Mtume Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – alipofikia umri wa ukamilifu, umri ambao akili ya mwanadamu huwa imepevuka na kukomaa, umri wa miaka arobaini.
Huu ukawa ndio wakati muafaka wa kupewa kazi nzito, ngumu na yenye kuhitaji subira ya kutosha.
Kazi ya kuinusuru jamii yake na kiza totoro cha ushirikina. Hapo ndipo Mwenyezi Mungu Mtukufu akamkabidhi dhamana ya utume, awabashirie watu wema kupata pepo ya milele kwa kumfuata na awakhofishe na adhabu kali ya moto wa milele wale wote watakaomkadhibisha na kuacha kumfuata.
Awalinganie watu kuwatoa katika viza vya ushirikina kuwapelekea katika nuru ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu asiye na mshirika.
Katika usiku wa mwezi kumi na saba (17) Ramadhan mwaka wa kumi na tatu kabla ya hijra sawa na Mwezi Julai mwaka mia sita na kumi na moja (611) Miladia Mtume akiabudu faraghani ndani ya pango la Hiraa hapo ndipo ulipomshukia wahyi/ufunuo kwa mara ya kwanza.
Jibriil –Amani imshukie – malaika mwaminifu wa wahyi alimtokezea na kumwambia
“Soma” Mtume akamjibu
“Mimi si mwenye kusoma” Jibril akamshika Mtume na kumgandamizia kifuani kwake kama vile anamkaba, kisha akamuachia na kumwambia tena
“Soma” Mtume akamjibu kama alivomjibu mwanzo
“Mimi si mwenye kusoma” Jibril akamkamata tena na kumgandamiza na kumwambia
“Soma” hii ikiwa ni mara ya tatu, Mtume akauliza
“Nisome nini ?” Hapo sasa Jibril ndipo akamwambia :
SOMA KWA JINA LA MOLA WAKO ALIYEUMBA, AMEUMBA MWANADAMU KWA PANDE LA DAMU. SOMA NA MOLA WAKO NI KARIMU SANA. AMBAYE AMEMFUNDISHA (Binadamu elimu zote hizi) KWA WASITA (msaada) WA KALAMU (zilizoandika vitabu, watu wakapata elimu) AMEMFUNDISHA MWANADAMU (chungu ya) MAMBO ALIYOKUWA HAYAJUI” [96:1-5]
Kisha Jibriil akashika njia akaenda zake, naye Mtume kwa wepesi akarejea kwa mkewe Bi Khadija akiwa amejawa na khofu kubwa kutokana na kiumbe mgeni, malaika kwa mara ya kwanza.
Akasema “Nifunikeni ! Nifunikeni!” Mkewe akamfunika maguo kutokana na alivyokuwa akitetemeka kama mtu mwenye homa kali kabisa.
Alipotulizana ndipo akamuuliza kulikoni, mbona yuko katika hali hiyo? Mtume akamuhadithia mkewe hali ilivyokuwa mwanzo hadi mwisho na kusema
“Ninaichelea nafsi yangu na shetani/pepo mbaya” mkewe akamtuliza na kumwambia
“Sivyo hivyo ! Wallah Mwenyezi Mungu kamwe hatokufedhehesha. Kwani unaunga udugu, unasema kweli, unasaidia mnyoge, unamkirimu mgeni, unawapa sadaka masikini na unasaidia katika majanga”
Halafu ndipo Bi Khadijah alipoamua kumpeleka Mtume kwa mwana wa ammi yake Waraqah ibn Naufal, huyu alikuwa ni mwanachuoni mwenye elimu ya vitabu vitakatifu kabla ya Qur-ani {Taurati, Zaburi na Injili}.
Bi Khadijah akamuhadithia binamu yake yote yaliyomtokea Mtume kama alivomueleza mwenyewe. Waraqah kutokana na elimu aliyokuwa nayo akamtoa wasiwasi Mtume na kumwambia
“Huyu ndiye Naamus {Jibril} aliyekuwa akimshukia Issa bin Maryam, basi furahi kwani wewe ndiye Mtume wa umati huu”
Baada ya hapo wahyi ulikatika kwa kipindi kirefu, kukawa hakuna mawasiliano yoyote baina ya mbinguni na ardhini.
Kukatika huku kwa wahyi hakukuja kwa bahati mbaya tu, bali hekima yake ilikuwa ni kuizidisha shauku na kiu ya Mtume kwa wahyi.
Mtume akapatwa na huzuni kuu na akawa akienda na kurudi pangoni Hiraa, huenda pengine Jibril atamjia tena, lakini wapi hakumuona.
Hali ilikuwa hivyo mpaka Mtume akadhania kuwa Mola wake amemkasirikia na kumtupa. Baada ya kipindi hicho kigumu ndipo Wahyi ulipoanza kushuka tena na Mola wake akamtuliza kwa kumwambia :
“HAKUKUACHA MOLA WAKO WALA HAKUKASIRIKA (nawe Ewe Nabii Muhammad) NA BILA SHAKA (kila) WAKATI UJAO (utakuwa) NI BORA KWAKO KULIKO WAKATI ULIOTAGULIA” [93:3-4]
Kisha tena ikamshukia kauli yake Mola :
“EWE ULIYEJIFUNIKA MAGUO. SIMAMA UONYE (viumbe) [74:1-2].
Huu ndio ukawa ndio mwanzo wa kazi na safari ndefu yenye taabu na misukosuko mikubwa ya kufikisha ujumbe wa Mola wake Mtukufu kwa watu wote.