WAISLAMU / WAUMINI WA MWANZO

Natija ya ulinganiaji wa siri wa Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ilikuwa ni kuingia katika uislamu baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki zake na kuwafanya ndio waumini wa mwanzo.

Miongoni mwa mazao ya ulinganiaji huu ni mkewe Bi Khadija, huyu alimuamini Bwana Mtume na akausadiki ujumbe aliokuja nao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

 Bi Khadijah alimuunga mkono Nabii Muhammad kwa hali na mali akimpunguzia kero na maudhi aliyokuwa akiyapata kutoka kwa watu wake.

Ally bin Abi Talib, mtoto wa ammi yake Mtume alikuwa ni mwingine aliyemuamini na kumkubali.

Huyu alikuwa ni kijana mwenye umri usiopindukia miaka kumi na alikuwa akilelewa na Mtume, ikiwa ni kumpunguzia ammi yake mzigo mkubwa wa familia uliomlemea.

Mtume alipopewa utume rasmi, Ally aliingia chumbani na kumkuta akisali na mkewe Bi Khadijah. Ally akasimama akiwaangalia mpaka wakamaliza kuswali, ndipo akamuuliza Mtume juu ya kitu kipya hiki alichokiona.

Mtume akamwambia :

“Hii ndio dini ya Mwenyezi Mungu aliyoichagua yeye mwenyewe na akawatumilia kwa dini hii mitume wake. Basi ninakulingania umuabudu Allah pekee asiye na mshirika na uwakufuru (uwakane miungu sanamu) Lata na Uzzah”.

Ally akasema :

sijapata kulisikia jambo hili kabla ya leo, basi sitakata shauri mpaka nimwambie Abuu Twalib (baba). Mtume akachelea asije akaifichua siri yake kabla yeye mwenyewe hajaitangaza, akamwambia :

“Ewe Ally ikiwa husilimu basi nifichie siri hii na usimwambie mtu yeyote”.

Usiku ule, Ally akakesha akifikiria kile alichokiona na kukisikia mchana wake kutoka Nabii Muhammad.

 Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa hekima azijuazo mwenyewe akautia na kuujaza Uislamu ndani ya moyo wa Sayyidna Ally.

Kulipopambazuka, akadamkia kwa Mtume na kumuuliza : ulinitangazia/ulinieleza nini vile, jana ? Mtume akamjibu :

 “Ushuhudie kwamba hapana Mola afaaye kuabudiwa kwa haki ila ALLAH pekee asiye na mshirika na uwakane Lata na Uzzah na ujiepushe na miungu washirika”. Sayyidna Ally akasilimu na kuuficha uislamu wake kwa kumchelea baba yake.

Ulipofika wakati wa swala Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – alikuwa akitoka kwa uficho pamoja na Sayyidna Ally, wakienda kuswali kwenye viunga/maboma ya mji wa Makkah.

 Walikuwa wakikaa huko mpaka jioni na waliendelea na zoezi hili kwa muda mrefu. Siku moja Ammi yake Mzee Abu Twalib akawafuma wakiswali.

Akamuuliza : ewe mwana wa ndugu yangu, ni dini gani hii unayoifuata ? Mtume akamjibu :

“Ewe Ammi yangu, hii ndio dini ya ALLAH, dini ya malaika wake, dini ya mitume wake na dini ya baba yetu Ibrahim, ALLAH amenitumiliza kwa waja na dini hii. Nawe ammi yangu, ndiye una haki zaidi kwangu kuliko mtu yeyote nikupe nasaha na kukulingania kwenye uongofu na ndiwe una haki zaidi ya kuniitikia na kuniunga mkono !”. Abuu Twalib akamjibu Mtume :

 Ewe mwana wa ndugu yangu wee, mimi siwezi kuiacha dini ya baba zangu na itikadi yao, lakini ninakuahidi hutodhurika na chochote maadam ni hai. Kisha akamwambia Ally : Ewe mwanangu, nduguyo hakukulingania ila ni kwenye kheri, basi ninakuusia umlazimu.

Kama walivyosilimu Bi Khadijah na Sayyidna Ally katika nyumba ya Mtume, pia alisilimu kijana na mtumishi wake Zayd bin Harithah.

Sayyidna Abuu Bakri alikuwa ni mpenzi wa watu, mjuzi wa nasabu za makurayshi, tajiri na mfanyabiashara mashuhuri.

Huyu alikuwa ni rafiki mkubwa wa Bwana Mtume na alimpenda upeo, Mtume alipomueleza juu ya Uislamu, pale pale bila ya kufikiri wala kusita alimuamini Mtume na kusilimu.

Mtume anaeleza juu ya ulinganiaji wake na kusema :

“Sikumlingania mtu kwenye uislamu ila alisita kwanza isipokuwa Abu Bakri”.

Kisha naye akaanza kuutangaza uislamu kwa siri kwa kila aliyemuamini miongoni mwa rafiki zake.

Wakasilimu kwa wito wake : Sayyidna Uthman ibn Affan, Zubeir ibn Al-awwaam, Abdulrahman ibn Auf, Sa’ad ibn Abi Waqqaas, na Twalhah ibn Ubeydillah. Akawaleta kwa Mtume na wakasilimu mbele yake.

Hawa ndio watu wa mwanzo kabisa kuingia katika uislamu na wakawa ndio matofali ya mwanzo wa jengo imara la Uislamu, na wao ndio nguzo madhubuti na imara za jengo hili mpaka likaweza kusimama na kufikia hivi ilivyo leo.

Kadhalika mlezi wake Bwana Mtume, Ummu Ayman hakubakia nyuma bali alimuamini Mtume na kusilimu.

Baadaye Mtume alimuoza mama huyu kwa mtumishi wake na mwanawe wa kupanga Zayd bin Harithah. Zayd bin Harithah alikuwa akijulikana kama Zayd bin Muhammad kutokana na ada ya waarabu wakati ule, wao walimzingatia mtoto wa kupanga kama mtoto wa kumzaa, hivyo basi walimpa huyu mtoto wa kupanga haki ya kumrithi baba yake wa kupanga na yeye kurithiwa naye.

Uislamu ulipokita mizizi Mwenyezi Mungu alibatilisha na kuifuta ada na desturi hii waliyoizoea kwa miongo ya miaka.

Miongoni mwa waislamu wa mwanzo haachi kutajwa Swuhayb Arrumiy, huyu alikuwa ni mtumwa.

Pia alislimu Ammaar bin Yaasir ambaye anasimulia jinsi alivyosilimu, anasema : Nilimwona Mtume wa Mwenyezi Mungu akiwa hana aliyemfuata ila watumwa watano wanawake wawili na Abu Bakri”.

Kadhalika alisilimu baba yake Mzee Yasir na mama yake Sumayyah.

Abdallah bin Masoud, mchunga kondoo/mbuzi wa makurayshi pia alichomozewa nyota ya uislamu.

Huyu alikuwa akiingia wakati wowote kwa Mtume na hapakuwa na wa kumzuia na akitembea mbele ya Mtume.

Mbali na hayo, alikuwa akimngojelea Mtume wakati alikuwa akikoga na akimuamsha alalapo na isitoshe akimbebea na kumvisha Mtume viatu vyake. Haya yote yanaonyesha na kudhihirisha namna yalivyokuwa mapenzi ya Ibn Masoud kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Abu dhari Al-Ghifariy, mkazi wa vitongojini, fasaha wa lugha, Said bin Zayd na mkewe Fatmah bint Khattab; dada yake Sayyidna Umar, Lubaabah bint Al-Haarith mkewe Sayyidna Abbas ammi yake Mtume, Ubaadah bin Al-Haarith mtoto wa ammi yake Mtume, Abu Salamah Abdallah ibn Abdil-Asad mtoto wa shangazi yake Mtume, na mkewe Ummu Salamah, Uthmaan ibn Madh-‘uun na nduguze Qudaamah na Abdullah.

Hili pia ni kundi la watu walioongozwa na Mwenyezi Mungu na kupata fursa na bahati ya kuwa waumini wa mwanzo.

Kadhalika katika jumla ya waliosilimu mwanzo ni Khalid ibn Said, baba yake mzee Said bin Al-aaswi alikuwa ni mmoja wa viongozi wa makurayshi aliyeheshimika sana.

Siku moja Khalid aliota kwamba anatumbukia shimoni, akaja Bwana Mtume akamuwahi na kumuokoa. Asubuhi, kulipopambazuka akamuendea Mtume na kummuliza : Unalingania nini ewe Muhammad ? Mtume akamjibu :

“Ninakulingania umuabudu Allah pekee asiyekuwa na mshirika na uache kuyaabudia mawe yasiyosikia, yasiyoona, yasiyodhuru wala kunufaisha na kuwatendea wema wazazi wako. Usimuue mwanao kwa kuchelea ufakiri, usiyakurubie mambo machafu ya dhahiri na siri, usimuue mtu, usile mali ya yatima, upime mizani kwa uadilifu usipunje, uwe muadilifu katika hukumu zako hata kama unaowahukumu ni ndugu na jamaa zako na utekeleze ahadi ulizotoa”.

Khalid alikuwa akimsikiliza Mtume kwa makini sana huku maneno ya kweli yatokayo katika kinywa cha Mtume yakiupenya moyo wake na kuujaza tele Uislamu na hivyo kumfanya asilimu. Baadaye akasilimu kaka Amir bin Said.

Hivi ndivyo walivyoingia watu hawa katika Uislamu, Mtume hakuwa na upanga akiwatenza nguvu na kuwalazimisha kuingia katika dini, kama wanavyodai maadui wa Uislamu. Mtume atawezaje kulifanya hilo, wakati tayari ana muongozo usemao :

 “HAKUNA KULAZIMISHWA (mtu kuingia) KATIKA DINI. UONGOFU UMEKWISHA PAMBANUKA NA UPOTOFU. BASI ANAYEMKATAA SHETANI NA AKAMUAMINI ALLAH, BILA SHAKA YEYE AMESHIKA KISHIKO CHENYE NGUVU KISICHOVUNJIKA” [2:256]

Kadhalika ni vema ikafahamika kuwa Mtume hakuwa na mali iliyowavutia hawa waufuate Uislamu ili wapate kunufaika na mali hiyo.

Bali wengi miongoni mwao walikuwa ni watu matajiri wenye kumiliki mali nyingi kama vile Sayyidna Abu Bakr, Sayyidna Uthman bin Affaan, Khalid bin Said na wengineo wengi.

Watumwa waliomfuata walikubali kustahmili taabu na mateso makubwa waliyoyapata kutoka kwa mabwana wamiliki wao kwa ajili tu ya kusilimu na kumuamini Allah na Mtume wake.

Haya tutasema nini kwa watumwa hawa wainuao dini kwa gharama ya adhabu na mateso makali ambayo yalipelekea baadhi yao kupoteza maisha yao ?!

Ukiwa u mtu mkweli na muadilifu hutoacha kukubali kuwa hii ni HIDAYA waliyotunukiwa na Mwenyezi Mungu watu hawa, kwani sio akili wala matashi ya mtu kufuata kitu kisichoonekana manufaa yake papo kwa papo na kukhitari adhabu na mateso.

Hii ni NURU ya dini iliyowachomozea na wala si uhodari wa Mtume katika kuwalingania, seuze kutumia nguvu mtu mmoja kwa watu wote hawa ?!

Mola wetu Mtukufu tunakuomba uwawie radhi, mabwana hawa watukufu uliowachagua kuwa maswahaba wa Mtume wako –Rehema na Amani zimshukie

 

 

WAISLAMU / WAUMINI WA MWANZO

Natija ya ulinganiaji wa siri wa Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – ilikuwa ni kuingia katika uislamu baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki zake na kuwafanya ndio waumini wa mwanzo.

Miongoni mwa mazao ya ulinganiaji huu ni mkewe Bi Khadija, huyu alimuamini Bwana Mtume na akausadiki ujumbe aliokuja nao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

 Bi Khadijah alimuunga mkono Nabii Muhammad kwa hali na mali akimpunguzia kero na maudhi aliyokuwa akiyapata kutoka kwa watu wake.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *