Upepo wa pepo ya Allah ukawavumia waislamu katika uwanja wa mapambano, maisha ya ulimwengu huu wakayaona hayana thamani.
Kufa shahidi kukawa na ladha mno kwao kuliko kitamu cho chote ukijuacho. Ladha hii ya kufa shahidi ikamlevya swahaba Umeir Ibn Al-Humaam-Allah amuwiye radhi-kiasi cha kumfanya kupiga makelele kutokana na furaha iliyofurutu:
“Eh! Hivi kumbe kinachonizuia kuingia peponi ni kuuawa na makafiri hawa?” Baada ya kusema maneno hayo, akazitupilia mbali tende alizokuwa nazo mkononi akizila huku akisema:
“Kama mimi nitaendelea kuwa hai mpaka nimalize kuzila tende hizi, bila shaka huo ni uhai mrefu mno”.
Huyoo akajitoma katika uwanja wa mapambano mtomo wa mshale huku akiimba mashairi ya kuhamasisha na kupandisha mori.
Ladha ya kufa shahidi kwa ajili ya kuipigania dini ya Allah ikamsukuma swahaba mwingine Auf Ibn Al-Haarith-Allah amuwiye radhi-kumuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kitu/jambo linalomfurahisha Mola kwa mja wake pindi akilitenda.
Nae Bwana Mtume akamjibu:
“Kuutosa kwake (huyo mja) mkono wake kwa adui hali ya kuwa mtupu”.
Kusikia kauli hiyo ya Bwana Mtume, pale pale akaivua deraya (armour) yake akaitupilia mbali na akauchukua upanga wake na kujitosa mapambanoni mtupu mtupu bila ya kubali mauti yatamshinda au atayashinda yeye.
JESHI LA ALLAH MAPAMBANONI.
Allah akalipa jeshi lake msaada kwa rehema zake, msaada uliozidisha hamasa zao za kuipigania dini yake kwa thamani ya nafsi zao.
Joto la kufa shahidi likapanda kupita kiasi na zikarudifika nguvu zao kiasi cha kujihisi mmoja wao kuwa ni tosha ya mushrikina kumi.
Akahisi kuwa mkono (msaada) wa Allah uko juu ya mkono wake, kutokana na hisia hizi ukawa unatukutika upanga wake na kupiga.
Analenga shabaha huku akijihisi kuwa miongoni mwa jeshi la Allah lisiloonekana. Ukadogeka wingi wa mushrikina machoni mwa waumini kwa msaada wa Allah, hili likawapandisha mori wa mashambulizi.
Wakaanza kuwashambulia mushrikina mshambulio wa mbwa-mwitu kwa kondoo na kuwafagia ufagizi wa mumbwi (torrent).
Anga la khofu likaugubika uwanja wa mapambano, nyoyo za mushrikina zikajawa na khofu kuu na miili yao kuzizima kwa uoga wakati ambapo nyoyo za waumini zilijaa nguvu, ujasiri na ladha ya vita. Kuhusiana na msaada huu wa Allah kwa waumini tunasoma:
“HAKIKA IMEPATIKANA ALAMA KUBWA KWENU(nyinyi) KATIKA YALE MAKUNDI MAWILI YALIYOKUTANA (siku ya vita vya Badri), KUNDI MOJA LIKIPIGANA KATIKA NJIA YA ALLAH, NA JINGINE MAKAFIRI. (Makafiri) WAKAWAONA (waislamu) ZAIDI KULIKO WAO MARA MBILI KWA KUONA KWA MACHO, NA ALLAH HUMTIA NGUVU KWA NUSRA YAKE AMTAKAYE. KWA YAKINI KATIKA HAYO YAKO MAZINGATIO (makubwa) KWA WENYE BUSARA”. [3:13]
BWANA MTUME AMUOMBA MSAADA MOLA WAKE.
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alitulia tuli kibandani mwake, akiufuatilia kwa makini mwenendo wa vita na il-hali moyo wake ukiwa umefungamana na Allah Bwana Mlezi wake.
Wakati mwingine hulazimika kushuka kuja kitimtimni kuipandisha ari na mori wa waislamu na kuwashajiisha kupigana.
Na mara nyingine hupanda kibandani kwake akimuomba na kumtaka msaada Mola wake, katika jumla ya dua yake alikuwa akisema:
“Ewe Mola wa haki wee! Ninakuomba unitimizie ahadi na miadi yako. Ewe Mola wa haki wee! Ikiwa litaangamia kundi hili leo hutaabudiwa baada yake katika ardhi. Ewe Mola wa haki wee! Nipe nusra yako uliyoniahidi. Ewe Mola wa haki wee! Zitie khofu nyoyo zao na itetemeshe miguu yao (wasiweze kuthibiti)”.
Bwana Mtume aliendelea kumuomba na kumtaka msaada Mola wake mpaka ikamuanguka shuka yake aliyokuwa amejitanda mabegani mwake.
Sayyidina Abuu Bakri-Allah amuwiye radhi-akalazimiana naye, akamuwekea mtandio wake na akawa anamwambia kwa kumuonea huruma kutokana na hali aliyonayo:
“Ewe Nabii wa Allah, jipe muda katika kumuomba kwako Mola wako, kwani bila ya shaka atakutekelezea aliyokuahidi”. Bwana Mtume akazama katika dua zake hadi likampata pepeso la usingizi, akasinzia kidogo kisha akazinduka il-hali akiwa amejawa furaha, akamwambia Abuu Bakri: “Furahi ewe Abuu Bakri, imekuja nusra ya Allah. Jibril huyoo ameshika hatamu za farasi wake akimuongozea kwenye vumbi la vita”.
Bwana Mtume akawashukia maswahaba wake kwenye uwanja wa mapambano, akiwabashiria nusra ya Allah na kuwaambia:
“Panieni, wingi wao huo karibuni hivi utaendeshwa mbio na watageuza migongo yao wakikimbizana. Atakayemuua mtu ni yake yeye mali aliyonayo (muuawa huyo) na atakayemteka mateka ni milki yake mateka huyo”.
Bishara na hamasisho hili la Mtume likawaongezea nguvu waislamu, wakawashambulia makafiri kisawasawa. Makafiri wakahemewa na kusambaratika kutokana na kasi ya mashambulizi haya mpaka wakapoteza nguvu na muelekeo wa mapambano.
MUSHRIKINA WAENDESHWA MBIO.
Mushrikina walipoona yaliyowapata viongozi wao, khofu ikawatambaa mioyoni mwao, wakaanza kutupa mizigo yao ili kupunguza uzito.
Wakitimua mbio kutoka katika uwanja wa mapambano ili kujiokoa na mauti. Kuona hivyo waislamu nao wakawakimbiza na kuwateka waliodiriki kuwakamata miongoni mwao na kuichukua ngawira mali yao yote waliyoiacha nyuma.
Wakati waislamu wakiwachukua mateka mushrikina, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alimtazama swahaba wake Sa’ad Ibn Muaadh-Allah amuwiye radhi. Akaona usoni mwake ishara ya uchukivu wa linalofanywa na wenzake (yaani uchukuaji wa mateka), akamwambia:
“Ewe Sa’ad, ninakuona kama kwamba hukifurahii kitendo cha wenzako hawa?” Akajibu: “Ndio, wallah! Ewe Mtume wa Allah, huu ndio ushindi wa kwanza aliotupa Allah dhidi ya mushrikina. Kwa hali hii basi, kuwaua watu hawa kunapendeza zaidi kwangu kuliko kuwabakisha na kuwachukua mateka”.
Vita vikamalizika kwa kusambaratika makundi ya mushrikina mbele ya nguvu ya imani ya kweli.
Wakauawa katika vita hivi mushrikina sabini, miongoni mwao akiwa ni Abu Jahli aliyekuwa shetani wa vita hivi na Umayyah Ibn Khalaf.
Kadhalika wakachukuliwa mateka mushrikina sabini akiwemo ami yake Mtume; Abbas Ibn Abdul-Mutwalib na Aqeel Ibn Abuu Twalib (mwana wa ami yake).
Mushrikina waliosalia wakatimua mbio kurudi Makkah wakiwaacha waislamu kukichukua ngawira kila walichokiacha nyuma yao. Ama kwa upande wa waislamu, waliofuzu kufa shahidi ni kumi na wanne tu. Ubaidah Ibn Al-Haarith akiwa ni miongoni mwa mashahidi hawa, huyu ni yule aliyejeruhiwa vibaya wakati wa ‘Mubaarazah’.
Ni vema ikakumbukwa kwamba vita hivi vya Badri vilianza asubuhi ya mwezi kumi na saba-Ramadhani-mwaka wa pili wa Hijrah(17Ramadhani/02 A.H.)
Karibu sawa na tarehe 13Machi, mwaka 624 A.D. na vikamalizika alasiri ya siku hiyo hiyo. Vita vilipomalizika kwa waislamu kupata ushindi mkubwa uliotokana na msaada wa Allah, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akaamrisha kuzikwa kwa mashahidi wa vita hivi.
Pia akaamrisha kutumbukizwa miili ya mushrikina latika kisima kilichokauka maji. Walipotumbukizwa kisimani humo, Bwana Mtume alisimama kisimani pale akaita:
“Enyi watu mliomo kisimani humu, ewe Utbah Ibn Rabeeh, ewe Sheibah Ibn Rabeeh, ewe Umayyah Ibn Khalaf na ewe Abuu Jahli (akawaita kwa majina wengi wa maiti waliomo kisimani mle). Je, mmeyakuta mliyoahidiwa na Mola wenu kuwa ni kweli? Kwani mimi nimeyakuta aliyoniahidi Mola wangu (ya kuwa nitakushindeni) kuwa ni ya kweli. (Anasema mama Aysha): Maswahaba wake wakamuuliza: “Ewe Mtume wa Allah, unazungumza na wafu (kwani wanasikia)?” Mtume akawaambia: “Hamkuwa nyinyi ni wenye kuyasikia zaidi niyasemayo kuliko wao, lakini wao hawawezi tu kujibu”.
Baada ya kumalizika shughuli za mazishi ya mashahidi na utupwaji wa miili ya mushrikina, Bwana Mtume akawatuma watu wawili kupeleka bishara ya ushindi Madinah.
Alimtuma Abdullah Ibn Rawaahah kwenda kutoa khabari za bishara kwa watu wa nyanda za juu za Madinah na kwa watu wa nyanda za chini alimtuma Zayd Ibn Haarithah.