Uislamu ukazidi kusambaa katika mji wa makkah na khabari zake kuenea pande zote za mji huo, na watu wakaingia katika uislamu makundi kwa makundi.
Hapa ndipo Mtume-Rehema na Amani zimshukie – akaitumia fursa hii kwanza kuikosoa miungu sanamu ya Makurayshi kwa nini mnayaobudia masanamu yasiyodhuru wala kukunufaisheni?
Miungu wasiyoweza kujisaidia wao wenyewe, vipi watakusaideni nyinyi? Miungu wasioweza kujilinda wao wenyewe vipi watakulindeni nyinyi?
Kwa ujumla Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie – akawa anawaonyesha Makurayshi ubaya na upotofu wa itikadi yao na dini wanayoifuata.
Hapa ndipo makurayshi walipozinduka na kuiona khatari inayowakabili kutokana na dini hii mpya aliyokuja nayo Bwana Mtume.
Ili kukabiliana na mawimbi makubwa ya dini hii, Makurayshi wakaanza kumfanyia Mtume namna mbalimbali za kero na maudhi kiasi walichoweza.
Isitoshe wakawa wanamcheza shere khasa khasa anapotoka kwenda kuswali- Wakamzulia kwamba Mtume ni mwendawazimu asiye na akili na wakati mwingine wakisema ni mchawi na mara nyingine wakimwambia kuwa ni kuhani na muimba mashairi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu akiyakanusha madai yao hayo na kusisitiza kwamba Mtume wake Muhammad hana hata sifa moja miongoni mwa sifa hizo walizomzulia.
Mwenyezi Mungu aliapia hilo na kusema
“BASI NAAPA KWA MNAVYOVIONA NA MSIVYOVIONA KWA HAKIKA HII NI KAULI ILIYOLETWA NA MJUMBE (WA ALLAH) MWENYE HISHIMA (Kubwa). WALA SI KAULI YA MTUNGA MASHAIRI (Kama mnavyosema). NI MACHACHE SANA MNYOYAAMINI. WALA SI KAULI YA MCHAWI (kama mnavyodai). NI KIDOGO KABISA KUWAIDHIKA KWENU. NI UTEREMSHO UTOKAO KWA MOLA WA VIUMBE VYOTE” [69:38-43].
Pamoja na ukweli huu juu ya Nabii Muhammad bado Makurayshi hawakumuamini bali ulikuwa kama ndio kichocheo cha upinzani.
Makurayshi wakaanza kuwatahadharisha na kuwazuia watu wasikutane na mtume na wala wasimsikilize kabisa.
Hatua zote hizi hazikusaidia kitu wala kuwaletea Makurayshi nafuu yeyote. Kwa hivyo wakaamua kukutana katika mkutano wa dharura ili kujadili juu ya hii dini mpya ya Nabii Muhammad.
Dini ambayo imekuwa ni hatari kubwa inayokaribia kuimeza na kuiua kabisa dini yao ya ushirikina. Wakabadilishana mawazo na rai jinsi ya kufagilia mbali dini hii mpya inayowataka waache ibada ya miungu wengi kuja kwenye ibada ya Mungu Mmoja wa Pekee asiye na mshirika.
Vijana wa Kikurayshi ambao mara nyingi ni watu wenye hamasa, jazba na mori. Hawa waliona njia bora ya kuimalizia mbali dini hii ni kuukata kabisa mzizi wa fitna.
Na hili halipatikani ila ni kwa kuuwawa Nabii Muhammad haraka iwezekanavyo kabla sumu yake haijatapakaa na kuathiri zaidi. Ama wazee, ambao hawa mara nyingi uzoefu umeonyesha ni watu wanaotawaliwa na hekima na busara.
Hawa waliona ni vema wakaketi chini pamoja na Nabii Muhammad ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hili la mgogoro wa dini kwa njia ya salama na amani.
Rai hii ya wazee ikapita na kukubaliwa. Japo teule la wazee likaenda kukutana na Mtume na kijaribu kumshawishi aachane na hii dini mpya aliyokuja nayo ambayo inaigawa jamii ya Kikurayshi.
Aache kuikosoa miungu yao na arudi katika dini ya wahenga. Bwana Mtume- Rehema na Amani zimshukie- hakuwafikiana nao na akawaambia kama alivyofundishwa na mola wake :-
“SEMA ENYI MAKAFIRI! SIABUDU MNACHOABUDU WALA NYINYI HAMUMUABUDU NINAYEMUABUDU. WALA SITAABUDU MNACHOABUDU. WALA NYINYI HAMTAMUABUDU NINAYEMUABUDU. NYINYI MNA DINI YENU NA MIMI NINA DINI YANGU” [109:1-6]
Makurayshi walipoona kwamba jitihada zao hizi hazizai matunda na Bwana Mtume anazidi kuwa mkaidi, hataki kuwasikiliza, wakamkemea vikali aache mara moja kuitukana miungu na aache kuwatenganisha, la haachi basi hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Likateuliwa jopo kwenda kuonana na Ami yake Mtume –Mzee Abu Twalib – ambaye alionekana kuwa ndio ngome na himaya ya Mtume.
Wajumbe wa jopo hili walikuwa pamoja na Utbah bin Rabiah, Shaybah bin Rabiah, Abu Sufyan bin Harb, Al-aaswi bin Hisham, Al-waliid bin Mughiyrah na wengineo. Wakamwambia Mzee Abu Twalib :
“Ewe Abu Twalib, hakika mwana wa nduguyo amewatukana miungu wetu na kuikosoa dini yetu na kusema kuwa wahenga wetu walikuwa katika upotofu. Sasa, tunakutaka umzuie aachane na sisi tupambane nae wenyewe” Abu Twalib akawajibu kwa maneno mazuri, wakaenda zao.
Mtume akaendelea na kazi yake, akiidhihirisha na kuitangaza dini ya haki. Makurayshi kuona hivyo wakamuendea tena Mzee Abu Twalib na kumwambia :
Ewe Abu Twalib, wewe kwetu ni mtu mwenye heshima, cheo na utukufu. Sisi tulikuomba umzuie mwana wa nduguyo nawe hukutaka kumzuia. Nasi – Wallahi – sasa hatuna tena subira juu ya suala hili. Hatutokubali kutukaniwa wahenga wetu na miungu wetu. Sasa, ima umzuie au nyinyi na sisi tupambane mpaka apatikane mshindi.
Kisha wakashika njia na kwenda zao. Mzee Abu Twalib akaachwa njia panda akiwa hajui afanye nini.
Kutengana na jamii yake, hili lilikuwa jambo zito sana kwake na kumuacha mwana wa nduguye aadhibiwe na Makurayshi, hili pia lilikuwa jambo zito kabisa.
Afanyeje sasa katika kipindi hiki kigumu ambamo Makurayshi hawana tena mzaha na wako tayari kufanya lolote kuilinda hadhi na heshima ya dini yao.
Akamuita mwanawe na kumwambia : Ewe mwana wa ndugu yangu, jamaa zako wamenijia na kuniambia jambo kadha wa kadha.
Basi nakuomba unionee huruma mimi na ujionee huruma wewe kutokana na hasira za jamaa zako, na wala usinitwishe mzigo nisioweza kuubeba.
Mtume akadhania Ami yake sasa anamtupa mkono na kuwaachia nafasi wapambane naye, kutokana na kauli yake hiyo. Bwana Mtume –Rehema na Amani zimshukie – akamjibu Ami yake na kumwambia :
“Wallah! Lau wataliweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi katika mkono wangu wa kushoto ili kunishinikiza niache jambo hili, nisingeliacha katu mpaka Mwenyezi Mungu aipe ushindi dini yake au mimi niangamie!”.
Kisha Mtume akampa mgongo Ami yake kutaka kuondoka huku analia. Ami yake akamuita : Njoo ewe mwana wa ndugu yangu !.
Mtume akaja, akamwambia : “Nenda ewe mwana wa ndugu yangu, na sema utakalo. Wallah sitokusalimisha kwa jambo baya, kamwe.”
Makurayshi walipoona kwamba Mzee Abu Twalib hataki kumkataza mwanawe wakamuendea na Ammaarah bin Waliid bin Mughira, wakamwambia :
Ewe Abu Twalib, huyu hapa Ammaarah bin Waliid kijana mzuri kuliko wote wa Makurayshi, mtwae awe mwanao na umsalimishe kwetu huyu mwana wa nduguyo ambaye ameikhalifu dini yako na dini ya baba zako na amewafarikisha jamaa zako, tuachie tumuue.
Mzee Abu Twalib akawajibu : Wallah ni kibaya mno kitendo mnachonitaka nikifanye! Mnanipa mwanenu nikuleleeni kisha nikupeni mwanangu mumuue ?
Hili Wallah kamwe halitakuwa !. Msimamo huu wa Ami yake Mtume haukuwafurahisha Makurayshi hata kidogo bali ulizidi kuamsha na kuchochea hasira na ghadhabu za Makurayshi dhidi ya Mtume.
Mzee Abu Twalib akaona kadhia hii imekuwa kubwa, hawezi kuikabili peke yake. Akaamua kuwakusanya jamaa zake Banii Hashim na kuwaeleza yote yaliyojiri baina yake na Makurayshi tangu mwanzo mpaka mwisho.
Wakaanza kushauriana cha kufanya, hatimaye wakaafikiana kwa kauli moja kulinda hadhi na heshima yao. Wasimame imara safu moja kumlinda na kumtetea Mtume hata kama hayuko pamoja nao kiitikadi pamoja na kwamba hili litawagharimu sana