Mushrikina wakaja siku iliyofuatia wakiwa wamewakusanya watu wao na kuvitapanyia vikosi vyao kila upande.
Upande aliokuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakapeleka kikosi kikali ndani yake akiwemo shujaa wao Khalid Ibn Al-Waleed.
Waislamu wakapambana nao na kutoa upinzani mkali, mapambano yakaendelea mpaka usiku mwingi.
Ukali wa mapambano ukamlazimisha Mtume wa Allah na maswahaba wake kutoondoka hata kwa dakika chache sehemu zao za mapambano.
Wala hapana hata mmoja aliyepata mwanya wa kuswali Adhuhuri, Laasiri, Maghribi wala Ishaa. Haki iliendelea hivyo mpaka pale Allah alipowafunua mushrikina na kila kundi likarejea kambini kwake tayari kwa mapambano ya siku ya pili.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipofika kambini kwake akamuamuru Bilali kuadhini na kisha akakimu kwa ajili ya swala ya Adhuhuri.
Baada ya kuswaliwa Adhuhuri kukakimiwa kwa ajili ya swala nyingine zote zilizosalia bila ya kuadhiniwa. Mtume na maswahaba wake wakazikidhi swala zote zilizowafutu katika kitaanani cha vita.
Baniy Quraydhwah wakapanga kuivamia Madinah usiku, khabari hizo zikamfikia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.
Akampeleka Salamah Ibn Aslama pamoja na watu mia mbili na Zayd Ibn Haarithah pamoja na kundi la watu mia tatu kuulinda mji wa Madinah.
Khofu ya kuwachelea Baniy Quraydhwah dhidi ya wanawake na watoto wa Kiislamu Madinah ilipewa nafasi kubwa na Mtume kuliko hao Makurayshi na Ghatwfaani walioko mbele yao.
Mushrikina wakawazingira na kuwatia kati waislamu kiasi cha kuwafanya wachanganyikiwe wasijue la kufanya.
Hali ikawa mbaya sana, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akaanza kumuomba Mola wake akisema:
“Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba kwa ahadi na miadi yako! Ewe Mola wa haki wee! Ukitaka hutoabudiwa. Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba utukinge na shari yao, utunusuru nao na asikushinde asiye wewe”.
Waislamu wakamjia Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kumuuliza: Je, iko dua yo yote tuombe kwani tayari nyoyo zimeshapanda kooni (kutokana na mshindo mkuu wa vita)? Mtume akawajibu:
“Naam, semeni: Ewe Mola wa haki wee! Tunakuomba uzisitiri aibu zetu na uziaminishe khofu zetu”.
Ibn Sa’ad-Allah amrehemu-anasema:
“Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake wakawekwa mzingironi kwa kadiri ya siku kumi na kitu. Mpaka kila mmoja wao akapatwa na msongo wa moyo, Mtume wa Allah akataka kuituliza hali hiyo kwa kufanya suluhu na Ghatwfaani. Aandikiane nao mkataba wa kuwapa theluthi moja ya mavuno ya tende za Madinah ili wajitoe katika majeshi shirika na washike njia kurudi makwao. Answari wakaipinga azma hii ya Mtume kwa kuwa itawadhalilisha na kuwatia unyonge wa milele mbele ya macho ya walimwengu. Mtume wa Allah akakubaliana na shauri lao hilo na kuitupilia mbali azma yake.”
Bishara za faraja:
Mpaka dakika hii Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake-Allah awawiye radhi-walikuwa wameshafanya kila waliwezalo.
Na wamemaliza juhudi zao zote katika kuitetea na kuilinda imani yao na mji wao kiasi cha kutobakisha kitu katika nguvu/uwezo wa kibinadamu.
Hapo ndipo ulipoingilia kati uwezo na nguvu za ki-Mungu ili kuwasaidia waumini hawa walioipigania dini ya Allah haki ya kuipigania. Ghafla mwenendo wa vita ukageuka na kubadili mwelekeo wake kiasi cha kuwashangaza watu namna yake:
“…WALA HAPANA YE YOTE AYAJUAYE MAJESHI YA MOLA WAKO ILA YEYE TU…” [74:31]
II. Khadaa ya Nuaim Ibn Masoud:
Miongoni mwa mambo ambayo Allah alimfanyia Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-na waumini katika vita hivi ni kuwaletea Nuaim Ibn Masoud Al-Ashjaiy akiwa muislamu tayari. Akasema:
“Ewe Mtume wa Allah, hakika mimi nimekwishasilimu na hakuna ye yote katka watu wangu anayejua juu ya huku kusilimu kwangu, basi niamuru ulitakalo”.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia:
“Hakika si vinginevyo, wewe ni mtu mmoja tu katika Ghatwfaani, basi lau ungetoka ukenda kuwakatisha tamaa nasi kama unaweza. Ingelikuwa ni bora zaidi kuliko kubakia pamoja nasi hapa, basi haya toka kwani vita ni khadaa”.
Huyoo Nuaim Ibn Masoud akatoka mpaka kwa Baniy Quraydhwah na alikuwa akinywa pamoja nao katika zama za Jahilia, akawaambia:
“Enyi Baniy Quraydhwah! Kwa yakini mnayajua vema mapenzi yangu kwenu na khususan urafiki ulio baina yangu nanyi”. Wakamjibu:
“Wewe sema tu, kwani wewe kwetu si mwenye kutuhumiwa kwa ubaya”. Hapo ndipo akaanza kuwaambia:
“Hakika Makurayshi na Ghatwfaani si kama nyinyi, huu mji (Madinah) ni mji wenu ambao ndani yake kuna mali, watoto na wake zenu. Na hakika hawa Makurayshi na Ghatwfaani wamekuja tu kumpiga vita Muhammad na watu wake (hawana kitu hapa), nanyi mmekwishachukua uamuzi wa kuwasaidia (katika vita yao hii). Wao wakiiona fursa wataitumia (kufikia malengo yao) na mambo yakiwa kinyume na matarajio yao, haoo watashika njia na kurudi makwao na kukuacheni peke yenu na mtu huyu (Mtume). Nanyi hamna ubavu wa kupambana nae peke yenu, kwa ajili hii mimi ninakushaurini msiingie vitani pamoja na watu hawa mpaka muwachukue rehani watukufu wao”.
Kisha kuwaambia hivyo, huyoo akatoka mguu mosi mguu pili kuwaendea Makurayshi, nao akawaambia:
“Bila shaka enyi kusanyiko la Makurayshi mnayajua vema mapenzi yangu kwenu na kumuacha kwangu Muhammad. Hakika limenifikia jambo ambalo naona ni haki yangu kukufikishieni kama ushauri nasaha kwenu, basi tafadhalini nifichieni siri”. Wakasema:
“Tutakufichia”. Akawaaambia:
“Mnajua, Mayahudi wamekwishajuta kumsaliti kwao Muhammad na wamempelekea ujumbe: Ya kwamba sisi tume shayajutia tuliyoyatenda, basi je yakuridhi wewe sisi tuwachukue watu katika Makurayshi na Ghatwfaani, tuwasalimishe kwako uzikatilie mbali shingo zao. Kisha sisi tusimame nawe mpaka tuwamalize waliosalia?” Halafu akawaendea Ghatwfaani na kuwa ambia maneno hayo hayo.
Ulipofika usiku wa kuamkia Jumamosi na hili lilikuwa katika jumla ya mambo ambayo Allah alimfanyia Mtume wake na waumini.
Abu Sufyaan alimtuma Ikrimah Ibn Abu Jahli kwenda kwa Baniy Quraydhwah akiliongoza kundi katika Makurayshi na Ghatwfaan, awaambie:
“Hakika sisi hatutaendelea kukaa hapa, ngamia na farasi wetu wanaangamia kwa njaa, kwa ajili hii jiandaeni kwa vita kesho asubuhi tummalize Muhammad”.
Baniy Quraydhwah nao wakasema:
“Hakika siku hiyo (Jumamosi) ni siku ya Sabato ambayo sisi hatufanyi kazi yo yote ndani yake nanyi nyote mnayajua vema yaliyowafika walioikhalifu amri hii miongoni mwetu. Pamoja na yote haya sisi hatutapigana upande wenu mpaka mtupe rehani watu wenu wawe mikononi mwetu ili iwe ni uthibitisho kwetu. Kwani sisi tunachelea vita ikikuelemeeni mtashika njia na kurudi makwenu na kutuacha sisi na mtu huyu katika mji wetu nasi hatuna ubavu juu yake”.
Wajumbe waliporejea na majibu hayo ya Baniy Quraydhwah, wakasema:
“Wallah, ametuambia kweli Nuaim Ibn Masoud”.
Wakapeleka tena wajumbe kuwaambia: “Wallah, hatutakupeni rehani aslani, mkitaka tokeni pamoja nasi tukapigane na kama hamkufanya hivyo, basi makubaliano yetu yamevunjika”.
Baniy Quraydhwah wakasema: “Wallah, amesema kweli Nuaim Ibn Masoud!” Kwa mbinu na hila hii ya Ibn Masoud, Allah akawa ameuvunja umoja na nguvu yao na kuwatapanya.