAONA RAHA MNAPOWARUDISHA JIONI NA MNAPOWAPELEKA MALISHONI ASUBUHI. NA (wanyama hao pia) HUBEBA MIZIGO YENU KUPELEKA KATIKA MIJI MSIYOWEZA KUFIKA ISIPOKUWA KWA MASHAKA NA TAABU. HAKIKA MOLA WENU NI MPOLE SANA (na) MWENYE REHEMA NYINGI NA (amewaumba) FARASI NA NYUMBU NA PUNDA ILI MUWAPANDIE NA (wawe) MAPAMBO…” (16:5-8)

Utafahamikiwa kutokana na aya hizi kwamba wanyama manufaa mengi sana kwa wanadamu.

 Wanyama wana sifa nyingi za kimaumbile zinazoshabihiana na zile za binadamu.

Miongoni mwa sifa hizo ni kushikwa na kiu na njaa, kuugua, kuona baridi au joto, kuhitajia mahala pa kulala, kuchoshwa na kazi ngumu na kadhalika.

Kwasababu hizi imemlazimu mwanadamu kumuhurumia mnyama kwa kumpa chakula na maji ya kutosha, kumpa malazi mazuri, kumtibu anapoumwa, kutomkalifisha kufanya kazi asizoziweza na kutomuadhibisha wakati wa kumchinja.

Amesema Bwana Mtume katika hadithi aliyoipokea Abu Hurayrah:

“Wakati mtu mmoja alipokuwa akienda (njiani) akashikwa na kiu kikali sana. Akashuka kisimani akanywa maji kisha akatoka, kutahamaki akamuona mbwa akihema na kula mchanga kutokana na kiu. Akajisemea (nafsini mwake): kimempata huyu kiu kama kilichonipata mimi. Akakijaza maji kiatu chake, kisha akakishika kwa mdomo wake akapanda (kutoka kisimani kuja juu). (Akanywa) mbwa akakata kiu, akamshukuru Mwenyezi Mungu, akasamehewa yule mtu madhambi yake. Wakauliza (maswahaba): Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sisi tunapata ujira kwa (kuwafanyia wema) wanyama? (Mtume) akajibu: “kuna ujira katika kila ini bichi (mnyama hai)” Al-Bukhaariy.

Katika hadithi hii tunamuona mwanadamu huyu anachukua taabu anaingia kisimani kuchotea mbwa maji na kumnywesha.

Yote haya yanatokana na huruma iliyomo moyoni mwa mtu yule, isingelikuwa huruma asingeweza kufanya aliyoyafanya.

Tabia na kitendo chake hiki cha huruma kimekuwa ni sababu ya kusamehewa dhambi zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *