Kabla hatujaanza kuzungumzia mambo yanayotengua tayamamu ni vema tukaziangalia kwanza nukta kadhaa muhimu katika suala zima la kutayamamu. Nukta zenyewe ni hizi zifuatazo:
1 : KUTAYAMMAMU BAADA YA KUINGIA WAKATI WA SWALA
Yeyote ambaye zimepatiakana kukamilika kwake sababu zinazomuhalalishia kutayamamu badala ya kutawadha au kuoga, haimuelei na kumjuzia kutayamamu kwa ajili ya swala ya fardhi ila baada ya kuingia wakati wa swala hiyo.
Ni lazima kutayamamu huko kuwe ndani ya wakati na sio nje yake. Huo ndio utaratibu unaopatikana katika kauli yake Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie :
“Popote pale mtu katika umati wangu itakapomdiriki swala, basi na aswali.” Bukhaariy
” Popote inaponidiriki swala hupangusa (hutayamamu) na kuswali” Ahmad.
Riwaya mbili hizi tulizozitaja zinafahamisha kwamba kutayamamu huwa wakati wa kuidiriki swala, na kuidiriki swala hakupatikani ila baada ya kuingia wakati wake hiyo swala husika. Haya ndiyo mafahamisho na eleweko la hadithi mbili hizi, elewa !
2: KUTAYAMAMU KWA KILA SWALA YA FARDHI:
Kisheria mtu huruhusiwa kuswali kwa tayamamu moja swala moja tu ya fardhi na tayamamu moja swala nyingi awezazo za suna ikiwa ni pamoja na swala ya jeneza (maiti) ijapokuwa swala hii si suna bali ni fardhi ya kutoshelezeana kama tutakavyokuja kuona katika masomo yetu yajayo. Kauli ya jumla tunaweza kusema :
- Tayamamu moja – Fardhi moja
- Tayamamu moja – Suna nyingi
Kwa mantiki hii, mtu akitaka kuswali atayamamu tena hata kama tayamamu yake ya kwanza haijatenguka.
Maelekezo haya yanaihusu swala ya fardhi inayoswaliwa ndani ya wakati ( ADAA) au ile inayoswaliwa nje ya wakati wake (KADHAA).
Haya ndiyo mafundisho ya Bwana Mtume – Rehema na amani zimshukie – yanayopatikana katika riwaya iliyopokelewa na Ibn Umar – Allah awawiye radhi – amesema ( Ibn Umar katika kuelezea tayamamu ya Mtume) “akitayamamu kwa kila swala hata kama hakuhuduthi”. Al-Baihaqiy.
3: KUTAYAMMAMU HUWA NI BADALA YA JOSHO LA FARDHI KAMA KUNAVYOKUWA BADALA YA UDHU.
Mtu anapopatwa na mojawapo ya mambo yanayomuwajibishia josho la kisheria.
Rejea somo la nne kipera/kipengele cha nne na akawa hawezi kutumia maji kwa sababu tulizokwishazielezea katika masomo yaliyotangulia au hakuweza kupata maji mahala alipo, basi tayamamu itamtoshelezea josho hilo.
Tunakusudia kusema kuwa atayamamu badala ya kuoga na kupata ruhusa na uhalali wa kuyafanya yale yote aliyokuwa haruhusiwi kuyafanya kisheria.
Hivyo ndivyo tunavyofahamishwa na tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu :
“……NA MKIWA NA JANABA BASI OGENI NA MKIWA WAGONJWA AU MMO SAFARINI, AU MMOJA WENU AMETOKA CHOONI AU MMEINGILIANA NA WANAWAKE, NA HAMKUPATA MAJI, BASI KUSIDIENI (tayamamuni) UDONGO (mchanga) ULIO SAFI …..” (5:6)
Kadhalika hayo ndiyo maelekezo yanayopatikana kutokana na riwaya iliyoipokelewa na Imraan Ibn Huswayn – Allah awawiye radhi amesema : tulikuwa safarini pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu – rehema na amani zimshukie, (Mtume) akawaswalisha watu (maswahaba). Tahamaki huyo ni mtu amejitenga, Mtume akamuuliza,
“Ni lipi lililokuzia kuswali?. Akajibu : Nimepatwa na janaba na hakuna maji (ya kuoga), (Mtume) akamwambia: “ Tumia mchanga, hakika huo unakutosha” Bukaariy na Muslim.
VITENGUZI VYA TAYAMAMU
Tayamamu hutenguka na kubatilika kwa kupatikana mambo yafuatayo :
1. Mambo yote yanayotenguka na udhu tuliyoyataja katika mlango wa udhu (rejea).
2. Kupata maji baada ya kuyakosa. Hii ni kwa sababu kutayamamu ni badala ya maji, kwa mantiki hii itakapopatikana asili (maji) hubatilika badala (tayamamu).
Haya ndiyo mafundisho ya Uislamu kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Abu Dharri –Allah amuwiye radhi – kwamba Mtume wa mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – amesema :
hakika udongo (mchanga) ulio safi ni tahara ya muislamu hata kama hakupata maji kwa miaka kumi. Atakapoyapata maji basi na ajitwaharishe nayo kwani kufanya hivyo ndio bora” Abuu Daawoud.
Hadithi hii inafahamisha kubatilika kwa tayamamu kwa kupatikana maji
TANBIHI :
1. Mtu akiyapata maji baada ya kumalizika kwa swala (baada ya kuswali), swala yake itakuwa ni sahihi na haimpasii wala kumuwajibikia kuikidhi swala hiyo.
Kadhalika lau atayapata maji baada ya kuanza kuswali, basi na aikamilishe swala nayo itakuwa ni sahihi.
Lakini katika hali hii ni vema zaidi iwapo ataikata swala ili atawadhe na kuswali kwa udhu.
Atafanya hivyo ikiwa muda upo wa kutosha kutawadha na kuswali ndani ya wakati yaani kabla ya kutoka wakati wa swala husika.
2. Uwezo wa kuyatumia maji. Hili ni kwa mtu aliyekuwa mgonjwa na akashindwa kutumia maji katika udhu au josho. Huyu akipona, hana tena ruhusa ya kutayammamu kwa sababu ya kuondoka jambo lililompa uhalali wa kutayamamu ambalo ni ugonjwa.
3. Kuritadi yaani kutoka katika Uislamu – tunamuomba Mola wetu Mtukufu atukinge na