MAZINGATIO (ITIBARI) KUTOKA VITA VYA UHUD

1.      KUSHINDWA KATIKA VITA VYA UHUD KULIKUWA NI DARASA (FUNDISHO/SOMO) MUHIMU KWA WAISLAMU WOTE KWA UJUMLA WAO.

Mtu atakayetafakari kwa kina hali ya mambo ilivyokuwa katika vita vya Uhud, na akayachunguza kwa makini matukio na picha za mambo zilivyokuwa.

Bila ya shaka ataamini kwamba vita hivi na matokeo yake vilikuwa ni jambo ambalo hapana budi kutokea kwake.

Isitoshe vita hivi vilikuwa ni somo/fundisho ambalo ni lazima waislamu walipate katika kipindi hiki cha uchanga wa Uislamu kwa ajili ya ustawi wake katika siku za usoni.

 Kushindwa katika vita vya Uhud ndio lilikuwa pigo zito la kwanza lililowapata waislamu wengi ambao Allah aliwanusuru katika vita vya Badri na ilhali walikuwa ni wachache ukiwalinganisha na hasimu wao.

Baada ya nusra hii ya Allah katika vita vya Badri, ilijengeka dhana katika nafsi za waislamu kwamba ushindi katika vita vyo vyote ni suala la kimaumbile tu ambalo huja lenyewe.

Ni suala lisilo na uhusiano hata kidogo na hali na mazingira halisi. Ni suala lisilotegemea mwenendo na sababu halisi za ushindi, halisuhubiani wala kuambatana na kuyashinda matamanio na tamaa za nafsi.

Ni suala lisilohitaji kuthibiti na kuwa imara mbele ya shida na hali ngumu na kuelekea na kujitupa mikononi mwa Allah Mshindi Mtoa ushindi.

Hii ndio dhana iliyokuwa imekita mizizi ndani ya nyoyo za waislamu, dhana iliyokurubia kuwa imani. Ndipo Allah Mola Mtukufu akataka kuwafundisha waja wake kwamba haupati ushindi ila yule mwenye kujitwalia sababu na akaandaa mazingira ya ushindi.

Bila ya kusahau kwamba hashindwi ila yule mwenye kuandaa mazingira na mwanya wa kushindwa. Pia akataka waja wake wafahamu kwamba kamwe Allah hatawatupa waja wake waumini maadam wanamtakasia yeye tu nia na amali zao.

Likiwashughulisha naye jambo miongoni mwa vitu vya kilimwengu hata wakamsahau, nae atawaacha kwa kadri ya kushughulika kwao na hilo lililowashughulisha nae.

 Wala hatakuwa pamoja nao mpaka wao wawe pamoja nae kwa nyoyo, hisia (fikra), dhahiri na batini yao.

 

2.      WAISLAMU WALIKWENDA UHUD BILA YA KUWA NA MSHIKAMNO NA MAFUNGAMANO YA KWELI.

Ni ukweli unaodhihirika wazi kwamba katika vita hivi zilikuwepo  sura na rangi mbali mbali. Matukio yakapunga kufuatana na mawimbi (mpungo) ya nyoyo na nia za watu zilivyokuwa.

Waislamu walivitokea vita hivi na ilhali kidhahiri wakionekana ni watu wamoja, wenye dhamira na nia moja. Watu wanaolipukwa na mori wa kukutana na adui, wenye kuchemkwa na shauku ya kufa kwa ajili ya dini ya Allah. Watu hawa hawakwenda masafa marefu, khilafu ikadhihiri baina yao na ukinzani ukazitambaa safu zao.

Abdullah Ibn Ubayyi akajitoa na kumega theluthi ya jeshi, hili likalifanya jengo lililokamatana kuanza kuvunjika.

Nguzo za jengo hili zikalegalega kiasi cha kukurubia kuanguka upande wake mmoja lau si Allah kuwadiriki waumini kwa rehema zake.

Banu Sulaym na Banu Haarithah wakazuia ukinzani ambao ulikurubia kujitokeza:

“(Kumbuka) MAKUNDI MAWILI MIONGONI MWENU YALIPODHAMIRIA KUFANYA WOGA (na kwenda zake kama walivyokwenda zao wale wanafiki). NA ALLAH AKAWA MLINZI WA YOTE MAWILI HAYO (Kwa hivyo yakahifadhika, hayakufanya mabaya hayo). NA WAISLAMU WAMTEGEMEE ALLAH (tu basi)”. [3:122]

Kwa hivyo basi, utawaona waislamu wanakwenda katika vita hivi wakiwa katika hali inayoshabihiana kwa karibu kabisa na ile hali waliyokuwa nayo Makurayshi wakati wakienda katika vita vya Badri.

Naam, kwa kushindwa huku Allah aliwakashifia (aliwafichulia) waumini nyoyo zenye maradhi ya unafiki zilizojificha miongoni mwa jamii yao.

 Na kwa ushindwa huu Allah akawa amewalinda waislamu na shari nyingi ambazo zingeliwapata kutokana na kuwa pamoja na wanafiki hawa.

Lakini pamoja na yote haya, bado tunalazimika kukiri kwamba kitendo hiki cha kushindwa kwa dhati yake kilisababishwa na udhaifu fulani uliokuwepo upande wa waislamu. Ambukizo la udhaifu huu lilikurubia kutambaa katika safu za waislamu, lakini Allah akaleta salama yake.

 

3.      WARUSHA (WATUPA) MISHALE WALIIKHALIFU AMRI YA MTUME WA ALLAH.

Vita vilipouma ukajitokeza udhaifu mwingine uliosababisha mzozo au ugomvi baina ya watupa mishale wao kwa wao. Wakapapatikia ngawira na kuikhalifu amri  ya Bwana Mtume pamoja na kuwatahadharisha kwake kutoondoka mahala alipowapangia.

Ni jambo lisilo na shaka kwamba utii ndio msingi/uti wa mgongo wa nidhamu ya jeshi na ni anuani ya unyoofu (Ikhlasi) ya mwanajeshi.

 Ni juu ya msingi huu wa utii ndio amiri/kamanda jeshi mkuu huchora/hupanga mikakati yake na huainisha mahala pake pa kupigania.

Kwa mantiki hii  basi, ni dhahiri kuwa pasipo na utii hapana mikakati, hii ni kwa sababu kamanda mkuu huweka mikakati yake baada ya kuyakadiria mazingira yote yanayomzunguka katika uwanja wa mapambano. Ni juu ya makadirio haya ndio huchora mikakati ya kufuata ili kuziba mianya yote inayoweza kutumiwa na adui kwa namna moja au nyingine kuleta madhara.

 Kwa mikakati hii anakuwa amejidhaminia ushindi na nusra dhidi ya adui yake. Na tukumbuke kwamba wakati kamanda anapoweka mikakati yake na kuchora hatua za kupita katika vita, huwa ana yakini kwamba kila hatua itafikia lengo lake.

Sasa katika hali hii unapokosekana utii bila ya shaka mikakati yote itakuwa imefisidika na kuacha mambo kwenda shaghlabaghla ambapo mwisho wake huwa ni mbaya kama tulivyoona.

Haya ndio yaliyojiri/yaliyotokea katika vita vya Uhud, tunawaona watupa mishale wakiikhalifu amri ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ambaye ndiye kamanda mkuu.

Wakamuasi amiri wao; Abdullah Ibn Jubeir ambaye ndiye aliyekuwa kamanda wa kamandi (kikosi) yao. Wakaondoka mahala walipopangiwa na kwenda kuhodhi ngawira kwa mapenzi na raghba yao.

Kwa kitendo chao hiki cha uasi, mikakati iliyowekwa na kamanda mkuu ikafisidika. Maasi haya ya kamandi hii ikawa ni sababu tosha ya kufisidika kwa mikakati mizima ya vita.

Na huku kufisidika kwa mikakati kukawa ni sababu ya mgongano ndani ya jeshi, mgongano ambao ukawa ni sababu ya ushindi kugeuka ushindwa. Tena ushindwa uliokurubia kuwa ni kusagwasagwa lau si ulinzi na wema wa Allah.

Naam, ni lipi khasa lililowapelekea warusha mishale hawa kuikhalifu amri ya Bwana Mtume? Je, ulikuwa ni uasi tu na kujitoa katika twaa ya kamanda mkuu?

Au ilikuwa ni pupa ya kugombea ngawira? Riwaya zote zilizopokewa katika kulitaja tukio hili zinakongamana kwamba watupa mishale hawa waliasi amri ya amiri wao; Abdullah Ibn Jubeir.

Na kwamba amiri wao huyu aliwahadharisha na matokeo ya kukhalifu amri na isitoshe akawakumbusha wasia na maonyo waliyopewa na Mtume wa Allah.

Halafu zinawafikiana riwaya kwamba wao watupa mishale hawakuacha malindo yao ila mpaka walipoona adui kesha endeshwa mbio na wakawaona wenzao wakikusanya ngawira katika hali ya amani. Vyo vyote itakavyokuwa katika suala hili, marejeo yetu sote ni katika Qur-ani Tukufu iliyolisifu tukio hili kuwa ni maasi.

Na kwamba ni udhaifu wa kibinadamu uliozivaa nyoyo hizi zilizoamini, udhaifu uliowapondoa na lengo kuu walilokuja kupigana kwa ajili yake. Ukawapeleka katika lengo duni la kujipatia vitu vya kilimwengu vipitavyo na kusababisha wapate jazaa kwa jinsi ya amali yao:

“…AKAKUPENI (Allah) HUZUNI JUU YA HUZUNI. (Amekusameheni hivyo) ILI MSISIKITIKE (sana) KWA YALE YALIYOKUPOTEENI WALA KWA (misiba) ILIYOKUSIBUNI. NA ALLAH ANA KHABARI ZA YOTE MNAYOYATENDA”. [3:153]

Hivi ndivyo waislamu walivyojua kawaida/kanuni za Allah zinazopita kwa viumbe vyake. Wakatambua kwamba ushindi haupatikani ila kwa kuwepo sababu za ushindi.

Na wakafahamu kwamba kushindwa si suala la sadfa tu bali husababishwa na sababu zake. Wakajua kuwa Allah yu pamoja na waumini muda wa kuwa wao wako pamoja nae kwa hali zao zote. Na huwatupa mkono pindi wakimsahau kwa kushughulishwa na mambo ya kidunia.

Wakaona namna Allah alivyowanusuru juu ya adui wao wakati nia yao ilikuwa ni kuipigania dini yake. Nia yao hii ilipogeuka kukusanya ngawira, Allah akawaacha na ushindi walioupata ukageuka kuwa ushindwa mbaya kabisa:

“NA ALLAH ALIKUKAMILISHIENI MIADI YAKE (ya kuwa mtawashinda). BASI MKAWAUA KWA IDHINI YAKE. MPAKA MLIPOREGEA NA MKAGOMBANA KATIKA SHAURI LILE NA MKAASI BAADA YA YEYE KUKUONYESHENI MLIYOYAPENDA (hapo ndipo alipoacha kukunusuruni). WAKO MIONGONI MWENU WANAOPENDA DUNIA, NA WAKO MIONGONI MWENU WANAOPENDA AKHERA. KISHA (Allah) AKAKUEKENI MBALI NAO (hao makafiri, msiweze kuwashinda) ILI AKUTIENI ADABU. NAYE SASA AMEKUSAMEHENI. NA ALLAH NI MWENYE IHSANI NYINGI JUU YA WANAOAMINI”. [3:152]

 

MAZINGATIO (ITIBARI) KUTOKA VITA VYA UHUD

1.      KUSHINDWA KATIKA VITA VYA UHUD KULIKUWA NI DARASA (FUNDISHO/SOMO) MUHIMU KWA WAISLAMU WOTE KWA UJUMLA WAO.

Mtu atakayetafakari kwa kina hali ya mambo ilivyokuwa katika vita vya Uhud, na akayachunguza kwa makini matukio na picha za mambo zilivyokuwa.

Bila ya shaka ataamini kwamba vita hivi na matokeo yake vilikuwa ni jambo ambalo hapana budi kutokea kwake.

Isitoshe vita hivi vilikuwa ni somo/fundisho ambalo ni lazima waislamu walipate katika kipindi hiki cha uchanga wa Uislamu kwa ajili ya ustawi wake katika siku za usoni.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *