UTUKUFU WA NAFSI / KUJITHAMINI

Uislamu unamtaka muislamu ajithamini mwenywe kabla ya kudai kuthaminiwa na jamii.

Yeye mwenyewe aseme kauli au atende matendo yatakayompa thamani na daraja mbele ya Mola Muumba wake, Mtume wa Allah, waumini wenziwe na jamii ya wanadamu kwa ujumla. Tusome:

“…….NA UTUKUFU HASA NI WA ALLAH NA MTUME WAKE NA WA WAUMINI LAKINI WANAFIKI HAWAJUI”. (63:8)

Utukufu wa nafsi/kujithamini sambamba na kujithaminisha ni mali na pambo la muumini.

Kwa sababu hii ndiyo sifa inayomfanya mtu azikwae ngazi kuufikia utukufu, daraja na heshima.

Chanzo kikuu cha sifa hii ni mtu kujijua kwanza yeye mwenywe ni nini atende au asitende nini na kwa nini, sambamba na kuijua nafsi yake mbele ya Mola wake na mbele ya viumbe wenzake.

Mtu akiyatambua yote hayo, itampelekea na kumuongoza kujiheshimu yeye mwenyewe ili jamii imuheshimu pia. Atajichunga katika kauli, matendo, uvaaji, utembeaji na namna zake nyingine za kuchanganyika na jamii.

Ikumbuke kuwa utakavyojitokeza kwa jamii ndivyo jamii itakavyokupokea.

Turejee na tupekue kurasa za historia, tutamkuta Mtume wa Mwenyezi Mungu-Rehema na Amani zimshuke- anajitokeza kwa jamii yake katika sura ya ukweli na uaminifu na jamii nayo inampokea na kumkubali kuwa ni Mkweli Muaminifu.

Mtu akijipamba na sifa hii ni lazima tu atajulikana kupitia kauli/matendo yake ya kila siku na hayo ndiyo tunayoyaita matunda ya utukufu wa nafsi/kujithamini.

Miongozi mwa matunda mapevu na matamu ya mti huu ni:-

1.   Kujipamba na tabia njema.

Mtu akijithamini ni lazima atakuwa na tabia njema. Tabia njema ndiyo sifa kuu aliyokuwa nayo Bwana Mtume-Rehema  na Amani zimshukie, Mola wake anamsifia:

“NA BILA SHAKA WEWE UNA TABIA NJEMA KABISA” (68:4).

Kadhalika tabia njema ndiyo ilikuwa sababu ya mafanikio aliyoyapata Mtume wa Mwenyezi Mungu na kufanikiwa kufanya mapinduzi yaliyobadilisha hali na itikadi za watu kwa muda mfupi tu. Mola wake anamkumbusha juu ya hili, anamwambia

“BASI KWA SABABU YA  REHEMA ITOKAYO KWA ALLAH UMEKUWA LAINI KWAO (Ewe Muhammad) NA KAMA UNGEKUWA MKALI NA MWENYE MOYO MGUMU BILA SHAKA WANGALIKUKIMBIA…….” (3:159).

2.   Kusubiri juu ya matatizo na majanga mbalimbali .

Mtu mwenye kujithamini utu wake anapofikwa na matatizo mbalimbali ya kimaisha kama maradhi, dhiki ya maisha, misiba hapapatiki wala kubabaika.

Hii ni kwa sababu anaelewa fika na kuamini kuwa yote yamfikayo ni mtihani kutoka kwa mola wake.

Kwa hiyo husubiri na kutafuta ufumbuzi kutoka kwa Mola Mwenyezi. Kuhusiana na tabia hii ya mwanadamu kupapatika anapofikwa na matatizo, Qur-ani inasema

“ KWA HAKIKA BINADAMU AMEUMBWA HALI YA KUWA MWENYE PAPATIKO, INAPOMGUSA SHARI HUWA MWENYE FAZAA” (70: 19-20).

Muumini hauvunji utu wake anaposibiwa na matatizo na shida kadha wa kadha kwa kuwaendea waganga na watabiri. Kujithamini humzuilia kabisa na hilo na husema:

 “……NAMI NINAMKABIDHI (namwachia) ALLAH MAMBO YANGU: HAKIKA ALLAH ANAWAONA WAJA (wake wote) “ (40: 44.)

3.   Huwa haonyeshi uhitaji wake.

Muumini huitukuza nafsi yake kwa kutokuudhihirisha uhitaji wake kwa watu.

Si tabia ya muislamu kupita huku na kule akimueleza kila mtu shida na matatizo yake. Bali shida zake hubakia kuwa ni siri  isiyofichuliwa ila kwa watu maalum wanaomuhusu tu, halalami kwa kila mtu. Qur-ani inawataja watu hawa:

“….ASIYEWAJUA HALI ZAO ANAWADHANI KUWA NI MATAJIRI KWA SABABU YA KUJIZUIA KWAO (na kuomba) UTAWAFAHAMU (kuwa wahitaji) KWA ALAMA ZAO (zinazoonyesha ufakiri, lakini) HAWAOMBI WATU WAKAFANYA UNG’ANG’ANIZI………” (2:273).

4.   Watu humuheshimu.

Mtu akijithamini yeye mwenyewe bila shaka atawathamini na wenziwe na hivyo kuziba kabisa mianya ya kuvunjiwa heshima na kufanyiwa utovu wa adabu.

Hili linatokana na ukweli kwamba ni maumbile ya mwanadamu kutenda kama anavyotendewa. Ukimtukana nae atajibu, ukimdharau nae atakudharau, ukimpenda nae atakupenda, ukimuheshimu nae  atakuheshimu.

Hayo ni sehemu ya umbile aliloumbiwa mwanadamu.

Inatakikana kwa muumini mwenye akili  na kujithamini asijiingize katika kusema na kutenda kila ambalo litakuwa ni sababu ya kudharauliwa na kuvunjiwa heshima. Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – anatuambia:

“ Haitakikani kwa muumini kujidhalilisha. (Maswahaba) wakamuuliza: vipi atajidhalilisha? Akawajibu: “kwa kujiingiza kwenye mabalaa asiyoyaweza”.

 

UTUKUFU WA NAFSI / KUJITHAMINI

Uislamu unamtaka muislamu ajithamini mwenywe kabla ya kudai kuthaminiwa na jamii.

Yeye mwenyewe aseme kauli au atende matendo yatakayompa thamani na daraja mbele ya Mola Muumba wake, Mtume wa Allah, waumini wenziwe na jamii ya wanadamu kwa ujumla. Tusome:

“…….NA UTUKUFU HASA NI WA ALLAH NA MTUME WAKE NA WA WAUMINI LAKINI WANAFIKI HAWAJUI”. (63:8)

Utukufu wa nafsi/kujithamini sambamba na kujithaminisha ni mali na pambo la muumini.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *