ABU SUFYAAN AHIMIZA MAKURAISHI KUENDA KUIHAMI MALI YAO

Khabari za Mtume kuuvizia msafara wa Makurayshi utokao Shamu kurejea Makkah kupitia Madinah zilivuja na kumfikia Abuu Sufyaan; kiongozi wa msafara ule.

Bila kuchelewa Abuu Sufyaan akamtuma mjumbe kwenda mjini Makkah kuwapasha Makurayshi khabari ile na kuwaelezea juu ya uwezekano wa kupoteza mali yao, ikiwa hawatachukua hatua za tahadhari kwa haraka.

Akamuagiza mjumbe wake kutumia kila njia iwezekanayo kuhakikisha kuwa anawahamasisha watu kutoka kuja kuuhami msafara dhidi ya Mtume na maswahaba wake.

Mjumbe huyu aliutambua umuhimu wa dhima aliyoibeba, akaandaa mazingira yatakayomsaidia kufikisha haraka ujumbe wa Abuu Sufyaan kwa watu wa Makkah.

Alipokaribia kufika mjini Makkah akamkata sikio ngamia wake, akaitupa sogi yake na kuichana kanzu yake na akaanza kupaaza sauti jangwani, akisema:

“Enyi kusanyiko la Makurayshi, msafara msafara! Mali zenu pamoja na Abuu Sufyaan, Muhammad amezitokea na maswahaba wake, sidhani kama mtaudiriki (kabla Muhammad hajautia mkononi)! Msaada msaada!”

Naam, kutokana na mazingira haya yaliyoandaliwa barabara, haraka Makurayshi wakakiitikia kilio kile cha msaada, mori ukawapanda wakasema:

Hivi huyu Muhammad na maswahaba wake wanadhania msafara huu ni kama ule wa Ibn Al-Hadhwramiy (waliouteka)?

Sivyo hivyo, Wallah atatutambua, tena atatambua kwamba sivyo hivyo! Makurayshi wakatoka haraka tayari kuuhami msafara wao kwa gharama yo yote ile iwayo.

Mwenye uwezo akamsaidia asiye na uwezo ili naye atoke na ambaye hakuweza kutoka mwenyewe basi alimtafuta mtu wa kutoka badala yake.

Wanazuoni wa sira na tarekh wanasema: Kwamba Umayyah Ibn Khalaf alitaka kubakia nyuma, asitoke. Uqbah Ibn Abiy Muaitw akamuendea akiwa na chetezo na bukhuri (ubani/uvumba/udi). Akaviweka mbele yake naye akiwa amekaa katika baraza ya jamaa zake (Makurayshi wenziwe), akamwambia:

Jifukize ewe Abuu Aliy, kwani hakika si vinginevyo wewe ni katika wanawake (wasioweza kutoka)”.

 Umayyah akahisi soni na kuona haya, pale pale akainuka ili kuwaonyesha kwamba yeye sio mwanamke. Akaenda kujiandaa na akatoka pamoja na watu wengine kwenda kuuhami msafara wao.

 

ABUU SUFYAAN ATOROKA NA MSAFARA:

Abuu Sufyaan akauongoza msafara ule huku akipeleleza khabari za Mtume na maswahaba wake njiani. Akaenda mpaka alipokaribia Badri akauacha nyuma msafara kwa tahadhari.

Akaenda mbele peke yake mpaka akafika sehemu ya maji pale Badri.

Hapo akawauliza watu khabari za waislamu, akafahamu kutokana na maelezo aliyoyapata kwamba kuna wapanda ngamia wawili walipiga kambi huko kilimani.

Walipita pale kuchota na kunywa maji kwa muda, kisha wakashika njia na kuondoka zao.

Abuu Sufyaan akaenda mpaka katika kile kilima alichoelezwa, akachunguza pale walipokita ngamia wawili wale.

Akachukua kinyesi chao akakisukasuka mkononi mwake, akagundua kina athari ya tende. Akatambua kwamba wapanda ngamia wawili hao aliolezwa wanatokea Madinah.

Akasema: “Wallah! Hiki ni chakula cha wanyama wa Yathrib (Madinah) na hapana shaka hawa ni majasusi wa Muhammad wamekuja kupeleleza khabari zetu”.

Akarejea haraka pale alipouacha msafara na kuuelekeza kubadili muelekeo wa Badri na badala yake uelekee mwambao wa bahari ukiiacha Badri kushotoni kwake.

Kwa hila na mbinu hii Abuu Sufyaan akaweza kuutorosha msafara na hivyo kuziokoa mali za Makurayshi zisiingie mikononi mwa Mtume.

 

BONDE LA BADRI.

Hebu turejee nyuma kidogo ili tuweze kulijua vema eneo au mahala hapa panapoitwa “Badri”.

 Badri hili ni bonde ambalo lilikuwa ni mahala pa msimu wa biashara wa makabila mbali mbali ya Kiarabu kila mwaka.

Hukutanika hapo na kufanya gulio kubwa sana, ambapo bidhaa za kila aina zilipatikana. Badri hali kadhalika lilikuwa ni eneo mashuhuri lenye maji katika njia ya Makkah-Madinah.

Pia Badri ndio ilikuwa stesheni ya kupumzikia misafara ielekeayo Shamu kutokea sehemu mbali mbali.

Kutoka hapo Badri mpaka Madinah kuna umbali wa kiasi cha kilometa zipatazo mia moja na sitini.

Mahala hapa ni eneo tambarare la mchanga lenye vilima vyenye mteremko mkali upandae wa Kaskazini na Mashariki.

Upande wa Magharibi kuna eneo lenye mafungu ya mchanga na upande wa kusini kuna miamba yenye mteremko usio mkali.

Vimeenea vijito vya maji vinavyolikata bonde hili kutokea upande wa mashariki kuelekea magharibi.

 Vijito hivi hujikata na kuwa vijito vidogo vidogo vilivyoenea huku na huko na kuwa mithili ya visima vingi.

Wasafiri wapitao hapo huvijengea kuta visima hivi na kuvifanya kuwa mithili ya mahodhi (basin) makubwa ya kuhifadhia maji.

Mpaka hapa tunataraji maelezo haya yatakuwa yamekupa taswira ya Badri kiasi cha kuelewa tunapoitaja Badri tunaongelea mahala pa namna gani.

 

MTUME ATAMBUA KUTOKA KWA MAKURAYSHI NA ANAWATAKA USHAURI MASWAHABA WAKE WAFANYE NINI ILI KUKABILIANA NA HALI HIYO.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alisonga mbele na maswahaba wake mpaka wakafika katika bonde liitwalo “Dhafiraan”.

Hapo ndipo zilipomfikia khabari kwamba Makurayshi wametoka wote kwa ujumla wao kuja kuuhami msafara wao.

Pia wakamjia wale wajumbe wake wawili aliowatuma kule “Buyuut-Suq-yaa”, wakamueleza khabari za upelelezi wao kuhusiana na msafara ule wa Makurayshi.

Baada ya kupokea taarifa zote mbili; taarifa ya kutoka kwa Makurayshi na ile ya upelelezi. Bwana Mtume aliwakusanya maswahaba wake na kuwapasha khabari zile na kuwataka ushauri wafanye nini katika kukabiliana na kundi hilo kubwa la Makurayshi linalowajia.

Likawepo kundi miongoni mwao ambalo halikupenda kukabiliana na Makurayshi kivita bila ya kuwa na maandalizi ya kutosha ya vita.

Wakasema wao wametoka kwa ajili ya kuteka msafara na wala sio vita, wakamwambia Bwana Mtume: “Kwa nini hukutuambia kuwa tunakuja vitani ili tupate kujiandaa!”

Mtume wa Allah hakuufurahia uoga huu wa maswahaba wake katika kukabiliana na Makurayshi, akafikiria matokeo ya hali ile, akawakariria kauli yake:

 “Mnalionaje suala la kupigana na watu hawa (Makurayshi)?” Wakamjibu:

“Wallah, hatuna uwezo (nguvu) wa kupigana na adui, sisi tuliukusudia msafara”. Kusikia jawabu hilo, pale pale uso wa Mtume ukabadilika na ikadhihiri ghadhabu yake usoni mwake.

 Hapo ndipo maswahaba wakadiriki khatari inayowakabili ikiwa watayakhalifu matashi ya Mtume wa Allah.

Likasimama kundi moingoni mwao na kutoa wito wa vita, Abuu Bakri akainuka na kusema maneno ya kuhamasisha.

Umar naye akasimama na kuamsha ari na mori wa maswahaba, kisha akasimama Miqdaad Ibn Amri akasema:

“Ewe Mtume wa Allah, tekeleza alilokuamrisha Allah na sisi tuko pamoja nawe. Wallah, hatusemi kukuambia wewe kama Baniy Israili walivyomwambia (Mtume wao) Musa : “…NENDA WEWE NA MOLA WAKO MKAPIGANE, SISI TUTAKAA HAPA (kungojea nini litakalokuwa)…”

 Lakini sisi (tunasema) nenda wewe na Mola wako mkapigane na sisi ni wenye kupigana pamoja nanyi.

Tunaapa kwa yule aliyekutumiliza kwa haki lau ungeenda nasi mpaka Barkil-Ghimaad (hii kwa wakati huo ndio ilionekana kuwa sehemu ya mbali kabisa, inasemekana ilikuwa pande za Yemen), tungelivaa panga zetu pamoja nawe mpaka tufike huko”.

Bwana Mtume akamwambia Miqdaad umenena vema na akamuombea dua njema.

Kisha Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: “Nipeni ushauri enyi watu”, akiwalenga Maanswari, kwani wao ndio waliokuwa wengi.

Na ikumbukwe kwamba tayari walikuwa wamempa huko nyuma kabla ya kuhamia Madinah ahadi ya kumlinda ndani ya miji yao.

Ama nje ya miji yao ahadi hiyo hawakuitoa, kwa hivyo suala hili linabakia kuwa katika khiari yao. Mtume alipokwisha kusema hivyo, akasimama Sa’ad Ibn Muaadh na kusema: “Huenda unatukusudia sisi ewe Mtume wa Allah?” Mtume akajibu: “Ndio khasa”. Sa’ad akasema:

“Bila ya shaka wewe umelitokea jambo fulani na Allah akakuondoshea jambo jingine. Basi litazame hilo alilokuondoshea wewe Allah na ulitekeleze hilo.

Hakika sisi tumekuamini na kukusadiki wewe na tumeshuhudia kwamba uliyokuja nayo ni haki (kweli).

 Na tumekupa ahadi zetu za usikivu na utii, labda ewe Mtume wa Allah unachelea kuwa Maanswari wanaona kuwa hizo ni ahadi za kukunusuru ndani ya miji yao tu (na sio nje yake). Mimi ndiye ninayewasemea na kuwajibia Maanswari:

Nenda ewe Mtume wa Allah ukutakapo, iunge kamba ya umtakaye na ikate ya umtakaye, msalimishe umtakaye na mpige vita umtakaye.

 Twaa katika mali zetu ukitakacho na utakachokichukua katika mali zetu chapendeza mno kwetu kuliko utakachokiacha. Amri yo yote utakayoitoa sisi tutaamrika, endelea ewe Mtume wa Allah na ulilolikusudia, sisi tu pamoja nawe.

Tunaapa kwa yule aliyekutumiliza kwa haki, lau ungelituonyesha bahari hii na ukaiingia, basi nasi tungeliingia pamoja nawe na wala hasingebakia nyuma ye yote miongoni mwetu.

 Hatuchukii wewe kutukutanisha na adui yetu kesho, sisi ni wastahamilivu wa vita, wakweli wakati wa mapambano.

Huenda Allah akakuonyesha kwetu yale yatakayoyaburudisha macho (moyo) yako, songa mbele kwa baraka za Allah”.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafurahi na kifua chake kikakunjuka kwa kusikia maneno hayo yenye ukweli na utii ndani yake. Akasema:

“Enendeni kwa baraka za Allah na ikupateni bishara njema. Hakika Allah ameniahidi mojawapo ya mataifa (mapote) mawili, wallah kama kwamba mimi ninayaona maanguko ya watu hao”.

 

 Lirejee tukio hili katika Qur-ani ukitaka:

“(Atakunusuruni) KAMA ALIVYOKUTOA MOLA WAKO KATIKA NYUMBA YAKO KWA HAKI, NA KUNDI MOJA LA WALIOAMINI HALIPENDI (utoke). WAKABISHANA NAWE KATIKA ( lile jambo la) HAKI BAADA YA KUBAINIKA (haki ile wanachukia kwenda huko vitani) KAMA KWAMBA WANASUKUMWA KATIKA MAUTI NA HUKU WANAONA. NA (kumbukeni) ALLAH ALIPOKUAHIDINI MOJA KATIKA MATAIFA MAWILI YA KWAMBA NI LENU. NANYI MKAPENDA MPATE LILE LISILO NA NGUVU, NA ALLAH ANAPENDA KUTHUBUTISHA HAKI KWA MANENO YAKE NA (anapenda) KUIKATA MIZIZI YA MAKAFIRI. ILI KUTHUBUTISHA HAKI NA KUIONDOA BATILI, HATA WAKICHUKIA WATU WABAYA” [8:5-8]

 

ABU SUFYAAN AHIMIZA MAKURAISHI KUENDA KUIHAMI MALI YAO

Khabari za Mtume kuuvizia msafara wa Makurayshi utokao Shamu kurejea Makkah kupitia Madinah zilivuja na kumfikia Abuu Sufyaan; kiongozi wa msafara ule.

Bila kuchelewa Abuu Sufyaan akamtuma mjumbe kwenda mjini Makkah kuwapasha Makurayshi khabari ile na kuwaelezea juu ya uwezekano wa kupoteza mali yao, ikiwa hawatachukua hatua za tahadhari kwa haraka.

Akamuagiza mjumbe wake kutumia kila njia iwezekanayo kuhakikisha kuwa anawahamasisha watu kutoka kuja kuuhami msafara dhidi ya Mtume na maswahaba wake.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *