Muislamu hukiangalia chakula na kinywaji kwa jicho la kukizingatia kuwa ni wasila/chombo cha kumfikishia katika malengo ya maisha yake ya siku hata siku.
Muislamu hakitazami chakula/kinywaji kwa dhati yake kama ndio upeo wa makusudio na malengo yake.
Kwa hiyo basi, Muislamu haishi ili ale na kunywa bali anakula na kunywa ili aishi. Anakula na kunywa kwa ajili ya kuhifadhi usalama wa afya ya mwili wake, kwani ni kupitia mwili huu ndio huweza kumuabudu Mola wake. I
bada hii ndio humfanya astahiki kupata utukufu, mafanikio na neema za maisha ya milele ya akhera.
Muislamu hali au kunywa kwa dhamira ya kula na kunywa tu, au kwa matamanio, bali hali ila kwa kusikia njaa na kadhalika hanywi ila kwa kiu.
Na hii ni kanuni muhimu ya afya aliyotuwekea Bwana Mtume – Rehma na Amani zimshukie – aliposema :
“ Sisi ni watu hatuli mpaka tusikie njaa na tukila basi hatushibi (kupita kiasi)”.
Lau watu wa leo tungejilazimisha kuifuata kanuni hii, basi tungeliepukana na maradhi mengi. Kwani asilimia kubwa ya maradhi yanayomsibu huanzia tumboni, kutokana na kula na kunywa ovyo ovyo.
Kwa hivyo basi, muislamu anapaswa kujilazimisha kufuata taratibu za kisheria katika kula na kunywa kwake. Taratibu/adabu hizi tutazigawa katika mafungu/sehemu tatu zifuatazo :
a) ADABU/TARATIBU ZA KUFUATWA KABLA YA KUANZA KULA :
1. Kwanza kabisa Muislamu ahakikishe anaandaa na kukipata chakula chake kwa njia za halali, kwa kuitekeleza kauli ya Mola Mtukufu
“ENYI MLIOAMINI ! KULENI VIZURI TULIVYOKURUZUKUNI …” [2:172]
Muradi na mapendeleo ya chakula kizuri ni chakula cha halali na sio uzuri wa ladha.
Kwani ladha hutofautiana baina ya mtu na mtu.
2. Anuie kwa kula na kunywa kwake kupata afya na nguvu ya kumuabudu Mola wake ili apewe thawabu kwa atachokila au kukinywa cha nia hiyo. Kwani jambo la MUBAAH hugeuka kwa nia njema kuwa TWAA ambayo Muislamu hulipwa thawabu kwa kulitenda.
3. Aoshe mikono yake kabla ya na baada ya kula.
4. Akiweke chakula chake kwenye sahani/sinia chini na sio mezani, ka kuwa hili la kulia chini hupelekea zaidi unyenyekevu. Na haya ni kwa mujibu wa kauli ya swahaba Anas bin Malik –Allah amuwie Radhi – Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – hakupata kula juu ya meza.
ZINDUKA: Si haramu kula chakula juu ya meza, bali SUNA ni kula chini ukiwa umeketi mkekani/jamvini au katika busati na vitu kama hivyo.
5. Akae kwa unyenyekevu wakati wa kula. Akalie matumbo ya nyayo zake, mguu wa kulia aunyooshe wima na nyayo yake juu ya ardhi, na aukalie ule wa kushoto kama alivyokuwa akikaa Bwana Mtume. {kielelezo}Bwana Mtume anatueleza namna ya ukaaji wake wakati wa kula, anasema : “Sili hali ya kuchegemea (kitu), hakika si vinginevyo mimi ni mja (Mtumwa wa Allah) ninakula kama alavyo mja na ninakaa kama akaavyo mja” Abu Dawuud na Tirmidhiy.
6. Aridhie na kutosheka na chakula kilichopo na wala asikitie kasoro/aibu. Kikimpendeza akile na kama hakikumridhia basi na akiache bila ya kutoa maneno yasiyo mazuri. Haya ni kwa mujibu wa hadithi iliyopokelewa na Abuu Hurayrah – Allah amuwie radhi – : “Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – kamwe hakupata kukitia aibu/kasoro chakula akipendezewa hukila na kisipompendeza basi hukiacha” Abu Dawuud na Tirmidhiy.
7. Asile peke yake bali ale pamoja na wenziwe; mgeni, mkewe, wanawe, au hata mtumishi wake. Hii haimaanishi kwamba kula peke yake ni haramu, la hasha bali ni vyema kula pamoja na wengine. Hili linatokana na kauli ya Nabii Muhammad –Rehema na Amani zimshukie – aliposema : “Kusanyikeni pamoja katika chakula chenu mtabarikiwa ndani yake” Bukhariy na Muslim. Kwa hivyo utaona chakula cha pamoja hubarikiwa, kinyume na chakula cha mtu mmoja peke yake.
b) ADABU/TARATIBU ZA KUFUATWA WAKATI WA KULA :
1.Muislamu anatakiwa aanze kula kwa kupiga BISMILLAH kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Atakapoanza kula mmoja wenu basi na alitaje jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu, akisahau kulitaja jina la Mwenyezi Mungu Mtukufu mwanzoni mwake (huko kula) basi aseme (pale atakapokumbuka) BISMILLAHI FIY AWWALIHI WA AKHARIHI (Kwa jina la Mwenyezi Mungu mwanzoni na mwisjoni)” Bukhariy na Muslim.
2.Amalizapo kula amshukuru Mwenyezi Mungu aliyemruzuku. Kufanya hivyo ni kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – aliposema :
“Atakayekula chakula na kusema {kiarabu}: (ALHAMDU LILLAHIL-LADHIY ATW-‘AMANIY HADHA WARAZAQANIYHI MIN GHAYRI HAWLIN MINNIY WALAA QUWWAH)
Maana yake :
(Ninamshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenilisha (chakula) hiki na akaniruzuku bila ya uwezo wala nguvu zangu).
3. Amege tonge dogo na alitafune vema kabla ya kulimeza. Ale sehemu inayomuelekea ya sahani. Huu ni utekelezaji wa maneno ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipomwambia (swahaba wake) Umar bin Salamah :
“Ewe kijana, mtaje Mwenyezi Mungu (uanzapo kula) na kula kwa mkono wa kulia na kula katika sehemu (upande) ikuelekeayo” Al-Bukhariy
4. Arambe sahani na vidole vyake baada ya kula, kabla hajavipangusa kwa leso au kunawa. Haya ni kwa mujibu wa kauli ya Mtume – Rehema na Amani zimshukie – :
“Atakapokula chakula mmoja wenu, asivipanguse vidole vyake mpaka avirambe” Abuu Dawuud na Tirmidhiy.
5. Kikimdondoka chochote katika akilacho, akiokote na kukipangusa kisha akile. Huu ni mwongozo wa Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alipotuambia :
“Litakapodondoka tonge la mmoja wenu, basi aliokote, alipanguse na kulila na asimuachie shetani” Muslim.
Kwa hivyo ni vema kabla ya kula kitandikwe kitambaa kikubwa kisafi au chochote kinachofanana na kitambaa, ili chakula kitakapodondoka kidondokee hapo.
6. Asikipulize chakula cha moto na wala asikile mpaka kipoe. Kadhalika asipulizie ndani ya maji wakati wa kunywa bali apulizie nje ya chombo.
Muongozo huu tunaupata kutokana na hadithi iliypokewa na Anas bin Malik –Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – “alikuwa akipumua mara tatu katika kunywa” Bukhariy na Muslim. Maana yake anakunywa funda anapumua, kisha anakunywa tena na kupumua kisha anamalizia kunywa na kupumua. Na hadithi iliyopokelewa na Abuu Sai’d – Allah amuwie Radhi – kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani zimshukie – amekataza kupulizia wakati wa kunywa. Tirmidhiy.
7. Asile zaidi ya uwezo wake, yaani ajiepushe na kushiba sana. Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuasa :
“ …… NA KULENI (vizuri) NA KUNYWENI (vizuri) LAKINI MSIPITE KIASI, HAKIKA YEYE (Allah) HAWAPENDI WAPITAO KIASI (wapindukiayo mipaka)” [7:31]
Pia kujiepusha kula sana ni kuifanyia kazi kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie “Hajapatapo mwanadamu kujaza chombo kilicho na shari kuliko tumbo lake, vyamtosha mwanadamu vijitonge vitavyousimamisha uti wake wa mgongo. Kama hakufanya hivyo (ikiwa hapana budi kula) basi theluthi moja iwe ni ya chakula na theluthi (ya pili) iwe ni ya maji na theluthi (ya mwisho) iwe ni ya pumzi” Ahmad, Ibn Majah na Hakim.
8. Asiwatazame machoni wenzake wakati wa kula ili wasione haya, wakashindwa kula. Bali inatakiwa ayainamishe macho yake kwenye chakula.
9. Asifanye jambo lolote litakalowachefua wenzake wakati wa kula. Asiukung’utie mkono wake katika sahani, asikiinamie chakula kisije kikadondoka kitu kutoka mdomoni mwake na kuangukia sahanini.
Akiung’ata mkate kwa meno yake, basi asikichovye kipande kilichosalia katika bakuli la mchuzi. Kadhalika anatakiwa asizungumze na kuvitaja vitu vichafu vichafu vitakavyochefua wenzake wakati wa kula kama vile mavi na mfano wake.
c) ADABU/TARATIBU ZA KUFUATWA BAADA YA KULA :
1. Aurambe mkono wake, kisha aupanguse kwa kitambaa au anawe.
2. Akiokote chakula kilichodondoka wakati wa kula, kwani kufanya hivyo ni katika kushukuru neema ya Mwenyezi Mungu, mtoa riziki.
3. Ayachokoe meno yake, kisha asukutue ili kukiweka safi kinywa chake ambacho kwacho humdhukuru Mola wake na huzungumza na wenzake. Pia usafi wa kinywa ni kwa manufaa ya meno ili yaendelee kuwa salama na imara.
4. Amshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu baada ya kula au kunywa kwa kuitekeleza kauli ya Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Pigeni BISMILLAH mnapotaka kula na mumshukuru mnapomaliza” . Na amesema Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
“Atakapomaliza kula mmoja wenu aseme : {kiarabu}
(ALLAHUMMA BAARIK LANAA FIYHI, WAZIDNAA KHAYRAN MINHU) (Ewe Mola wa haki tubarikie katika chakula hiki, na utuzidishie kilicho kheri/bora kuliko hiki)
Na akinywa maziwa aseme :
(ALLAHUMMA BAARIK LANA FIYHI WAZIDNAA MINU) (Ewe Mola wa haki, tubarikie katika maziwa haya na utuzidishie)
Kwani hakitoshelezi katika chakula na kinywaji ila maziwa” Ahmad, Abuu Dawuud, Ibn Majah, Tirmidhiy na Al-Bayhaqi kutoka kwa Ibn Abbas – Mola awawie Radhi-.
Yaani Maziwa ndio CHAKULA KAMILI kinachoweza kuchukua nafasi ya chakula na maji.
5. Muislamu anatakiwa asile njiani huku anatembea wala asile sokoni.
Hii inatokana na kauli ya Nabii Muhammad – Rehema na Amani zimshukie – “Kula sokoni ni uduni”