KUWA NA MSIMAMO

Kuwa na msimamo, hii ni sifa muhimu na ya msingi ambayo ndiyo inayotakiwa iutawale na kuudhibiti utendaji wa kila siku wa muislamu.

Kwa hiyo basi, ili muislamu aweze kuutekeleza uislamu wake katika nyanja zake zote za maisha, mahala popote, wakati wowote na katika mazingira na hali yoyote ile iwayo, basi ni lazima alivae vazi na joho hili la msimamo ili aweze kupata ufanisi na tija katika utendaji wake huo.

Nini maana au tunakusudia nini tunaposema kuwa na msimamo ? Hebu tuingie katika mgodi huu wa Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – tuyachimbe madini haya ya thamani “msimamo”.

Siku moja, mtu mmoja alimuendea Bwana Mtume na kumtaka ushauri akasema; Niusie ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Bwana Mtume akamwambia;

“Sema; Nimemuamini Allah, kisha uwe na msimamo.” Ahmad. Muslim, Tirmidhiy, Nasai na Ibn Maajah. Kupitia mafundisho haya, tunaipata taswira ambayo inatoa maana ya kuwa na msimamo kwa mujibu na muktadha wa Imani ya kiislamu. Kuwa na msimamo ni pamoja na:

  1. kuamua kwa kukata shauri.
  2. Kusimamia utekelezaji wa maamuzi hayo.
  3. Kuyaheshimu maamuzi hayo kwa gharama yoyote.
  4. Kuishi kwa mujibu wa maamuzi hayo

Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa na msimamo ni kuifuata njia iliyonyooka, ambalo hili halitopatikana ila baada ya kuijua hiyo njia nyoofu yenyewe.

Kwa mantiki hii, ili msimamo uwe msimamo na ukubalike hivyo ni lazima uwe unatokana na ujuzi/elimu, kama msingi na nguzo kuu ya msimamo.

Kinachofuatia baada ya kuijua na kufuata hiyo njia nyoofu ni utendaji kwa mujibu wa dira, maelekezo na muongozo wa njia nyoofu hiyo. Utekelezaji huu ni lazima uegemezwe katika vigezo viwili, ambavyo ni:- :

 1. Maamrisho. Mwenye msimamo wa kweli na haki ni lazima msimamo wake huo, umsukume kutekeleza amri / maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kama alivyoyapata katika njia nyoofu. Popote pale aikutapo amri ni lazima aamrike pale pale bila ya kusita, kuwa na khiyari au kujishauri kwanza.
 2. Makatazo. Kipimo bora cha kuupima msimamo wa mtu ni pale utakapoonekana msimamo wake huo umefanikiwa na kumudu kuikataza, kuikemea na kuizuia nafsi yake kutenda yale yote aliyokatazwa kupitia njia nyoofu. Mwenye msimamo imara, wa kweli na haki ni yule ambaye hujitahidi upeo wake kujiepusha na kujiweka mbali kabisa na yale aliyokatazwa na Mola Muumba wake.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, mtu hatoambiwa na wala hatokubalika kuwa ana msimamo mpaka kwanza alijue hilo analoliwekea masimamo, kisha ndipo aamue kulifuata. Akishaamua na kuchagua kulifuata, aheshimu uamuzi wake huo. Heshima ya uamuzi wake huo iwe ni pamoja na kulinda na kusimamia utekelezaji wake.

Mtu atakapozifuata taratibu zote hizi, hapo ndipo Uislamu unamvisha nishani ya msimamo. Nishani hii ya juu kabisa inaambatana na zawadi nono ifuatayo:, tutafakari na tuzingatie :

WALE WALIOSEMA: “MOLA WETU NI ALLAH KISHA WAKAWA NA MSIMAMO (Wakenda mwendo mzuri), HAO HUWATEREMKIA MALAIKA (Wakati wa kutoka roho wakawaambia) : MSIOGOPE WALA MSIHUZUNIKE NA FURAHINI KWA PEPO MLIYOKUWA MKIAHIDIWA” [41:30]

 Tunafahamu kutokana na aya hii kwamba, kuwa na msimamo katika maisha haya ndio tegemeo na silaha kuu itakayomsaidia na kumuokoa mtu na huzuni na khofu ya siku nzito.

Hii ni siku ya kubadili maisha, kutoka maisha haya ya ulimwengu huu kwenda maisha yenye kanuni tofauti, maisha ya akhera.

Hapo ndipo mja anapoanza kuvuna na kufaidi matunda mabivu na matamu ya mmea bora ” msimamo” alioupanda katika maisha yetu haya,

Ni vema Muislamu akatambua na kuelewa kwamba suala la kuwa na msimamo si suala la utashi na matakwa ya mtu bali hii ni agizo na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mtume wake seuze sisi wafuasi wa Mtume huyu. Tusome:

” BASI (Ewe Mtume !) ENDELEA NA UWONGOFU (uwe na msimamo) KAMA ULIVOAMRISHWA, (wewe) NA WALE WANAOELEKEA (kwa Allah) PAMOJA NAWE, WALA MSIRUKE MIPAKA. HAKIKA YEYE ANAYAONA YOTE MNAYO YATENDA.” (11:112)

Msimamo thabiti uliojengwa katika maana na misingi ya Uislamu ni lazima uyaguse na kuyaathiri maeneo yaufuatayo :-.

 1. Ulimi: Mtu aunyooshe ulimi wake katika kupima na kufikiri kwanza kabla hajaamua kusema analotaka kulisema.

Auzoeshe ulimi wake kumshukuru na kumuhimidia Mola wake, kusema kweli, kukemea maovu, kama vile dhuluma, rushwa, ukandamizaji na kadhalika.

Ni kutokana na umuhimu, hatari na mchango wa kiungo hiki muhimu cha mwanadamu katika maisha ya mwanadamu, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuambia :-

“Atakayenidhaminia (atakayenichukulia dhamana) ya kilichomo baina ya taya mbili (ulimi) na kilicho baina ya miguu yake (tupu), ninamchukulia dhamana ya (kuingia) peponi”. Bukhaariry na Muslim

 1. Nafsi. Kutokana na ukweli kuwa nafsi ya mwanadamu humvutia sana kwenye uovu, kama tunavyosoma”

“….KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU….” (12:53)

Ni lazima msimamo wa mja umjengee ukuta imara na madhubuti baina yake na maovu.

 Hapo ndipo ataweza kumtii kikamilifu Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mtume wake na wenye mamlaka juu yake (Wanaotumia kitabu cha Allah katika mamlaka yao).

Ataweza kuwa na haya ya kweli kwa Mwenyezi Mungu na viumbe wenzake, ataheshimu na kutekeleza haki ya Mola wake na haki za viumbe wenzake, atayajua majukumu na wajibu wake kwa Mola Muumba wake na viumbe wenzake.

 1. Moyo: Hii ndilo eneo linaloathiri utendaji mzima wa mtu, utendaji huo ukiwa ni wa kheri wenye baraka na radhi za Mola au ni ule wa shari unaoambatana na ghadhabu na hasira za Mola Mwenyezi.

Ukweli huu unathibitishwa na kauli ya Mtume wa Allah. Rehema na amani zimshukie:

“….Ehee ! Hakika mwilini kuna pande la nyama ambalo litakapotengenea hutengenea mwili mzima na litakapofisidika, hufisidika mwili mzima, ehe ! jueni pande hilo ni moyo”. Bukhaariry na Muslim.

Ni kutokana na taathira hii ya moyo katika mwili mzima wa mwanadamu, ndio ikawa ni lazima msimamo wa mja uuathiri moyo ili utoe utendaji na maelekezo mema kwa mwili mzima.

Uujenge moyo kuwa katika hali ya kuzikhofu adhabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu, jambo ambalo natija yake ni twaa kwa Allah, na moyo uwe katika hali ya kutaraji kupata radhi za Allah na natija yake ni kutenda amali zake zote kwa ajili ya Allah pekee.

Msimamo ukiyaathiri maeneo hayo ndipo mtu anastahiki kuvikwa nishani na taji tulilolitaja huko nyuma.

Hebu sasa kupitia Qur-ani tujaribu kuiangalia athari ya msimamo uliotokana na kujua na kisha kuamua. Tusome na tuzingatie kisa hiki cha Nabii Musa, firauni na wachawi wa firauni :

“BASI WACHAWI WAKAANGUSHWA (wakapinduliwa chini) WANASUJUDU NA KUSEMA : ” TUMEMUAMINI MOLA WA HARUNI NA MUSA.” (firauni) AKASEMA : “OH ! MNAMUAMINI KABLA SIJAKUPENI RUHUSA ! BILA SHAKA YEYE NDIYE MKUBWA WENU ALIYEKUFUNZENI UCHAWI. KWA HIYVYO NITAKUKATENI MIKONO YENU NA MIGUU YENU KWA KUTAFAUTISHA (mkono wa kulia na mguu wa kushoto na mkono wa kushoto na mguu wa kulia) NA NITAKUSULUBUNI (nitakuwambeni) KATIKA MASHINA YA MITENDE, NA BILA SHAKA MTAJUA (wakati huo) NI NANI KATIKA SISI (mimi au mungu wake Musa) ALIYE MKALI WA KUADHIBU NA KUENDESHA (kuiendeleza adhabu yake). WAKASEMA (Wachawi) HATUTAKUKHITARI WEWE KULIKO ZILE ISHARA WAZIWAZI (za haki) TUNAAPA KWA YULE ALIYETUUMBA (hatutakuhitari wewe). BASI FANYA UNAVYOTAKA KUFANYA. WEWE UNAWEZA KUTOA HUKUMU INAYOHUSIANA NA MAISHA HAYA YA DUNIA TU. KWA YAKINI TUMEMUAMINI MOLA WETU ILI ATUSAMEHE MAKOSA YETU NA UCHAWI ULE ULOTUSHURUTIZA (kuufanya). NA ALLAH NDIYE BORA NA WA KUDUMU (siyo wewe)” [20:70-73]

Huu ndio uliokuwa msimamo wa wachawi wale wanyonge mbele ya Firauni Mtawala mwenye nguvu na majeshi.

Wachawi hawa wasingethubutu na kujasiri kumwambia mfalme huyu ukweli unaouma na kuuchoma moyo kama msimamo wao haukutokana na kujua na kisha kuamua.

Wachawi hawa walimjua Nabii Musa fika na wala hakupata kuwa mwanafunzi wa yeyote miongoni mwao, kwa hivyo wakatambua ni wazi kuwa hayo wamuonayo akiyafanya na kuushinda uchawi wao hayatokani na nguvu za uchawi walioziamini bali ni lazima iko nguvu nyingine isiyoshindika ambayo si ya Musa.

Hapo ndipo wakakata shauri kumuamini Mussa, kisha, wakawa na msimamo thabiti katika kuitetea na kuilinda Imani yao hiyo, bila ya kusalimu amri kwa firauni.

 

KUWA NA MSIMAMO

Kuwa na msimamo, hii ni sifa muhimu na ya msingi ambayo ndiyo inayotakiwa iutawale na kuudhibiti utendaji wa kila siku wa muislamu.

Kwa hiyo basi, ili muislamu aweze kuutekeleza uislamu wake katika nyanja zake zote za maisha, mahala popote, wakati wowote na katika mazingira na hali yoyote ile iwayo, basi ni lazima alivae vazi na joho hili la msimamo ili aweze kupata ufanisi na tija katika utendaji wake huo.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *