SOMO LA KWANZA – VITA VYA AHZAABU (KHANDAQ).

Mapenzi ya kuangamiza ndiyo yaliyowasukuma Mayahudi  kukusanya makundi (Ahzaabu) ya Waarabu dhidi ya Mtume na maswahaba wake.

Mapenzi ya kuangamiza ndiyo yaliyowasukuma Mayahudi  kukusanya makundi (Ahzaabu) ya Waarabu dhidi ya Mtume na maswahaba wake.

Nafsini mwa Banin-Nadhwiyr suala la kutolewa na kufukuzwa Madinah halikuwa ni jambo jepesi hata kidogo kiasi cha kuachwa lipite hivi hivi tu.

Wala halikuwa ni jambo lenye kukoma athari zake kwa kumalizika kwake. Haikuwa hivyo kwa sababu Madinah ndio palikuwa mahala pao na mahala pa wahenga wao kwa karne kadhaa.

Pamoja na mandhari ya ustahamilivu na furaha waliyoionyesha wakati walipokuwa wakitoka, bado kusahau kwao halikuwa ni jambo rahisi.

Kwani nyoyo zao zilikuwa zikitokota chuki dhidi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na maswahaba wake.

Mbele za macho yao hawa walionekana kuwa ni wavamizi waliowatoa kwa nguvu katika ardhi yao na kuwalazimisha kuyaacha makazi yao, ngome, silaha, mashamba, biashara, mali na mifugo yao.

Na isitoshe wavamizi hawa hawa kuwaruhusu kuchukua katika mali zao hizo ila kiasi kidogo tu kinachoweza kubebwa na ngamia wa kila mmoja wao.

Kwa hali hii fikra zao zote zikawa ni kutaka kujilipia kisasi na kuwaangamizilia mbali maadui na wanyang’anyi hawa. Wawashushie pigo moja la kifo litakalo wasambaratishia mbali kama si kuwafyeka kabisa.

Haya ndio yaliyozijaza nyoyo zao hasadi na chuki kwa Mtume huyu aliyekuja na ulinganio wake katika mji wao.

Ujaji uliowapokonya nafasi, cheo na hadhi ya kidini waliyokuwa wakiishikilia na kuitumia kuwaongoza wazalendo waarabu washirikina wa Madinah na makabila mengine ya Kiarabu katika miji mingine.

 Mlingano huu uliendelea kukua na kuenea kwa kasi huku wafuasi wake wakiongezeka siku hata siku na hivyo kuwafanya kuwa na nguvu kubwa ya kuweza kujihami dhidi ya adui wa wito wa dini yao hiyo.

Ni nguvu hii ndio iliyowawezesha waislamu kuwatoa wao Mayahudi Madinah kikundi kikifuatiwa na kingine na hali ya kuwa wao ni miongoni mwa wazalendo wa mahala hapo waliokuwa na hadhi na sauti.

Ni kwa ajili ya yote haya ndio mayahudi wakaziunganisha nafsi zao na fikra ya kulipa kisasi.

Wakaanza kutafuta fursa ya kummaliza Mtume na maswahaba wake.

Kwa kufanya hivyo, wote kwa pamoja Mayahudi na Waarabu watakuwa wamepumzika na shari ya hii dini mpya.

Na amani, salama na utulivu utakuwa umerejea katika rasi (peninsula) hii kama ilivyokuwa kabla ya kuingia kwa da’awah hii Madinah.

 

Makurayshi waliitilia mashaka nia/dhamira ya Mayahudi, shaka hii ikawasukuma kuwauliza swali hili: Dini yao (Makurayshi) na dini ya Muhammad ni ipi iliyo bora?

Hivi ndivyo walivyofikiri Banin-Nadhwiyr, na wakakongamana juu ya dhamira hii ya kulipa kisasi.

Akatoka Huyay Ibn Akhtwab na Sallaam Ibn A-Haqiyq pamoja na kundi la watukufu wao kwenda kuyakusanya makundi dhidi ya Mtume na waislamu.

Ujumbe huu wa viongozi wa Mayahudi ukafika Makkah kwa Makurayshi na kuwataka waungane nao katika kumpiga Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

Wakawaambia: Sisi tutakuwa pamoja nanyi mpaka tumng’oe na kumfagilia mbali”.

Makurayshi walipoisikia kauli hii ya Mayahudi, wakaingiwa na shaka kuelekea dhamira/nia ya Mayahudi. Shaka yao hii ikawafanya kusita kutoa ushirikiano kwa Mayahudi dhidi ya Muhammad ambaye ni mkurayshi mwenzao.

Pia waliitilia mashaka dini yao na wakataka kupata uhakika na kupima baina yake na dini aliyokuja nayo Muhammad.

Dini inayolingania kumuabudu Allah pekee, dini inayolingania tabia njema na adabu murua. Hivi ndivyo walivyofikiria Makurayshi na kuona vyo vyote ilivyokuwa Mayahudi ndio walioanza uadui na uchokozi.

 Na kwamba Muhammad na maswahaba wake hawakuwa na uchaguzi ila kujilinda nafsi zao, itikadi yao na haki yao ya kuitangaza itikadi yao hii kwa watu.

Na kisha kuwaachia watu uhuru wa ama kuiamini au kuikufuru.

Naam, huenda ni fikra kama hizi ndizo zilizowasukuma Makurayshi kuwaambia wajumbe wa Banin-Nadhwiyr waliowajia:

“Enyi kusanyiko la Mayahudi! Bila shaka nyinyi ndio watu wa kitabu cha mwanzo na mna ujuzi/elimu ya kile tunachokhitilafiana sisi na Muhammad. Basi hebu tuambieni dini yetu ndio bora au dini yake (Muhammad)?”

Kwa kuwa Mayahudi walikuwa wakitafuta kuungwa mkono na Makurayshi katika vita vyao dhidi ya Mtume, hawakukawia ila walijibu:

“Dini yenu ndio bora kuliko dini yake, kwa hivyo basi nyinyi ndio mnaoistahiki haki kuliko yeye”.

Hivi ndivyo mfundo, hasadi na uadui dhidi ya Mtume na da’wah yake ulivyowasukuma Mayahudi kutokuogopa kushuhudia uovu.

Ya kwamba shirki ni bora zaidi kuliko tauhidi na kwamba miungu ya mushirikina ni bora kuliko mungu wa Muhammad; Bwana Mlezi wa viumbe wote.

Na kwamba desturi na mapokeo wanayoyafuata mushrikina ni maongofu zaidi kuliko itikadi na mila anayoilingania Muhammad-Rehema na Amani zimshukie.

Hivi ndivyo walivyojasiri kuukanusha msingi wa dini yao wenyewe ambao ni kumuamini Allah peke yake bila ya kumshirikisha na cho chote. Wakayafanya yote hayo kwa ajili tu kumpiga vita Mtume mwenye kuilingania imani iliyo sawa kabisa na yao na mwenye kuikemea shirki, madhambi na machafu. Hapo ndipo Allah Taala akaishusha kauli yake tukufu:

 “HUWAONI WALE WALIOPEWA SEHEMU YA (kufahamu) KITABU (cha Allah)? WANAAMINI MASANAMU NA UPOTOFU NA HUSEMA JUU YA WALE WALIOKUFURU KUWA WAO WAMEONGOKA ZAIDI KATIKA NJIA (ya haki) KULIKO WALE WALIO AMINI. HAO NDIO ALLAH ALIOWALANI NA AMBAYE ALLAH AMEMLANI BASI HUTAMUONA KUWA NA MWENYE KUMNUSURU”. [4:51-52]

Kauli hiyo ya Mayahudi iliwafurahisha mno Makurayshi na kuwafanya waichangamkie na kuipokea propaganda ya kumpiga vita Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Kwa hivyo wakaanza kujiandaa na suala hili.

 

Mayahudi walikusanya makundi ya mushrikina mpaka ikafikia idadi yao watu alfu kumi:

Baada ya kupata waliloliendea kwa Makurayshi, huoo ujumbe wa Makurayshi ukaondoka kuipeleka propaganda yao kwa Ghatwfaani.

Huko nako wakatoa wito wa kumpiga vita Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na kuwafahamisha kwamba Makurayshi wamesha kubali kushirikiana nao katika azma yao hii.

Wakainogesha propaganda yao hii chafu kwa kuwaahidi Ghatwfaani donge nono la kupata mavuno ya tende za Khaybar kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Donge hili watalipata mara tu baada ya kumshinda Muhammad, kwa tamaa ya donge nono hili koo zote za Ghatwfaani zikawaitika Mayahudi katika ombi lao hilo.

Hivi ndivyo Mayahudi walivyopata washirika wa kuwasaidia katika dhamira yao hii, makundi kwa makundi na kuyachochea makabila dhidi ya Mtume.

Wakawakusanya wale wote wenye kisasi kwa Mtume wa Allah katika makabila ya Kurayshi, Ghatwfaani, Asadi, Suleim na washirika wao katika makabila ya Waarabu.

Idadi yao ikafikia kiasi cha watu alfu kumi, jeshi hili kubwa likaondoka kuelekea Madinah kwa kishindo kikubwa chini ya ukamanda wa Abu Sufyaani Ibn Harbi. Hiyo ilikuwa ni katika mwezi wa Shawwal mwaka wa tano (5) Hijiria (Februari 627 A.D.).

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *