KUMALIZIKA DAURI YA KWANZA

Vita vikaanza rasmi kwa ‘mubaraza’; mtu wa upande huu akipambana na yule wa kule na waliobakia wakishuhudia.

Akatoka mtu mmoja katika safu za washirikina akitaka mtu wa kupigana nae kwa mubaraza. Swahaba Zubeir Ibn Al-awaam akamtokea, akapambana nae na kumuua.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akafurahishwa na ushindi huu wa mwanzo dhidi ya adui, akapiga takbir kuonyesha furaha yake hii.

Waislamu wakaipokea takbir hii tukufu, anga likarindima kwa takbir zao huku wakimvaa adui yao na ilhali wakipiga ukelele wa vita:

“Ua ua!” Sayyidina Aliy Ibn Abiy Twaalib-Allah amuwiye radhi-akamshambulia mshika bendera wao; Twalhah Ibn Abiy Twalhah na kufanikiwa kumuua.

Baada ya kuuawa huyu adui wa Mungu; Twalhah bendera ya mushrikina ikachukuliwa na kupeperushwa na nduguye; Uthmaan Ibn Abiy Twalhah.

Sayyidina Hamzah Ibn Abdul-Mutwalib-Allah amuwiye radhi akamshmabulia na kumuua. Bendera sasa ikawa inapeperushwa na ndugu yao akiitwa Abuu Said, Sayyidina Sa’ad Ibn Abiy Waqaasw-Allah amuwiye radhi-akamlenga mshale na kumuacha akianguka maiti.

Alipouawa kafiri huyu, wakaanza kupokezana bendera watoto wanne wa Twalhah; mshika bendera wa mwanzo, nao wote wakiuawa mmoja baada ya mwingine.

Hatimaye bendera ikaokotwa na kupeperushwa na kijana mtwana wao aliyeitwa Swuaab, nae pia akauawa akiiacha bendera kuanguka chini bila ya kupata wa kuiokota na kuipeperusha.

Mushrikina wakaendeshwa puta, nguvu yao ikavunjika na safu zao zikameguka, waislamu wakawashambulia shambulizi la kweli.

Wakiwashushia dharuba za panga, chomo za mikuki na tupo za mishale zilizowasambaratisha kabisa wasiweze kuhimili mapigo.

 Wakawa hawana la kufanya ila kutimua mbio na kuwaacha wanawake wao wakipiga mayowe ya mtu aombaye msaada wa dharura na kulia kilio cha huzuni.

Huku wakikimbizana kuepuka kuchukuliwa mateka. Waislamu nao kwa upande wao wakawakimbiza maadui zao wakiwaua na wengine wakafanikiwa kukimbia mbali kabisa na kambi yao.

Waislamu wakaitumia fursa hii kwa kuanza kukusanya ngawira huku wakiamini kuwa warusha mishale bado wanaendelea kuwalinda dhidi ya shambulio lo lote kutokea nyuma.

 

WATUPA MISHALE WAONDOKA MAHALA WALIKOWEKWA NA BWANA MTUME NA KUUGEUZA USHINDI KUWA USHINDWA NA MAANGAMIVU.

Watupa mishale waliokuwa jabalini wakadhania kwamba vita imemalizika na tayari mushrikina wameshashindwa.

Dhana hii isiyo na msingi wala mashiko, ikawasahaulisha wasia wa Mtume na kuona kuwa hakuna sababu ya wao kuendelea kubakia jabalini hapo.

Wakachelea kupitwa na wenzao katika zoezi zima la ukusanyaji wa ngawira, wakaambizana:

“Kipi kinachotubakisha hapa na ilhali Allah ameshamuangamiza adui kwa mikono yetu? Hao wenzenu wanachukua ngawira, nanyi ingieni mkachukue ngawira pamoja nao”.

Amiri wao; Abdullah Ibn Jubeir alipoona uroho wa ngawira umewatambaa na kuwavaa watu aliopewa kuwaongoza. Akaanza kuwakumbusha wasia waliopewa na Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie.

Akawatahadharisha na matokeo mabaya ya kukhalifu amri ya Mtume wa Allah na kumuasi. Lakini wapi sikio la kufa halisikii dawa, tahadhari na makumbusho yote hayo ikawa ni mithili ya kumpigia mbuzi gitaa.

Hao nao wakajitoma katika kambi ya mahasimu wao wakikusanya ngawira, huku wakimuacha amiri wao jabalini pale na watu wasiozidi kumi. Kuondoka kwao kukaifanya ngome iliyokuwa ikiwalinda kwa nyuma waislamu kuwa wazi, inayoweza kupenywa na adui kirahisi kuliko ilivyokuwa mwanzo.

Kamanda shupavu wa mushrikina Khaalid Ibn Al-Waleed alikuwa akikimbia kisengerenyuma (kinyumenyume) huku akiyakazia macho yake jabalini.

Alipoona watupa mishale wakiziacha sehemu zao, akaamua kuitumia vema fursa hii ya kosa baya lililofanywa na waislamu.

Akapanua wigo wa vita akarejea kwa nyuma akiwaongoza wapiganaji wake, akizitumia ardhi za uficho kama njia na chochoro zake.

Akaenda akifuatiwa nyuma na Ikrimah Ibn Abiy Jahli akiipeperusha bendera ya batili dhidi ya haki. Wakafanikiwa kupenya na kufika jabalini penye ngome ya waislamu inayowalinda kwa nyuma yao.

Wakawafagia na kuwaondosha kirahisi mno watupa mishale wachache waliokuwa wamethibiti katika lindo lao baada ya wenzao wengi kuondoka kwenda kukusanya ngawira.

Fagiafagia hii ikawawezesha kuzivaa safu za waislamu kwa kutokea nyuma kwa ghafla isiyotazamiwa wala kutegemewa. Mushrikina wakasonga mbele kwa kasi ya nguvu baada ya mkimbizano wa nguvu, wakiwashambulia waislamu kwa mori mkuu. Amrah Bint Alqamah akaitwaa bendera iliyokuwa imetupwa chini na kuinyanyua juu kuwaita wote waliokuwa wamekimbia baada ya kipigo cha awali.

 Waislamu wakajikuta wamezingirwa na adui yao kiasi cha kushindwa kutoa upinzani utakaomrejesha adui nyuma.

Wakauliwa waislamu wengi takriban sabini na kuwaacha wengi wakiwa wameumizwa vibaya sana. Safu za waislamu zikachangukana, wakagongana na kupelekea kushambulia bila ya mpango maalumu kiasi cha kuuana wenyewe kwa wenyewe bila ya kujua.

 

KIYOWE CHENYE MVUTO CHAWADHOOFISHA WAISLAMU MARA DUFU.

Katikati ya kizaizai na kitatange hiki kikuu ukasikika uyowe uliosikiwa barabara na watu ukisema: “Muhammad tayari amekwishauawa”.

Waislamu wakachanganyikiwa na uyowe huu na kutikiswa nao sana na kuwaacha wakitambaliwa na hisia za woga mkubwa.

Nafsi zao zikaingiwa na fikra ya kujitoa na kuona kuwa hakuna sababu ya kuendelea na vita. Hisia za woga na fikra za kujitoa ikawa ni sababu ya kugawika waislamu makundi mengi.

Wako miongoni mwao walioona kwamba kukimbia ndio suluhisho pekee na wako walioamua kuthibiti na hima yao yote ikiwa ni kuzilinda nafsi zao au kupigana mpaka wauawe.

Kadhalika lilikuwepo kundi ambalo mashambulizi yale ya ghafla na ya nguvu yaliwaondoshea kabisa matumaini ya kunusurika, wakaamua kusalimu amri. Pia wako waliohemewa wasijue cha kufanya.

Wakati yote haya yakijiri, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa nyuma ya maswahaba wake akiwaita:

“Njooni kwangu enyi waja wa Allah! Njooni kwangu enyi waja wa Allah! Njoo kwangu ewe fulani! Njoo kwangu ewe fulani! Mimi ndiye Mtume wa Allah!”.

 Lakini wapi watu wamehamanika na kivangaito kilichowapata bila ya kutazamia, litapatikana wapi katika hali hiyo sikio la usikivu? Tim haooo watu wanatimka mbio, hawausikii wito wa Mtume wa Allah ila sauti na kelele tu. Hivi ndivyo Qur-ani Tukufu inavyoeleza hali ilivyokuwa:

“(Kumbukeni) MLIPOKUWA MKIKIMBIA MBIO, WALA NYINYI HAMUMSIKILIZI YO YOTE, HALI MTUME ALIKUWA ANAKUITENI, YUKO NYUMA YENU. AKAKUPENI (Allah) HUZUNI JUU YA HUZUNI. (Amekusameheni hivyo) ILI MSISIKITIKE (sana) KWA YALE YALIYOKUPOTEENI WALA KWA (misiba) ILIYOKUSIBUNI…” [3:153]

Shetani mlaaniwa akaitumia vema fursa hii ya kupapatika na kuhemewa kwa waislamu, akaanza kuzitia maradhi ya wasiwasi nyoyo nyonge na kuzitelezesha nafsi dhaifu.

Naam, maradhi haya mabaya yakawasibu waislamu kama alivyolenga shetani, baadhi ya waislamu wakafikia kusema:

“Kwa nini tuendelee kupigana ikiwa Muhammad amekwisha uawa? Rejeeni kwa jamaa zenu nao watakupeni amani”.

Kuhusina na hali hii tunasoma:

“WALE WALIORUDI NYUMA (waliokimbia) MIONGONI MWENU SIKU AMBAYO MAJESHI MAWILI YALIPOKUTANA (katika vita vya Uhud-jeshi la makafiri na la waislamu),SHETANI NDIYE ALIYEWATELEZESHA KWA (sababu ya) BAADHI YA (makosa) WALIYOYAFANYA. NA ALLAH NI MWINGI WA KUSAMEHE (na) MPOLE SANA”. [3:155]

Maswahaba wengine walidhania kwamba huo ndio mwisho wao na ndio mwisho wa Uislamu kwani hakuna atakayesalimika kutokana na nguvu ya makafiri. Hivi ndivyo walivyosema kama walivyonukuliwa na Qur-ani Tukufu:

“…TUNGEKUWA NA CHO CHOTE KATIKA JAMBO HILI TUSINGEUAWA HAPA…” [3:154]

 

KUMALIZIKA DAURI YA KWANZA

Vita vikaanza rasmi kwa ‘mubaraza’; mtu wa upande huu akipambana na yule wa kule na waliobakia wakishuhudia.

Akatoka mtu mmoja katika safu za washirikina akitaka mtu wa kupigana nae kwa mubaraza. Swahaba Zubeir Ibn Al-awaam akamtokea, akapambana nae na kumuua.

Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akafurahishwa na ushindi huu wa mwanzo dhidi ya adui, akapiga takbir kuonyesha furaha yake hii.

(more…)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *