BWANA MTUME ATOKA MAFICHONI NA KUELEKEA MADINA

Makurayshi walipokata tamaa ya kumtia mbaroni Mtume wa Allah na kuamini kwamba tayari atakuwa nje ya mipaka ya himaya yao.

Hapo ndipo Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipoitumia fursa hiyo kutoka pangoni mle, tayari kwa safari ya kuelekea Madinah.

Lilikuwa ni jambo lisiloingia katika dhihni na fikra  za makurayshi kwamba Mtume anaweza  kuwaponyoka bila ya kumkamata.

Baada ya kukaa pangoni thauri kwa muda usiopungua siku tatu, ndipo alipokuja yule mtaalamu wa njia waliyemkodi.

Akaja na wale ngamia wawili aliopewa na Abuu Bakri – Allah amuwiye radhi – kwa ajili ya safari yao hiyo na ngamia mwingine kwa ajili yake yeye.

 Bila ya kupoteza muda, wote watatu, Bwana Mtume, swahibu yake na mtaalamu wa njia, wakaanza kujiandaa kwa ajili ya safari ndefu iliyosheheni hatari njia nzima.

Ibn Is-haaq – Allah amrehemu – anasimulia:

 “Abuu Bakri- Allah amuwiye radhi – alivisogeza vipando viwili vile kwa Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie – akampa yule aliye bora na kumwambia

“Panda,  nakufidia baba na mama yangu!” Mtume  akasema:

“Mimi siwezi kumpanda ngamia asiye wangu” Akasema (Abuu Bakri) Huyo ni wako ewe Mtume wa Allah (Mtume) akasema

” Hapana, niambie umemnunua kwa thamani gani?” Akajibu

“Kiasi kadha wa kadha” (Mtume) akasema:

“ Nimekubali kumchukua kwa thamani hiyo: (Abuu Bakri) aksema, “Huyo ni wako tu ewe Mtume wa Allah”) Wakapanda na kuanza safari………………..

Bi Asmaa bint Abuu Bakri – Allah amuwiye radhi yeye na babiye – alikuwa amewaletea chakula maalum cha safari na  kukihifadhi katika chombo kinachoweza kuchukulika kiurahisi safarini.

Mtume autupia mji wa Makkah jicho la kwaheri .

Msafara huu wa Mtume ukaanza safari kwa jina la Allah wakati giza lilipochukua nafasi ya nuru ya mchana na mwezi kutawala mahala pa jua.

Msafara huu ulikuwa ni mwanzoni mwa mwezi wa mfunguo sita. Msafara ulipoielekea njia ya Madinah tayari kuondoka, Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akageuka nyuma na kuutazama mji wa Makkah mtazamo wa kwaheri kwa kitambo, kisha akasema,

“Wallah! Hakika mimi ninatoka ndani yako na il-hali ninajua kwamba wewe (Makkah) ndiwe kipenzi cha ardhi ya Allah mbele ya Allah na tukufu yake. Lau si watu wako (wakazi wako) kunitoa ndani yako (kwa nguvu) nisingelitoka.

Hii ni kwaheri iliyosheheni na kujaa uzalendo na mapenzi ya kweli kwa mji huu mtukufu ulio kipenzi cha Allah na Mtume wake. Kwa heri inayoashiria majonzi na masikitiko ya Mtume wa Allah juu ya kutengana na mji wake huu aliuzoea na kuupenda.

Mtaalamu wa njia awapitisha njia yenye usalama zaidi.

Msafara ulipoondoka, yule mtaalamu wa njia akautumia ujuzi na uzoefu wake kuwapitisha katika njia yenye usalama  na amani na akijiepusha kupita njia aliyohisi kuwa inaweza kuwa ni hatari kwao.

Hawakupita katika njia iliyokuwa ikitumika na watu wote inayoelekea nyanda za juu kaskazini.

Bali wao waliifuata ile njia isiyozoeleka ya nyanda za chini kusini ipitayo chini ya Makkah kuelekea upande wa Yemen.

Kisha wakaelekea Mashariki upande wa Pwani ya Ithamah, wakaenda mpaka walipoukaribia ukanda wa mwambao wa bahari (Red Sea) wakaelekea kaskazini wakiiacha njia iliyozoeleka.

Ramani  ifuatayo itakusaidia kuona jia alimopitia msafara tokea Makkah mpaka Madinah.

Wakaendelea na msafaa wao usiku kucha na nusu ya mchana, wakapumzika kutokana na uchovu chini ya mwamba.

Makurayshi watangaza zawadi nono kwa yeyote atakayemkata Bwana Mtume na kuwaletea akiwa hai au amekufa.

Makurayshi waliposhindwa kumpata Bwana Mtume wao wenyewe baada ya juhudi za makusudi, wakaamua kutafuta msaada kutoka kwa wakazi  wa vitongoji vilivyo nje ya mji Makkah.

Ili kuwahamasisha  kujituma na kuifanya kazi hiyo haraka iwezekenavyo, wakaweka  kivutio/Motisha.

 Wakatangaza zawadi nono ya ngamia mia moja kwa yeyote yule atakayewaletea Mtume, hasimu wao mkuu akiwa hai (mateka) au amekufa (maiti).

Ngamia mia moja ilikuwa ni dau kubwa mno kuwahi kutolewa katika historia ya Waarabu. Dau hili likawavutia na kuwashawishi wengi miongoni  mwa watu wa vitongoji kuingia katika wimbi la kumsaka Mtume wa Allah kwa tamaa ya kupata zawadi hii nono.

Kupata ngamia mia moja katika fikra zao hakukumaanisha kingine zaidi ya kuupiga teke umaskini. Miongoni mwa walowania na kupania kupata zawadi hii nono alikuwa ni Suraaqah Ibn Maalik.

Huyu ni mtu wa kabila lililokuwa likijulikana kama Bariy Mudlaj, hawa ni wakazi na wenyeji wa kitongoji kilichojulikana kama Qudayd (Fudhayd).

Kitongoji hiki kilipakana na pwani ya “Raabigh” Kabla ya kutangazwa kwa zawadi hii nono, tayari Suraaqah alikuwa amepata khabari kwamba kuna watu watatu wameonekena wakipita katika pwani yao.

Aliposikia tangazo lile akawa hana  sababu ya kuamini kwamba hao walionekana ndio hao watafutwao: bila shaka huyo atakuwa ni Muhammad na Wafuasi wake.

Tamaa ya zawadi ile nono ikamtambaa mwili mzima na kumshajiisha  kuingia msakoni. Akaanza kufuata mbiombio nayo zilizoachwa nyuma na Mtume na wenzake, akiwa na imani kuwa atakuta tu njiani.

Hebu na tumpe nafasi Imam Bukhaairy- Allah amrehemu – atupokelee hadithi kutoka kwa Ibn Shihaab ikielezea aliyoyasimulia Suraaqah mwenyewe  yale yaliyomkuta katika msako wake huo, anasema (Suraaqah)

“Walitujia wajumbe wa makafiri wa kikurayshi, wakaweka dau kubwa kwa yoyote yule atakayemkamata mateka au kumuua Mtume wa Allah na Abuu Bakri.

Wakati nilipokuwa nimekaa  katika mojawapo  ya baraza za kaumu yangu, mara ghafla akaja mtu mmoja  wa kabila letu akatusimamia huku sisi tukiwa tumekaa.

Akasema. Ewe Suraaqah hakika mimi nimeona muda mchache tu uliopita kiwingu cheusi (watu kwa mbali) ufukweni.

Ninadhani huyo atakuwa ni Muhammad na wenziwe tu. Suraaqah akasema: Nikatambua kwamba hao aliowaona ndio wenyewe khasa, nikamwambia:

Hao sio wao, lakini wewe umemuona fulani na fulani ambao wameondoka hapa hapa mbele ya macho yetu.

Kisha nikakaa kitambo kidogo katika baraza ile, halafu nikainuka nikaenda nikamuamuru mjakazi wangu atoke na farasi wangu mpaka nyuma ya kilima anisubiri hapo.

Nikautwaa mkuki wangu na kutoka nao kwa kupitia nyuma ya nyumba yangu.

Nikaenda mpaka kule alikokuweko farasi wangu akinisubiri nikampanda.

Nikamuendesha shoti mpaka nikawakaribia, farasi wangu  akanipiga mweleka na kunibwaga chini pwaa!

 Nikainuka  na kuupeleka haraka mkono wangu kwenye mkoba wangu wa mishale, nikatoa mishare ya  kupigia ramli.

Nikapiga bao (ramli) kwa mishare hiyo. Ukatoka mshare niuchukiano, nikaipuuzia mbali ramli ile, nikampanda tena farasi wangu Farasi wangu akaenda, mbio mpaka nikawakaribia tena kwa mara ya pili.

Nikawa namsikia Mtume wa Allah akisoma (Qur-an) bila ya kugeuka nyuma na Abuu Bakri akigeuka mara kwa mara. Hapo ndipo ilipozama mchangani miguu ya farasi wangu mpaka kufikia magotini.

Nikaruka kutoka juu yake, nikamkemea akainuka, kabla hajamaliza kuitoa mikono yake likatimka vumbi liloenea angani mithili ya moshi.

Nikapiga ramli tena na bado ukatoka ule ule mshare niuchukiao. Mpaka hapo sikuwa na hila tena ila kuwatolea mwito wa amani, wakasimama, wakasimama.

Nikampanda farasi wangu mpaka nikawafikia. Kutokana na yote yaliyonisibu, ikanipitia moyoni kuwa ibla ya shaka jambo hili la Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie litadhihiri tu.

Nikamwambia hakika ndugu zako wamekuwekea dau na nikawaeleza khabari za namna watafutwavyo, nikawapa pamba (chakula cha safari).

Hawakunikatalia wala kuniomba ila waliniambia: Wapoteze watu nasi (usiwaambie njia tupitayo). Nikamuomba aniandikie hati/mkataba wa amani, akamuamrisha Aamir Ibn Fuhayrah aniandikie katika kipande cha ngozi. Kisha Mtume wa Allah, huyoo akaenda zake”.

Ummu Maabad

Msafara ukaendelea  katika hali ya machovu makubwa katikati ya vumbi la jangwani, ukistahamili joto liunguzalo. Kila walipochoka, basi walipiga kambi kupumzika katika vitongoji, vya njiani.

Wakawatafuta wenyeji ili pengine  wanaweza kupata maji au chakula.

Wakaenda katika hali hiyo mpaka wakapita kwa Umuu Ma’abad, mwanamke karimu wa kabila la Khuzaah.

 Alikuwa amekaa mbele ya khema lake, akiipa misafara ipitayo hapo maji na chakula. Walipofika hapo Mtume akamuomba awauzie tende au nyama, lakini hawakuambulia kitu chochote.

Akawajibu huku akionyesha masikitiko yake.

Wallah, lau tungelikuwa na chochote cha kukuandalieni, msingelikuwa na haja ya kuomba au kutoa thamani” Na huo ulikuwa ni mwaka wa ukame.

Amesema Ibn Sa’ad – Allah amrehemu – akipokea riwaya kutoka kwa Abuu Ma’abad (mumewe Ummu Ma’abada)

“Mtume wa Allah – Rehema na Amani zimshukie  akamuangalia mbuzi aliyekuwepo pembeni mwa Khema, akasema (akauliza)  Huyu ni mbuzi gani ewe Ummu Ma’abad?)”

Akajibu:

“Mbuzi huyu ameshindwa kwenda machungani (Malishoni) pamoja na wenziwe kutokana na udhaifu (Mtume) akauliza (tena) “Je, anayo (anatoa) maziwa?” Akajibu: “yeye ni dhaifu mno haiwezi kutoa maziwa “ (Mtume) akasema: “Je, unanipa idhini ya kumkama (Maziwa)?” Akajibu (Ummu Ma’abad):

 “ Naam, ikiwa unaona kuwa anakamika!” Mtume- Rehema na Amani zimshukie – akamuitisha mbuzi yule, akampapasa akaomba:

 “ Ewe Mola wa haki wee! Mbarikie (mama huyu) kwa mbuzi wake huyu! “(Anaendelea kusema Ibn Sa’ad):

 mbuzi yule akaitanua miguu yake na chuchu zake zikajaa maziwa tele. Mtume akaagiza kiletwe chombo kikubwa kiwezacho kuwashibisha watu wote. Akakama maziwa tele ndani yake, akampa mama yule akanywa mpaka akatosheka, kisha akawapa wenziwe mpaka wakatosheka. Halafu yeye Mtume ndie akawa wa mwisho kunywa maziwa na akasema:

Mnyweshaji watu ndie huwa wa mwisho kunywa” Kisha akamkama tena mara ya pili, akamuachia mama yule maziwa yale, hao washika njia na kuondoka.

Haukupita muda mrefu mumewe Abuu Ma’abad akarudi akiwaswaga mbuzi na kondoo wakondefu. Alipoyaona maziwa yale tele alistaajabu na akauliza.

Mmeyapata wapi maziwa haya na il-hali mbuzi hawakuwepo hapa nyumbani? Akajibu (Ummu Ma’abad) Wallah hapana, ila hakika ya hjali ametupitia mtu mwenye baraka, mazungumzo yake yalikuwa hivi na hivi. Akasema: Wallah, mimi namdhania huyo ndie mtu (jamaa) wa Makurayshi wanayemtafuta. Ewe Umuu Ma’abad hebu nisifie hivyo……………………”

Ummu Ma’abad akaanza kumsifia mumewe namna Mtume alivyo, umbile lake, tabia zake, uzungumzaji wake, haiba yake na …………na……………Akasema (Abuu Ma’abad):

“ Wallah, huyo ndiye mtu wa Makurayshi tuliyetajiwa khabari zake! Lau ningemkuta ewe Ummu Ma’abad, ningetaka kufuatana nae, na nikipata upenyo nitamfuata, nitamfuata tu!”

BWANA MTUME ATOKA MAFICHONI NA KUELEKEA MADINA

Makurayshi walipokata tamaa ya kumtia mbaroni Mtume wa Allah na kuamini kwamba tayari atakuwa nje ya mipaka ya himaya yao.

Hapo ndipo Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipoitumia fursa hiyo kutoka pangoni mle, tayari kwa safari ya kuelekea Madinah.

Lilikuwa ni jambo lisiloingia katika dhihni na fikra  za makurayshi kwamba Mtume anaweza  kuwaponyoka bila ya kumkamata.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *